Ijumaa, 24 Novemba 2017

BIKIRA MARIA HAKUWA NA WATOTO WENGINE ZAIDI YA YESU KRISTO
Enyi vijana, ninaendelea kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali mliyoniomba niyatolee ufafanuzi. Leo ni zamu ya swali la kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu au la. Kwa swali hili, naomba nianze kwa kumpa pole Mama Bikira Maria. Pole kwa sababu baada ya kuwazalia wanadamu Mkombozi, shukrani anayopata haikidhi haja. Mnajua, kutendewa ubaya na mtu uliyemfaa inauma sana tena mno.
Lakini, ndivyo inavyodhihiri kwa Bikira Maria. Saa hii hii, wapo wanadamu wanaotoka jasho na kusema mengi wakitaka adharauliwe kama bahasha inavyodharauliwa baada ya barua kutolewa ndani yake. Wapo wanaosema anaheshimiwa mno wakati alikuwa adharauliwe kabisa. Wapo wanaokereka na heshima inayooneshwa kwake. Wapo wanaotibuka nyongo wakisikia watu wanafanya ibada katika miezi ya Mei, Agosti na Oktoba kusudi aendelee na maombezi yake kwa mwanawe. Wapo wanaopata hasira wanaposikia watu wakisali awaombee wanadamu kwa mwanawe kwa kupitia rosari, litania na sala mbalimbali. Wapo wasiotaka kusikia sala ya Salamu Maria. Wapo wanaochukia na kutamani kufumba macho wanapoiona picha au sanamu ya Bikira Maria imewekwa kwa  heshima mahali pazuri.
He, weye, kuna mengi wasiyoyataka wasiompenda. Nadhani Mama Bikira Maria angelikuwa anaishi bado hapa duniani, mara kwa mara, angelikuwa anaanguka chini kwa shinikizo la damu kwa kuwa angelikuwa anaishi katika ushahidi endelevu wa methali ya “Shukrani ya punda mateke”. Lakini sivyo. Kwa kuwa yeye alikingiwa dhambi ya asili  na vile vile kwa kuwa alikumbana ana kwa ana na kituko cha kutoshukuriwa kule Kana, hata baada ya kuwaombea watu muujiza wa maji kugeuzwa divai, “angelipotezea” yote hayo na kusema tu, “Mwanangu uwasamehe, maana hawajui walitendalo. Ni maajabu ya mtu kupenda boga asilitake ua lake.” Si siri, tangu alipokuwa hapa duniani, dhambi ilikuwa si jambo lake. Kwa nini? Kwa sababu kwa kukingiwa dhambi ya asili Mama Bikira Maria alikuwa “baunsa” kiroho. Haya ya kutoshukuriwa inavyostahiki yalikuwa kwake na bado yangali kwake mambo ya kitoto tu.

Lakini, tuachie hayo pembeni, tujikite kwenye mada halisi ya leo. Ni hivi, watu wengine hupeperushia bendera mambo ya kuambiwa, kwa mfano, mintarafu swali kama Maria alikuwa na watoto wengine au la. Wengi wa wale wanaowauliza Wakatoliki kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo, hawajasoma Biblia wenyewe kwa kusudi la kutafuta jibu la swali hilo. Kumbe, leo nataka kuliweka jambo hili sawa.
Kuna makundi mawili ya watu wanaouliza swali hili: kundi la watu ambao hawakusoma Biblia hata kidogo na kundi la walioisoma. Watu wa kundi la kwanza wamewasikia watu wakiuliza swali hilo au  wamepata wenyewe kuulizwa swali hilo na wao ndio wanauliza pia swali hilo hilo. Si kitu. Kwa wale waliosoma Biblia na kisha kuibuka na swali hili najua huwa wanakorofishwa na nukuu hizi mbili: Mt 1:25 na Mk 6:1-3. Kwa hawa, baada ya kusoma Mt 1:25 na Mk 6:1-3 huhisi Maria alijamiiana na Yosefu na hivyo kuwazaa watoto wengine mbali ya Yesu. Si kitu. Lakini, yote juu ya yote, ni kwamba watu wa makundi yote mawili huvurugwa na majina ya “watoto wa Maria” wanaotajwa na Biblia kuwa  Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na  mmoja wa dada zao aliyeitwa Salome. Hapo ndipo linapoibuka swali ninalotaka kulijibu leo.

Sikiliza. Tutakuwa na jibu refu hivi punde, lakini tukijibu kifupi ni kwamba Bikira Maria hakuwa na mtoto mwingine zaidi ya Yesu Kristo na yeye mwenyewe kama alivyokuwa bikira kabla ya kumzaa Yesu, alibaki bikira wakati wa kumzaa Yesu na baada ya kumzaa Yesu (rejea Mt 1:25). Hii ndiyo sababu Wakatoliki tunamheshimu Maria kama Bikira wa daima.

Sasa twende kwenye maelezo marefu. Ni hivi, usiniambie lolote, najua neno fulani kuhusu wewe. Najua unataka kunibisha hata kabla sijaanza somo. Lakini kabla sijakupatia jibu kwa swali lako yafaa tujikumbushe vyanzo vya swali. Vyanzo hivyo ndivyo chokochoko yenyewe. Mazingira yanayoibusha swali hili yanaanzia kwenye aya hii hii Mt 1:25. Aya hii ni chokochoko ya swali letu kwa sababu ya utata wa maneno yake: “Lakini hakulala naye hadi Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu”. Maana ya maneno haya ndiyo inayowatatanisha wengi. Yaani, kwa maneno hayo inaonekana kana kwamba Yosefu, hapo baadaye alimjua Maria na kumzalia watoto wengine, hao wanaonekana kutajwa katika Mk 6:1-3. Lakini, tulia, mambo hayapaswi kueleweka hivyo.
Nakufafanulia. Awali ya yote, kusudi tujue kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine au la, yafaa kusoma Mt 1:25, Mk 6:1-3 na 15:40.47, 16:1 na hatimaye kuyafafanua mazingira ya Yn 19:25-27.  Hebu twende pole pole.
SWALI LINAANZIA MT 1:25
Aya hii haizungumzii nyakati za mbele isipokuwa inashughulikia uzazi wa Yesu kwamba alizaliwa bila mchango wa kimapenzi wa Yosefu. Kwa hali hiyo, habari za ndoa ya Bikira Maria na Yosefu haziwezi kutoshelezwa na maelezo hayo tu. Basi, kwa kusudi la kuyafahamu vizuri maisha ya wanandoa hao wawili, Mapokeo Matakatifu, yaani taarifa za masimulizi ya wale walioishi wakati wa Yesu, Yosefu na Maria ni muhimu. Hao basi, ndio waliolipokeza Kanisa taarifa kwamba  Maria alibaki bikira, kabla, wakati na baada ya kumzaa  Yesu.
Utaniuliza swali, je, Mapokeo Matakatifu yana uhalali wowote? Jibu ni ndiyo. Uhalali wa mapokeo umedokezwa kwenye Biblia yenyewe kwa namna mbili. Mosi, binadamu tunaambiwa  tuwaulize wazee wetu watueleze mambo ya kale (rejea Kum 32:1-12 na Yer 6:16). Basi, kati ya mambo hayo ya kale ni mambo kama haya yahusuyo ndoa ya Yosefu na Maria na uzazi wa Yesu Kristo Bwana wetu.
Pili, Biblia inatuambia kwamba mambo yaliyoandikwa ni machache tu nayo yamechaguliwa kukidhi haja ya kuwasadikisha watu Yesu Kristo alikuwa ni nani na kwa kumsadiki kwamba alikuwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa watu, wanadamu waupate uzima wa milele. Kumbe, kwa dokezo hili, lazima tuelewe kwamba mambo yaliyoachwa pasipo kuandikwa kwenye Biblia ni mengi kuliko yaliyomo kwenye Biblia. Ndiposa, imeandikwa kwamba mambo hayo yangeliandikwa yote dunia isingaliweza kutosha kuyashika maandishi husika (rejea Yn 20:30-31, 21:25).
Lakini, mambo hayo ambayo hayakuandikwa si kwamba yamepotea yote. Wale walioyashuhudia na kuyajua ndiyo wanaotufikishia kwa masimulizi yao ya kupokezana (1Yoh 1:1-4). Usinibishe. Biblia inadokeza kwamba mambo yote yaliyotufikia yalianzia kwenye kusimuliana kwa kupokezana. Yale yaliyoishia kuandikwa ndiyo yakatufikia kama Biblia (Agano la Kale na Jipya) na mengine yaliyokosa kuchaguliwa na kuandikwa ndiyo hayo yanayoendelea kama masimulizi bado. Hii ni kusema basi Biblia ni mapato ya mapokeo na ni mapokeo vile vile maana tumeipokea Biblia kutoka kwa wale waliotuandikia na kuidhinisha maandishi yenyewe. Agano la Kale liliidhinishwa mwaka 95 B.K. na Agano Jipya katika karne ya pili B.K. Hapa ndipo ulipo uhalali wa Mapokeo Matakatifu katika Kanisa. Je, umenipata uzuri?
SWALI LINAKOMAA KATIKA MK 6:1-3
Acha tusonge mbele. Tukisonga mbele na nukuu zetu, baada ya Mt 1:25 tunafika kwenye Mk 6:1-3 iliyo sawa na Mt 13:53-58 na Lk 4:16-30. Aya hizi zinasimulia habari za watu wa Nazareti kukwazika na maneno sawia na matendo ya Yesu Kristo. Katika kushangaa kwao, watu wa Nazareti wanajigamba kwamba wanawajua ndugu zake Yesu. Ndipo wanawataja “mabaunsa” wa kiume wanne: Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni. Hata hivyo, dada zake hawaorodheshwi.
Orodha ya “mabaunsa” hawa ndiyo inayopambisha moto fikra za watu kwamba walikuwa watoto wa Maria mama wa Yesu na hivyo Yesu kutozaliwa peke yake katika tumbo la mama yake. Aya inawataja vijana hao wa kiume na wa kike wasiotajwa majina kwa cheo cha kuwa ndugu wa Yesu. Ndipo swali halali linapoibuka, kama ndivyo inawezekanaje kuwa Yesu alikuwa mtoto pekee wa Bikira Maria? Poa. Hili si swali lililokosa jibu Bibliani.
BIBLIA YENYEWE INAJIBU SWALI LETU
Biblia ina ajabu moja, huwa inaibua swali na kujijibu yenyewe. Kumbe, mashaka yote ya kwamba vijana na dada waliotajwa katika Mk 6:1-3 ni ndugu wa Yesu au la, yanafutwa na Mk 15:40. 47 na 16:1. Akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni walikuwa watoto wa nani, jibu lipo katika aya hizi. Katika aya hizi wanatajwa wanawake waliokuwa wamesimama chini ya msalaba wa Yesu siku ile ya kusulibiwa kwake. Kumbe, katika kuwataja kwake tunaona wazi kwamba jina Maria lilikuwa likitumiwa na wanawake wengi na mmoja wa akina Maria hao alikuwa ni mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni na, katika mstari huo huo, kuwa hata mama wa wale dada waliodokezwa katika Mk 6:1-3 na Mt 13:53-58.
Tusibishane, leo tusome, maana tusiandikie mate na wino ungalipo. Mwandishi anatuandikia hivi, “Walikuwako pia wanawake wakitazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome, na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose”. Kutajwa kwa Maria huyu wa mwisho pasipo  kuandikwa neno “mama” na kivumishi cha moja kwa moja “yake Yesu” au “wa Yesu” ndiko kunakotuonesha kwamba Maria mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni hakuwa Maria mama yake Yesu. Vinginevyo mwandishi angeliandika na kivumishi cha moja kwa moja kama alivyofanya mwandishi wa Injili ya Yohane.
Mwandishi wa Injili ya Yohane ameweka mambo kama yalivyokuwa, “Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa na Maria Magdalena” (rejea Yn 19:25).
Kama jambo hili linagomba nitaeleza sasa hivi kwa mfano wetu wenyewe. Ikiwa wewe una ndugu zako wa tumbo moja, mathalani, Damas, Pius, Corbinian, Imelda na Melina, siku utakapotembelewa nao, yule atakayekujulisha ujio wa mama yako, labda aliye nje na mahali ulipokaa, atasema moja kwa moja, “Kuna mama yako nje, anataka kukuona” au “Kuna mama yako mzazi nje, anataka kukuona”. Huyo mwelezaji akisema,  “Kuna mama yao akina Damas, Pius, Corbinian, Imelda na Melina nje anataka kukuona” kuna mawili ama hajui kwamba yule ni mama yako mzazi au kwamba yule si mama yako ndiyo maana anakutajia majina ya watoto wake kusudi upate kumtambua vizuri”.
Kwa kesi yetu hii, mwandishi wa Injili ya Marko hawezi kufafanuliwa kwa hilo la kwanza eti kwamba hamkujua sawa sawa mama wa Yesu au la. Hata kama alisimuliwa habari hii na Mtume Petro, kwa vile mwandishi asivyokuwa mtume mwenyewe, asingelikosa kujulishwa vyema habari za mama wa Yesu. Kwa mantiki hii, limebaki hilo la pili tu kwamba yule Maria hakuwa mama wa Yesu isipokuwa mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni tu. Na hivi yeye ametuandikia hivi tupate kuwapambanua vyema akina Maria wale wengi.
MAZINGIRA YA YN 19:25-27 YANASHADIDISHA HOJA
Mazingira ya Yn 19:25-27 ndiyo yanayotukamilishia ukweli kwamba Bikira Maria hakuwa na mtoto wala watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo Bwana wetu. Kwa nini? Kwa sababu watoto wa kiyahudi walisisitiziwa sana kuwatunza wazazi wao hata kama wakiwa wazee au wagonjwa (rejea Mit 19:26, 23:22-25, 28:14, YbS 3:3-18). Basi kitendo cha Yesu kumkabidhi mama yake kwa rafiki yake ni ishara wazi kwamba “mabaunsa” akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni na dada zao waliotajwa katika Mk 6:1-3 na sehemu zinazosadifu hawakuwa ndugu wa moja kwa moja wa Yesu. Basi, kwa kuwa walikuwa na wazazi wao wenyewe, jukumu lao lilikuwa kwao na si kwa Maria, mama wa Yesu.
Hii ni kusema, Yesu alikuwa peke yake, vingineyo mabaunsa hayo na dada hao, baada ya kifo cha kaka yao Yesu, ndio wangelichukua jukumu la kumtunza mama yao na si huyo rafiki wa Yesu. Kifupi, kitendo cha Yesu kumkabidhi rafiki yake mama yake, ni ushuhuda wa upweke wake.
Aidha, kitendo hicho ni ushuhuda wa mambo mawili mengine ya msingi sana. Mosi, ni ushuhuda wa kwa nini Bikira Maria aliwachukua watoto wa Maria mwingine na kukaa nao. Yaani kwa vile Yesu alikuwa mtoto pekee naye alikuwa akitembea huko na huko, mama Maria aliwachukua watoto wa Maria huyo mwingine kusudi apate “kampani” maana mwanamke na watoto ni mate na ulimi. Tena, mama yao wenyewe alikuwa katika utume wa hiyari wa kumfuata na kumtumika Yesu (rejea Mk 15:40). Hapa pameandikwa hivi: “Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia.”
Pili, ni ushuhuda unaodokeza kifo cha Yosefu, mume wa Maria na baba mlishi wa Yesu. Hapa tunapashwa habari kwamba Yosefu alikuwa ameshakufa na hivyo hakuwapo duniani wakati Yesu anakufa msalabani. Kwa vipi? Kwa sababu Yesu asingeliweza kutenganisha ndoa ya “wazazi” wake. Kama Yosefu angelikuwa mzima, pasipo mashaka yoyote, angeliendelea na matunzo ya mkewe na  hivi kitendo cha Yesu kumkabidhi mama yake kwa rafiki yake kingelikuwa kitendo haramu. Kitendo chake kingelikuwa kitendo cha kutenganisha ndoa nzima.
MSAADA WA LUGHA ZA KISEMITI
Hatimaye, ieleweke kwamba neno “ndugu” katika lugha za Kisemiti, mathalani, Kiebrania na Kiarabu, na hivyo tafsiri yake katika Kigiriki “adelphoi” (wingi kwa kiume) au “adelphai (wingi kwa upande wa kike), ni neno pana sana. Katika lugha za Kisemiti, “ndugu” inamaanisha wote, ndugu wa damu, wa ukoo na jamaa wote wa karibu. Ndipo watoto wa mama mdogo au mkubwa ni ndugu. Watoto wa baba mkubwa au mdogo ni ndugu. Binamu wote ni ndugu na kadhalika. Hivi “ndugu” wa Yesu kwa Maria waliotajwa katika Injili inawezekana walikuwa ama watoto wa mama mdogo au mama mkubwa au hata watoto wa shangazi yake.
Kwa kumalizia basi, naomba matumizi haya ya neno “ndugu” yasituletee “ushangazi” mwingi  hasa sisi Waswahili. Sisi nasi tunalitumia neno hilo kwa mapana hayo hayo ya Kisemiti. Ndiposa, ukweli umebakia na unadumu ule ule mmoja: Maria hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo na hivyo Maria alikuwa bikira, kabla, wakati na baada ya kumzaa Yesu Kristo. Narudia nishindilie hoja iliyojibiwa: Yesu alikuwa mtoto wa pekee wa Bikira Maria na hivyo Maria hakuwa na watoto wengine wa ziada.
HATIMA
Natumaini jibu langu limekuelea. Na sasa, ili uulambe utamu wake vizuri, hebu malizia kwa kuzisoma aya zote tulizozijadili kwa mfululizo wa kimantiki kama ifuatavyo:
Mt 1:25 - “Lakini (Yosefu) hakulala naye hadi Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu”.
Mk 6:1-3 -   “Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akafuatwa na wanafunzi wake. Siku ya Sabato ilipofika alianza kufundisha katika sinagogi. Wengi walipomsikia walishangaa, wakasema, ‘Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya? Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria, na ndugu yao akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?’ Basi, wakawa na mashaka naye.”
Mk 15:40 – “Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia.”
Yn 19:25-27 - “Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa na Maria Magdalena”. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, ‘Mama!, Tazama, huyo ndiye mwanao.’ Halafu akamwambia yule mwanafunzi, ‘Tazama, huyo ndiye mama yako.’ Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake”.
Mk 15:47 – “Nao Maria Magdalena na Maria mama yake Yose walipaona alipolazwa”.
Mk 16:1 – “Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalena na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.”
Mwishoni kabisa, najumlisha niliyosema kama ifuatavyo: Yosefu hakujuana na Bikira Maria kwa kumpisha Mungu aliyemtwaa mkewe kwa matumizi maalumu. Zaidi sana, Mt 1:25 haisemi kwamba baada ya kumzaa Yesu, Yosefu alijitwalia haki yake ya ndoa na mwishowe Mk 6:1-3 lazima ieleweke katika mazingira ya Kisemiti ambapo hata jamaa na ndugu wa familia moja hujulikana kama “ndugu”. Kwa hali hiyo, majina ya akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na Salome wao hayasemi lo lote dhidi ya ubikira wa mama Maria. Mwisho wa yote Mk 15:40.47 na 16:1 zinakata maneno kwa kutuambia kwamba akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na Salome walikuwa na mama yao wenyewe. Na ndiyo kisa Yesu alipaswa kumtafuta mtu mwingine kumtunza mama yake kama tunavyosoma katika Yn 19:25-27.
Kwa mara nyingine kwa herini. Ikiwa jibu hili hujalielewa vyema nakuomba uisome mada yangu mara mbili au mama tatu. Ukifanya hivyo, sitegemei kabisa kwamba utatoka kapa mara zote hizo. Kwa heri!
NI AIBU KWA MKRISTO KUPAGAWA NA SHETANI
Natamatisha mada ya Bikira Maria kutokuwa na watoto zaidi ya Yesu Kristo. Ilikuwa rahisi kama maji. Mk 6:1-6 imejibiwa vizuri na Mk 15:40.47 na 16:1-2. Acha jazba, usome sehemu hizi kwa utulivu. Yesu alikuwa mtoto pekee wa Mama Bikira Maria. Kwa kutamatisha mada hiyo, maana yake wakati wa kuwaleteeni mada nyingine ndiyo umejifungua.
Lakini, kabla sijawaleteeni mada nyingine katika mfululizo wa kujibu maswali yenu, karibuni vijana kwa kibwagizo cha mwezi. Kibwagizo chetu ni aibu kubwa tena kubwa sana kwa Mkristo kupagawa na Shetani. Lakini, hebu tuwekane sawa kabla hatujapiga mbizi kwenye kibwagizo chetu. Shetani yupo na anaweza kumpagaa mwanadamu lakini ni aibu ikiwa mwanadamu huyo ni MKRISTO. Kwa nini? Nitakujibu mwenyewe tena mara moja. Ni aibu kwa sababu ni ushahidi wa wazi kwamba kuna kitu si sawa kwake. Ni ushahidi kwamba hajasimama wima Kikristo. Mkristo alipaswa aogopwe na Shetani kwa sababu ya vipengele vinne: ushindi wa Kristo, ulinzi madhubuti alionao, silaha sita anazomvalia Shetani na mbinu aliyopaswa kuitumia. Nitaeleza kwa mapozi kipengele kimoja baada ya kingine. Haya tuanze na tufuatane vizuriMa.

USHINDI WA KRISTO: Pasina shaka yoyote Kristo amemshinda Shetani na hayo ni mapato tarajiwa ya mradi wake mkubwa wa kuwakomboa wanadamu. Mapato ya kazi ya Kristo hayakuwa ya kitoto. Yesu aliachilia kwa muda fahari zake za kimungu, akajifanya mtu kwa kuutwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake Bikira Maria ili kwa damu na nyama yake amtolee Mungu sadaka iliyotukuka kwa upatanisho na Baba. Soma sehemu zifuatazo uelewe vyema fumbo la umwilisho: Yn 1:1-14, Lk 1:26-48, Plp 2:6-11 na Ebr 10:5-10.
Kwa kifupi, Kristo amemshinda Shetani kwa niaba ya wanadamu wote. Ushindi wake siyo wa kutafutwa na tochi. Ulikuwa ushindi wa kipigo cha mbwa kwa Shetani. Kwa damu yake azizi na sadaka yake ya msalabani, yeye ameung’oa, kuharibu, kuangamiza na kuuteketeza ufalme wa Shetani na mahali pake amejenga na kupanda ufalme wa Mungu (Yer 1:4-10). Mwenyewe alisema: “Lakini ikiwa  ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwsha fika kwenu. Au anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang’anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang’anya mali yake”.
Kwa kusema hivi Yesu hakuwa anausifia ujambazi, isipokuwa kuwahakikishia wanadamu kwamba yeye ndiye “baunsa” atakayemzidi nguvu Shetani, mfalme wa dunia kwa wakati ule, na kisha kuwanyakua watu waliokuwa chini ya milki yake na kuwafanya wafuasi wake, yaani WAKRISTO. Wakristo tumenyakuliwa na Kristo kutoka ufalme wa Shetani, tukaingizwa naye katika ufalme wa Mungu kwa Ubatizo. Ndiyo maana kazi hii tukufu inaitwa Injili, yaani Habari Njema ya Furaha kwa wanadamu wa kila mwendo wa maisha (Lk 4:18). Asiyebatizwa peke yake ndiye mwanadamu anayebahatisha bahatisha  bado nje ya ufalme wa Kristo. Lakini huyo naye siku atakapobatizwa tu atajiwekea sawa mambo yake. Sasa inakuwaje Shetani aliyefungwa na Yesu Kristo aishi ndani ya yule aliyekombolewa naye? Ndipo inapokuja aibu kwa “Mkristo aliyepagawa”. Tumwulize kwa haki, kulikoni tena? Sasa naeleza kidogo mambo yanavyoshangaza kwa Mkristo anayeweweseka, kutetemeka, kulialia, kuanguka anguka na kugaagaa eti kwa kupagawa na Shetani. Jamani, mambo!

ULINZI MADHUBUTI ALIONAO MKRISTO: Mkristo analindwa kwa namna sita: amepakwa mafuta ya wakatekumeni siku ya Ubatizo wake, ana malaika mlinzi, ana majina ya Yesu na Maria, analindwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo, yupo kwenye ngome ya Kanisa na ana akili na utashi.
• Mkristo amepakwa mafuta ya wakatekumeni: Mkristo amepakwa mafuta ya wakatekumeni siku ya Ubatizo wake kwa kinga yake dhidi ya Shetani. Au tuseme hatujui maana ya mafuta yale wanayopakwa wabatizwa kifuani? Basi, leo sikiliza. Siku ya ubatizo Mkristo alipakwa mafuta ya wakatekumeni kifuani kumwinga Shetani. Sasa Shetani anarudije kuishi ndani ya Mkristo? Kama nyumba ilifagiliwa na jambazi aliyekuwa anajificha humo ametimuliwa, jambazi huyo anarudije kukaa ndani ya nyumba ile ile tena? Amepitia mlangoni au wapi? Kwa vipi mwenye nyumba amemwacha afike tena? Je, amevunja dirisha?
Hakika kuna kitu Mkristo alichofanya hata kumpatia Shetani fursa ya kurudi tena. Hakika si bure, maana imeandikwa: “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika asipate. Hapo husema, ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka’, lakini anaporudi na kuikuta tupu imefagiliwa na kupambwa, huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali yake mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu’” (Mt 12:43-45).
Je, unanibisha bado? Unataka kusema sijaeleweka? Kama hujanielewa nitakufafanulia kwa kuhoji. Shetani anapataje fursa ya kuja siyo tu kuichafua nyumba ya Mkristo bali kuja kukaa tena kama Mkristo mwenyewe hana hatia? Mkristo amefanya nini hata mafuta ya wakatekumeni aliyopakwa siku ya Ubatizo wake yakachotora (expire)? Kwa maneno mengine, Mkristo alilingana na chupa ya dawa ya kunguni, iweje kunguni aishi ndani yake tena? Ndipo inapokuja aibu kwa Mkristo mhusika.
• Mkristo ana malaika mlinzi: Kila mwanadamu amepewa malaika mlinzi mmoja wa kumlinda. Imeandikwa, “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu. Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori…” (Kut 23:20-23). Soma pia jinsi tulivyo na malaika wetu mbele ya uso wa Mungu (Mt 18:10). Je, imeeleweka sawa sawa?
Sasa nisikilize vizuri. Shetani ni malaika na malaika mlinzi ni malaika. Ikiwa ndivyo, Shetani anamshindaje tena malaika mlinzi  wa mtu hata yeye kuhamia kabisa moyoni mwa mwanadamu huyo? Bila shaka, ni kwa sababu ya Mkristo kutoshirikiana vyema na malaika wake mlinzi. Bila shaka, kwa sababu ya ufurufuru na dhambi zake binafsi, Mkristo ashikani mkono na malaika wake mlinzi. Kumbe, ndipo inapokuja tena aibu kwake.
• Mkristo ana majina ya Yesu na Maria kinywani na moyoni mwake: Majina ya Yesu na Maria “yanamtoa baruti” Shetani kwa sababu anayaogopa sana. Ni majina ya “wabaya wake” waliomshinda katika ushirikiano wao. Yaani kila majina hayo yanapotamkwa Shetani hutoka mbio. Basi, ikiwa Mkristo anayatamka majina haya pasipo Shetani kukimbia, Shetani anamjua mtu huyo kwamba ni mnafiki au anayataja majina hayo bure na pasipo heshima yoyote.
Katika kitabu cha Matendo ya mitume, watoto wa Skeva, watoa pepo wa Kiyahudi, ambao kwa kawaida walikuwa wanawatoa pepo kwa kumpachika mgonjwa vitu vya kunuka pamoja na kumtukana Shetani matusi makubwa makubwa, walilitumia jina la Yesu pasipo kumwamini Yesu mwenyewe. Shetani aliwafedhesha kadamnasi siku hiyo.
Imeandikwa hivi: “Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia,  wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: ‘Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri’.
“Watoto saba wa Skeva, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, ‘Ninamfahamu Yesu, namjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?’ Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skeva wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi ana asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote wakaingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. Waamini wengine walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya imani ya kishirikina hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha hamsini elfu. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi” (Mdo 19:11-20).
Je, unaelewa sasa ninachosema? Nakuomba leo uchague kuelewa. Kumbe, jina la Yesu si la kutaniwa na kutajwa ovyo ovyo. Ndipo, kwa Kkujibari na fedheha za mtindo wa fedheha ya watoto wa Skeva, Kanisa Katoliki liliweka Sheria ya Kanisa na. 1172 paragrafu 1 na 2 ili atakayelitumia jina la Yesu alitumie kwa hadhi yake naye afanikiwe kupunga pepo wa kweli.
Sheria hii inasema mtu wa kuwinga pepo awe padre aliyeruhusiwa na Askofu, kwa maandishi, baada ya kubainika kuwa na sifa nne binafsi: uchaji, ujuzi, busara na uadilifu. Padre mwenye sifa hizi anayeweza kufanikisha upungaji pepo wa kweli, la sivyo ni uzandiki, usanii na “upangaji miujiza” tu.
• Mkristo analindwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo: Yesu Kristo ametangaza ulinzi wa pekee kwa wafuasi wake kiasi hiki walipaswa wasimwogope Shetani kana kwamba ni yatima wa kiroho. Mtu ukiwa na kaka yako mwenye nguvu sana lazima ujisikie salama kabisa. Yesu ndiye kaka yetu wa namna hiyo, Shetani anatuhangaishaje tena? Sikiliza jinsi Yesu alivyolizungumzia jambo hili yeye mwenyewe. Tunasoma alisema ifuatavyo: “Kondoo wangu huisikia sauti yangu, nami nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele, nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. Mimi na Baba tu mmoja” (Yn 10:27-30). Sikiliza maneno hayo ya kulindwa vizuri kabisa!
Sasa, hadi Mkristo anapagawa anatokaje mikononi mwa Yesu Kristo? Ikiwa ametoka kweli mikononi mwa Yesu naye kugeuzwa “nyumba ya Shetani” kuna kitu kibaya kweli kweli alichokifanya kiroho. Ni nini hicho asichokwenda kukifuta kwenye kiti cha Kitubio? Ndipo inapokuja tena aibu kwake.
• Mkristo yupo kwenye ngome ya Kanisa: Mtu awapo na wenzake, hupata kulindwa na mshikamano wake na wenzake. Kule kuwa kati ya watu wengi tu ni ngome ya ajabu. Wingi wa wanakanisa ni ngome. Mtu aliye ndani ya ngome yupo salama. Mtu aliyejishikamanisha na kundi ni salama, hata awe ni mzee sana, mgonjwa sana au mtoto sana. Kinyume chake, mtembea pweke, au mtu yeyote awapo nje ya ngome huwa chambo cha Shetani anayezunguka zunguka huko na huko akitafuta mtu anayezubaa zubaa ammeze (1Pet 5:8). Kifupi, nje ya ngome ya Kanisa si salama. Mtu kutembea na kulala nje ya ngome ya Kanisa ni kujihatarisha mwenyewe. Shetani hawezi kumvaa Mkristo aliyekamilika isipokuwa “mzee katika imani”, “mgonjwa katika imani” au “mtoto katika imani”. Mtu kama huyo ni chambo rahisi cha Shetani.
Lakini, ilitakiwa chambo cha Shetani asiwe Mkristo bali mtu wa imani au dini nyingine asiyeishi katika ngome ya Kanisa kwa kuwa hajaiingia bado. Sasa ikiwa kweli Mkristo amepagawa na Shetani anatupa ushahidi kwamba ametoka nje ya ngome ya Kanisa. Ni ushahidi kwamba hana mshikamano wa kweli na Kanisa. Lakini ni kwa nini? Kumbe, ndipo inapokuja aibu kwake. Aheri mtu kama huyo ajirudishe haraka haraka ndani ya Kanisa.
• Mkristo na akili na utashi: Vipaji vya akili na utashi ndivyo vinavyomfanya mwanadamu awe sura na mfano wa Mungu (Mwa 1:26-28). Kwavyo anaweza kuchagua mema na kukataa mabaya. Lakini ikiwa mtu hatumii vipaji hivi anakuwa dhaifu kama ng’ombe au mbuzi vile. Na mtu dhaifu namna hiyo, Shetani anampenda kiasi cha kuhamia kwake moja kwa moja kwani si chochote isipokuwa mtu laini kama mchicha, tembele au mlenda. Kifupi, mtu wa namna hiyo ni mboga ya Shetani.

SILAHA SITA MKRISTO ANAZOMVALIA SHETANI: Mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso amependekeza silaha sita za kumvalia Shetani: ukweli, uadilifu, hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani, imani, kuupokea ukombozi na neno la Mungu.
Kuhusu jambo hili, Mtume Paulo ametuandikia ifuatavyo: “Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama dirii kifuani, na hamu ya kutanga Habari Njema ya amani iwe kama buti miguuni mwenu. Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. Ukubalini ukombozi kama kofia yenu ya chuma (helmeti) na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu” (Efe 6:14-18).
Kutokana na haya, Mkristo anayetutangazia wenzake kwamba amepagawa na Shetani anatuambia kwamba ametindikiwa ukweli, uadilifu, hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani, imani, kukubali ukombozi na neno la Mungu. Je, kali eh? Ukweli ndiyo ulivyo hautazami sura wala majira. Basi, ndivyo lilivyo neno la Mungu linakata pale mfupa ulipoungana na nyama! Mkristo aliyepagawa na Shetani anatupa ushahidi wa wazi kwamba hajamvalia Shetani silaha zilizopendekezwa na Mtume Paulo, yaani ni kama mtu anayetembea katika nchi ya baridi na fulana tu.

MBINU ALIYOPASWA MKRISTO KUITUMIA: Yakobo alitoa mbinu nzuri ya kumshindia Shetani ndiyo kumpinga Shetani na kumkaribia Mungu. Ameandika hivi, “Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Shetani naye atawakimbieni. Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenye enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki! (Yak 4:7-8). Kumbe, kwa maneno haya, Mkristo kupagawa na Shetani ni ushahidi kwamba hajafanya juhudi za kutosha kumpinga Shetani na wala hajafanya juhudi za kutosha kumkaribia Mungu. Kifupi, Mkristo huyo ana hatia binafsi. Ndipo hapo inapokuja tena aibu kwake.

HATIMA
Narudia mara kurudia. Kwa Mkristo kupagawa na Shetani ni dalili ya shida yake mwenyewe, yaani dhambi yake mwenyewe. Kwa sababu hii ilikuwa aone haya na hivyo ajifiche mbele ya Wakristo wenzake. Ilikuwa augue peke yake moyoni mwake na kujirudi katika vipengele nilivyovieleza katika kibwagizo hiki. Niruhusu nitumie lugha ya picha kali sana. Ashkum si matusi, Mkristo kupagawa na Shetani ni kama mtu mzima kutokwa na haja ndogo au kubwa hadharani, ni aibu.
Ni aibu kwa sababu mtu mzima asiye mgonjwa, anategemewa kujizuia asitokwe na haja mbele ya watu. Kumbe, mkasa kama huo huonewa haya ya uso. Hauonewi fahari, isipokuwa humlazimisha mtu mzima kwenda kujificha mahali pa faragha, kujisafisha, kujitia manukato na kurudi hadharani kwa soni ya aina yake. Hivi ingekuwa aibu kwa Mkristo kutetemeka, kuweweseka, kulialia, kuanguka na kugaagaa hadharani, mathalani, kwenye mkutano wa sala, kongamano seuze kanisani kwa hoja eti amepagawa na Shetani. Ni aibu kwake mwenyewe na aibu isionewe fahari.
Lakini, ajabu siku hizi Wakristo, tena si mmoja bali kwa makumi na mamia, wanakula mieleka hadharani na kugaagaa eti wamepagawa na Shetani. Ajabu ya Firauni! He, Shetani amewajaa Wakristo hivi, kana kwamba Kristo hamkumshinda Shetani kwa niaba yao! Aibu! Jamani, aibu! Wakristo wengi hivi wana mapepo! Huku ni kuufedhehesha Ukristo. Eti watu wakisema hawautaki Ukristo kwa sababu Wakristo wengi ni “nyumba za Shetani”, tutashangaa! Tutashangaa nini wakati tunasema hivyo kwa vitendo vyetu wenyewe? Tushangae nini, kwani watu hawatuoni tunapoanguka hadharani kama embe dodo? Jamani, mchezo wetu ni kifo cha dini yetu wenyewe. Tukome kuuaibisha Ukristo hivi. Tukomeke!
NATOA MWITO. MAMBO YA KUPAGAWA, TUSIFANYIE MASIHARA KWA HESHIMA YA DINI YETU YA HESHIMA SANA. TANGU SASA, KILA MKRISTO AONE AIBU KUDHIHIRIKA KWAMBA AMEPAGAWA NA SHETANI. NI AIBU INAYOTANGAZA HADHARANI KWAMBA HAYUKO SAWA KIIMANI NA AIBU HAIONESHWI NJE. KAMA MTU UNA PEPO CHUTAMA KWENYE KONA YA MBALI HUKO USAIDIWE SIRINI NAWE UTAPONA.
LAKINI KABLA YA MSAADA MWINGINE WOWOTE JIPELEKE MWENYEWE KWANZA KWENYE KITUBIO UKAONDOE HICHO KILICHOMFUNGULIA SHETANI MLANGO WAKO! NAKUOMBA USIJISINGIZIE KUTOKUWA NA DHAMBI (REJ. 1YOH 1:8-110). LAKINI KAMA KWELI HUNA DHAMBI YOYOTE, BASI, SHIDA YAKO NI YA KISAIKOLOJIA TU. HUENDA NI NUROSISI AU SKIZOFRENIA AU “MULTIPERSONALITY” AU UMANYETO (HYSTERIA) NA KADHALIKA. KAMA NDIVYO ITENGENEZE SHIDA HIYO KWA MATIBABU YA KISASA (PSYCHOTHERAPY)! USISUBIRI TENA KITU. UKICHANGANYIKIWA ZAIDI UTAPELEKWA MIREMBE BURE! OOOH! HUKO MBELE USISEME HAKUKUWA NA PADRE ALIYEONYA. HAITAKUWA KWELI, NILIKUWEPO MIMI!
MWAFRIKA ANAPASUKA VIPANDE KWA SABABU WALIMU WAKE WENGI MNO
Baada ya mjadala wetu uliopita tusonge mbele na mada zetu. Kama ninavyoahidi ninaandikia moja moja mpaka ziishe kwenye benki. Leo ni suala la utengamano wa Mwafrika. Mwafrika si mmoja. Mwafrika ni mtu wa kuhurumiwa. Anapaswa ahurumiwe kwa sababu anapasuliwa vipande vipande na walimu wake ambao ni wengi mno. Usinibishe. Ni hivi, kuna wengi mno wanaompatia Mwafrika majibu kwa matatizo yake. Si siri, majibu yanapokuwa mengi lazima yatakuwepo ya uongo, hususan yale yanayofungamanishiwa malipo ya kutatanisha.
Kitu kinachoshangaza ni hiki, tatizo hata likiwa moja, Mwafrika atashauriwa kwa namna zisizopungua sita na watu sita tofauti. Nitajieleza kwa mfano wala usihangaike. Chukulia matatizo yafuatayo: ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu.
Mwenye matatizo kama haya ole wake asijitulize. Akijitembeza tu “ametembezwa”. MOSI, akimwendea mwalimu wa Chuo Kikuu atamweleza kwa namna ya kutinga na nukuu za vitabu vikubwa sababu za ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu. Atamshauri dawa za aina mbalimbali hata mwenye dhiki anaweza kuona kizunguzungu. Kwa huyu anaweza kuacha “mshiko kidogo” kama asante kwa huduma. Haya, mwache huyo pembeni.
PILI, akimwendea mtu aliyejinyakulia wadhifa wa kutoa mapepo atampa jibu dogo tu kwa yote hayo. Yeye atamweleza kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu ni matatizo yanayosababishwa na mapepo na dawa yake ni kutolewa mapepo tu. Si siri, kwa mtu huyo na maswahiba wake kila kitu watakieleza kama pepo: kukosa ajira pepo, kukosa mke au mume pepo, malaria pepo na kadhalika. Yaani kwao matatizo mengi jibu moja - mapepo na dawa moja –kutolewa pepo.
Ndiyo kisa, yeye na wenzake wanafundisha, kwa bidii, kuwasemesha watu sala ya toba na kuwapaka mafuta kwa kusudi la kuwatoa watu mapepo.  Kwa mtu huyo aliyejinyakulia wadhifa wa kutoa mapepo watu, baada ya huduma ya kutolewa mapepo, atatolewa “upepo” mfukoni pia. Lakini, basi, mwache huyo naye pembeni.
TATU, mwenye dhiki huyo huyo akienda kwa mganga wa kienyeji ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu, vyote vinatokana na kurogwa na dawa yake ni kupewa kinga tu dhidi ya ulozi.
Zaidi ya hayo, mshirikina huyo atamwaminisha “mteja” wake mambo mazuri chungu mzima, kwa mfano, kwamba kuruka ni jambo rahisi tu kwani ni kitendo cha kukaa juu ya ungo mdogo, au kumpanda fisi, au kujiingiza ndani ya pembe ndogo, kufumba macho na kuruka kwenda anakotaka kwa spidi ya ajabu. Hapo hapo, ataaminishwa kwamba akitaka kupata cheo wala asihangaike maana ni kitu rahisi sana, akifunga moyo wake na kumkata kidole albino atakuwa amemaliza kazi. Aidha, akitaka kupata pesa asiumize kichwa kwani ni kitendo cha kumiliki “chuma ulete” na pesa kuhamia kwake. Hata kulima kusimkoseshe usingizi hata kidogo kwani ni shauri dogo tu kama ilivyo kunywa uji, yaani akitaka kulima shamba kubwa ni shauri la kupata dawa ya kuwaamshia watu waliolala na kuwapeleka shambani kwake na vivyo hivyo akiwa na mizigo mizito, kwa dawa yake mahsusi, ataweza kuwaamsha watu na kuwabebesha mizigo yake yote na kwa namna hiyo hahitaji gari lolote lile.
Lakini, mwishoni mwa shughuli za mganga wa kienyeji, “mteja” atakuwa amemwachia, kwa kadiri ya maneno yam ganga mwenyewe, mathalani, jogoo mweupe anayejifunza kuwika, mbuzi mwenye kidevu, nazi sita zilizovunwa katikati ya wiki, upande mmoja wa kitenge kisichofuliwa na lundo la kufaa la noti nyekundu. Mwache huyo pia pembeni.
NNE, kishapo mwenye dhiki huyo akijifikisha kwa mganga wa kitabu au muumini wa imani za majini, ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na majini na dawa yake ni ndogo tu, ndiyo kusomewa dua na kusilimu kuwafukuza majini. Kwa ushauri wa aina hii, mwenye dhiki anaweza kusilimishwa papo hapo.
Muumini wa imani za majini akiwa Mkristo baada ya kusema matatizo ya mteja wake yanasababishwa na majini atatoa suluhisho la “kukemea majini” na mwishowe kummwagia maji ya baraka mteja wake. Lakini, wote hao wawili watamalizia kwa kumwomba mteja wao asante katika sura ya pesa. Haya, tuwaache hawa wawili pembeni.
TANO, mwenye dhiki huyo huyo akienda kwa muumini wa nadharia ya laana anayewaendeshea watu “maombezi ya nguvu” ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na laana na dawa yake ni ndogo tu, yaani kuzikataa dhiki hizo kwa sala ya kukemea, kuvunja mti wa familia au ukoo na kufanya ibada ya kufunguliwa. Mwishoni, huko kwa muumini wa nadharia ya laana, mteja husika, atakuwa ametakiwa kuacha kitu anachofikiri kinaweza kuwa mchango wa ukarimu kwa huduma za maombezi.
HATIMAYE, SITA, mwenye dhiki huyo akijing’azisha kwa mchungaji ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na dhambi zake mwenyewe na dawa yake ni ndogo tu, ndiyo kumkiri Yesu kwa kinywa, kuongozwa katika sala ya toba na kisha kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wake. Kifupi, atashauriwa “aokoke” kusudi mambo yake yakae sawa. Mambo hayo, wandugu! Nadhani mmenipata uzuri katika kauli zangu.
Lakini, kabla hajaondoka kwa mchungaji husika, mwenye dhiki wetu, atakuwa ametakwa achangie awezavyo kusudi mchungaji na mkewe wapate kujikimu na hivyo kupata nguvu ya kuendeleza huduma kwa watu. Ndipo atakuwa ameshaelekezwa atume pesa kwenye MPESA, AIRTEL MONEY, TIGO PESA au atume chochote kwenye akaunti fulani ya CRDB, Axim Bank, NMB, NBC na kadhalika. Kumbe, tumwache mchungaji naye pembeni.
Naona nimesema kutosha nataka leo nisikuchoshe. Nafurahi leo kufaulu kukuambia ya kutosha pasipo kukuchosha. Lakini hapo ndipo linapokuja swali moja halali sana: “Katika hao wote sita Mwafrika amsikilize nani hasa?” Jibu langu ni sijui, kazi kwake mwenyewe.
Lakini hapo ndipo inapokuja ole yake, ole ya utengamano wake wa kimwili na kiroho. Mwenye dhiki wetu, hadi anamaliza safari yake ya kujitembeza huko na huko kwa watu AMEPASUKA. Yaani, kama atakuwa hajapasuka vipande atakuwa ameshageuka mhangaikaji mkubwa, kwani ndiyo hivyo atakuwa juzi alimtegea sikio huyu, jana alimtegea sikio fulani, leo anamtegea fulani, kesho mwingine na keshokutwa mwingine.
Matokeo ya kutangatanga kwake yatakuwa kushindwa kujua kwa kuelekea kwa sababu “miluzi” ameshapigiwa mingi mno. Lakini tusisahau wahenga wamezoea kusema, “Miluzi mingi humpoteza mbwa njia”.
Kumbe, kwa kadiri yangu, hii ni moja ya sababu zinazomfanya Mwafrika ashindwe kukua na kuendelea. Mwafrika hana utulivu wa kubuni kitu cha kwake. Anategemea “wasemavyo” wengine. Lakini, kwa maisha ya namna hii, Mwafrika anajinyima fursa ya kufikiri peke yake. Amejizoeza na anaendelea kujizoesha kuwangoja wengine wamemfafanulie kinachomsibu, yakiwa maelezo ya kweli heri, yakiwa ya uongo sawa pia. Hayo ni mintarafu roho na mwili wake.
Ndiyo kisa, kimwili, anajikuta akisubiri watu wavumbue vitu yeye “ashambaikie” tu. Ndivyo alivyoshambaikia viatu, nguo, saa, radio, tochi, umeme na kadhalika. Na ndivyo anavyoendelea kushambaikia simu (sasa smartphones), baiskeli, pikipiki, bajaji, magari, treni, ndege na kadhalika. Kwa kweli, inasikitisha, Mwafrika hana chake cha kujivunia mbele ya watu wa mataifa mengine mbali ya ngoma.
Sasa nahitimisha kwa kusema ombi moja. Vijana katika ghubu hilo, dumuni katika kulisikilza Kanisa kwani hilo huelezea mambo yote pasipo dawa kumbakumba. Linapambanua mambo kwanza, litakutengea vizuri, matatizo ya kimwili, matatizo ya kijamii, matatizo ya kiuchumi, matatizo ya kitamaduni, matatizo ya kisaikolojia na kadhalika.  Ndipo, pamoja na kukulea katika imani iliyotukuka litakushauri umkimbilie elimu kwa sababu si maungwana uangamie kwa kukosa elimu (rejea Isa 5:13 na Hos 4:6).
Jisomee vifungu hivi wewe mwenyewe. Babu Isaya alisema, “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa” na Hosea anarudia jambo hilo hilo akisema, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.” Kwa sababu hii, leo nakuasa sana wewe uchomoke huko uliko! Nakusihi, usiwe mmoja wa watu wanaoangamia kwa kukosa maarifa na tena usisahau watu wameshabadili ile methali ya zamani iliyosema, “Wajinga ndio waliwao” kuwa “Wenye imani iliyokaa henamu ndio waliwao”.
Kumbe, wewe usiwe mmoja wa wanaoliwa leo. Utamaliziwa pesa yako. Pesa ya biashara yako au kilimo chako itaishia mikononi mwa wajanja na watu wakishashikishwa pesa hawajui “reverse”. Utamaliziwa mbuzi wako. Utamaliziwa kuku wako. Utamaliziwa bata wako. Utamaliziwa kondoo wako. Utamaliziwa ng’ombe wako nawe kuzama katika utapiamlo wa kiroho na kimwili kadhalika. Matokeo ya jumla yatakuwa kuishiwa pesa mfukoni na imani rohoni. Chonde, chonde, jizatiti; matatizo yako yasiwe mtaji wa ‘wapiga hela’ leo. KWA HERI TENA!
KESI YA BIBLIA KUBWA NA BIBLIA NDOGO, MUNGU MKUBWA NA MUNGU MDOGO
Vijana tunaendelea na mada zetu. Nadhani nimewapeni muda wa kutosha kutafakari mada yetu ya mwisho, yaani juu ya imani inayotudumaza ya “uchawi” au “ushirikina”. Leo nina mada ya ajabu kidogo, lakini ndiyo itakayoweza kuweka wazi sababu ya malumbano yanayojitokeza au pengine yanayoendelea kati yetu Wakristo. Kifupi, mzizi mkuu wa malumbano yetu ni kuwapo kwa Biblia kubwa na Biblia ndogo na hivyo kuwa na Mungu mkubwa na mungu mdogo. Wakristo tuna Biblia mbili na hivyo inaonekana tuna miungu miwili, Mungu mkubwa wa Biblia kubwa na mungu mdogo wa Biblia ndogo. Hiki ni kisa cha kushangaza, lakini ndivyo kilivyo, na leo nitasema ukweli ili mambo yawe bayana kwetu sote. Hiki ni kisa cha Kanisa Katoliki kuwa na Biblia kubwa na hivyo kuwa na Mungu mkubwa kuliko mungu wa makanisa mengine.
Hebu nianze na jambo lililo dhahiri zaidi. Wala hatuna mashaka, tuna Biblia mbili tofauti, Biblia kubwa (vitabu 72 au 73) na Biblia ndogo (vitabu 66). Kumbe, kwa vile makanisa mengine yana Biblia ndogo, yaani ya vitabu 66 tu, yana Mungu mdogo. Nahukumu kwa kufuata maweza yao. Yupo  mungu mdogo kwa sababu hajui na wala hawezi mengi sana. Mungu mdogo hatofautiani sana na mimi Pd. Titus Amigu. Atakuwa hajui mengi ya kesho. Atakuwa hakumbuki alichosema. Atakuwa mwongo. Ataweza kusingiziwa mengi na kadhalika. Mkasa huu unatokeaje? Unatokea kwa sababu Biblia ya vitabu 66 ni ndogo. Udogo huu ni pendekezo la mwanadamu mmoja tu. Ni hivi, udogo huo umetokana na Martin Luther, hapo mwaka 1517 kuchagua kuwafuata Wayahudi wa Palestina ambao walivikataa vitabu vya Wayahudi wenzao waliokuwa wakikaa huko Aleksandria, Misri.
Wayahudi waliokuwa wakikaa nje ya Palestina (Diaspora) walikuwa na vitabu vingi zaidi. Inaonekana jamii yao ilikuwa na waandishi wengi hodari. Jambo hilo si ajabu. Wamakonde, Wandonde, Waigbo, Wanubi, Wajerumani, Wamarekani au Wachina wanaokaa nje ya nchi yao wanaweza kuwa hodari zaidi kuliko watu waliobaki kwao. Kumbe, Wayahudi waliokuwa wakikaa nje ya Palestina, ndio Diaspora, waliandika vitabu vingi vizuri. Ndiyo kisa walipovitafsiri vitabu hivyo katika Kigiriki wakatoka na vitabu vingi zaidi kuliko wenzao waliobaki Palestina. Tafsiri hii ya Maandiko ilifanywa huko Misri chini ya ushauri wa Mfalme Philadelphus (Ptolemy II) katika miaka ya 285 -247 Kabla ya Kristo.
Kwa taarifa yako, Wakatoliki wanafuata orodha yenye vitabu 45 au 46 katika Agano la Kale na vitabu 27 katika Agano Jipya. Agano la Kale lina vitabu 45 au 46 kutokana na kusigana katika kuvihesabu vitabu viwili, kitabu cha Nabii Yeremia na kile cha Maombolezo. Baadhi ya watu huvihesabu kama vitabu viwili kutokana na kusadiki kwamba vimeandikwa na waandishi wawili tofauti wakati watu wengine husema vitabu hivyo vimeandikwa na mwandishi mmoja na hivyo ni kitabu kimoja tu. Kumbe, vitabu hivyo vikihesabiwa kama viwili, Agano la Kale linakuwa na vitabu 46 wakati vikihesabiwa kama kimoja , idadi ya vitabu vya Agano la Kale hushuka kwa kitabu kimoja na hivyo kuwa 45 tu.
Makanisa ya Kiprotestanti hufuata orodha iliyokuwa au inayofuatwa bado na Wayahudi huko Palestina, orodha yenye vitabu 24 katika Agano la Kale kutokana na kuvihesabu vitabu vyote 12 vya manabii wadogo (Hosea, Yoeli, Amosi, Obadia, Yona, Mika, Nahumu, Habakuki, Sefania, Hagai, Zekaria na Malaki) kama kitabu kimoja. Lakini, vitabu hivyo vikitenganishwa na kuhesabiwa kimoja kimoja, orodha hiyo hutanuka na idadi ya vitabu kupanda hadi 39 katika Agano la Kale.
Vitabu saba na sehemu za vitabu zinazoleta tofauti hiyo ni vitabu vya Tobiti, Yudithi, 1 na 2 Makabayo, Hekina ya Sulemani, Yoshua ben Sira, Baruku na Barua ya Yeremia pamoja na sehemu zifuatazo: Wimbo wa Vijana Watatu kwenye Tanuru (Dan 3:24-90), Simulizi la Susana (Dan 13) na Hadithi ya Bel na Joka (Dan 14).
WAYAHUDI WA DIASPORA WALIKUWA NA VITABU ZAIDI:  Tunaulizana. Kwa nini Wayahudi wa Diaspora walikuwa na vitabu zaidi? Asili ya tofauti hii ni ukweli kwamba hapo zamani kabla ya orodha ya vitabu (canon) vya Agano la Kale, yaani Biblia ya Kiyahudi haijafungwa rasmi, Wayahudi waliokuwa wakiishi uhamishoni, yaani nje ya Palestina (Diaspora), walikuwa na vitabu vingi zaidi kuliko vile walivyokuwa navyo Wayahudi wenzao waliokuwa wakiishi bado huko Palestina (Israeli au Uyahudi). Nimeshaomba jambo hili lisichukuliwe kama ajabu ya pekee sana kwani uandishi waweza kustawi popote pale hata nje ya nchi fulani. Kwa hali hii, tunaweza kusema kwamba huko nje ya Palestina walikuwepo Wayahudi waandishi wazuri wengi zaidi.
Ukweli huu unashuhudiwa na taarifa iliyotufikia kwa kumbukumbu ya Barua ya Aristes. Barua hiyo inasimulia kwamba Wayahudi wa huko Aleksandria (Misri) walipoonekana wakishindwa kusoma vitabu vyao vya dini katika lugha ya Kiebrania, mfalme Philadelphus (Ptolemy II) aliyeishi kati ya 285 na 247 K.K. aliamua kuwasaidia kuvitafsiri vitabu vyao katika lugha ya Kigiriki kilichotawala katika Diaspora.
Basi, waliitwa watafsiri kutoka Israeli sita sita kutoka kila kabila la Israeli. Hivi,  jumla yao kutoka makabila 12 ilikuwa 72 (au 70 kwa makumi ya karibu). Barua ya Aristes inasema watafsiri hao walifungiwa katika vyumba 72 tofauti kila mmoja na kutafsiri vitabu alivyopewa katika siku 72. Barua inatangaza ajabu kubwa kwamba mwishoni mwa kazi yao, tafsiri zao zilipolinganishwa, zilifanana neno kwa neno. Kumbe, hii ndiyo tafsiri maarufu ya Agano la Kale inayojulikana kwa Kilatini hadi leo hii kama Septuaginta (yaani 70 ambayo kwa Kilatini huandikwa hivi LXX).
Lakini ajabu kubwa zaidi ilikuwa kwamba, kiidadi, vilipolinganishwa vitabu vya Agano la Kale la Septuaginta, ilizidi vile vilivyokuwa vikisomwa huko Palestina (Israeli au Uyahudi) kwa vitabu saba na sehemu za vitabu nilizotaja hapo juu.
JE, WAKRISTO WA MWANZO WALIPOKEA TAFSIRI YA SEPTUAGINTA? Ndiyo, tena ndiyo kubwa, kwani tangu enzi hizo, ndiyo karne ya kwanza na ya pili, Agano la Kale la tafsiri ya Septuaginta ndilo lililopokelewa na Kanisa la Kristo. Hiyo ndiyo tafsiri iliyopokelewa na kutumika sana na mababa wa Kanisa, kama vile, Tertuliani,  Ambrose, Augustino wa Hippo na kadhalika hasa kwa vile walikuwa weledi wa Kigiriki na hawakujua Kiebrania cha kutosha.
Zaidi ya hayo, tafsiri ya Septuaginta ambayo ilikuwa katika Kigiriki ilioana vyema na vitabu vya Agano Jipya (27) ambavyo tangu mwanzo viliandikwa katika Kigiriki cha kawaida (ndiyo koine, yaani Kigiriki cha kawaida) wakati vitabu vya Wayahudi huko Palestina vilikuwa bado vikitumiwa katika Kiebrania, tena Kiebrania cha zamani.
Basi, Agano la Kale la tafsiri ya Septuaginta likapata kuwa sehemu ya Biblia ya Kanisa la Mungu hata ikatafsiriwa pamoja na Agano Jipya katika Kilatini cha kawaida (ndiyo Vulgata) na akina Mt. Jerome, msimamizi wa taaluma ya Biblia.
Kumbe, ndiyo Biblia (LXX na Agano Jipya) hii iliyotumika na Kanisa na Wakristo wa Magharibi (kwani Wakristo wa Mashariki, ndio Waorthodoksi wana orodha ya vitabu vya Biblia kubwa zaidi, yaani vitabu zaidi ya 73) hadi karne ya 16. Septuaginta ilikuwa na vitabu 45 au 46 kujumlisha vitabu 27 vya Agano Jipya na hivyo kufanya Biblia ya Kanisa la Mungu kuwa na jumla ya vitabu 72 au 73.
Lakini, ajabu ya kupinduka chali ikatokea katika karne ya 16. Ni katika karne hii, Martin Luther aliposababisha mtengano wa Kanisa naye kuifumua Biblia kwa kuviondoa vitabu vile saba na sehemu za vitabu nilizowatajia, yaani, Tobiti, Yudithi, 1 na 2 Makabayo, Hekima ya Sulemani, Yoshua bin Sira, Baruku na Barua ya Yeremia pamoja na Wimbo wa Vijana Watatu kwenye Tanuru (Dan 3:24-90), Simulizi la Susana (Dan 13) na Hadithi ya Bel na Joka (Dan 14).
Ndiyo kusema basi, tangu wakati wa Martin Luther, Wakristo wote wanaojitenga na Kanisa Katoliki huamua kumsikiliza Martin Luther na hivyo kuiacha orodha ya Septuaginta (yaani Biblia ya Wayahudi wa uhamishoni) na kuifuata ile ya Palestina, yaani ile yenye vitabu pungufu kwa saba na ushehi. Ndiyo kisa basi, hadi leo hii, makanisa yote ya Kiprotestani na madhehebu yake mapya yanayozaliwa kila kukicha, hufuata orodha yenye vitabu vichache wakati Kanisa Katoliki likiendelea na orodha ile asilia kwa Wakristo yaani Septuaginta.
Hivi, kuhusu idadi ya vitabu kwenye Biblia, asikudanganye mtu yeyote yule, iwe amekujia na “suitcase” au na mkoba wa ngozi ya mbuzi. Si kwamba WAKATOLIKI WAMEONGEZA VITABU kwenye Biblia isipokuwa ni kinyume chake kwani ukweli ni kwamba Martin Luther AMEVIPUNGUZA VITABU kwenye Biblia.
Usinikodolee macho! Unashangaa nini? Hii ni hesabu ya kawaida, hata chekechea haiwashindi kuilewa. Kama ukianza na namba 72 au 73 ukashuka hadi 66 maana yake umetoa au umepunguza. Ingekuwa kwamba mtu ameanza na namba 66 na kupanda nayo hadi 72 au 73 ingekuwa kweli ameongeza. Kumbe, haikuwa hivyo, katika historia ya orodha rasmi ya vitabu vya Biblia, yaani canon.
Nadhani tumeelewana kabisa. Haya tuendelee. Hoja ya kufuata orodha ya vitabu vichache ni kwamba makanisa yaliyojitenga, kwa kadiri ya mawazo ya Martin Luther, huona kwamba vitabu vile vya ziada na sehemu zile za nyongeza havikuvuviwa, yaani havikuangaziwa na Roho Mtakatifu katika uandishi wake. Ndipo, basi, Wakristo wote wanaomsadiki, kumsikiliza na kumfuata Martin Luther, huita vitabu hivyo na sehemu za Maandiko nilizozitaja kwa msamiati wa Kigiriki ‘apokrifa’.
Kumbe, Kanisa Katoliki, kwa upande wake, linavitambua bado vitabu hivyo pamoja na sehemu zile za nyongeza kwamba vimevuviwa na kwamba vinastahili kuitwa orodha ya nyongeza, ama kwa maneno mengine, ORODHA YA PILI ya vitabu vitakatifu, maana vimetoka kwa Wayahudi wenyewe tena wakati ule ule waandishi wengine wa kimungu walipokuwa wakiyaandika Maandiko Matakatifu katika nchi ya Palestina (Israeli au Uyahudi). Ndipo basi, Kanisa katoliki huviita vitabu hivyo na sehemu nilizokutajia kwa jina lililotoholewa kutoka Kigiriki, ‘DEUTEROKANONI’, yaani ‘ORODHA YA PILI’.
MASWALI MADOGO MAWILI:
Swali 1. Pd Martin Luther alitoa hoja kuwa havikuvuviwa na Roho Mtakatifu. Lakini Kanisa Katoliki linatambua vilivuviwa na Roho Mtatikatifu kwa kuwa vilitoka kwa Wayahudi walewale japo walikuwa uhamishoni.
Je, wakati wa kukusanya vitabu vya Biblia Wayahudi waliwakataa Wayahudi wenzao waliokuwa uhamishoni walipokuja na mafundisho ya Biblia ile ile??

Jibu: Ndiyo, Wayahudi waliwakataa Wayahudi wenzao. Kiujumla, Wayahudi wa Palestina walivikataa vitabu tulivyovitaja pamoja na sehemu za vitabu ya Esta na Danieli. Walivikataa hasa kwa sababu Wakristo walikuwa wanavitumia tayari katika kufafanulia mafundisho yao. Ndiyo kisa, kuvikataa huku kulifanyika huko Jamnia mwaka 95 Baada ya Kristo. Kabla yake, vitabu hivyo vilikuwa vinatumika kwa kujulikana kabisa, kwa mfano kitabu cha Yoshua ben Sira kilikuwa kikitumika na Wayahudi wote kama kitabu cha kiada katika kuwafundisha vijana maadili.
     
Swali 2. Je, Kanisa Katoliki limezingatia hoja zipi za msingi  zinazosahihisha hoja alizotumia Pd. Martin Luther katika kuvipunguza vitabu hivyo ukiachana na hiyo ya kuvuviwa na Roho Mtakatifu alikosema.

Jibu: Hoja ya kwanza - kukataa kwa Martin Luther kunabainisha kwamba hakujua Maandiko Matakatifu maana nukuu za vitabu alivyovikataa zipo kwa namna moja au nyingine katika nukuu za waandishi wa vitabu vya Agano Jipya, kwa mfano, Waraka kwa Waebrania na nyaraka kwa watu wote zaYakobo na Petro. Hii inamaanisha alikataa kitu ambacho kipo kwenye Biblia tayari. Ilikuwa kama mtu kukataa nyama iliyokaa juu ya wali wakati mchuzi wake umeshachanganywa na wali huo huo unaokula.
Hoja ya pili: Mafundisho ya vitabu alivyovikataa yalikuwa yanajulikana na jumuiya za Kikristo, yalikuwa hayapingani na mafundisho yaliyokuwa kwenye vitabu alivyovikubali, yalikuwa mafundisho yanayoweza kuhimiza imani na upendo na kadhalika, mambo ambayo kwa yenyewe yalikuwa vigezo (criteria) vya kuteulia vitabu vilivyoingia katika orodha ya vitabu vya Agano Jipya vilivyoandikwa na Wakristo wenyewe.

Huenda nimekuporomoshea mambo mapya mno na huenda, kichwani na moyoni mwako, unadhani nimesahau hoja ninayoijenga. La hasha! Nimekutaarifu kwamba Biblia ya Wakristo ilipunguzwa kutoka vitabu vya asilia 72 au 73 hadi vitabu 66. Kwa mkasa huo, Biblia ilifanywa NDOGO na kwa kufanywa huko ndogo Mungu akakumbwa na balaa la kupunguzwa kutoka Mungu mkubwa hadi kuwa MUNGU mdogo. Kwa nini? Kwa sababu mambo anayoshuhudiwa katika vitabu vile 7 na sehemu zilizokanwa na Martin Luther yatakanwa kwake. Sasa hivi nitakupa mifano kusudi usipupe pupe kana kwamba nimekunasisha kwenye mtego wa kware. Katika mada zote nakusudia kukuelimisha vyema.
MIFANO YA KUPUNGUZA VITABU SABA KULIVYOATHIRI MAFUNDISHO YA KIKRISTO
1. KWA KUKATAA KITABU CHA TOBITI, lazima mtu ukatae fundisho la watakatifu na malaika kuwa na uwezo wa kuwaombea wanadamu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na Tobiti 12:11-21. Hapa pameandikwa hivi:
“‘Sasa nitawajulisheni ukweli wote bila kuwaficheni chochote. Nilikwishawaambia kwamba yafaa kuitunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tobiti! Wewe ma Sara mlipokuwa mnasali wakati ule, mimi ndiye niliwasilisha sala zenu mbele ya Bwana aliye mtukufu. Na kila ulipokuwa unawazika wafu, mimi niliwasilisha matendo yako mbele yake. Wakati wewe hukusita hata kidogo kuinuka na kukiacha chakula ukaenda kumzika mtu aliyekufa, Mungu alinituma nikujaribu. Lakini pia alinituma kukuponya na kumwokoa mke wa mwanao, Sara. Mimi ni Rafaeli, mmoja wa wale malaika saba wanaokaa tayari daima mbele yake Bwana aliye mtukufu kumtumikia’.
“Tobiti na Tobia wakashikwa na hofu kubwa, wakasujudu wakiogopa sana. Lakini Rafaeli akawaambia: ‘Msiogope! Muwe na amani. Mtukuzeni Mungu milele. Mimi nilipokuwa kati yenu haikuwa kwa kutaka kwangu mwenyewe, bali kwa kutaka kwake Mungu. Yeye ndiye mnayepaswa kumsifu. Ninyi mlidhani mliniona nikila chakula, lakini ni kwa kuonekana tu na haikuwa hivyo. Basi, sasa mtukuzeni Bwana duniani na kumshukuru. Mimi narudi sasa kwake yeye aliyenituma kutoka juu. Andikeni mambo hayo yote yaliyokukia.’ Kisha Rafaeli akatoweka, wasimwone tena. Basi, wakamsifu Mungu kwa nyimbo, wakamshukuru kwa ajili ya matendo yake makuu aliyowafanyia malaika wake Mungu alipokuwa amewatokea.”
Kumbe, kama huna kitabu hiki katika Biblia yako lazima ushindwe kujua na kukubali kweli mbili: mosi, kwamba malaika na watakatifu wanawasilisha sala mbele ya Mungu nao wanaripoti juu ya matendo  yetu mema. Kumbe, ni kwa sababu ya ukweli huu, Wakatoliki hawasiti kuwaomba malaika na watakatifu mbalimbali wawaombee kwa Mungu. Hapo ndipo zinapoingia sala na ibada mbalimbali kwa Bikira Maria AWAOMBEE wanadamu wote, wema kwa wakosefu, wazima kwa wafu. Ukweli huu unaungwa mkono kwa kiashirio kizuri kilicho katika maombezi ya Maria kwa Yesu ili waliokuwa wanaishiwa divai wasaidiwe (soma Yn 2:1-12).
Pili, kwamba Bikira Maria, malaika na watakatifu hawaabudiwi isipokuwa kupitia kazi zao na maombezi yao Mungu anatukuzwa. Hakika ukisoma vizuri Tobiti 12:11-21, utajua kwamba Bikira Maria, malaika na watakatifu hawaombwi kwa wenyewe bali wanaombwa wasimame kama waombezi wa wanadamu “wanaolimbana” na malimwengu haya yanayowachachafya.
Lakini kutokana na mtu kukataa jambo mahali fulani, hulazimika akatae popote na chochote kitakachoelekea kupindua msimamo wake. Kumbe, kanusho moja huzaa kanusho lingine hata kama ni kwa kulazimisha tu. Ndiyo kisa basi, mtu anaposhuhudia mambo ya watakatifu kuwa na uwezo wa kuombea kwa kunukuu Ufu 5:8, 8:3-4, huwa kama anayechota maji kwa pakacha tu.
2. KWA KUKATAA KITABU CHA HEKIMA YA SULEMANI, lazima ukatae fundisho la Hekima (Roho Mtakatifu au Yesu Kristo) kuwa Nafsi ya Mungu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na Hekima ya Sulemani 9: 6.9-12. Hapa pameandikwa hivi:
“Hata kama mtu yeyote akiwa mkamilifu kiasi gani, bila Hekima atokaye kwako atakuwa bure tu. Hekima yupo pamoja nawe, naye ajua matendo yako, alikuwa pamoja nawe wakati ulipouumba ulimwengu. Hekima anajua yanayokupendeza na yaliyo sawa kulingana na amri zako. Umpeleke, basi kutoka mbingu tukufu, kutoka kiti chako cha enzi kitukufu, ili akae nami na kufanya kazi pamoja nami, nipate kujifunza yale yanayokupendeza, maana Hekima anajua na anaelewa mambo yote, naye ataniongoza kwa busara katika matendo yangu, kwa utukufu wake atanilinda, hapo matendo yangu yatakubalika, nitawahukumu watu wako kwa haki na kustahili kuwa katika kiti cha enzi cha baba yangu.”
Basi, kama huna kitabu hiki katika Biblia yako lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli kwamba katika Mungu kuna Nafsi, Mwana na Roho Mtakatifu. Kama hutakaidi kabisa basi utasema Yesu alikuwa ni mwanadamu mwema tu na Roho Mtakatifu nguvu za Mungu kutendea kazi tu. Huko ndiko kutakuwa kuzikana Nafsi mbili za Mungu kati ya tatu tunazopaswa Wakristo kuzikiri.
3. KWA KUKATAA KITABU 2 MAKABAYO, lazima ukatae uhalali wa kuwaombea marehemu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na 2Mak 12:38-45. Hapa pameandikwa hivi:
“Kisha Yuda aliwaongoza watu wake kwenda mjini Adulamu. Hiyo ilikuwa siku kabla ya Sabato, kwa hiyo wakajitakasa kadiri ya desturi ya Kiyahudi, kisa wakaadhimisha Sabato hapo. Siku iliyofuata waliona ni harakia na muhimu kukusanya miili ya wenzao waliokuwa wameuawa vitani, na kuizika katika makaburi ya wazee wao. Lakini katika kila maiti, walikuta zimefichwa nguoni sanamu ndogondogo za miungu iliyoabudiwa Yamnia, jambo ambalo sheria inawakataza Wayahudi kuzivaa. Hapo kila mtu alijua kwa nini hao walikuwa wameuawa.
“Hivyo, wakazisifu njia za Bwana, hakimu mwenye haki, afichuaye vilivyofichika na wakamwomba Bwana awafutilie mbali dhambi hiyo. Kisha Yuda yule mtu mwadilifu, akawataka watu waepuke dhambi, kwa sababu walikuwa wamejionea wenyewe yaliyokuwa yamewapata wale waliokuwa wametenda dhambi. Pia alichangisha kutoka kwa watu wake fedha ipatayo drakma elfu mbili akapeleka Yerusalemu kwa ajili ya dhabihu ya kuondolea dhambi. Yuda alifanya tendo hilo jema kwa sababu aliamini juu ya ufufuo wa wafu. Kama asingekuwa na imani kwamba wafu watafufuliwa, ingekuwa ni upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. Lakinii akiwa anatazamia tuzo nzuri waliowekewa waliokufa wakiwa waaminifu kwa Mungu hilo lilikuwa wazo jema na takatifu. Kwa hiyo, Yuda alitolea dhabihu ya upatanisho ili wapate kuondolewa dhambi zao”.
Kama huna kitabu hiki katika Biblia yako lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli huu. Wakatoliki huwa tunawaombea marehemu si kwa sababu tunampelekea Mungu maombi mapya la hasha, ila kwa sababu sala zetu zilishajulikana na Mungu kabla mtu yule hajafa, wakati mtu anakufa na baada ya mtu yule kufa. Mungu anayejua yaliyopita, yaliyopo na yajayo ndiye Mungu mwenyezi. Mungu asiyejua hivyo si mwenyezi, huyo ni sawa na Pd. Titus Amigu tu.
4. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA, lazima ukatae mafundisho ya ulazima wa imani kuwekwa katika matendo kwa maana jambo hilo limekaziwa na kitabu kizima. Kitabu hiki kilichokuwa kikitumiwa kama kitabu cha kiada mwanadamu anahimizwa aishi vyema maana ndilo deni kwa akili na utashi alivyopewa kwa kutofautishwa na wanyama wafugwao na hayawani wanaoishi kwa silika tu. Yoshua ben Sira inazungumzia uzuri wa kuishi kiadilifu katika kila uwanja, malezi, kazi, urafiki, heshima, ndoa na kadhalika. Kumbe, kwa kukikataa kitabu cha Yoshua ben Sira sawa na Hekima ya Sulemani, lazima mtu akane umuhimu wa matendo katika kumtafuta Mungu naye ajikite zaidi kwenye misimamo ya “kwa neema tu” na “kwa imani tu” maana huna mafundisho mazuri juu ya matendo yaliyotukuka. Kumbe, hapo ndipo alipolazimika Martin Luther kuishia.
5. KWA KUTAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima ukatae mafundisho ya uhalali wa kunywa divai kwa wakati wake na kiasi chake kwa maana jambo hilo limeandikwa katika YbS 31:25-31. Hapa pameandikwa hivi:
“Usijioneshe kwuwa hodari wa kunywa mvinyo, maana mvinyo umewaangamiza wengi.  Tanuru hupima ugumu wa chuma na mvinyo hupima mioyo ya watu katika shindano la wenye kiburi. Mvinyo ni kama uhai kwa mtu ukinywa kwa kiasi. Maisha yafaa nini bila mvinyo? Imeumbwa iwafurahishe wanadamu. Kunywa mvinyo wakati wake na kwa kiasi, kwaleta shangwe moyoni na furaha rohoni. Lakini kunywa mvinyo kupita kiasi kunaleta kuumwa kichwa, uchungu na fedheha. Ulevi huongeza hasira ya mpuumbavu akajiumiza mwenyewe. Humdhoofisha na kumwongezea majeraha. Usimkaripie jirani yako kwenye mvinyo, wala usimdharau anapoifurahia karamu. Usimwambie neno la kumwonya wala umsimsumbue kwa kumtaka alipe deni”.
Kumbe, kama huna kitabu hiki katika Biblia yako, lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli wa kwamba divai si haramu ikinywewa kwa wakati wake na kwa kiasi. Lakini, huu ndio ukweli uliomruhusu Yesu awe anakula na kunywa anapoalikwa na vile vile uliomruhusu awape watu waliokuwa kwenye sherehe ya harusi ya Kana divai (“oinos” siyo “gleukos”) ya kutosha.
6. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima ukatae fundisho la sakramenti ya Kitubio au Upatanisho kwa maana fundisho hilo limedokezwa katika YbS 5:4-7. Hapa pameandikwa hivi:
“Usiseme, ‘Nimetenda dhambi lakini nimepata balaa gani?’ Usitegemee kupata msamaha hata kuongeza dhambi juu ya dhambi. Usiseme, ‘Huruma yake ni kubwa, yaye atanisamehe dhambi zangu nyingi’. Kumbuka, yeye ana huruma na ghadhabu na hasira yake huwakumba wenye dhambi. Usichelewe kumrudia Bwana wala usighairishe kurudi siku hata siku. Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla na wakati wa hukumu utaaangamia.”
Hali kadhalika, KWA KUKATAA KITABU CHA BARUKU, lazima ukatae pia fundisho la sakramenti ya Kitubio au Upatanisho kwa maana fundisho hilo limedokezwa vile vile katika Baruku 4:27-30. Hapa pameandikwa hivi:
“Jipeni moyo wanangu na kumlilia Mungu kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni. Kama vile mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu mara kumi zaidi. Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa hizi atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele. Jipe moyo, ee Yerusalemu, Mungu aliyekuita kwa jina lako atakufariji.”
Kumbe, kama huna kitabu cha Baruku katika Biblia yako, lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli huu kwamba Mungu alikusudia kuwaasisia wanadamu sakramenti ya Upatanisho au Kitubio. Sakramenti hii ndiyo sakramenti inaiyotendea haki sadaka ya msalaba aliyoitolea Yesu kwa ufanisi mkubwa.
7. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima mtu ubaki katika utumwa wa kuamini ndoto hata baada ya Yesu kuufikisha ufunuo kileleni (Mk 9:7-8, Ebr 1:1-4). Lakini neno la Mungu lasema ndoto zote ni upuuzi, isipokuwa zile zitokazo kwa Mungu tu (yaani zinazotokea mara kadhaa, kuwa na ujumbe maalumu na ujumbe wake kutopingana na mafundisho ya Kanisa). Jambo hili limeandikwa katika YbS 34:1-8.
Hapa pameandikwa hivi: “Mtu mjinga huwa na matumaini ya bure na ya uongo. Ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka. Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo ndivyo alivyo mtu anayeamini ndoto. Ndoto ni kama kioo, sura inayoukabili uso. Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na uchafu? Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo? Kupiga bao, ramli na ndoto ni upuuzi, akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua. Usizitie maanani ndoto isipokuwa kama zinatoka kwa Mungu Mkuu. Maana ndoto zimewadanganya wengi na wale wanaozitumaini wameaibishwa. Sheria ni kamili bila udanganyifu huo, nayo hekima ni kamilifu kwa mtu mwaminifu.”
Kumbe kwa kutumia Biblia ndogo, kwa maana ya kwamba isiyo na kitabu cha Yoshua ben Sira mwanadamu utaendelea na kusumbuka kutafuta maana ya kila ndoto. Zaidi ya hayo, utanunua vitabu vyote vinavyodaiwa kutafsiri ndoto za watu na hali kadhalika kuhangaika kuwaendea “wafasiri wa ndoto” wote ijapokuwa wenyewe ni waongo wasiojua jambo lolote la ajabu.
8. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima mtu ukatae uhalali wa dawa za asili hata kama zinatumiwa kwa uadilifu kwa maana jambo hilo limeandikwa katika YbS 38:1-14. Hapa pameandikwa hivi:
“Mpe daktari heshima anayostahili, kwa sababu ya huduma zake kwako, kwa vile naye aliumbwa na Bwana. Maana kipaji chake cha kuponya chatoka kwa Mungu Mkuu naye hupata zawadi kutoka kwa mfalme. Ujuzi wa dakrari humfanya maarufu, naye huheshimiwa miongoni mwa wakuu. Bwana  aliumba dawa zote kutoka ardhini na mtu mwenye nusara hawezi kuzidharau. Je, si kwa kijiti maji yaligeuzwa kuwa mazuri ili Mungu awaoneshs watu nguvu zake? Bwana aliwapa watu maarifa na ujuzi ili atukuzwe katika kazi zake za ajabu. Kwa dawa huwapaonya watu na kuondoa maumivu, mchanganya dawa hutengeneza mchanyiko wake. Kazi za Bwana hazina mwisho, afya yote duniani hutoka kwake.
“Mwanangu, ukiugua usiwe mzembe juu ya ugonjwa, bali mwombe Bwana naye atakuponya. Acha makosa yako, uamue kutenda mema, na kutakasa moyo wako dhambi zote. Mtolee Bwana dhabihu ya harufu nzuri na dhabihu ya unga safi. Umiminie dhabihu zako mafuta  kadiri unavyoweza kupata. Kisha mengine mwachie daktari maana Bwana ndiye aliyemuumba; usikubali akuache maana unamhitaji.  Kuna wakati ambapo kupona kuwategemea madaktari. Maana nao pia wanamwomba Bwana ili awape mafanikio katika uchunguzi wao na katika kuponya ili kuokoa maisha. Mtu aliyetenda dhambi dhidi ya  Muumba  wake mwache aangukie mikononi mwa daktari.”
Kumbe, usipokuwa na Biblia yenye nukuu hii, utakuwa “unapinduka pinduka tikitaka” nyingi za kiakili kutaka kuhakikisha kwamba dawa za asili, kwa zenyewe, ni haramu.
Nakomea hapa. Nadhani nimekujengea vyema hoja na kukutolea mifano mizuri kwamba makanisa mengine yana mungu mdogo kwa sababu ya kutumia Biblia ndogo. Kitendo cha kupunguza vitabu vya Biblia kutoka 72 au 73 hadi 66 kimetupa nje mafundisho mazuri ya Kanisa na kubana uelewa wa mafundisho yanayodumishwa na Kanisa Katoliki. Matokeo yake ya jumla ni kuzaliwa kwa mabishano endelevu kwa sababu ya kutofautiana vitabu vya rejea.
Na hili ni jambo la kawaida kama watu wanajadiliana jambo, tuseme la Fizikia, hawawezi kuelewana ikiwa mmoja anatumia muhtasari wa darasa la saba (yaani muhtasari mdogo) wakati mwingine anatumia kitabu cha Sekondari kwa mfano kitabu cha A.F.ABBOT. Kumbe, mtu anayehama kutoka Kanisa Katoliki, Kanisa lenye Biblia kubwa na hivyo lenye Mungu mkubwa na kuhamia kanisa lenye Biblia ndogo na hivyo kujihusisha na mungu mdogo lazima ajiunge katika taabu ya kwanza kujielewesha na kishapo kuyatetea mafundisho madogo. Naomba mnipate uzuri. Kwa heri kwa leo pia!

Pd. Titus Amigu

Jumanne, 11 Julai 2017

HISTORIA HALISI YA WASABATO: AIBU TUPU
Ndugu zanguni nitaendelea na mada yetu ya “viboko hamsa wa ishirini” lakini naomba nikatishe kidogo nipate kujibu swali moja linalojirudia rudia sana. Swali lenyewe naulizwa kwa namna nyingi mno. Mtu wa mwisho ameniuliza akisema hivi: “ Asante sana baba gombera mstaafu, hivi huyu Bi Ellen G. White ni nani katika Kanisa Katoliki? Mbona amekuwa akishambulia sana Kanisa Katoliki au kuna makanisa mengine huanzishwa na misingi yao ni lazima kushambulia Kanisa Katoliki?
Jibu fupi: Bi Ellen G. White ni mmojawapo wa waanzilishi wa kanisa la Wasabato lakini fundi sana wa kulitukana Kanisa Katoliki. Yeye hakuwamo ndani ya Kanisa Katoliki na wala hakujihusisha nalo kwa nia njema isipokuwa aliondokea kuongoza kulitukana.
Wala si siri yapo makanisa ambayo huanzishwa na misingi yao ni lazima kulishambulia Kanisa Katoliki kwa sababu zao mbalimbali. Kanisa mojawapo kati ya hayo ndilo kanisa aliloshiriki Bi. Ellen White kulianzisha yaani kanisa la Sabato. Inasikitisha sana na kukera sana, lakini tutafanyaje. Ndiyo hivyo tena, kisera, kanisa la Sabato limepania kulibomoa Kanisa Katoliki. Sisi hatuwezi kuwachukulia hatua ya kiuhalifu isipokuwa kufahamishana kama ninavyokusudia kufanya ili tukae chonjo nalo tu. Kumbe kwa busara ya maisha, anayekuwinda walau mjue tu kusudi ujue namna ya kumkwepa. Wala si lazima upigane naye.
Sasa kusudi vijana mmwelewe vizuri mtu huyo aheri nikupeni historia nzima ya kuanzishwa kwa kanisa la Wasabato. Katika historia hiyo mtaona aibu ya kushindwa utabiri wa mwisho wa dunia. Cha kushangaza waliposhindwa kutabiri mwisho wa dunia kama walivyojinasibu kuweza, wakageukia kulitukana Kanisa Katoliki ambalo halina kosa lolote na halikuwafanya chochote.
Hivi acheni niitumie fursa ya kujibu swali hili kwa kuwaleteen historia halisi ya Kanisa la Wasabato. Nawaanikieni hadharani aibu yao, aibu inayowatia hasira na hasira yenyewe kuilekeza kwa Kanisa Katoliki ambalo halijawakosea.
Jibu hili nimewahi kuliandika kwenye Gazeti la Kiongozi na vile vile kulirusha hewani kwa njia ya radio. Lakini kwa kuwa bado naendelea kuulizwa, kwa mitindo mbalimbali, kila uchao napenda nilijibu tena sasa kwa kupitia ukurasa wangu wa Facebook. Sina nia ya kuleta uchochezi. Najibu swali kwa kadiri inavyostahili tu.
Jibu refu: Wakatoliki tunatukanwa kwa sababu Wasabato wanajaribu kufunika aibu yao ya kihistoria na wanadhani matusi ndiyo njia ya kuliua Kanisa Katoliki. Hawajui kwamba matusi hayawezi kumharibu mtu isipokuwa kumfedhesha mtukanaji tu. Waungwana hawatukani. Kumbe, aheri tuielewe historia ya dhehebu la Wasabato au S.D.A tupate kuwapuuza wanaotutukana huku wakijiabisha wenyewe. Basi, historia hiyo ya aibu inayofichwa ndiyo hii ifuatayo:
Ni hivi ndugu zanguni, kwa kuiweka bayana historia ya Wasabato, tuambatane katika kuwaelewa watu wanne ambao hutajwa kama watangulizi au waasisi wa dhehebu la Wasabato. Mwishoni nitayapembua waliyofundisha kibiblia na kisaikolojia.
Mtu wa kwanza ni William Miller, wa pili ni Hiram Edson, wa tatu ni Joseph Bates na wa nne na wa mwisho awe Bi Ellen G. White.
Tukianza na Bw. William Miller, yeye alizaliwa mwaka wa 1782 katika mji wa Pittsfield, Massachusetts, huko Marekani.  Ingawa alizaliwa katika familia ya Kikristo, aliuacha Ukristo alipokuwa kijana mbichi.  Kwa kweli hakuiamini Biblia kuwa neno la Mungu.  Basi, akajiunga na jeshi. Baada ya kutumika kama mwanajeshi kwa muda mfupi, akaishi kama mkulima.  Kumbe, mwaka wa 1816, akaongoka na kuurudia Ukristo wake kwa kasi mpya.  Kwa kweli, tangu mwaka huo wa kuongoka kwake, Bw. William Miller alisoma unabii kwa kina na hasa unabii uliohusu kurudi kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. 
Kumbe, kutokana na kujifunza huko, Bw. William Miller akashawishiwa kwamba mwisho wa dunia ungetimia mwaka 1843.  Kifupi, Bw. William Miller alishawishiwa kufundisha jinsi hiyo na unabii wa kitabu cha Danieli 9:24-27, unabii unaohusu majuma sabini yaliyowekwa kwa ajili ya watu wa Mungu, taifa la Israeli.
Zaidi ya hayo, katika Danieli 8:13-14, kuna unabii wa watakatifu wawili wanaoulizana lini patakatifu patatakaswa.  Mintarafu unabii huo, Bw. William Miller alitafsiri kwamba patakatifu patakapotakaswa, ni dunia hii iliyochafuliwa na dhambi za kila sampuli.  Kwa maoni yake, mwaka wa 1843 B.K., ndio mwaka ambao Yesu Kristo angerudi katika dunia iliyonajisiwa kupita kiasi na dhambi na hivyo kuitakasa kabisa kwa kuwapo kwake. 
Msimamo huu ulimfanya awe maarufu sana katika sehemu nyingi za Marekani, na hatimaye akawa mhubiri mkubwa wa dhehebu la Kibaptisti.  Kwa kuwa mwisho wa dunia ulikuwa unaambatana na kurudi kwa Yesu Kristo, ambako kwa Kiingereza huitwa “Christ’s Advent”, wafuasi wake walianza kujulikana kama “Adventists” au kwa Kiswahili “Waadventisti”, yaani “Watu watarajiao kurudi kwa Kristo”. Ijapokuwa mwanzoni hakutaja tarehe bayana ya kurudi kwa Yesu, punde si punde alisema kurudi kwa Yesu kungekuwa kati ya tarehe 21 Machi, 1843 na 21 Machi, 1844. 
Baada ya mambo kufikia hapo, mfuasi mmoja wa Bw. William Miller aliyeitwa Samwel Snow, akawa jasiri zaidi na kutaja kwamba Kristo angerudi tarehe 22 Oktoba, 1844 saa 6.00 usiku; yaani ndipo parapanda litakapopulizwa, mbingu kukunjwa kama kurasa, na Yesu Kristo kufika  kwa utukufu mwingi.  Lakini mambo hayakutukia hivyo walivyohubiri. Basi, kwa vile Kristo hakurudi kama walivyotarajia, Bw. Miller akakiri kukosea kwake, lakini akawaonya wafuasi wake wasisahau kwamba Kristo atarudi upesi. 
Kwa bahati mbaya, Bw. William Miller alifariki mnamo mwaka 1849 ndoto yake ya kumwona Yesu akirudi upesi ikiwa bado haijatimia.  Hadi hapo, ieleweke kwamba Bw. William Miller, hakuwahi kuwa Msabato.  Hivyo kama Mbaptisti, alikuwa anasali siku ya Bwana, yaani Jumapili au Dominika. Kutokana na kutokutumia kwa utabiri wa Bw. William Miller wafuasi wake wengi wakarejea nyuma.
Basi, tumwachie Bw. William Miller hapo, nasi tusonge mbele tukamwangalie mtu wa pili, yanii Bw. Hiram Edson.  Kwa bahati, bwana huyu alikuwa kati ya Waadventisti wachache waliobaki baada ya kuvunjika moyo kwa wafuasi wengine wa William Miller kutokana na kutorudi kwa Kristo kama ilivyotazamiwa.  Kwa upande wake  kwa kusudi la kuwafariji wenzake kwenye huzuni yao, yeye alidai kwamba Mungu alikuwa ametoa jibu kwa aibu yao kwani alipata mafunuo juu ya kile kilichofanyika siku hiyo ya tarehe 22 Oktoba, 1844. 
Kwa jinsi gani? Sikiliza. Alifundisha kwamba alioneshwa kulikuwa na hekalu mbinguni mfano wa hekalu la duniani. Akadai hekalu hilo lilikuwa na sehemu mbili: patakatifu na patakatifu pa patakatifu, yaani sawa na lilivyokuwa hekalu la Kiyahudi zamani zile.  Kumbe, kilichofanyika siku hiyo ya tarehe 22 Oktoba,  ni kwamba Kristo alitoka patakatifu na kuingia patakatifu pa patakatifu.  Akasema kwisha Yesu kuingia patakatifu pa patakatifu atabaki humo mpaka siku atakapokuja duniani mara ya pili. 
Mintarafu swali, Yesu anafanya nini siku zote hizo? Akasema Yesu anafanya ‘hukumu ya upelelezi’ kwa Kiingereza “investigative judgement”.  Kwa maelezo hayo mapya akadai kwamba kitu alichokuwa amekosea Bw. William Miller kilikuwa tafsiri tu, kwa maana kwamba utakaso uliofanywa tangu siku ile ya tarehe 22 Oktoba haukuwa wa dunia hii, bali wa patakatifu pa patakatifu katika hekalu hilo la mbinguni.
Kwa namna hii, Bw. Hiram Edson akawa Mwadventista wa kwanza, hata kabla hajawa Msabato, kuleta duniani maelezo ya kuwafariji wenzake kwa kutorudi kwa Kristo siku ya tarehe 22 Oktoba 1844.  Hivi basi, mchango wake mkubwa kwa teolojia ya Wakristo ambao baadaye walijiita Wasabato ni suala  hilo la ‘hukumu ya upelelezi’.  Kifupi, kwa maelezo hayo, Wasabato wanafundisha kwamba Yesu Kristo, tangu 22, Oktoba 1844 yuko huko mbinguni, katika patakatifu pa patakatifu akichunguza kwa kina maisha ya Wakristo wote ambao majina yao yapo katika kitabu cha uzima wa milele na kuamua nani anastahili kufutiwa dhambi zake zilizosamehewa wakati alipoamini.  Hivyo, kila mtu anayeonekana kurudi nyuma, naye hakutubu dhambi zake zote, anafutwa jina lake kutoka katika kitabu cha uzima na hivyo huko, mwishoni mwa historia, atakosa nafasi katika ufufuo wa kwanza.  Kinyume chake, kwa upande wao, wote ambao walitubu dhambi zao, majina yao yanabaki kitabuni pasipo kufutwa, nao watafufuliwa katika ufufuo wa kwanza.
Ndugu zangu, hadi hapa umeshagundua mafundisho ya uongo. Mbinguni hakuna hekalu. Huo ndio ukweli wa kibiblia maana mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anatuandikia habari za maono yake matakatifu mintarafu Yerusalemu ya mbinguni akisema “Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana  Mungu Mwenyezi na Mwanakondoo, ndio hekalu lake” (Ufu 21:22). Sasa iweje Bw. Hiram Edson amzungumzie Yesu anayetoka patakatifu kuingia patakatifu pa patakatifu? Zaidi ya hayo, mafundisho ya hukumu ya upelelezi ni uzushi kwa sababu ni matokeo dhahiri ya tafsiri potofu ya neno la Mungu. 
Haya tuachane naye, nasi twende tukamwangalie mtu wa tatu, ambaye ni Bw. Joseph Bates.  Kikazi, Bw. Joseph Bates alikuwa baharia.  Bada ya kustaafu kwake alihamia Fair Haven, katika jimboni Massachusetts, huko huko Marekani.  Kwa kweli, Bw. Joseph Bates ni mmoja wa viongozi maarufu  wa Waadventisti.  Yeye aliposoma maandishi ya Thomas Prebble kuhusu Sabato, alishawishiwa kuamini kwamba Sabato ya Wayahudi ilikuwa siku halali kwa watu wote wa Mungu kuabudu.  Basi, akaandika kijitabu chake kilichoitwa, “The Seventh Day Sabbath, a Perpetual Sign””. 
Baada ya kitabu hicho Bw. Joseph Bates aliendelea kuandika vijitabu kuhusu Sabato.  Hivi bwana huyu anakumbukwa sana na Wasabato kwa mchango mkubwa katika kuirudisha Sabato ya Agano la Kale. Kwa kweli, ni yeye aliyekuwa wa kwanza kutafsiri siku ya Jumapili kama siku ya alama ya mnyama; na kwamba siku ya Sabato ndiyo muhuri wa Mungu kwa watu wake walio waaminifu, yaani Waadventisti Wasabato 144,000 (rej. Ufu 7:4). 
Kutokana na ushawishi wake huu, kuabudu siku ya Jumamosi, kukaanza kupata nguvu nyingi, zilizoambatana na vitisho vya hukumu kali kwa wanadamu wote wasioishika Sabato  ya Agano la Kale. Kifupi, miongoni mwa Waadventisti waliomfuata Bw. Joseph Bates kwa karibu, walikuwa ni James na mkewe Ellen White.  Kumbe, Bi Ellen White ndiye aliyeuendeleza usabato, kwa motomoto zaidi kuliko watu wengine wote naye anaheshimiwa na Wasabato kama nabii wao.  Kwa hali hii ya mambo, yafaa tumalizie historia hii fupi kwa kumwangalia mwanamama huyo hata kama ikiwa kwa kifupi sana.
Ndugu zanguni, Bi Ellen G. White, anafahamika pia kwa jina la Bi Ellen Gould Harmon. Ni kwamba kabla hajaolewa alikuwa anaitwa Ellen Gould Harmon na baada ya kuolewa kwake na mpenziwe James White, aliyekuwa mhubiri wa kibaptisti aliyekuwa muadventisti hapo tarehe 30 Agosti, 1846 akajulikana kama Bi Ellen Gould White.
Kwa kufupisha mambo, Bi Ellen Gould Harmon alizaliwa mwaka 1827 huko Goharm, jimboni Maine, maili kumi hivi toka Portland.  Akiwa mtoto mdogo bado, wazazi wake walihamia Portland kwenyewe.  Hapo mwanzoni, yeye pamoja na familia yake walikuwa wafuasi wa dhehebu la Methodisti.  Kumbe, familia ya akina Ellen ilijiunga na uadventisti baada ya Bw. William Miller kuhubiri mjini Portland katika mwaka wa 1840 na 1842.  Lakini kwa kuwa familia hiyo ilisadiki maneno  ya Bw. William Miller, kanisa lao la Methodisti liliitenga familia hiyo. Familia nzima ilitengwa kwa sababu ya kuyapokea mafundisho ya Kiadventisti.  Kwa ujumla, mchango wa Bi Ellen White ulianza kama alivyodai mwenyewe kwamba alipokea maono mengi nyakati mbalimbali, maono ambayo baadaye yalimfanya ajulikane kama nabii wa Waadventisti.  Inasemekana maono yake ya kwanza yalimjia mwezi Desemba, 1844, yaani si muda mrefu sana baada ya watu kukatishwa tamaa na kutokurudi kwa Yesu Kristo. 
Bi Ellen White aliingia ulingoni akidai kuliona kundi la Waadventisti wakisafiri katika njia yenye mwanga wa utukufu, huku wakiongozwa ya Yesu hadi walipoufikia mji wa Mungu.  Bi Ellen akadai kwamba baada ya kuonywa katika maono ya pili asikae kimya juu ya yale aliyooneshwa, alilazimika kutangaza na kuyahubiri maono yake wazi mahali pengi.  Kuanzia hapo, Waadventisti wa Portland na Maine wakaanza kumtambua Bi Ellen White kama nabii wao na kusisitiza kwamba Roho Mtakatifu alikuwa juu yake na kwamba ilikuwa ni lazima unabii wake ufuatwe na Waadventisti wote popote pale walipokuwa. 
Kama jambo hilo halitoshi, mwezi Februari 1845, Bi Ellen White alidai kupata maono yaliyothibitisha maono ya Bw. Hiram Edson mintarafu kitu kilichotokea hapo tarehe 22 Oktoba 1844, yaani kwamba Yesu alikuwa ameingia patakatifu pa patakatifu katika hekalu la mbinguni.  Zaidi ya hapo alidai kwamba miaka miwili baadaye, alipata maono mengine ambapo alidai kwamba alichukuliwa na kupelekwa katika hekalu la mbinguni.  Alisema kwisha kufikishwa mbinguni, kwanza kabisa aliingizwa patakatifu na baadaye patakatifu pa patakatifu ambapo aliona amri kumi zikiwa ndani ya sanduku la agano.
Tukiwa tayari kusonga mbele, tunaweza kujiuliza swali dogo la kuchangamsha bongo zetu. Hebu tujiulize, hivi, humo patakatifu pa patakatifu Bi Ellen White alikumta Yesu akifanya hukumu ya kipelelezi? Tukikijibu  wenyewe,  ndugu yangu, jibu ni kwamba suala hilo haligusiwi ilivyotarajiwa. Basi, acha tuzidi kumfuatilia katika madai ya maono yake. Bi Ellen White anasema alipong’aza macho yake kwenye sanduku la agano la humo hekaluni, aliona amri ya sabato ikiwa imezungukwa na utukufu na hapo eti akang’amua kwamba amri ya kushika Sabato ilikuwa kubwa zaidi.
Ndugu yangu, hadi hapo, tukimpima Bi Ellen White kibiblia, anaongeza uongo mwingine mbaya. Uongo wa kwanza ni ule wa kuliona hekalu mbinguni wakati mbinguni, Maandiko Matakatifu yanasema hakuna hekalu (rejea tena Ufu 21:22). Uongo wa pili ni huu wa kuhesabu amri ya kushika Sabato kama amri kuu kwani amri ya kwanza na kubwa kupita zote, kadiri ya Yesu Kristo mwenyewe, ni ile ya kumpenda Mungu huku ikifuatiwa na ya pili yake, yaani ile ya kumpenda jirani kama tunavyojipenda sisi wenyewe (rej. Mt 22:34-40).
Lakini basi, ndugu zanguni, maono aliyopata Bi Ellen White yakawa, kwake na hatimaye kwa Wasabato wote, kurunzi la kutafsiria  Maandiko Matakatifu yote.  Ndipo, kwa njia ya vitabu vingi alivyoandika, mafundisho ya Kiadventisti yakasambazwa. Hivyo, tangu wakati huo, Waadventisti Wasabato, huitafrisi Biblia kwa vipimo vya maono ya White, na siyo kuyatafsiri maono ya Bi White kwa vipimo vya Biblia.  Je, si ajabu ya mwaka hiyo? Basi, ndugu yangu, fumbuka macho ya roho yako, uyaone na kuyapima mambo haya sawa sawa pasipo kiwi cha macho! Usitoe hoja ya uongo!
Basi, kwa kukata maneno, Bi Ellen White ndiye aliyewapandikiza chuki Wasabato dhidi ya Kanisa Katoliki. Amelifanya hilo kwa kupitia vitabu vyake vingi vyenye chuki ambavyo vinasomwa na kutumiwa na Wasabato karibu kama misahafu.  Kwa taarifa yako, baadhi ya vitabu hivyo ni, kama vile, Vita Kuu, Afya na Raha na Siri ya Ushindaji. Ndani ya vitabu hivi Kanisa Katoliki linatukanwa na kushtakiwa kuhusika na maovu mengi. Kwa mfano, wanashtakiwa kuondoa amri ya kuabudu Sabato. Wanashtakiwa kuabudu sanamu. Wanashtakiwa kumwabudu Bikira Maria. Wanashtakiwa kumwabudu Baba Mtakatifu (Papa) ambaye eti ndiye mnyama anayetajwa katika kitabu cha Ufu 13:1-18. Wanashtakiwa kufundisha mambo ya kidunia badala ya ufalme wa Mungu. Wanashtakiwa kuongeza vitabu kwenye Biblia na mengine mengi ya namna hiyo yanayosikika mitaani na katika mahubiri yao. Mungu utuhurumie!
Ndugu zanguni, kwa ujumla, kanisa la Wasabato likawa muungano wa vikundi vitatu vya Waadventisti: mosi, kikundi cha Bw. Hiram Edson, kilichosisitiza zaidi mafundisho ya huduma ya Yesu patakatifu pa patakatifu mbinguni; pili, kikundi cha Bw. Joseph Bates, kilichosisitiza zaidi kufuata Sabato ya Agano la Kale; na tatu kikundi cha Bi Ellen G. White, kilichomwona Bi Ellen kama nabii ambaye unabii wake ni lazima ufuatwe na Waadventisti wote duniani.
Vikundi hivi vilipoungana Waadventisti Wasabato wakapata kujichipusha duniani. Mwaka 1860, jina la Seventh Day Adventist lilichaguliwa nalo likawa jina rasmi la Waadventisti hao.  Kishapo, mwezi Mei, 1863, katika mkutano mkuu wa kwanza, uliokuwa na wawakilishi kutoka majimbo yote Marekani, isipokuwa jimbo la Vermont, kanisa la Wasabato likazaliwa rasmi duniani.
Basi, tukipiga muhtasari wa historia ya Wasabato, tuseme tu kwamba mwasisi wa Waadventisti Bw. William Miller alikuwa ni Mbaptisti lakini mwanzilishi wa Wasabato yaani Bi Ellen G. White alikuwa ni Mmethodisti. Hata hivyo, kwa kuhitimisha sehemu hii, yafaa sote tukumbuke kwamba makanisa hayo mawili, yaani Wabaptisti na Wamethodisti si chochote isipokuwa matawi ya kanisa la Anglikana, kanisa lililoanzishwa na Mfalme Henry VIII wa Uingereza hapo mwaka 1534 baada ya kukasirika kukataliwa na Kanisa Katoliki kumwacha mkewe aliyeshindwa kumzalia  mtoto wa kiume.
WASABATO MITUME WA MATUSI DHIDI YA KANISA LA KWELI
Msomaji wangu bila shaka umeiona historia ya aibu na ya zigzaga ya Wasabato. Wasabato wenyewe huificha sana historia hiyo, hasa kwa wafuasi wao wanaoingia katika kanisa lao putaputa. Hufichwa ukweli kama paka wanaosafirishwa katika gunia. Kwa nini? Wanafichwa ili wasiujue ukweli walikotokea wasije wakajua kwamba wamekosea njia kiimani.
Kifupi, madai yao kwamba Baba Mtakatifu, Kanisa Katoliki au Mfalme Constantino ndio waliobadili Sabato kwenda Jumapili ni mojawapo ya matusi ya Wasabato. Wenyewe wanahubiri hayo kwa jasho jingi kabisa wakati ni kusepetuka kwa uelewa na fichio la aibu yao katika kushindwa kwao katika utabiri wa tarehe ya mwisho wa dunia, tarehe ambayo Yesu  Kristo, Bwana wetu na Maandiko yanatuambia kwamba haitabiri kabisa.  Kwa maneno mengine, ndiyo matawi ya chuki iliyokosewa mwelekeo na uongo wa binadamu dhidi ya wanadamu wenzake.
Tusisahau, kutokana kushindwa hoja na aibu kubwa waliyoipata mbele ya ukweli unaoshikiliwa na kufundishwa na Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki, Wasabato na makanisa mengine wameamua kutumia mbinu ya kujikosha kwa matusi makali.  Wameamua kujitwika utume wa matusi wakati mwingine hata matusi ya nguoni. Kwa vyovyote, Wakatoliki hawana namna rahisi ya kukabiliana na madai hayo ya kimatusi. Usistaajabu haya kufanyika hivi. Kwa mtindo wa vijijini, ukishindwa hoja kwa mtu fulani unaanza kumtukania wazazi wake, nyumba yao na kadhalika.
KUITUNZA SABATO NI KUSHEREKEA MKESHA WA SIKU YA UHURU
Kuitunza Sabato mbele ya Dominika ingelingana na kusherekea mkesha wa siku ya uhuru badala ya siku ya uhuru yenyewe. Taifa litakalofanya hivyo litachekesha na labda litakuwa la watu punguani. Aidha mtu kupita huko na huko kuwahimiza watu washerehekee mkesha wa uhuru badala ya siku ya uhuru wenyewe ingelikuwa sawa na kucheza Ze Comedy.
Nani amegeuka mkondo wa mambo hata kugeukia tena Sabato wakati Wakristo wa kwanza kwa kumwelewa vyema Yesu Kristo walishaitupilia mbali?  Jibu ni wazi. Ni mmoja wa waanzilishi wa dhehebu la Wasabato, yule mama anayejulikana kama nabii. Kwa taarifa yako waanzilishi wa dhehebu la Wasabato ni akina Hiram Edson, Joseph Bates, E.G. Harmon na Hellen White. Katika hawa aliyekuja na moto wa kurudisha Sabato ni huyo mama ambaye alikuwa mke wa E.G. Harmon. Mwanamke huyo anaheshimiwa na Wasabato kama nabii na vitabu vyake , kama vile Vita Kuu, Afya na Raha na Ushindaji, vinasomwa na Wasabato karibu kama misahafu.
WASABATO WASIMNYANYASE YEYOTE
Maono ya uwongo ya Bi Hellen yasiwe sababu ya kuwanyanyasia Wakristo wasio Wasabato. Wala si siri, makanisa yanayofuata mabadiliko yaliyoletwa na Mungu mwenyewe kutoka Sabato kwenda Dominika yananyanyaswa kweli kweli na kauli za Wasabato wanaomfuasa Bi Hellen White. Lakini, hivi unabii wa mama huyo ni wa kweli hata tutishike nao? Hapana, wala si wa kweli. Unabii wa mama huyu lazima tuukatae. Kwa nini tuukatae?
TUHIMIZANE TUMKATAE BI HELLEN NA MAONO YAKE
Ni kwa sababu kuna sababu tatu zinazotuhalalisha tumkatae Bi Hellen White kama nabii. Mosi, kitabu cha Ufunuo kinaonesha kufungwa kwa unabii, yaani kwamba baada ya mambo yaliyoandikwa humo kusingekuwa na ufunuo wowote wa pekee. Ukamilifu wa ufunuo ulitokea katika ujio wa Yesu Kristo. Alichosema yeye ndicho kitu cha kilele. Sasa Bi Hellen anakujaje na mapya kumpikua Yesu Kristo? Tunasoma, “Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi, amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akavichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu, amefanyika bora kupita malaika kwa kadiri jina alilorithi liliyo tukufu kuliko lao” (Ebr 4:1-4).
Si hivyo tu hata mintarafu ufunuo wa zamani mihuri yake imevunjwa na Yesu Kristo mwenyewe, sasa unabii wa Hellen White unaanzia wapi? Tunasoma, “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, Ni nani astahiliye kukifungua kitabu na kuzivunja muhuri zake. Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kikifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.
Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwanakondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja , akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya Mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya wakatakatifu, nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaaa hicho kitabu na kizifungua muhuri zake, kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme wa makuhani, kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchi” (Ufu 5:1-10).
Mintarafu kusasambua ovyo ufunuo wa Mungu, mwandishi wa kitabu cha Ufunuo alishakatazwa, sasa Bi Hellen White anapata wapi nguvu ya kuja na ufunuo mpya? Kuhusu marufuku hiyo tunasoma, “Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike” (Ufu 10:4). Hatimaye, maneno ya ufunuo yaliachwa wazi bila muhuri kwa vile yalivyokuwa njiani kutimia. Juu ya jambo hili, tunasoma hivi: “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki kwa maana wakati huo umekaribia” (Ufu 22:10). Sasa Bi Hellen White anaongezaje maneno ya ufunuo mpya?
Pili, tuukatae unabii wake kwa vile zile anazoziita njozi, kama elfu mbili hivi, ni batili kwani zinaonesha jinsi alivyojaa chuki kwa Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki nasi tunajua kwamba si kazi ya Mungu Roho Mtakatifu kumjaza mtu chuki kali hivyo dhidi ya mwanadamu mwingine. Kazi hiyo hufanywa na Shetani nayo huonesha kwamba moyo wa mtu umejaa uovu kwani kilichomjaa mtu moyoni ndicho kimtokacho. Tunasoma, “Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema  katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake”  (rej. Lk 6:43-45). Hakika chuki dhidi ya Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki inatoka katika moyo uliofurika uovu. Na kwa jinsi hii maono yake hayawezi kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Tatu, tuukatae unabii wake kwa sababu mafundisho yake yanaonesha kwamba haijui Biblia. Hoja hii ya tatu nimeshaishuhudia tayari. Nimesema ameota ndoto akaona huko mbinguni kuna hekalu wakati Maandiko yanatakaa jambo kama hilo (rej. tena Ufu 22:22-24). Kisha nimeshashuhudia kwamba kule kusisitiza kwamba Sabato ndiyo amri kuu kunapingana na kile alichotuambia Bwana wetu Yesu Kristo aliyesisitiza kwamba amri kuu ni upendo (rej. tena Mt 22: 34-40).  Naomba itoshe nilivyokuambia nawe uyapuuze maono ya Mrs. Harmon tunayemchambua hapa.
MAJIBU KWA MASHTAKA YA ZIADA
Nikiendelea kidogo, naomba ruksa nijibu mashtaka mawili sambamba wanayotoa Wasabato dhidi ya Wakatoliki: mosi kwamba ndio mnyama yule Shetani aliyejipa jukumu la kubadili majira na pili kwamba Kanisa lenyewe linakiri kufanya hivyo katika Katekisimu zake na katika vitabu vya waandishi fulani fulani wa Kanisa Katoliki.
Mintarafu hoja ya kwanza ni hivi mnyama ni Bi Hellen White aliyethubutu kumpinga Mungu. Mungu aliibadili siku ya Sabato yeye akijipa jukumu la kuirudisha kwa maelezo ya maono yake batili kabisa. Tumeshaonesha jinsi yalivyo batili kwa kadiri ya mizani na darubini ya Maandiko Matakatifu.
Halafu mintarafu hoja ya pili ni hivi Kanisa linajihusisha na mabadiliko hayo si kama ‘mtendaji’ kwani hakuna mkutano mkuu (mtaguso) wowote wa Kanisa Katoliki uliojadili hoja ya Sabato na kuamua kuibadili kwenda Dominika ila kwamba Mungu aliibadilisha Sabato pale alipoanzisha enzi ya Israeli mpya yaani Kanisa.  Natumaini wasomaji wangu hoja hii si ya kitaalamu mno kiasi cha kutonielewa ninachosema. Ninasema hivi Kanisa linajisikia kuhusika na ubadilishaji wa Sabato kwenda Dominika kwa vile Mungu aliufanya kuanzia pale lilipoanza kuwako nalo kwa mamlaka uliyopata kutoka kwa Mungu ikayasimamia na kuyaendeleza mabadiliko hayo.
MALUMBANO SASA YAKOME
Naomba hadi hapa shtaka la kwamba Kanisa Katoliki limebadili majira, yaani kutoka Sabato kwenda Dominika (Jumapili), lififie kabisa. Si unajua kwamba hoja yenyewe hukokotolewa kutoka Dan 7:25 mahali palipoandikwa, “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye Juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye Juu, naye ataazimu kubadili majira na sheria”. 
Kama unavyoisoma sasa, hoja hii haitaji Kanisa Katoliki bali kwa kinyume chake inawataja Wasabato wenyewe. Ndugu zangu Wasabato haliwafahamu jambo hili kwa sababu ndivyo ilivyo, “Jambo usilolifahamu ni sawa na usiku wa giza.” Kwa vipi? Ni hivi, kama Yesu kwa maneno na matendo yake alisema Sabato si lolote na wala si chochote “maana mtu hakuuumbwa kwa ajili ya Sabato”, mtu anayesema Sabato ndiyo yote katika yote ndiye anayeazimu kubadili majira na sheria. Na moja kwa moja mtu huyo anakuwa ndiye mpinga Kristo kwa sababu anapingana na kauli ya Kristo mwenyewe. Hilo ndilo alilofanya nabii Hellen na kuwasadikisha maelfu ya watu kauli yake kengeufu.
Aidha, kama Yesu alisema kwamba amri kuu ni upendo (rej. Mt 22:37) na akataka iwatambulishe wafuasi wake popote watakapokuwa (rej. Yn 13:35), anapokuja nabii Hellen na kusema eti amri kuu ni Sabato ni upinga Kristo wa wazi wazi na kumfuasa mpinga Kristo kama huyo ni kuwa wapinga Kristo wadogo wadogo nyuma ya huyo mkubwa. Ona ushuhuda wa Maandiko Matakatifu. Bila shaka, hata wewe unakumbuka Yesu aliulizwa swali juu ya amri ya kwanza na kuu naye akatoa jibu mwafaka hata wasomi na walimu wa enzi zake wakamvulia kofia.
Tunasoma, “Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu: Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii” na wakati akiwaaga wanafunzi wake jioni iliyotangulia kifo chake alisema na kuagiza, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn 13:35). Sasa Nabii Hellen anathubutuje kusema kinyume cha maneno hayo ya Kristo ambaye tumepewa tumsikilize? Kama huo si upinga Kristo wenyewe ni nini tena? Hukumu mwenyewe; wewe ni mtu mzima. Hivi wewe na mimi na sisi sote hatukumbuki maneno ya Maandiko Matakatifu, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye” (Mk 9:7)? Na kwa upande wetu, kwa nini, tunamsikiliza binadamu tena? “Tumechanganyikiwa” au “tumerogwa”?
UCHAMBUZI WA KISAIKOLOJIA WA WALIOHUSIKA NA HISTORIA HII YA AIBU
Jina Ugonjwa Tunaoweza Kumtuhumu Upinga Kristo Wake Ulipo
William Miller Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kujaribu kuitaja tarehe ya mwisho wa dunia Kukokotoa tarehe ya mwisho wa dunia kinyume na Mk 13:32.
Samwel Snow Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kujaribu kuitaja tarehe ya mwisho wa dunia Kukokotoa tarehe ya mwisho wa dunia kinyume na Mk 13:32.
Hiram Edson Schizophrenia – kuona hekalu ambalo halipo mbinguni na kudai mwisho wa ulimwengu umeshatokea.  Kuota ndoto ya kuliona hekalu mbinguni ni kinyume cha Ufu 21:22-23.
Joseph Bates Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kuunga mkono uongo kwamba mwisho wa ulimwengu umeshatokea. Kuidharau Jumapili, siku aliyoitumia Bwana kufanya mambo yote makubwa.
Hellen White Schizophrenia – kuona hekalu ambalo halipo  Kuota ndoto ya kuliona hekalu mbinguni ni kinyume cha Ufu 21:22-23 na kudai Sabato ndiyo amri kuu kinyume na Mt 22:34-40.

MASWALI NA MASHTAKA 12 MAARUFU YA WASABATO KWA WAKATOLIKI
i. Sabato ndiyo siku ya kuabudu iliyoamriwa. Wakatoliki ndio walioifuta Sabato na kuweka Jumapili.
ii. Wakatoliki wanafuata mapokeo ya binadamu, hawajui na wala hawafuati Maandiko Matakatifu.
iii. Baba Mtakatifu ndiye mnyama yule anayewakilishwa na namba 666. Namba hiyo imeandikwa kwenye kofia na mavazi yake.
iv. Wakatoliki wameifuta amri ya pili ya Mungu. Wamefanya hivyo ili waabudu sanamu.
v. Wakatoliki wanaabudu sanamu. Tazama sanamu makanisani mwao!
vi. Kwa nini Wakatoliki wanakunywa pombe wakati imekatazwa kwenye Biblia?
vii. Wakatoliki wanamwabudu Bikira Maria. Kwa nini wanamfanyia heshima kubwa isivyostahili?
viii. Je, Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo?
ix. Kanisa Katoliki linafanya makosa kuwatangaza wanadamu kuwa watakatifu. Mwanadamu ana uwezo gani wa kumtangaza mtu mwingine kuwa mtakatifu?
x. Wakatoliki wana sakramenti saba. Wana makosa kwa sababu hazijaandikwa kwenye Biblia.
xi. Kuungama ni kwa Mungu moja kwa moja. Kuna uhalali gani kwenda kuungama kwa mapadri wakati wenyewe wana dhambi?
xii. Wakatoliki wana hatia kubwa kwa sababu hawataki kuokoka. Kwa nini Wakatoliki ni wabishi hivyo?

Ndugu yangu Mkatoliki jaribu kuwa na majibu ya maswali haya, hutahangaishwa na Wasabato wowote katika imani yako na maisha yako yote. Kumbe, usipokuwa nayo siku zote utayumbishwa kama wimbi la baharini wakati ulipaswa kutulia tuli kama maji kwenye mtungi.
HATIMA: TUSIHANGAISHANE TENA JUU YA SABATO KWANI  ILIKUWA KIVULI TU
Kwa sasa Wakatoliki wote tuhitimisha fikra zetu kwa nukuu hii: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni KIVULI cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17).
Ndugu zanguni, kama inavyosomeka katika aya hizi, Sabato ilikuwa kivuli na kivuli hakishonewi suti. Sisi ni watu wazima tuachane na Sabato. Nina hakika tutaadhibiwa na Mungu kwa hatia ya kukipa hadhi kitu kisicho na uzito wa kimani.
Imeandikwa na
Pd. Titus Amigu (2016)