Jumanne, 11 Julai 2017

HISTORIA HALISI YA WASABATO: AIBU TUPU
Ndugu zanguni nitaendelea na mada yetu ya “viboko hamsa wa ishirini” lakini naomba nikatishe kidogo nipate kujibu swali moja linalojirudia rudia sana. Swali lenyewe naulizwa kwa namna nyingi mno. Mtu wa mwisho ameniuliza akisema hivi: “ Asante sana baba gombera mstaafu, hivi huyu Bi Ellen G. White ni nani katika Kanisa Katoliki? Mbona amekuwa akishambulia sana Kanisa Katoliki au kuna makanisa mengine huanzishwa na misingi yao ni lazima kushambulia Kanisa Katoliki?
Jibu fupi: Bi Ellen G. White ni mmojawapo wa waanzilishi wa kanisa la Wasabato lakini fundi sana wa kulitukana Kanisa Katoliki. Yeye hakuwamo ndani ya Kanisa Katoliki na wala hakujihusisha nalo kwa nia njema isipokuwa aliondokea kuongoza kulitukana.
Wala si siri yapo makanisa ambayo huanzishwa na misingi yao ni lazima kulishambulia Kanisa Katoliki kwa sababu zao mbalimbali. Kanisa mojawapo kati ya hayo ndilo kanisa aliloshiriki Bi. Ellen White kulianzisha yaani kanisa la Sabato. Inasikitisha sana na kukera sana, lakini tutafanyaje. Ndiyo hivyo tena, kisera, kanisa la Sabato limepania kulibomoa Kanisa Katoliki. Sisi hatuwezi kuwachukulia hatua ya kiuhalifu isipokuwa kufahamishana kama ninavyokusudia kufanya ili tukae chonjo nalo tu. Kumbe kwa busara ya maisha, anayekuwinda walau mjue tu kusudi ujue namna ya kumkwepa. Wala si lazima upigane naye.
Sasa kusudi vijana mmwelewe vizuri mtu huyo aheri nikupeni historia nzima ya kuanzishwa kwa kanisa la Wasabato. Katika historia hiyo mtaona aibu ya kushindwa utabiri wa mwisho wa dunia. Cha kushangaza waliposhindwa kutabiri mwisho wa dunia kama walivyojinasibu kuweza, wakageukia kulitukana Kanisa Katoliki ambalo halina kosa lolote na halikuwafanya chochote.
Hivi acheni niitumie fursa ya kujibu swali hili kwa kuwaleteen historia halisi ya Kanisa la Wasabato. Nawaanikieni hadharani aibu yao, aibu inayowatia hasira na hasira yenyewe kuilekeza kwa Kanisa Katoliki ambalo halijawakosea.
Jibu hili nimewahi kuliandika kwenye Gazeti la Kiongozi na vile vile kulirusha hewani kwa njia ya radio. Lakini kwa kuwa bado naendelea kuulizwa, kwa mitindo mbalimbali, kila uchao napenda nilijibu tena sasa kwa kupitia ukurasa wangu wa Facebook. Sina nia ya kuleta uchochezi. Najibu swali kwa kadiri inavyostahili tu.
Jibu refu: Wakatoliki tunatukanwa kwa sababu Wasabato wanajaribu kufunika aibu yao ya kihistoria na wanadhani matusi ndiyo njia ya kuliua Kanisa Katoliki. Hawajui kwamba matusi hayawezi kumharibu mtu isipokuwa kumfedhesha mtukanaji tu. Waungwana hawatukani. Kumbe, aheri tuielewe historia ya dhehebu la Wasabato au S.D.A tupate kuwapuuza wanaotutukana huku wakijiabisha wenyewe. Basi, historia hiyo ya aibu inayofichwa ndiyo hii ifuatayo:
Ni hivi ndugu zanguni, kwa kuiweka bayana historia ya Wasabato, tuambatane katika kuwaelewa watu wanne ambao hutajwa kama watangulizi au waasisi wa dhehebu la Wasabato. Mwishoni nitayapembua waliyofundisha kibiblia na kisaikolojia.
Mtu wa kwanza ni William Miller, wa pili ni Hiram Edson, wa tatu ni Joseph Bates na wa nne na wa mwisho awe Bi Ellen G. White.
Tukianza na Bw. William Miller, yeye alizaliwa mwaka wa 1782 katika mji wa Pittsfield, Massachusetts, huko Marekani.  Ingawa alizaliwa katika familia ya Kikristo, aliuacha Ukristo alipokuwa kijana mbichi.  Kwa kweli hakuiamini Biblia kuwa neno la Mungu.  Basi, akajiunga na jeshi. Baada ya kutumika kama mwanajeshi kwa muda mfupi, akaishi kama mkulima.  Kumbe, mwaka wa 1816, akaongoka na kuurudia Ukristo wake kwa kasi mpya.  Kwa kweli, tangu mwaka huo wa kuongoka kwake, Bw. William Miller alisoma unabii kwa kina na hasa unabii uliohusu kurudi kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. 
Kumbe, kutokana na kujifunza huko, Bw. William Miller akashawishiwa kwamba mwisho wa dunia ungetimia mwaka 1843.  Kifupi, Bw. William Miller alishawishiwa kufundisha jinsi hiyo na unabii wa kitabu cha Danieli 9:24-27, unabii unaohusu majuma sabini yaliyowekwa kwa ajili ya watu wa Mungu, taifa la Israeli.
Zaidi ya hayo, katika Danieli 8:13-14, kuna unabii wa watakatifu wawili wanaoulizana lini patakatifu patatakaswa.  Mintarafu unabii huo, Bw. William Miller alitafsiri kwamba patakatifu patakapotakaswa, ni dunia hii iliyochafuliwa na dhambi za kila sampuli.  Kwa maoni yake, mwaka wa 1843 B.K., ndio mwaka ambao Yesu Kristo angerudi katika dunia iliyonajisiwa kupita kiasi na dhambi na hivyo kuitakasa kabisa kwa kuwapo kwake. 
Msimamo huu ulimfanya awe maarufu sana katika sehemu nyingi za Marekani, na hatimaye akawa mhubiri mkubwa wa dhehebu la Kibaptisti.  Kwa kuwa mwisho wa dunia ulikuwa unaambatana na kurudi kwa Yesu Kristo, ambako kwa Kiingereza huitwa “Christ’s Advent”, wafuasi wake walianza kujulikana kama “Adventists” au kwa Kiswahili “Waadventisti”, yaani “Watu watarajiao kurudi kwa Kristo”. Ijapokuwa mwanzoni hakutaja tarehe bayana ya kurudi kwa Yesu, punde si punde alisema kurudi kwa Yesu kungekuwa kati ya tarehe 21 Machi, 1843 na 21 Machi, 1844. 
Baada ya mambo kufikia hapo, mfuasi mmoja wa Bw. William Miller aliyeitwa Samwel Snow, akawa jasiri zaidi na kutaja kwamba Kristo angerudi tarehe 22 Oktoba, 1844 saa 6.00 usiku; yaani ndipo parapanda litakapopulizwa, mbingu kukunjwa kama kurasa, na Yesu Kristo kufika  kwa utukufu mwingi.  Lakini mambo hayakutukia hivyo walivyohubiri. Basi, kwa vile Kristo hakurudi kama walivyotarajia, Bw. Miller akakiri kukosea kwake, lakini akawaonya wafuasi wake wasisahau kwamba Kristo atarudi upesi. 
Kwa bahati mbaya, Bw. William Miller alifariki mnamo mwaka 1849 ndoto yake ya kumwona Yesu akirudi upesi ikiwa bado haijatimia.  Hadi hapo, ieleweke kwamba Bw. William Miller, hakuwahi kuwa Msabato.  Hivyo kama Mbaptisti, alikuwa anasali siku ya Bwana, yaani Jumapili au Dominika. Kutokana na kutokutumia kwa utabiri wa Bw. William Miller wafuasi wake wengi wakarejea nyuma.
Basi, tumwachie Bw. William Miller hapo, nasi tusonge mbele tukamwangalie mtu wa pili, yanii Bw. Hiram Edson.  Kwa bahati, bwana huyu alikuwa kati ya Waadventisti wachache waliobaki baada ya kuvunjika moyo kwa wafuasi wengine wa William Miller kutokana na kutorudi kwa Kristo kama ilivyotazamiwa.  Kwa upande wake  kwa kusudi la kuwafariji wenzake kwenye huzuni yao, yeye alidai kwamba Mungu alikuwa ametoa jibu kwa aibu yao kwani alipata mafunuo juu ya kile kilichofanyika siku hiyo ya tarehe 22 Oktoba, 1844. 
Kwa jinsi gani? Sikiliza. Alifundisha kwamba alioneshwa kulikuwa na hekalu mbinguni mfano wa hekalu la duniani. Akadai hekalu hilo lilikuwa na sehemu mbili: patakatifu na patakatifu pa patakatifu, yaani sawa na lilivyokuwa hekalu la Kiyahudi zamani zile.  Kumbe, kilichofanyika siku hiyo ya tarehe 22 Oktoba,  ni kwamba Kristo alitoka patakatifu na kuingia patakatifu pa patakatifu.  Akasema kwisha Yesu kuingia patakatifu pa patakatifu atabaki humo mpaka siku atakapokuja duniani mara ya pili. 
Mintarafu swali, Yesu anafanya nini siku zote hizo? Akasema Yesu anafanya ‘hukumu ya upelelezi’ kwa Kiingereza “investigative judgement”.  Kwa maelezo hayo mapya akadai kwamba kitu alichokuwa amekosea Bw. William Miller kilikuwa tafsiri tu, kwa maana kwamba utakaso uliofanywa tangu siku ile ya tarehe 22 Oktoba haukuwa wa dunia hii, bali wa patakatifu pa patakatifu katika hekalu hilo la mbinguni.
Kwa namna hii, Bw. Hiram Edson akawa Mwadventista wa kwanza, hata kabla hajawa Msabato, kuleta duniani maelezo ya kuwafariji wenzake kwa kutorudi kwa Kristo siku ya tarehe 22 Oktoba 1844.  Hivi basi, mchango wake mkubwa kwa teolojia ya Wakristo ambao baadaye walijiita Wasabato ni suala  hilo la ‘hukumu ya upelelezi’.  Kifupi, kwa maelezo hayo, Wasabato wanafundisha kwamba Yesu Kristo, tangu 22, Oktoba 1844 yuko huko mbinguni, katika patakatifu pa patakatifu akichunguza kwa kina maisha ya Wakristo wote ambao majina yao yapo katika kitabu cha uzima wa milele na kuamua nani anastahili kufutiwa dhambi zake zilizosamehewa wakati alipoamini.  Hivyo, kila mtu anayeonekana kurudi nyuma, naye hakutubu dhambi zake zote, anafutwa jina lake kutoka katika kitabu cha uzima na hivyo huko, mwishoni mwa historia, atakosa nafasi katika ufufuo wa kwanza.  Kinyume chake, kwa upande wao, wote ambao walitubu dhambi zao, majina yao yanabaki kitabuni pasipo kufutwa, nao watafufuliwa katika ufufuo wa kwanza.
Ndugu zangu, hadi hapa umeshagundua mafundisho ya uongo. Mbinguni hakuna hekalu. Huo ndio ukweli wa kibiblia maana mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anatuandikia habari za maono yake matakatifu mintarafu Yerusalemu ya mbinguni akisema “Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana  Mungu Mwenyezi na Mwanakondoo, ndio hekalu lake” (Ufu 21:22). Sasa iweje Bw. Hiram Edson amzungumzie Yesu anayetoka patakatifu kuingia patakatifu pa patakatifu? Zaidi ya hayo, mafundisho ya hukumu ya upelelezi ni uzushi kwa sababu ni matokeo dhahiri ya tafsiri potofu ya neno la Mungu. 
Haya tuachane naye, nasi twende tukamwangalie mtu wa tatu, ambaye ni Bw. Joseph Bates.  Kikazi, Bw. Joseph Bates alikuwa baharia.  Bada ya kustaafu kwake alihamia Fair Haven, katika jimboni Massachusetts, huko huko Marekani.  Kwa kweli, Bw. Joseph Bates ni mmoja wa viongozi maarufu  wa Waadventisti.  Yeye aliposoma maandishi ya Thomas Prebble kuhusu Sabato, alishawishiwa kuamini kwamba Sabato ya Wayahudi ilikuwa siku halali kwa watu wote wa Mungu kuabudu.  Basi, akaandika kijitabu chake kilichoitwa, “The Seventh Day Sabbath, a Perpetual Sign””. 
Baada ya kitabu hicho Bw. Joseph Bates aliendelea kuandika vijitabu kuhusu Sabato.  Hivi bwana huyu anakumbukwa sana na Wasabato kwa mchango mkubwa katika kuirudisha Sabato ya Agano la Kale. Kwa kweli, ni yeye aliyekuwa wa kwanza kutafsiri siku ya Jumapili kama siku ya alama ya mnyama; na kwamba siku ya Sabato ndiyo muhuri wa Mungu kwa watu wake walio waaminifu, yaani Waadventisti Wasabato 144,000 (rej. Ufu 7:4). 
Kutokana na ushawishi wake huu, kuabudu siku ya Jumamosi, kukaanza kupata nguvu nyingi, zilizoambatana na vitisho vya hukumu kali kwa wanadamu wote wasioishika Sabato  ya Agano la Kale. Kifupi, miongoni mwa Waadventisti waliomfuata Bw. Joseph Bates kwa karibu, walikuwa ni James na mkewe Ellen White.  Kumbe, Bi Ellen White ndiye aliyeuendeleza usabato, kwa motomoto zaidi kuliko watu wengine wote naye anaheshimiwa na Wasabato kama nabii wao.  Kwa hali hii ya mambo, yafaa tumalizie historia hii fupi kwa kumwangalia mwanamama huyo hata kama ikiwa kwa kifupi sana.
Ndugu zanguni, Bi Ellen G. White, anafahamika pia kwa jina la Bi Ellen Gould Harmon. Ni kwamba kabla hajaolewa alikuwa anaitwa Ellen Gould Harmon na baada ya kuolewa kwake na mpenziwe James White, aliyekuwa mhubiri wa kibaptisti aliyekuwa muadventisti hapo tarehe 30 Agosti, 1846 akajulikana kama Bi Ellen Gould White.
Kwa kufupisha mambo, Bi Ellen Gould Harmon alizaliwa mwaka 1827 huko Goharm, jimboni Maine, maili kumi hivi toka Portland.  Akiwa mtoto mdogo bado, wazazi wake walihamia Portland kwenyewe.  Hapo mwanzoni, yeye pamoja na familia yake walikuwa wafuasi wa dhehebu la Methodisti.  Kumbe, familia ya akina Ellen ilijiunga na uadventisti baada ya Bw. William Miller kuhubiri mjini Portland katika mwaka wa 1840 na 1842.  Lakini kwa kuwa familia hiyo ilisadiki maneno  ya Bw. William Miller, kanisa lao la Methodisti liliitenga familia hiyo. Familia nzima ilitengwa kwa sababu ya kuyapokea mafundisho ya Kiadventisti.  Kwa ujumla, mchango wa Bi Ellen White ulianza kama alivyodai mwenyewe kwamba alipokea maono mengi nyakati mbalimbali, maono ambayo baadaye yalimfanya ajulikane kama nabii wa Waadventisti.  Inasemekana maono yake ya kwanza yalimjia mwezi Desemba, 1844, yaani si muda mrefu sana baada ya watu kukatishwa tamaa na kutokurudi kwa Yesu Kristo. 
Bi Ellen White aliingia ulingoni akidai kuliona kundi la Waadventisti wakisafiri katika njia yenye mwanga wa utukufu, huku wakiongozwa ya Yesu hadi walipoufikia mji wa Mungu.  Bi Ellen akadai kwamba baada ya kuonywa katika maono ya pili asikae kimya juu ya yale aliyooneshwa, alilazimika kutangaza na kuyahubiri maono yake wazi mahali pengi.  Kuanzia hapo, Waadventisti wa Portland na Maine wakaanza kumtambua Bi Ellen White kama nabii wao na kusisitiza kwamba Roho Mtakatifu alikuwa juu yake na kwamba ilikuwa ni lazima unabii wake ufuatwe na Waadventisti wote popote pale walipokuwa. 
Kama jambo hilo halitoshi, mwezi Februari 1845, Bi Ellen White alidai kupata maono yaliyothibitisha maono ya Bw. Hiram Edson mintarafu kitu kilichotokea hapo tarehe 22 Oktoba 1844, yaani kwamba Yesu alikuwa ameingia patakatifu pa patakatifu katika hekalu la mbinguni.  Zaidi ya hapo alidai kwamba miaka miwili baadaye, alipata maono mengine ambapo alidai kwamba alichukuliwa na kupelekwa katika hekalu la mbinguni.  Alisema kwisha kufikishwa mbinguni, kwanza kabisa aliingizwa patakatifu na baadaye patakatifu pa patakatifu ambapo aliona amri kumi zikiwa ndani ya sanduku la agano.
Tukiwa tayari kusonga mbele, tunaweza kujiuliza swali dogo la kuchangamsha bongo zetu. Hebu tujiulize, hivi, humo patakatifu pa patakatifu Bi Ellen White alikumta Yesu akifanya hukumu ya kipelelezi? Tukikijibu  wenyewe,  ndugu yangu, jibu ni kwamba suala hilo haligusiwi ilivyotarajiwa. Basi, acha tuzidi kumfuatilia katika madai ya maono yake. Bi Ellen White anasema alipong’aza macho yake kwenye sanduku la agano la humo hekaluni, aliona amri ya sabato ikiwa imezungukwa na utukufu na hapo eti akang’amua kwamba amri ya kushika Sabato ilikuwa kubwa zaidi.
Ndugu yangu, hadi hapo, tukimpima Bi Ellen White kibiblia, anaongeza uongo mwingine mbaya. Uongo wa kwanza ni ule wa kuliona hekalu mbinguni wakati mbinguni, Maandiko Matakatifu yanasema hakuna hekalu (rejea tena Ufu 21:22). Uongo wa pili ni huu wa kuhesabu amri ya kushika Sabato kama amri kuu kwani amri ya kwanza na kubwa kupita zote, kadiri ya Yesu Kristo mwenyewe, ni ile ya kumpenda Mungu huku ikifuatiwa na ya pili yake, yaani ile ya kumpenda jirani kama tunavyojipenda sisi wenyewe (rej. Mt 22:34-40).
Lakini basi, ndugu zanguni, maono aliyopata Bi Ellen White yakawa, kwake na hatimaye kwa Wasabato wote, kurunzi la kutafsiria  Maandiko Matakatifu yote.  Ndipo, kwa njia ya vitabu vingi alivyoandika, mafundisho ya Kiadventisti yakasambazwa. Hivyo, tangu wakati huo, Waadventisti Wasabato, huitafrisi Biblia kwa vipimo vya maono ya White, na siyo kuyatafsiri maono ya Bi White kwa vipimo vya Biblia.  Je, si ajabu ya mwaka hiyo? Basi, ndugu yangu, fumbuka macho ya roho yako, uyaone na kuyapima mambo haya sawa sawa pasipo kiwi cha macho! Usitoe hoja ya uongo!
Basi, kwa kukata maneno, Bi Ellen White ndiye aliyewapandikiza chuki Wasabato dhidi ya Kanisa Katoliki. Amelifanya hilo kwa kupitia vitabu vyake vingi vyenye chuki ambavyo vinasomwa na kutumiwa na Wasabato karibu kama misahafu.  Kwa taarifa yako, baadhi ya vitabu hivyo ni, kama vile, Vita Kuu, Afya na Raha na Siri ya Ushindaji. Ndani ya vitabu hivi Kanisa Katoliki linatukanwa na kushtakiwa kuhusika na maovu mengi. Kwa mfano, wanashtakiwa kuondoa amri ya kuabudu Sabato. Wanashtakiwa kuabudu sanamu. Wanashtakiwa kumwabudu Bikira Maria. Wanashtakiwa kumwabudu Baba Mtakatifu (Papa) ambaye eti ndiye mnyama anayetajwa katika kitabu cha Ufu 13:1-18. Wanashtakiwa kufundisha mambo ya kidunia badala ya ufalme wa Mungu. Wanashtakiwa kuongeza vitabu kwenye Biblia na mengine mengi ya namna hiyo yanayosikika mitaani na katika mahubiri yao. Mungu utuhurumie!
Ndugu zanguni, kwa ujumla, kanisa la Wasabato likawa muungano wa vikundi vitatu vya Waadventisti: mosi, kikundi cha Bw. Hiram Edson, kilichosisitiza zaidi mafundisho ya huduma ya Yesu patakatifu pa patakatifu mbinguni; pili, kikundi cha Bw. Joseph Bates, kilichosisitiza zaidi kufuata Sabato ya Agano la Kale; na tatu kikundi cha Bi Ellen G. White, kilichomwona Bi Ellen kama nabii ambaye unabii wake ni lazima ufuatwe na Waadventisti wote duniani.
Vikundi hivi vilipoungana Waadventisti Wasabato wakapata kujichipusha duniani. Mwaka 1860, jina la Seventh Day Adventist lilichaguliwa nalo likawa jina rasmi la Waadventisti hao.  Kishapo, mwezi Mei, 1863, katika mkutano mkuu wa kwanza, uliokuwa na wawakilishi kutoka majimbo yote Marekani, isipokuwa jimbo la Vermont, kanisa la Wasabato likazaliwa rasmi duniani.
Basi, tukipiga muhtasari wa historia ya Wasabato, tuseme tu kwamba mwasisi wa Waadventisti Bw. William Miller alikuwa ni Mbaptisti lakini mwanzilishi wa Wasabato yaani Bi Ellen G. White alikuwa ni Mmethodisti. Hata hivyo, kwa kuhitimisha sehemu hii, yafaa sote tukumbuke kwamba makanisa hayo mawili, yaani Wabaptisti na Wamethodisti si chochote isipokuwa matawi ya kanisa la Anglikana, kanisa lililoanzishwa na Mfalme Henry VIII wa Uingereza hapo mwaka 1534 baada ya kukasirika kukataliwa na Kanisa Katoliki kumwacha mkewe aliyeshindwa kumzalia  mtoto wa kiume.
WASABATO MITUME WA MATUSI DHIDI YA KANISA LA KWELI
Msomaji wangu bila shaka umeiona historia ya aibu na ya zigzaga ya Wasabato. Wasabato wenyewe huificha sana historia hiyo, hasa kwa wafuasi wao wanaoingia katika kanisa lao putaputa. Hufichwa ukweli kama paka wanaosafirishwa katika gunia. Kwa nini? Wanafichwa ili wasiujue ukweli walikotokea wasije wakajua kwamba wamekosea njia kiimani.
Kifupi, madai yao kwamba Baba Mtakatifu, Kanisa Katoliki au Mfalme Constantino ndio waliobadili Sabato kwenda Jumapili ni mojawapo ya matusi ya Wasabato. Wenyewe wanahubiri hayo kwa jasho jingi kabisa wakati ni kusepetuka kwa uelewa na fichio la aibu yao katika kushindwa kwao katika utabiri wa tarehe ya mwisho wa dunia, tarehe ambayo Yesu  Kristo, Bwana wetu na Maandiko yanatuambia kwamba haitabiri kabisa.  Kwa maneno mengine, ndiyo matawi ya chuki iliyokosewa mwelekeo na uongo wa binadamu dhidi ya wanadamu wenzake.
Tusisahau, kutokana kushindwa hoja na aibu kubwa waliyoipata mbele ya ukweli unaoshikiliwa na kufundishwa na Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki, Wasabato na makanisa mengine wameamua kutumia mbinu ya kujikosha kwa matusi makali.  Wameamua kujitwika utume wa matusi wakati mwingine hata matusi ya nguoni. Kwa vyovyote, Wakatoliki hawana namna rahisi ya kukabiliana na madai hayo ya kimatusi. Usistaajabu haya kufanyika hivi. Kwa mtindo wa vijijini, ukishindwa hoja kwa mtu fulani unaanza kumtukania wazazi wake, nyumba yao na kadhalika.
KUITUNZA SABATO NI KUSHEREKEA MKESHA WA SIKU YA UHURU
Kuitunza Sabato mbele ya Dominika ingelingana na kusherekea mkesha wa siku ya uhuru badala ya siku ya uhuru yenyewe. Taifa litakalofanya hivyo litachekesha na labda litakuwa la watu punguani. Aidha mtu kupita huko na huko kuwahimiza watu washerehekee mkesha wa uhuru badala ya siku ya uhuru wenyewe ingelikuwa sawa na kucheza Ze Comedy.
Nani amegeuka mkondo wa mambo hata kugeukia tena Sabato wakati Wakristo wa kwanza kwa kumwelewa vyema Yesu Kristo walishaitupilia mbali?  Jibu ni wazi. Ni mmoja wa waanzilishi wa dhehebu la Wasabato, yule mama anayejulikana kama nabii. Kwa taarifa yako waanzilishi wa dhehebu la Wasabato ni akina Hiram Edson, Joseph Bates, E.G. Harmon na Hellen White. Katika hawa aliyekuja na moto wa kurudisha Sabato ni huyo mama ambaye alikuwa mke wa E.G. Harmon. Mwanamke huyo anaheshimiwa na Wasabato kama nabii na vitabu vyake , kama vile Vita Kuu, Afya na Raha na Ushindaji, vinasomwa na Wasabato karibu kama misahafu.
WASABATO WASIMNYANYASE YEYOTE
Maono ya uwongo ya Bi Hellen yasiwe sababu ya kuwanyanyasia Wakristo wasio Wasabato. Wala si siri, makanisa yanayofuata mabadiliko yaliyoletwa na Mungu mwenyewe kutoka Sabato kwenda Dominika yananyanyaswa kweli kweli na kauli za Wasabato wanaomfuasa Bi Hellen White. Lakini, hivi unabii wa mama huyo ni wa kweli hata tutishike nao? Hapana, wala si wa kweli. Unabii wa mama huyu lazima tuukatae. Kwa nini tuukatae?
TUHIMIZANE TUMKATAE BI HELLEN NA MAONO YAKE
Ni kwa sababu kuna sababu tatu zinazotuhalalisha tumkatae Bi Hellen White kama nabii. Mosi, kitabu cha Ufunuo kinaonesha kufungwa kwa unabii, yaani kwamba baada ya mambo yaliyoandikwa humo kusingekuwa na ufunuo wowote wa pekee. Ukamilifu wa ufunuo ulitokea katika ujio wa Yesu Kristo. Alichosema yeye ndicho kitu cha kilele. Sasa Bi Hellen anakujaje na mapya kumpikua Yesu Kristo? Tunasoma, “Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi, amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akavichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu, amefanyika bora kupita malaika kwa kadiri jina alilorithi liliyo tukufu kuliko lao” (Ebr 4:1-4).
Si hivyo tu hata mintarafu ufunuo wa zamani mihuri yake imevunjwa na Yesu Kristo mwenyewe, sasa unabii wa Hellen White unaanzia wapi? Tunasoma, “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, Ni nani astahiliye kukifungua kitabu na kuzivunja muhuri zake. Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kikifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.
Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwanakondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja , akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya Mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya wakatakatifu, nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaaa hicho kitabu na kizifungua muhuri zake, kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme wa makuhani, kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchi” (Ufu 5:1-10).
Mintarafu kusasambua ovyo ufunuo wa Mungu, mwandishi wa kitabu cha Ufunuo alishakatazwa, sasa Bi Hellen White anapata wapi nguvu ya kuja na ufunuo mpya? Kuhusu marufuku hiyo tunasoma, “Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike” (Ufu 10:4). Hatimaye, maneno ya ufunuo yaliachwa wazi bila muhuri kwa vile yalivyokuwa njiani kutimia. Juu ya jambo hili, tunasoma hivi: “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki kwa maana wakati huo umekaribia” (Ufu 22:10). Sasa Bi Hellen White anaongezaje maneno ya ufunuo mpya?
Pili, tuukatae unabii wake kwa vile zile anazoziita njozi, kama elfu mbili hivi, ni batili kwani zinaonesha jinsi alivyojaa chuki kwa Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki nasi tunajua kwamba si kazi ya Mungu Roho Mtakatifu kumjaza mtu chuki kali hivyo dhidi ya mwanadamu mwingine. Kazi hiyo hufanywa na Shetani nayo huonesha kwamba moyo wa mtu umejaa uovu kwani kilichomjaa mtu moyoni ndicho kimtokacho. Tunasoma, “Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema  katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake”  (rej. Lk 6:43-45). Hakika chuki dhidi ya Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki inatoka katika moyo uliofurika uovu. Na kwa jinsi hii maono yake hayawezi kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Tatu, tuukatae unabii wake kwa sababu mafundisho yake yanaonesha kwamba haijui Biblia. Hoja hii ya tatu nimeshaishuhudia tayari. Nimesema ameota ndoto akaona huko mbinguni kuna hekalu wakati Maandiko yanatakaa jambo kama hilo (rej. tena Ufu 22:22-24). Kisha nimeshashuhudia kwamba kule kusisitiza kwamba Sabato ndiyo amri kuu kunapingana na kile alichotuambia Bwana wetu Yesu Kristo aliyesisitiza kwamba amri kuu ni upendo (rej. tena Mt 22: 34-40).  Naomba itoshe nilivyokuambia nawe uyapuuze maono ya Mrs. Harmon tunayemchambua hapa.
MAJIBU KWA MASHTAKA YA ZIADA
Nikiendelea kidogo, naomba ruksa nijibu mashtaka mawili sambamba wanayotoa Wasabato dhidi ya Wakatoliki: mosi kwamba ndio mnyama yule Shetani aliyejipa jukumu la kubadili majira na pili kwamba Kanisa lenyewe linakiri kufanya hivyo katika Katekisimu zake na katika vitabu vya waandishi fulani fulani wa Kanisa Katoliki.
Mintarafu hoja ya kwanza ni hivi mnyama ni Bi Hellen White aliyethubutu kumpinga Mungu. Mungu aliibadili siku ya Sabato yeye akijipa jukumu la kuirudisha kwa maelezo ya maono yake batili kabisa. Tumeshaonesha jinsi yalivyo batili kwa kadiri ya mizani na darubini ya Maandiko Matakatifu.
Halafu mintarafu hoja ya pili ni hivi Kanisa linajihusisha na mabadiliko hayo si kama ‘mtendaji’ kwani hakuna mkutano mkuu (mtaguso) wowote wa Kanisa Katoliki uliojadili hoja ya Sabato na kuamua kuibadili kwenda Dominika ila kwamba Mungu aliibadilisha Sabato pale alipoanzisha enzi ya Israeli mpya yaani Kanisa.  Natumaini wasomaji wangu hoja hii si ya kitaalamu mno kiasi cha kutonielewa ninachosema. Ninasema hivi Kanisa linajisikia kuhusika na ubadilishaji wa Sabato kwenda Dominika kwa vile Mungu aliufanya kuanzia pale lilipoanza kuwako nalo kwa mamlaka uliyopata kutoka kwa Mungu ikayasimamia na kuyaendeleza mabadiliko hayo.
MALUMBANO SASA YAKOME
Naomba hadi hapa shtaka la kwamba Kanisa Katoliki limebadili majira, yaani kutoka Sabato kwenda Dominika (Jumapili), lififie kabisa. Si unajua kwamba hoja yenyewe hukokotolewa kutoka Dan 7:25 mahali palipoandikwa, “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye Juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye Juu, naye ataazimu kubadili majira na sheria”. 
Kama unavyoisoma sasa, hoja hii haitaji Kanisa Katoliki bali kwa kinyume chake inawataja Wasabato wenyewe. Ndugu zangu Wasabato haliwafahamu jambo hili kwa sababu ndivyo ilivyo, “Jambo usilolifahamu ni sawa na usiku wa giza.” Kwa vipi? Ni hivi, kama Yesu kwa maneno na matendo yake alisema Sabato si lolote na wala si chochote “maana mtu hakuuumbwa kwa ajili ya Sabato”, mtu anayesema Sabato ndiyo yote katika yote ndiye anayeazimu kubadili majira na sheria. Na moja kwa moja mtu huyo anakuwa ndiye mpinga Kristo kwa sababu anapingana na kauli ya Kristo mwenyewe. Hilo ndilo alilofanya nabii Hellen na kuwasadikisha maelfu ya watu kauli yake kengeufu.
Aidha, kama Yesu alisema kwamba amri kuu ni upendo (rej. Mt 22:37) na akataka iwatambulishe wafuasi wake popote watakapokuwa (rej. Yn 13:35), anapokuja nabii Hellen na kusema eti amri kuu ni Sabato ni upinga Kristo wa wazi wazi na kumfuasa mpinga Kristo kama huyo ni kuwa wapinga Kristo wadogo wadogo nyuma ya huyo mkubwa. Ona ushuhuda wa Maandiko Matakatifu. Bila shaka, hata wewe unakumbuka Yesu aliulizwa swali juu ya amri ya kwanza na kuu naye akatoa jibu mwafaka hata wasomi na walimu wa enzi zake wakamvulia kofia.
Tunasoma, “Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu: Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii” na wakati akiwaaga wanafunzi wake jioni iliyotangulia kifo chake alisema na kuagiza, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn 13:35). Sasa Nabii Hellen anathubutuje kusema kinyume cha maneno hayo ya Kristo ambaye tumepewa tumsikilize? Kama huo si upinga Kristo wenyewe ni nini tena? Hukumu mwenyewe; wewe ni mtu mzima. Hivi wewe na mimi na sisi sote hatukumbuki maneno ya Maandiko Matakatifu, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye” (Mk 9:7)? Na kwa upande wetu, kwa nini, tunamsikiliza binadamu tena? “Tumechanganyikiwa” au “tumerogwa”?
UCHAMBUZI WA KISAIKOLOJIA WA WALIOHUSIKA NA HISTORIA HII YA AIBU
Jina Ugonjwa Tunaoweza Kumtuhumu Upinga Kristo Wake Ulipo
William Miller Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kujaribu kuitaja tarehe ya mwisho wa dunia Kukokotoa tarehe ya mwisho wa dunia kinyume na Mk 13:32.
Samwel Snow Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kujaribu kuitaja tarehe ya mwisho wa dunia Kukokotoa tarehe ya mwisho wa dunia kinyume na Mk 13:32.
Hiram Edson Schizophrenia – kuona hekalu ambalo halipo mbinguni na kudai mwisho wa ulimwengu umeshatokea.  Kuota ndoto ya kuliona hekalu mbinguni ni kinyume cha Ufu 21:22-23.
Joseph Bates Megalomania – kujidai kujua kuliko Yesu Kristo kwa kuunga mkono uongo kwamba mwisho wa ulimwengu umeshatokea. Kuidharau Jumapili, siku aliyoitumia Bwana kufanya mambo yote makubwa.
Hellen White Schizophrenia – kuona hekalu ambalo halipo  Kuota ndoto ya kuliona hekalu mbinguni ni kinyume cha Ufu 21:22-23 na kudai Sabato ndiyo amri kuu kinyume na Mt 22:34-40.

MASWALI NA MASHTAKA 12 MAARUFU YA WASABATO KWA WAKATOLIKI
i. Sabato ndiyo siku ya kuabudu iliyoamriwa. Wakatoliki ndio walioifuta Sabato na kuweka Jumapili.
ii. Wakatoliki wanafuata mapokeo ya binadamu, hawajui na wala hawafuati Maandiko Matakatifu.
iii. Baba Mtakatifu ndiye mnyama yule anayewakilishwa na namba 666. Namba hiyo imeandikwa kwenye kofia na mavazi yake.
iv. Wakatoliki wameifuta amri ya pili ya Mungu. Wamefanya hivyo ili waabudu sanamu.
v. Wakatoliki wanaabudu sanamu. Tazama sanamu makanisani mwao!
vi. Kwa nini Wakatoliki wanakunywa pombe wakati imekatazwa kwenye Biblia?
vii. Wakatoliki wanamwabudu Bikira Maria. Kwa nini wanamfanyia heshima kubwa isivyostahili?
viii. Je, Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo?
ix. Kanisa Katoliki linafanya makosa kuwatangaza wanadamu kuwa watakatifu. Mwanadamu ana uwezo gani wa kumtangaza mtu mwingine kuwa mtakatifu?
x. Wakatoliki wana sakramenti saba. Wana makosa kwa sababu hazijaandikwa kwenye Biblia.
xi. Kuungama ni kwa Mungu moja kwa moja. Kuna uhalali gani kwenda kuungama kwa mapadri wakati wenyewe wana dhambi?
xii. Wakatoliki wana hatia kubwa kwa sababu hawataki kuokoka. Kwa nini Wakatoliki ni wabishi hivyo?

Ndugu yangu Mkatoliki jaribu kuwa na majibu ya maswali haya, hutahangaishwa na Wasabato wowote katika imani yako na maisha yako yote. Kumbe, usipokuwa nayo siku zote utayumbishwa kama wimbi la baharini wakati ulipaswa kutulia tuli kama maji kwenye mtungi.
HATIMA: TUSIHANGAISHANE TENA JUU YA SABATO KWANI  ILIKUWA KIVULI TU
Kwa sasa Wakatoliki wote tuhitimisha fikra zetu kwa nukuu hii: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni KIVULI cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17).
Ndugu zanguni, kama inavyosomeka katika aya hizi, Sabato ilikuwa kivuli na kivuli hakishonewi suti. Sisi ni watu wazima tuachane na Sabato. Nina hakika tutaadhibiwa na Mungu kwa hatia ya kukipa hadhi kitu kisicho na uzito wa kimani.
Imeandikwa na
Pd. Titus Amigu (2016)

SWALI SI NANI KAIBADILI SABATO ISIPOKUWA NANI KAIRUDISHA
Vijana tumepafikia mahali patamu katika mada ya aibu ya Sabato. Mimi nilipataka hapo hapo. Sasa macho yenu yamefumbuliwa. Mpewa ushahidi wa kigeugeu cha wanaojinasibu kujua Biblia. Mnajionea wenyewe, linapokuja suala la Sabato, wale wale wanaojidai kunukuu Biblia kwa ushahidi wa kila kitu, pasipo haya, huiruka na kwenda kuwanukuu wanadamu. Kwa ajili ya swali la sabato watakwenda kunukuliwa Mfalme Konstantiono, au Kardinali fulani, au Papa fulani, au katekisimu fulani au kitabu fulani cha Kanisa Katoliki.
Leo Biblia imewekwa pembeni kabisa. Mnaona hapa ametajwa kardinali mmoja, mihadhara na katekisimu. Ndiyo hivyo haikuguswa Biblia isipokuwa Cardinal James Gibbons (1978); Catholic Priest T. Enright CSSR, Lecture at Hartford; Catholic Records (September 1, 1923), Ferraris Roman Catholic Prompta Bibliotheca, Vol. VI; Catholic American Sentinel (1893) na The Convert’s Cathechism of Catholic Doctrine (1957). Sina hakika kama maandishi haya wanayajua na wamesoma kweli. Nina mashaka hivi kweli « Umombo » unatosha kusomea maandishi hayo? Wamesoma au wamesomewa. Na sijui hata kama wanayo.  Mimi sijui.
Biblia imewekwa kando kabisa. Sana sana kama ni Maandiko, mtaona watakapotoa utetezi wa ziada, watakwenda kunukuu Agano la Kale na kukwepa nukuu za Agano Jipya. Watanukuu Agano la Kale utadhani wao ni Wayahudi. Kumbe, hiyo ndiyo njia ya mwongo inavyokwenda. Ni fupi kama mkia wa mbuzi. Watakwenda mbele na kurudi nyuma wakati huo huo, kwa kuwa hawatakuwa na pakushikia. Watakuwa wameleweshwa na hadithi za binadamu tu, akina William Miller, Samwel Snow, Hiram Edson, Joseph Bates na Ellen White. Vijana msizugike. Wanaowasumbueni wala hawafuati Maandiko isipokuwa hadithi na ndoto za hao watano niliowataja kwa majina.
Kumbe, Wakristo tuache masihara. Tuache kuruka tikitaka hivi. Leo ni leo naomba tubaki kwenye Biblia. Katika suala la Sabato, asisingiziwe mtu yeyote. Mungu mwenyewe ndiye aliyeifuta Sabato. Nukta. Soma Biblia katika sehemu tano zifuatazo, zinatosha kabisa: Isa 1: 13, Hos 2 :11, Ebr 4: 4-10,  Kol 2: 16-17 na Rum 14: 1-10. Naomba uzisome kwa mfululizo huu huu, utabaini ninachosema. Tafadhali usirukeruke.
Basi, kwa aya hizo, swali tunaloulizwa Wakatoliki ni batili. Eti tunaulizwa « Nani kabadili siku ya sabato kwenda Dominika au Jumapili? » Si hivyo. Mtu akisoma kweli Biblia, swali halisi ni: « Nani kairudisha Sabato? » Kitu kilitupwa nani kakiokota tena? Nani kaurudisha mkeka wa zamani?
Sasa kusudi msipate tabu ya kutafuta Biblia kuhakikisha ninayosema nanukuu mwenyewe aya nilizopiga hapo juu.
Kifupi, Isa 1 :13 na Hos 2 :11 zinaeleza kwamba Mungu alichukizwa na Sabato na akaahidi kuifutilia mbali.
Isa 1 :13 inasema: « Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana, ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, SABATO na mikutano ya ibada. Sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. »
Sikieni anavyosema Mungu mwenyewe siyo Mfalme Konstantino, Papa fulani, au Kardinali fulani au katekisimu fulani. Mungu mwenyewe anasema sabato ilikuwa ni ibada isiyo na maana na ibada iliyochanganyika na dhambi.
Hosea 2:11 inasema “Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato na sikukuu zote zilizoamriwa.” Mungu anaahidi kuifutilia mbali na Mungu hasemi uongo. Alifanya kweli.
Ebr 4 :4-10 inaeleza kwamba Sabato ilikuwa kazi bure. Haikutimiza malengo yake na hivyo Mungu anaifuta na kuiweka siku nyingine (ndiyo Dominika – Jumapili -  yaani siku ya Bwana ndiyo siku ya matukio yote makubwa – kufufuka, kuwatokea mitume, Pentekoste na hivyo kuanzisha Kanisa. Tusome: “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuiogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanyikana na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile: Kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu.
Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingalinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi yake. Basi,  na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano huo huo wa kuasi.”
Kol 2 :16-17  inaeleza kwamba Sabato ilikuwa kivuli na sote tunajua kivuli huwezi kukishonea suti labda uwe umekunwa « viroba ». Tusome: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.
Rum 14 :1-10 inasema mtu anayeililia Sabato ana imani dhaifu naye ni mtu wa kuhurumiwa tu. Tumeagizwa tusibishane naye, isipokuwa tuachane naye tu. Tusome: “ Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye kuhusu mawazo yake binafsi. Watu huhitilafiana mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kita kitu naye ambaye hula mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu maana Mungu anamkubali.
Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku; mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe, je! mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.”
SASA TWENDE KATIKA VINAGANAGA
SWALI: JE, NANI KAIRUDISHA SABATO KWISHA KUFUTWA NA MUNGU?
Mashtaka: Wakatoliki wote na viongozi wao hasa Papa  wameibadili Sabato kwenda Dominika (Jumapili). Mfalme Konstantino pia ndiye hasa  aliyeyafanya mabadiliko hayo na hivyo, kwa vyovyote, ni binadamu  na siyo Mungu  aliyefanya mabadiliko hayo. Kwa hali hiyo Wakatoliki wanafuata mapokeo ya wanadamu!
Jibu fupi: Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalifanywa na Mungu mwenyewe na mwisho wenyewe umetangazwa mara nne katika Biblia. Zizome sehemu hizo kama zinavyofuatana hapa: Hos 2:11, Ebr 4:4-10, Rum 14:4-10 na Kol 2:16-17. Kwa kifupi kabisa, Biblia inasema Mungu mwenyewe ndiye aliyebadili. Kilichotokea ni aibu tu, yaani waasisi wa Kanisa la Sabato kuirudisha sabato ambayo ilishatupwa na Mungu na Wakristo wa kwanza wakaanza kuitumia siku mpya, ndiyo Jumapili. Lakini bahati mbaya na kiroja cha mwaka ni kwamba Wasabato hawawaruhusu watu kuijua historia ya kurudishwa kwa sabato kwa mbinu mbili. Mosi ni kwa mbinu ya kukatazwa vitabu vya historia vinavyoelezea mkasa na aibu hiyo na pili kwa kufanya juhudi kubwa ya kulitukana Kanisa Katoliki ili watu wasiwe na muda wa kulitazama na kulihoji Kanisa la Sabato. Lakini, basi katika kijitabu hiki mimi ninajitolea kukufunulia aibu hiyo. Makinika nami.
Jibu refu: Mabadiliko Yalitabiriwa, Yalitangazwa, Yalifanywa na Yalitekelezwa
Biblia ipo wazi kabisa kuhusu mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili). Tufuatane.
Mosi, mabadiliko hayo yalitabiriwa na Hosea (rej. Hos 2:11-13). Yeye alitabiri akisema, “Tena nitaikomesha furaha yake yote na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi na sabato zake na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.” 
Pili, mabadiliko hayo yalifafanuliwa kwa maneno na matendo ya Yesu Kristo (rej. vifungu mbalimbali vya Injili, hususan, Mt 12:1-12, Mk 3:2-4, Lk 13:14-16, 14:1-5, Yn 9:16). Hata hivyo, Yesu hakueleweka wala kuaminika kutokana na fikra mgando za watu wa wakati ule, wakiwamo hata mitume wake mwenyewe.
Tatu, mabadiliko yametangazwa katika Ebr 4:4-10. Hapa tunasoma hivi, “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuiogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanyikana na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile: Kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu.
Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingalinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi yake. Basi,  na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano huo huo wa kuasi.”
Nne, Sabato imebainishwa kuwa ilikuwa kivuli tu Kol 2:16. Hapa tunasoma hivi, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.
Na hatimaye siku zote zimetangazwa katika Rum 14: 4-10 kuwa sawa mbele ya Mungu mwenyewe na kwamba anayegombea kutambuliwe tofauti ni mtu mwenye imani dhaifu, anayehitaji kuhurumiwa. Hapo tunasoma ifuatavyo tokea aya ya kwanza: “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku; mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe, je! mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.”
Hiyo ndiyo Barua kwa Waebrania, barua ambayo inatangaza vifo vya vitu vingi. Mambo mengi yalipinduliwa hivyo na Mungu mwenyewe. Hebu nikuorodheshea kidogo mambo yanayosimuliwa na Barua kwa Waebrania kwamba yalikufa kwa kusudi ya kuyapisha mambo mapya muhimu ya Agano Jipya. Inasimulia kwamba hekalu la Yerusalemu lilikufa kulipisha hekalu la kweli, yaani makazi ya Mungu mwenyewe mbinguni; ukuhani wa Kiyahudi ulikufa kuupisha ukuhani mkamilifu na wa milele wa Yesu Kristo pamoja na watu wote wanaobatizwa katika jina lake na sadaka za Kiyahudi zilikufa kuipisha sadaka timilifu ya Yesu Kristo msalabani. Kumbe ni katika tangazo hili la kifo, kitabu cha Ufunuo kinapotangaza kwamba Sabato iliuawa kuipisha Siku ya Bwana, yaani Jumapili.
Bila shaka Maandiko Matakatifu haya yanakukonga roho na kukubainishia kwamba mabadiliko yalifanya na Mungu mwenyewe. Tazama, tumesoma kwamba Mungu mwenyewe alimtabirisha Nabii Hosea mabadiliko aliyoyakusudia kutoka Sabato kwenda Jumapili yaani Dominika. Halafu, tumezitaja nukuu nyingi za Injili zinazomwonesha Yesu akiyaeleza mabadiliko hayo, ijapokuwa Wayahudi hawakumwelewa vilivyo. Kumbe baada ya kifo cha Yesu, mabadiliko hayo yalifanyika pale mitume wa Yesu walipopambazukiwa akilini mwao.
Hata hivyo, haikuwa wote walioelewa suala hilo, wengine wakawa bado wanaililia Sabato hiyo. Kufuatia kituko hicho, mwandishi wa Barua kwa Waebrania akawaandikia wazi wazi wazi habari hiyo (Ebr 4:1-10) naye Paulo akakizima kilio cha wasiokubali mabadiliko katika Rum 14:4-10 na kuwatawanyisha wapigakelele waliokuwa wakiwahangaisha wenzao juu ya Sabato na sikukuu zingine za kiyahudi kwa maneno murua yaliyomo katika Kol 2:16-17.
Mungu Mwenyewe Aliikataa Sabato na Mabadiliko Yake Yalitabiriwa
Sasa hebu tujipatie muda wa kuliweka jibu hili kirefu. Tufuatane kwa utulivu sasa. Awali ya yote, Biblia inaonesha kwamba Mungu alishamfanya Hosea ayatabiri mabadiliko hayo. Hosea 2:11 inasomeka wazi wazi kabisa: “Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato na sikukuu zote zilizoamriwa”. Neno Sabato katika Kiebrania “shabat” linamaanisha “kupumzika”. Kwa wayahudi siku hiyo ilikuwa siku ya Bwana wa huruma na walipaswa kuiweka wakfu kwake (rej. Law 23:3). Katika siku hiyo walimheshimu Mungu (rej. Mt 12:5, Yn 7:23) kwa kumtolea sadaka, kusali na kupumzika kazi kabisa (rej. Isa 56:2, 58:13-14).
Kama kivuli cha mapumziko halisi yatakayopatikana mbinguni kwa njia ya kifo na ufufuko wa Yesu Krsto, Mungu aliwawekea wayahudi Sabato kusudi wajipatie picha ya mambo halisi yajayo mbele yao. Ndipo alipowapa sababu za kujifunza kupumzika kama mazoezi ya maonjo ya mapumziko halisi. Sababu alizowapa zilikuwa tatu: kwanza kwamba wamwige Yeye mwenyewe aliyepumzika baada ya kukamilisha kazi ya kuumba ulimwengu pamoja na vitu na watu waliomo ndani yake (rej. Kut 20:8-11), pili kwamba Sabato ni ishara ya Mungu kwa wayahudi kwamba yeye ndiye aliyewatakasa na kuwafanya taifa lake teule (rej. Kut 31:13-18, Eze 20:20) na tatu waishike kama kumbukumbu ya kukombolewa kwao kutoka Misri (rej. Kum 5:11-15).
Kumbe kadiri Wayahudi walivyojaribu kuishika Sabato, kusudi kukwepa adhabu zilizotangazwa dhidi ya kuifuja Sabato, walizidisha ugumu. Walimu wa dini na waandishi waliifafanua amri ya Sabato na kuunga vipengele vingi sana hata ikawa ni mzigo mzito kwa watu. Aina thelathini na tisa za kazi zilikatazwa kufanywa katika siku ya Sabato, kati yake zikiwamo kazi za kuvuna, kuwinda, kuchuna ngozi, kufuta herufi mbili, kuandika herufi mbili, kuchoma mkaa, kupika, kutembea zaidi ya mwendo wa Sabato, kuponya magonjwa yasiyo ya dharura na kadhalika. Mambo yaliyokatazwa yalikuwa mengi sana na vipengele vidogo vidogo vikaongezeka hata amri yenyewe ikatisha kama miiba ya nungunungu. Zaidi ya hayo, zikawekwa Sabato chungu mzima, kama vile Sabato za ardhi, Sabato za miaka ndiyo jubilei mbali mbali na kadhalika (rej. Law 25:1 – 26:46).
Kwa mtindo huu wa mambo, ikadhihirika wazi kwamba mtu alikuwa anawajibika kwa Sabato kana kwamba aliumbwa kwa ajili hiyo, wakati Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu apate kustarehe na hivyo kujionjesha Sabato ya kweli itakayokuja mwishoni mwa historia.  Kifupi, kiutendaji, mtu aligeuzwa mtumwa kwa Sabato, starehe ikakosekana kukabaki mashaka na wasiwasi mwingi sana. Wayahudi waliiogopa sana Sabato, si hasa kwa sababu ya kumpenda na kumtii Mungu isipokuwa kwa sababu ya adhabu zake, hasa kuangamizwa kwa Yerusalemu na kupelekwa utumwani (rej. Yer 17:19-27, Eze 20:20-24).
Mabadiliko Yalitangazwa na Yesu Kristo
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalifafanuliwa kirefu kwa maneno na matendo ya Yesu Kristo (rej. sehemu mbalimbali za Injili). Mungu alipowaona wayahudi wakihangaika na Sabato akazidi kuchanua katika nia yake ya kuifuta. Ndipo, Bwana wetu Yesu Kristo, alipokuja akawaelimisha watu kwamba binadamu hakuumbwa mtumwa wa Sabato hata kidogo. Badala yake, Yesu Kristo, aliwaelimisha wote, kwa maneno na matendo yake kwamba Yeye alikuwa ni Bwana wa Sabato na hivyo, kwa mamlaka hayo na kwa utume wake aliopewa na Baba, anawaalika watu kutenda mema badala ya kujiumiza kwa wasi wasi wa kuivunja Sabato na hivyo labda kuadhibiwa na Mungu (rej. Mk 2:27f).
Yesu alijitangaza kuwa Mungu mwenye mamlaka ya kuibadili hiyo Sabato kwa sababu aliiweka yeye mwenyewe. Na hiyo ni kawaida na mantiki, aliyeitunga sheria ndiye anayeweza kuitangua. Yesu aliwaambia Wayahudi, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwandamu kwa ajili ya Sabato, Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia” (Mk 2:27f). Japokuwa Yesu alitangaza jambo hili, Wayahudi hawakumwelewa hata kidogo na kwa namna hiyo walimlalamkia yeye na wafuasi wake ambao kutokana na kumwelewa mwalimu wao walishaanza kuonesha dalili za kutoitilia maanani Sabato kwa mtindo wa kiyahudi (rej. Mt 12:1-12, 3:2-4, Lk 13:14-16, 14:1-5, Yn 9:16).
Hatimaye, Yesu alihitimisha mabadiliko yenyewe kwa kukamilisha matendo ya ukombozi katika siku ya kwanza ya juma (kwa hesabu za kiyahudi), ndio Jumapili au siku ya Bwana. Siku hiyo alifufuka katika wafu kwa utukufu mkuu. Kumbe hapo hapo, ukiangalia nyuma, utaona kumbe ilikuwa siku kama hiyo Mungu alipoumba ulimwengu kwa Neno, hii maana yake kwa ufufuko wake, Yesu aliye Neno, Mungu anaumba upya ulimwengu. Na tena siku ya namna hiyo hiyo, ndiyo atakayoitumia huko mbele kuwatokea wafuasi wake na hatimaye kuwaletea Roho Mtakatifu atakayelizindua Taifa jipya la Mungu, yaani Kanisa. Basi Pentekoste ikawa pia Jumapili. Kwa haya yote, Jumapili ikatekwa yote na Bwana na ndipo kifupi ikawa SIKU YA BWANA, kwa vile jinsi kila jambo kuu la Bwana, alivyokuwa akilifanya siku hiyo. Basi kwa Kilatini SIKU YA BWANA ndiyo DOMINIKA. Kwa hali hii basi akadhihirisha kwamba Yeye, aliyekuwa akisubiriwa ameshafika na yote yaliyokuwa yakifanyika na wayahudi, sikukuu za mwezi na hata Sabato yalikuwa ni vivuli tu (rej. Kol 2:16-17).
Juhudi hizi za Yesu hazikuzaa matunda mara moja. Kumbe, elimu aliyotoa Yesu Kristo kuhusu Sabato, kwa maneno na matendo tunayoyaorodhesha hapa, haikuingia kabisa vichwani mwa wayahudi na hata wafuasi wake walisitasita kuipokea. Kwa kisa hicho, baada ya Yesu kupaa mbinguni, wayahudi waliendelea kuishika Sabato na kukusanyika kwa ibada katika siku hiyo. Basi Mtume Paulo alipotaka kuwakuta Wayahudi wamekusanyika kwa wingi pamoja aliwatafuta katika siku ya Sabato (rej. Mdo 13:14,  42, 44, 16:13, 17:2, 18:4), kwa Wakristo alijua ilikuwa siku ya Dominika (rej. Mdo 20:7).  Hata hivyo, kiujumla, kwa sababu ya uzito na woga wa kubandukana na siku waliyoizoea kusudi kuifuata siku mpya, wafuasi wa Yesu walikuwa njia panda na hivyo wakawa wanahudhuria Sabato pamoja na wayahudi wote na SIKU YA BWANA ilipofika wakawa wanajikusanya peke yao ili kusali, kusoma maandishi yao (ndiyo yaliyogeuka baadaye Agano Jipya) na kuumega mkate (rej. Mdo 20:7).
Mabadiliko Yalitekelezwa na Wafuasi wa Yesu
Kitendo cha wafuasi wa Yesu kusali huku na huku, Sabato na Wayahudi na Dominika peke yao, hakikuchukua muda mrefu kubainika. Wakuu wa wayahudi waling’amua kwamba kuna wayahudi wenye tabia za pande mbili. Wanajiunga na ibada za wayahudi na kishapo siku ya pili yake wanasali peke yao, wakisoma maandishi yao na kumega mkate huku wakimkiri Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu na mkombozi wa wanadamu. Ndipo walipotunga ombi la kumi na mbili na kulitia kati ya sala yao ya maombi kumi na nane (tefillah), sala iliyokuwa ikisaliwa kila Sabato na wayahudi wote katika mwendo wao wa ibada.
Ombi la kumi na mbili halikuwa ombi, bali sala ya kulaani waasi wa dini na hivyo wakiwamo ndani yake Wakristo. Ombi hilo lilisema: “Kusiwe na tumaini kwa waasi wa dini na uung’oe kwa haraka utawala wenye kiburi (dola ya kirumi) katika siku zetu. Wanazareni (Wayahudi Wakristo) na ‘minim’ (Wayahudi wazushi) wafe mara moja; wafutwe kwenye kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki”. Mwisho mwa ombi hili, kama ilivyotakiwa kwa kila ombi, watu waliokusanyika kwa ibada iliwapasa kuitikia, “Utukuzwe wewe, Bwana unayenyenyekesha kiburi”.
Kwa kweli, kwa ombi hili au laana hii, Roho Mtakatifu, mfariji na mkumbushaji wa mafundisho ya Yesu, aliwakumbusha wafuasi wa Yesu kwamba Bwana wao alishawawekea siku mpya, yaani ile SIKU YAKE, ndiyo siku ya kwanza ya juma. Siku hiyo ilikuwa njema na bora kwa kila hali kwani ilikuwa ni siku ya ufufuko wa Bwana mwenyewe, siku ya kuimarishwa kwao na Roho Mtakatifu na kuzaliwa Kanisa la Kristo (Pentekoste), siku aliyoitumia Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya ufufuko wake na hata, kihistoria, siku Mungu alipoanza kuumba ulimwengu. Na mathali, Pasaka au ufufuko wa Bwana ni uumbaji mpya wa ulimwengu, siku ya kwanza ya juma ilikuwa kama siku mambo yalipoumbwa upya. Kwa sifa hizo zote, Wakristo wa mwanzo waligundua haja na uhalali wa kuhamia siku mpya na kuiadhimishwa kwa Bwana.
Basi Wakristo, mara wakaacha kabisa kuhudhuria ibada za Sabato, wakawa tangu wakati huo wanakusanyika Dominika tu.  Hivyo akitafutwa mtu aliyeanza kuiacha Sabato turudi hadi kwa mitume katika karne ile ile ya kwanza. Kwa nini walifanya hivyo? Walifanya hivyo kwa sababu walimwelewa vizuri Kristo kwamba busara inadai usishonee kiraka kipya kwenye nguo ya zamani na wala usitie divai mpya kwenye viriba vya zamani. Hayo aliyasema Yesu alipokuwa akiwaeleza Wayahudi kwamba mafundisho yake mapya hayaoani na desturi zao za kale. Alisema, “Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote” (rej. Mt 9:16-17).
Kifupi, wanafunzi wa kwanza wa Yesu, ndio mitume na wafuasi wengine, walioanza, kimatendo, kuachana na Sabato. Tena hayo yanashuhudiwa hata na maandishi ya kale pia. Mtakatifu Ignasio wa Antiokia, mtu ambaye alimfuatia Mtume Petro kama kiongozi wa jumuiya hiyo ya mahali maarufu sana, mahali ambapo jina  “Wakristo” lilianza pia kutumika (rej. Mdo 11:26), alipokuwa akienda kuuawa huko Roma aliandika barua saba za mafundisho na mawaidha muruwa kwa Wakristo. Kati ya barua hizo, ile iliyoelekezwa kwa wamagnesia, inasema wazi juu ya mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika. Ameandika hivi, “Watu (yaani Wakristo) ambao hapo awali walifuata mfumo wa kale wamefika kwenye tumaini jipya. Hawaifuati tena Sabato kwa sababu wanaweka kitovu cha maisha yao katika Siku ya Bwana, ambapo Yeye na kifo chake kilitupatia uhai” (rej. namba 6-9). Na kisha kuhusiana na Wakristo kung’ang’ania mambo ya kiyahudi anaendelea kusema, “Ni upumbavu kuwa na Yesu midomoni na wakati huo huo kufuata mila za kiyahudi” (rej. namba 10-15).
Wengine Walibaki Kuililia Sabato ya Kale
Hata hivyo, kuachana na Sabato hakukupokeleka na Wakristo wote. Ndiyo kisa basi Mtume Paulo na watu wengine waliomwelewa na kumwamini Yesu pasipo mashaka, hawakuacha kuwaelewesha Wakristo kuhusu mabadiliko hayo, asili yake na sababu zake na kwamba kama Wakristo hawakupasika kubabaishwa tena kuhusu sikukuu za kiyahudi na Sabato (rej.  Mdo 20:7, Kol 2:16, Rum 14: 4-10).
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yametangazwa katika Ebr 4:1-10. Mwandishi wa Barua  kwa Waebrania, alijihusisha na kuwaelewesha Wakristo juu ya mabadiliko ya siku kutoka Sabato kwenda Dominika au Jumapili. Ndipo alipowafafanulia kwamba Mungu alishaifuta Sabato na kuitangaza siku nyingine, ndiyo Dominika. Na sababu ya Mungu kuifuta Sabato ilikuwa moja tu, ilishindwa kuwaelekeza watu kwenye kusudio la kuwekwa kwake. Badala ya kuwaelekeza watu kwenye raha ya milele, iliwatia watu hofu na usumbufu mwingi tu. Kuhakikisha haya soma vizuri Ebr 4:1-10.
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalisubiriwa hata kimantiki kwa sababu Sabato yenyewe iliwekwa kama kivuli tu (rej. Kol 2:16). Mtume Paulo au mwandishi wa Barua kwa Wakolosai,  awaye ye yote yule, aliingia naye katika shauri hilo hilo la mahangaiko ya watu na mambo ya kiyahudi. Barua kwa Wakolosai inasema na kusisitiza kusudi kila mkristo afahamu wazi wazi kwamba sikukuu za kiyahudi pamoja na sabato vyote vilikuwa vivuli. Yesu alipofika, ukawa mwisho wa vitu hivyo na hivyo mtu asijaribu kuwababaisha Wakristo kwa kuwadai warejee huku kwenye mambo ya kiyahudi (rej. Kol 2:16-17).
Sabato Isivyo Chochote Kijiografia
Nadhani hatukupoteza muda daarasani tukisoma Jiografia. Somo hilo nalo linatufumbulia aibu ya Sabato. Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) ni pia mapinduzi ya uelewa mpevu kwa vile, mbele ya Mungu, siku zote ni sawa. Mungu ni mmoja na siku si jambo la kwake. Hivyo, ni wanadamu katika ufupi wao wa uhai wanaohangaika na siku, majuma, miezi, miaka, miongo, karne na milenia. Kwa Bwana miaka mingi ni kama siku moja tu na siku moja ni kama miaka mingi (rej. 2Pet 3: 8).
Basi kwa ukweli huu, siku yoyote inaweza kuadhimishwa kwani inaadhimishwa kwa Bwana na wala si kwa siku kama siku (rej. Rum 14: 4-10). Biblia, ni kitabu kilichoandikwa kwa uvuvio na si utunzi wa akili za waandishi tu. Hilo linadhihirika pia kwenye suala hili hili la Sabato. Kumbe Mtume Paulo alisemeshwa kinabii na Roho Mtakatifu atufunulie jambo lingelilojulikana vyema baadaye kwa kukua kwa elimu ya jiografia na kosmolojia. Mtume Paulo katika Rum 14:4-10 alisemeshwa atuambie tuache mabishano juu ya Sabato, kwa sababu, mbele ya Bwana, siku zote ni sawa. Jambo hilo kumbe ni kweli kama mtu atajielimisha  katika jiografia.
Kwa kweli, ukijua vizuri Jiografia huwezi kujisumbua na kuing’ang’ania siku inayoitwa Sabato au Jumamosi maana siku hiyo hiyo wakati huo huo mahali pengine ni Jumapili au Jumamosi. Unanibisha? Basi, hujui Jiografia au labda ulikariri tu huko darasani kwako. Ikiwa hivyo, kaa jamvini pako nikujuvye.  Ni hivi, Jiografia inaweka wazi kwamba, kutokana na kusigana kwa dunia kuliona jua, kuna siku mbili duniani. Wanakoliona jua kwanza ndiyo huingia asubuhi na mchana kabla ya kule kuliko na giza bado. Basi, mstari wa kufikirika unaoitwa “mstari wa tarehe wa kimataifa” (international date line) umechorwa sehemu fulani huko pande za New Zealand kuitenga dunia katika siku mbili zake. Ndipo basi, huko mashariki zaidi huwa siku nyingine tofauti na magharibi zaidi. Hivi, mathalani, upande wa mashariki ukiwa ni Jumamosi, upande wa magharibi ni Ijumaa ama mashariki kukiwa ni Jumapili, magharibi ni Jumamosi.  Kumbe kwa Mungu ni siku moja tu, Yeye hana siku za kusigana. Hivyo, kwa ukweli wa kijiografia, hakuna Jumamosi au Sabato iliyo Sabato. Inategemea ulipo, Sabato ile ile inaweza kuwa ni Jumapili au Ijumaa. Hivi, ubishi wa Sabato kama siku kuabudu duniani ni upuuzi mtupu.
Kama hujanielewa hebu nikulete, mara moja, kwenye kitendawili cha kitoto. Ikiwa watu, huku magharibi, watang’ang’ania kwenda kusali Jumamosi, watakuwa wamekwenda kusali siku gani kwani masaa yale yale kwa upande wa magharibi ni bado Ijumaa? Au siku moja baadaye, wengine watakapokwenda kusali waking’ang’ania kuwa Jumapili, wanakuwa wanakwenda kusali siku gani wakati huko magharibi ndiyo Jumamosi? Kumbe siku ni mbili kwa binadamu tunaotegemea kuzipima siku zetu kwa jua. Mbele ya Mungu, asiye na siku, siku yake ni moja ile ile. Kwa hali hiyo, ukweli unakuwa mmoja kwamba, mbele ya Mungu, siku zote ni sawa na hivyo ye yote anayekusudia kuadhimisha siku, aiadhimishe kwa Bwana tu asijisumbue na jina la siku (rej. tena Rum 14:4-10).
Tangu Zamani Wakristo Walikutana Dominika (Jumapili)
Kwa vile Wakristo waligundua kwamba Jumapili, ndiyo iliyokuwa siku yao, walijizoeza kukutana Jumapili kusali, kumsifu Mungu, kutoa sadaka na michango kwa ajili ya wenye dhiki. Kwamba mambo yalikwenda hivyo tunasoma katika Biblia hususan katika 1 Kor  16:1-2. Hapa tunasoma, “Kwa habari ya ile michango kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. Siku ya kwanza ya juma (ndiyo siku ya Bwana, Jumapili) kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.”
Kwa maneno haya, hakuna ubishi kwamba Wakristo walijipatia desturi ya kukutana Jumapili kwa sala na shughuli za pamoja. Na hivi walioing’ang’ania Sabato walikuwa watu wagumu wa kuyapokea mambo mapya, watu ambao hawakosekani katika shughuli na mahali popote duniani.
Kaisari Konstantino Aliipa Nguvu Kawaida Iliyokuwapo
Baada ya Biblia kuweka sawa habari za Sabato namna hiyo, na Wakristo kujasiri kuishika siku ya Bwana badala ya siku muflisi, Sabato, katika miaka ya karne ya nne, alitokea katika historia Kaisari aliyeupenda Ukristo. Yeye alikuwa ni matokeo ya sala za Wakristo kuwaombea viongozi wa dunia wausaidie Ukristo ukue duniani. Kaisari huyo aliitwa Konstantino, aliyetawala tangu 306-337 B.K., aliupatia Ukristo amani kutoka kwenye madhulumu ambayo makaisari wengi walikuwa wakilifanyia Kanisa. Yeye akatangaza rasmi kwamba ile siku inayoshikwa na Wakristo kwa masuala ya sala kwa Mungu wao iwe siku rasmi ya mapumziko kwa watu wote katika dola yake, yaani dola ya kirumi. Ndipo mapumziko ya Dominika yakawa rasmi tangu wakati ule. Hii maana yake ni kwamba Konstantino siye aliyeiunda Dominika na wala siye aliyeanzisha mambo ya ibada yawe katika siku hiyo. Yeye anakuja kuipatia Jumapili nguvu ya kidola tu.
Hapa huanzishwa hoja zisizo na miguu wala mikono.  Wengine humtaja Konstantino au Papa fulani, kama mwanzilishi wa Dominika.  Historia fupi iliyotolewa hapo juu, yaani mintarafu nyakati za Yesu na baadaye wanafunzi wake, ndiyo inayotuonesha kwamba Dominika ilianza kuwa siku ya ibada kwa Wakristo zamani za karne ya kwanza tayari na wala siyo katika karne ya nne. Basi, kichekesho cha kumtaja Konstantino au Papa fulani kama mwanzilishi wa Dominika kinaweza kulingana na kichekesho cha mtu atakayemtaja kiongozi fulani wa leo kama mwanzilishi wa taratibu ya kula au kuvaa kwa binadamu. Itakuwa ni kichekesho cha mwaka kwa sababu watu wamekuwa wakila na kuvaa hata kabla kiongozi huyo hajaliona jua la ulimwengu huu. Ndivyo ilivyo kwa Konstantino, hawezi kuanzisha kitu katika karne ya nne, kitu kilichoanza kabla hajazaliwa mwenyewe katika karne ya kwanza.
HATIMA
Nahitimishia hapo. Kumbe, sasa unganishia ile historia halisi ya kiroja cha kurudishwa kwa sabato walichokifanya akina William Miller, Samwel Snow, Hiram Edson, Joseph Bates na Ellen White kama nilivyowatangulizieni. Umeiona aibu hilo. Mbele ya wasomi na wachambuzi wa mambo hakuna tena mahali pa kufichia uso. Nawashukuruni kwa kuisoma hoja hii ndefu. Asanteni wote. Lakini mkitaka kuchangia msikose kuzisoma kurasa hizi kwa ukamilifu. 
Pd. Titus Amigu

BIBLIA INASEMA KWA UJUMLA NDOTO NI UBATILI (YbS 34:1-8)
Vijana, acheni tuwekane sawa kisayansi na kibiblia kuhusiana na suala la NDOTO. Tusisumbuke nazo mno. Zimeshapoteza maana yake ya kale kwa sababu ya ujio wa Yesu Kristo.
Ni hivi hapo zamani sana ndoto zilikuwa njia maalumu ya ufunuo lakini siyo sasa baada ya Yesu Kristo kukamilisha kazi yake hapa ulimwenguni. Hapo kale sawa, lakini siyo siku hizi. Ndiyo maana kuna ripoti za ndoto zilizowapatia ujumbe watu fulani fulani katika Biblia, yaani Agano la Kale na Agano Jipya. Wakati ule, njia nyingine ya ufunuo ilikuwa maono.
Lakini kwa kufika Kristo, Mwana wa Mungu, ulimwenguni, ufunuo ulifikia kilele na hivyo mambo ya ndoto na maono kutohitajika tena kwa namna ya pekee. Ndiyo maana imeandikwa, ”Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, lakini siku hizi za mwisho amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote, yeye ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akautegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia  wa Mungu Mkuu” (Ebr 1:1-3).
Wenzetu wengi wa mataifa yaliyoendelea wameshaachana na ndoto, kwa namna ya pekee Wayahudi, ndiyo maana wametuacha maili nyingi katika sayansi. Mwamini ndoto hawezi kutafiti mambo ya juu kwa sababu atabaki akijishughulisha na mambo ya maweruweru tu. Wenzetu wamejitahidi kujitoa katika mambo hayo yasiyo na miguu wala vichwa. Kwa nini? Kwa sababu hazina mashiko yoyote.
Kimsingi, tuliobaki tukihangaika na ndoto ni hasa sisi Waafrika. Siku zote, sisi ndio tuliozoea kushikilia walichotupa wenzetu. Sisi tunakuwa wa mwisho kuachana na waliyoachana na wenzetu. Mfano mkubwa ni imani za uchawi. Wenzetu wamejitahidi kuacha, lakini sisi inakuwa kama tumejipa hatimiliki. Kwa kweli, sisi Waafrika tu watu wa chini nasi tunaridhika sana na mambo ya chini, mathalani, laana, imani juu ya uchawi (ushirikina), ndoto na maono. Wakati wenzetu wanatafiti jinsi ya kwenda anga za mbali, sisi tumebaki kuamini na kutishika na mambo ya hapa chini “majini”, panya, mijusi, bundi, mende na kadhalika. Balaa kweli! Wenzetu wamekwenda mwezi na wamepeleka vyombo Mars na Jupiter! Inasikitisha. Siku hizi wenzetu wanafanya utafiti jinsi ya kuwapeleka wanadamu Mars, sisi tunahangaishana juu ya ndoto. Nimesoma leo mtandao mtu akijinasibu kujua zaidi ya Waafrika wenzake. Jambo hili lisivumilike. Ni mchango mbaya wa kudumazana.
Kumbe, sayansi inaweza kutusaidia kueleza ndoto ni nini. Ndugu zanguni, kuota ndoto ni jambo linaloendana na uwezo wa binadamu kulala usingizi. Ni hivi, Mungu ametupatia wanadamu uwezo wa kulala usingizi kwa makusudi ya kupumzisha na kukarabati ubongo wetu.
Kimaumbile na kisayansi, mwanadamu hulala usingizi wa aina mbili kwa kusiganishwa: usingizi mzito na usingizi mwepesi. Mungu ametuumba hivyo na sayansi imegundua hilo (YbS 43:31-33). Basi, tuendapo kulala, kwa kawaida huwa tunalala kwanza usingizi mzito masaa mawili, halafu usingizi mwepesi masaa mawili, kisha usingizi mzito masaa mawili tena na kishapo usingizi mwepesi masaa mawili tena na kadhalika. Mabadilishano haya huweza kufanyika mara tano kulingana na mtu alivyowahi kulala.
Usingizi mzito ni kwa ajili ya ubongo kupumzika na usingizi mwepesi ni kwa ajili ya ubongo kujikarabati. Wakati wa usingizi mzito ubongo hutulia sana. Ni wakati wa usingizi mwepesi ndipo mwanadamu anapoota ndoto. Kila siku, kila mwanadamu huota ndoto isipokuwa huwa tunazisahau. Mwota ndoto huambulia kukumbuka ndoto ya mwisho anayoigutukia.
Sasa sikiliza.  Kwa kuwa mwanadamu huota ndoto wakati wa usingizi mwepesi, huwa anaona kana kwamba jambo analoliota ni “live” wakati sivyo. Kwa kuwa analoliota ni jambo la ndotoni, mwotaji hukosa uwezo wa kuitawala ndoto yake. Hata kama ni ndoto ya kumwona mtu fulani, mwotaji hukosa uwezo wa kumkamata kwa sababu yote si kweli. Mwota ndoto hushindwa kumkamata mtu anayemwona ndotonio kwa sababu, kwanza mtu yule hayupo pale na mwotaji mwenyewe hushindwa kujimudu kwa sababu ya usingizi unaomwendesha.
Twendeni kwenye Biblia. Kwa ujumla ndoto ni upuuzi na kivitendo tunazipuuza. Sasa sijui kwa nini tunazitolea macho. Sikiliza. Eti, ukiota ndoto leo, umepata shilingi milioni moja nawe umekwenda kwa furaha madukani, huko umejinunulia viatu vipya, kofia, kikoi, suti, baiskeli na viroba vitatu vya unga na kubakiza chenji yako mfukoni, unapoamka asubuhi na kujikuta upo nyumbani pako bado na vitu hivyo havipo pale, unakwenda polisi kuripoti kwamba umeibiwa? Bila shaka huendi kuripoti polisi na ukithubutu kwenda kuripoti wizi wa namna hiyo, utaonekana “hamnazo” nawe pasipo ajizi utarudi na ngeu. Au tukiota ndoto tunakula wali kisha tunaamka pasipo kuuona, mbona hatuendi polisi kushtaki kwamba tumeibiwa wali? Ama tukiota ndoto tumepata fedha nyingi kisha tukaamka pasipo kuziona, mbona hatuendi polisi kushtaki kwamba tumeibiwa? Au ukiota ndoto umefika New York na kutumbua raha kule, unapoamka asubuhi na kujikuta upo nyumbani pako bado, unawauliza ndugu zako nani aliyekurudisha toka kwenye? Bila shaka humuulizi mtu habari hiyo kwa sababu unajua ni ndoto tu. Kivitendo hatubwetekei ndoto. Katika uelewa huo, Biblia inatusimanga ikisema,
“MTU MJINGA HUWA NA MATUMAINI YA BURE NA YA UONGO, NDOTO HUMPA MPUMBAVU MABAWA YA KURUKA. KAMA MTU ANAYEJARIBU KUSHIKA KIVULI NA KUFUKUZA UPEPO NDIVYO ALIVYO MTU ANAYEAMINI NDOTO. NDOTO NI KAMA KIOO SURA INAYOUKABILI USO. NI KITU GANI KIWEZACHO KUTAKASWA NA UCHAFU? JE, UKWELI WAWEZA KUPATIKANA KWA UONGO? KUPIGA BAO, RAMLI NA NDOTO NI UPUUZI, AKILI HUWA NA MAWAZO KAMA YA MAMA ANAYEJIFUNGUA. USIZITIE MAANANI NDOTO ISIPOKUWA KAMA ZIMETOKA KWA MUNGU MKUU MAANA NDOTO ZIMEWADANGANYA WENGI NA WOTE WANAOZITUMAINI WAMEAIBISHWA. SHERIA NI KAMILIFU BILA UDANGANYIFU HUO NAYO HEKIMA NI KAMILIFU KWA MTU MWAMINIFU” (YbS 34:1-8). Ndugu zanguni, nukuu hii nimeandika makusudi kwa herufi kubwa kusudi isomeke kirahisi na kusisitiza ukweli wake.
Kwa bahati mbaya, Wakristo wengi wasio Wakatoliki hawana fursa ya kuyajua Maandiko haya ya busara kubwa kwa sababu kwa kuingizwa mkenge na Martin Luther wanatumia Biblia ndogo, yaani Biblia iliyopunguzwa vitabu saba kutoka 73 hadi 66. Huu ndio mkasa aliouanzishwa Martin Luther miaka ile ya 1520. Kwa maoni yake binafsi kabisa akapunguza vitabu vya Biblia asilia kutoka 73 hadi 66 na hivi kujinyima mwenyewe na wafuasi wake neno la Mungu lililo kwenye vitabu vya Tobiti, Yudithi, Hekima ya Sulemani, Yoshua bin Siraki, Baruku, 1 na 2 Makabayo. Jamani huu ulikuwa mkasa wa aina yake!
Kumbe Biblia, kama inavyosomeka katika YbS 34:1-8, ilishatupilia mbali shauri la kuzitilia maanani ndoto, ndiyo maana Yesu hazizungumzii ndoto hata mahali pamoja katika Agano Jipya. Yesu alijijua kwamba yeye ndiye kilele cha ufunuo na hivyo kubwaga chini ndoto na maono. Hivi, kwa ujumla ndoto ni upuuzi mtupu.
Waafrika wengi huwa tunajitahidi kupuuza ndoto kama mzee Yoshua bin Siraki anavyotutaka. Lakini wengine wetu hawana nguvu na ushujaa wa kuzipuuza ndoto, hasa ndoto za majinamizi. Ndoto za majinamizi ni zile za kutisha, mathalani, kuota watu wakikufukuza, wakikutoboa macho, wakikutumbukiza lindini, wakikupiga pasi ya moto mgongoni na kadhalika. Watu hao wakiota ndoto za namna hiyo hushindwa kuzipuuza. Wao ndio kwanza hudhani kuna uchawi kwa sababu ya kujikuta wakiota ndoto za kutisha kama hizo. Husema katika ndoto hizo wameoneshwa wabaya wao “live”, jambo ambalo si kweli. Kifupi, wenzetu hao hushindwa kuzipuuza ndoto za majinamizi kama wanavyojitahidi kuzipuuza ndoto zingine wakati ndoto ni ndoto tu.
Nasisitiza, hizi ni ndoto maalumu tu. Jina la ndoto hizi za kutisha ni majinamizi, kwa Kiingereza “nightmares”, nazo zisichukuliwe kama ushahidi wa uwepo mambo ya “kichawi”. Ndoto za majinamizi ni mapato mengine ya ubongo kufanya kazi kwa fujo kunakotokea mtu akiwa usingizini, yaani mawimbi ya umeme wa mwilini ALPHA, BETA, THETA na DELTA yanapofanya kazi kwa msepetuko. Wakati wa ndoto za majinamizi ni wakati ambapo mambo ya kwenye mtima hujiibusha kwa fujo kutokana labda na kuchoshwa kwa ubongo ama na ugonjwa au kemikali zenye athari. Mawimbi ya mwilini ALPHA, BETA, THETA na DELTA huweza kufanya kazi isivyo kawaida kutokana na kulewa pombe, kulewa madawa ya kulevya, kuumwa malaria inayokimbilia kichwani, kusongwa na mawazo mazito, kutatizwa na matatizo ya ndoa na unyumba, kuchanganywa na matatizo ya jamii na kadhalika.
Kumbe, tunapoteza muda mwingi kuzijali ndoto zisizo na maana yoyote. Naomba makala hii iwaelimishe watu ambao wakiota ndoto za majinamizi wakamwona mtu ambaye kwa kawaida wanamwogopa kama “mchawi” akiwajia na kuwakaba koo au kuwatisha, husema kwamba mtu yule ni mchawi maana aliwajia usiku nao wamemwona “live”. Ndipo kwa kufuata ndoto hiyo humwendea mtu huyo na kutaka kumshambulia kwa ngumi, mateke au silaha. Lakini hiki ni kichekesho, mbona tukiota ndoto tunapinduka kwenye  gari, hatuendi kulishambulia gari lile? Mbona tukiota ndoto tunashambuliwa na simba kwa nini hatuendi porini kumtamfuta simba tumshambulie?
Ndoto hatuwezi kuzizuia kwa sababu hutokewa pasipo sisi kuzitawala. Wakati wa usingizi mwepesi ukishatufikia ndoto zinaweza kuja za rangi yoyote ile. Lakini ukitaka usiote ndoto za majinamizi ya watu wakikudhuru, ishi maisha yenye kuwapendeza watu na wala usiwe unalala na hofu zako kichwani au moyoni (Efe 4:26). Ishi na wote kwa amani na upendo, ndoto zako zitakuwa laini na tamu. Lakini ukiishi katika kisirani, hofu na wasiwasi tegemea kuota ndoto mbaya mbaya. Ni ukweli wa kiutafiti kwamba mtu mwenye msongo wa mawazo huota ndoto mara tatu au mara nne zaidi ya mtu asiyesumbuliwa na msongo wa mawazo.
Kwa taarifa yako, mwili nao hufanya kazi na kupumizika vile vile. Kila jioni na usiku, kati ya saa tatu jioni na saa kumi alfajiri, mwili unapopunguza shughuli zake mbalimbali zikiwamo shughuli za umeng’enyaji. Ndiyo kisa jioni ukila wali sinia moja, kunde  bakuli mbili, parachichi sita, mahindi ya kuchoma manne na kadhalika, ukaenda kulala hivyo, wakati mwili unapunguza shughuli zake, utavimbiwa vibaya. Utavimbiwa kwa sababu shughuli za umeng’enyaji zinapunguzwa huo na hivyo vyakula vyako havitameng’enywa. Ndiyo maana wanadamu hawavimbiwi mchana hata wakila sana.
Lakini mwili unapopunguza shughuli zake si kwamba hufa, la hasha. Wakati mwili unapopunguza shughuli zake usiku shughuli za kisaikolojia huendelea. Mathalani, hofu na hasira zote za mchana huzamwisha katika kutojitambua (subconscious). Hayo yanayomezwa usiku ndiyo yanayokuwa malighafi ya ndoto zetu. Ole wako mwili wako uwe unawameza watu mbalimbali unaowaogopa. Ole wako mwili wako uwe unameza hasira. Nakwambia hao unaowaogopa au unaowafanyia hasira siku moja watatokea katika ndoto zako za majinamizi na kukusumbua kwa vivuli vyao. Wanadamu hao hawatakuwa wachawi, bali picha zao zitakusulubu kwa sababu umefanya uzembe wa kuwameza wakiwa katika hali ya kutisha labda kwa kuzeeka kwao, kwa macho yao mekundu, au kwa vibiongo vyao au kwa mapengo yao ya vinywani na kadhalika. Mfano, watu wakimmeza bibi fulani kwa sura ya kutisha, watamwota mara kwa mara akiwavamia kiasi kwamba watamvumisha kuwa mchawi na hatimaye watu wale wanaweza kufikia katika kumchukulia hatua ya kumcharanga mapanga na kuumuua. Kifupi, watakuwa wamemwonea bure, wakati kosa ni lao wenyewe, yaani kule kummeza katika sura ya kutisha. Ndivyo yanavyowafika madhila ya ajabu ajabu wazee na vikongwe wetu. Mintarafu mwendo huu wa mambo, ushauri wangu wa bure ni kwamba tuwe tunalala kila siku kwa furaha na upendo. Kama Biblia inasema lolote kwako, basi soma tena Efe 4:26-27 uone jinsi Mtume Paulo alivyokushauri usibaki na hasira kutwa nzima.
Tuachane na kuzijali ndoto. Hapo juu tumesoma jinsi mzee Yoshua bin Siraki alivyotuandikia. Katika hayo aliyosema amesema ndoto (hali kadhalika maono) za kutilia maanani ni zile zitokazo kwa Mungu, ambazo kwa kweli lazima ziwe chache kwa vile Yesu Kristo amekamilisha ufunuo. Tunaweza kuzibaini ndoto zitokazo kwa Mungu ikiwa zinatimiza vigezo vitatu vifuatavyo: mosi, kutokea mara kadhaa, pili, kuwapo kwa ujumbe maalumu na tatu ujumbe huo kutopingana na mafundisho ya Kanisa Katoliki pale ujumbe wake unapopimwa kiteolojia, kiimani au kimaadili.
Kwa mujibu wa vigezo hivyo vitatu, usipokee ndoto iliyotokea mara moja tu. Ndoto isiyojirudia ni rahisi kutokana na shida fulani ya mwotaji mwenyewe mathalani ulevi au ugonjwa. Tena usipokee ndoto ambayo haina ujumbe wowote wa maalumu. Ndoto ya kutilia maanani lazima iwe na ujumbe maalumu maana kimsingi ufunuo umeshakamilika katika Yesu Kristo. Ndiyo kisa tumeambiwa tumsikilize yeye tu (Mk 9:7). Hali kadhalika, usipokee ndoto yenye ujumbe unaopingana na mafundisho ya kweli, kwa mfano, kutumwa kuiba, kutumwa kumuua mtu, kutumwa kufanya tendo la ndoa na mtu fulani, kuagizwa kutokwenda kanisani, kuagizwa kuwataja watu  kuwa “wachawi” na kadhalika.
Vivyo hivyo kuhusu maono. Maono kwa ujumla ni ubatili isipokuwa kama yametoka kwa Mungu. Maono yaliyotoka kweli kwa Mungu hutimiza vigezo vitatu tulivyovitajaa hapo juu, la sivyo ni utapeli mtupu. Lakini, watu wengine hujitafutia “ujiko” kwa kutoa “ushuhuda” dhalili wa kutokewa eti na Mungu au watakatifu au marehemu wa kale. Basi, simama kidete usije ukadanganywa na watu waliozoea kuwadanganya wanadamu wenzao kwa kutoa ushuhuda wa maono yasiyokidhi vigezo vyovyote. Wapuuze watu wa namna hiyo. Hivyo wala usipokee kama kweli maono yaliyotokea mara moja tu, ni rahisi maono hayo kutokea kutokana na shida fulani ya mwotaji mwenyewe, mathalani, ulevi au ugonjwa wake wa akili. Hali kadhalika, usipokee maono ambayo hayana ujumbe wowote wa pekee. Nasisitiza, kama ni maoni ya kutilia maanani lazima yawe na ujumbe maalumu maana kimsingi ufunuo umeshakamilika katika Yesu Kristo (Ebr 1:1-3). Kama kweli Mungu atataka kutupatia ufunuo wa ziada kwa mtindo wa ndoto au maono lazima kutakuwa na ujumbe maalumu maana utakuwa tofauti na ufunuo wa Bibliaa, jambo ambalo halina umuhimu wa pekee leo hii.
Nimesema mengi nikiwaasa tuachane na kuzijali ndoto kwani neno la Mungu linatuasa tufanye hivyo (YbS 34:1-8). Hata hivyo sina furaha wala amani. Kinachonitisha na kunisikitisha mimi ni kwamba vijana na wengine wanaojinasibu kuwa “wasomi” wanatudidimiza Waafrika wenzao katika mambo dhalili kama ndoto, laana, imani za uchawi (ushirikina), hofu juu ya majini na hofu juu ya Frimasoni, badala ya kujaribu kutuvusha wenzao katika kudharaulika ambako kumetosha sasa. Yaani badala ya kutusaidia Waafrika wenzao tupate uwezo wa kushindana na watu wa mabara mengine  katika sayansi ndani ya karne hii ya sayansi na teknolojia, wao wanatudidimiza wenzao matopeni. Yana faida gani mafundisho juu ya ndoto, mafundisho juu ya laana, mafundisho juu ya imani za uchawi (ushirikina), mafundisho juu ya majini na hofu juu ya Frimasoni na kadhalika? Hata hivyo, vijana na watu wa aina hiyo wanatuaandikia wenzao “vimakala” na vijitabu koko vikijaribu kutoa tafsiri za ndoto. Ninameviona vikiuzwa na kununuliwa vitabu juu ya ndoto na tafsiri zake. Vitabu vibaya sana hivyo. Ni vitabu vyenye kumtia mtu matumaini feki. Ni kutupotezea muda na kutudumaza. Kuyasoma na kumakinika na maandishi kama hayo ni kujididimiza, sana sana ni kujiongezea hofu na wasiwasi na hatimaye kujikosesha kujiamini. Ni kujifunga pingu kichwani na mikononi. Ni kujikosesha nguvu ya kufikiri na kuyakabili mambo ya dunia hii macho kwa macho. Ndugu zanguni, katika “kupigika” kama huku, kusomeshana mambo ya ndoto ni kutia chumvi kwenye vidonda vyetu wenyewe. Ni kuziba fursa za Waafrika kuchangamkia mambo ya maana zaidi ya karne hii ya ishirini na moja. Kumbe, hata kama kungekuwa na mwanga wa vijana wa Afrika kuchipuka katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia watachinjiwa  baharini tu.
Kwa kumalizia, nawasihi tusome tena na tena masikitiko ya Baba Mtakatifu Benedikto XVII na. 93 anapotusikitikia Waafrika kwa kujifunga wenyewe minyororo ya kutojiamini. Kwa herini vijana!

UFAFANUZI WA MANENO CHRISTMAS NA X-MAS
Mada ile ya NI SAA YA KUJIAMINI ITAENDELEA karibuni. Lakini kwa leo nina jambo moja la kuweka sawa. Vijana kadhaa wameniomba nitoe maelezo kuhusiana na maneno “CHRISTMAS” na “X-MAS” maana wanachanganywa na wenzao. Kifupi, maelezo yanayosambazwa kwenye mitandao yetu ni kwamba “Christmas” ni sahihi na “X-mas” siyo sahihi.  Maelezo haya yanayosambazwa si sahihi, ni ya uongo.
Tukianzia kwenye maneno hayo, kwa karibu kabisa tunarudi kwenye maneno ya lugha ya Kiingereza cha enzi tatu:  Kiingereza cha zamani, Kiingereza cha enzi ya miaka ya kati (karne 5 hadi15) na Kiingereza cha siku hizi.
Kwa Kiingereza cha zamani “Christmas” ilitamkwa “Cristes maesse” na maana yake ilikuwa “Christ’s festival” yaani sikukuu ya Kristo.
“Crist” ndiyo “Christ” ndiyo  Kristo. Kristo maana yake “Mpakwa” ndiyo inayotafsiri jina la Kiebrania (lugha ya Wayahudi)  “Meshiah”, yaani “Mpakwa wa Bwana” . “Meshiah” ndiyo tunayotamka sisi Waswahili kama Masiya au Masiha. 
Neno  “maesse”  maana yake “festival”  yaani sikukuu au sherehe. Katika Kiingereza za enzi ya kati “Cristes maesse” ilinyooshwa na kuwa “Cristemas” ndipo katika Kiingereza cha siku hizi ikafika kutamkwa na kuandikwa “Christmass”.
Yaani hapa tunacheza na maendeleo ya lugha ya Kiingereza katika matamshi na maandishi tu. Hadi hapo nadhani nimeeleweka.
Lakini suala la CHRISTMAS na X-MAS linarudi kwenye lugha ya Agano Jipya ndiyo Kigiriki au Kiyunani. Jina hilo “Crist” au “Christ” limetoholewa kutoka jina “CHRISTOS” ndiyo Kristo (tukifupisha kwa kudondosha “s” ya mwishoni). Walatini (watu wa Dola ya Rumi) wakatamka “CHRISTUS” ndiyo Kristu (tukifupisha kwa kudondosha “s” ya mwishoni). “Christos” maana yake ni Mpakwa, Masiya au Masiha. Masiya au Masiha yenyewe inatoholewa kutoka jina la Kiebrania  “Meshiah” kama nilivyoonesha hapo juu. Waingereza hutohoa “Meshiah” na kuandika na kutamka “Messiah”.
Kumbe katika Kigiriki au Kiyunani, “CHRISTOS” huandikwa kwa herufi ndogo "Χριστός” na kwa herufi kubwa “XPICTOC” au “ΧPIΣTOΣ” au kwa sanaa “XPISTOS”. Katika Kigiriki hiyo “X” siyo “eksi” bali ni “ch” na hiyo “P” siyo “pi” bali “r”.  Hivi kwa Kigiriki “XPI” husomwa “Chri.”
Halafu, kutokana na herufi “X” na “P” kusimama mwanzoni mwa jina “XPISTOS” au "XPICTOC", Wakristo wa mwanzo walizitumia herufi hizo mbili kufupisha jina “CHRISTOS” hivyo wakawa wanaandika wakibebanisha “X” na “P” na kuzaa alama moja maarufu sana mnayozoea kuiona kwenye nguo za misa au vitambaa vya altareni na kwenye vitabu. Ni alama ya “P” iliyokatwa mguuni kwa mstari -- au X.
(Poleni, hapa nashindwa kuichora. Herufi za Kigiriki zinagoma).
Kwa maelezo haya basi, “X-MAS” si neno tofauti na “CHRISTMAS”. Ni neno lile lile isipokuwa badala ya kuandika CHRIST kirefu watu wanafupisha kwa X tu. Ndipo inapotokea X-MAS mahali pa CHRISTMAS. Hivyo hiyo “X” ya mwanzoni haimaanishi “mkasi” wenye maana ya “kukata” au “hakuna” bali “X” yenye kufupisha jina “CHRISTOS”  na “MAS” huko mwishoni kumaanisha “SIKUKUU” au “SHEREHE”.
Kwa hiyo, asiwadanganyeni mtu wala asiwababaisheni mtu kwamba “X-MAS” maana yake “HAKUNA KUSANYIKO LA KRISTO” eti kwa vile “MAS” ni neno la Kigiriki linalomaanisha “MKUSANYIKO”. Hakuna neno la Kigiriki MAS linalomaanisha MKUSANYIKO. Iweni na amani, vijana. Hata mtu akilazimisha maneno ya Kigiriki maneno yote yanayokaribiana na MAS japo kwa maandishi na matamshi hakuna neno lenye maana ya mkusanyoko. Tazama maneno yaliyopo ni “μασάομαι” lenye maana ya kuuma, kung’ata, “μαστιγόω”lenye maana ya mchapo wa kiboko au kuadhibu, “μαστίζω”lenye maana ya kuchapa, “μάστιξ” lenye maana ya pigo la mjeledi na maradhi na “μαστός” lenye maana ya kifua. Kama msomavyo hapa katika maneno haya hakuna neno linalomaanisha “MKUSANYIKO”.
Basi, vijana kuweni na amani. X-MAS si neno tofauti na CHRISTMAS. Ni neno lile lile isipokuwa badala ya kuandika CHRIST kwa urefu watu wanafupisha kwa X tu. Nawatakieni maandalizi mema ya Krismasi au Noeli.
Kwisha kumaliza somo hili la lugha ya Kiingereza na Kigiriki naomba kuwaongezea mambo kidogo.
Majina: sikukuu hii huitwa pia Kuzaliwa (Nativity) au Yule. Ni sikukuu ya utamaduni wa Kikristo. Maana yake ni kukumbuka na kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Na kwa vile ni shauri la Mungu kutupatia sisi wakosefu zawadi ya Mkombozi, katika kuadhimisha sikukuu hii zawadi hutawala. Ni sikukuu inayosherehekewa kwa mikusanyiko, upambaji wenye ishara nyingi kama vile miti ya Krismasi na dhifa za keki, kula na kunywa pamoja. Tarehe ya kuadhimisha katika Kanisa la Magharibi na baadhi ya Makanisa ya Mashariki  pamoja na walimwengu wengine ni tarehe 25 Desemba. Lakini katika baadhi ya Makanisa ya Mashariki huadhimishwa tarehe 7 Januari. Na katika makanisa ya Kiarmeni huadhimishwa tarehe 6 Januari.
KILA LA HERI KWENU NYOTE!

KIBWAGIZO CHA SIKUKUU
Kila mara tunadaiana aya za Biblia ili kuthibitisha hoja zetu. Jamani si lazima kila hoja ithibitishwe na aya fulani ya Biblia kwani sisi Wakatoliki tunaamini kwamba mafundisho yetu ya imani yanachimbuka kwenye Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu. Mapokeo Matakatifu yapo katika mkufu wa kupokezana mafundisho mazuri toka enzi za Yesu hadi leo hii.
Tusisahau, walikuwepo watu walioishi, kula, kunywa na kuwagusa akina Yesu, Maria na kadhalika.Soma 1Yoh 1:1-4. Watu hao hawakuwa vipofu wala punguani. Tukubali macho, masikio na vichwa vyao vilirekodi mengi ya kweli. Kama wametuambia kitu tunaweza kuwasadiki. Hata Mtume Paulo alitumia Mapokeo Matakatifu kutangaza kweli za Kanisa. Soma 1Kor 11:23.
Ukisoma Yn 20:30-31 na 21:25 utaona kwamba kuna mengi ambayo hayakuandikwa kwenye Biblia. Sasa hayo yasiyoandikwa kwenye Biblia si kwamba yote ni uongo. Kumbe ili kuyapata yaliyo ya kweli kati ya hayo tunahitaji kutumia akili pia (Mt 22:37).
Hatumwabudu Mungu kwa mabavu na mtulinga tu. Tumeambiwa tutumie akili katika kumwamini Mungu. Kwetu sisi wakatoliki akili na imani havipingani. Ndiyo maana kuamini, kwa mfano, kwamba Pilato, Petro, Mtume Yuda Thadei, Mtume Yohane, Bartolomeo, Paulo, Barnaba, Maria Magdalena, Maria wa Kleopa na wengine wamekufa hatuhitaji kusoma katika Biblia habari za vifo vyao, la sivyo ingelitupasa kuamini kwamba wote hao bado wako hai kwa sababu Biblia inawaonesha wangali hai lakini hairipoti kwamba walikufa.
Na tena katika Biblia hiyo hiyo haijaandikwa kwamba ni lazima tuamini kilichoandikwa kwenye Biblia tu. Nionesheni aya ilipoandikwa kwamba inatupasa kuamini mambo yanayoandikwa kwenye Biblia tu. Mkionesha aya hiyo nitavua kofia yangu na kuibwaga mavumbini.HERI YA SIKUKUU KWENU NYOTE TENA!

WALIMU WA KANISA

Mwalimu wa kanisa ni jina la Heshima Ambalo kwa Nadra kanisa Katoliki linampa Mtakatifu, Ambaye ktk maisha ,Mafundisho na Maandishi yake alionesha Na Kueneza Mwanga wa pekee ktk Masuala ya Imani ,Maadili na Maisha ya kiroho.

     Tamko la Kwamba Mtakatifu Fulani ni Mwalimu wa kanisa lote linategemea Utambuzi wa Karama maalum ya hakima Ambayo alijaliwa na Roho Mtakatifu kwa Faida ya kanisa ikibainishwa  na athari njema ya Mafundisho yake ktk Taifa la Mungu.(Papa Benedicto XVI, Barua ya kitume ya 7 October 2012).

Mpaka sasa,ktk miaka karibu 2000 ni Mababu wa kanisa wanne muhimu zaidi upande wa magharibi :

•Gregori (540-640)-1298*
•Ambrosi wa mirano(340-397)-1298*
•Augustino wa Hippo,Doctor Gratiae (354-430)-1298*
•Jerome (347-420)-1298*

Mwaka 1568 Walitangazwa mababu wa kanisa wanne muhimu zaidi upande wa Mashariki, pamoja na Thoma wa Akwino ,Mwalimu bora wa karne za kati Upande wa Magharibi.

•Yohane Krisostomo(347-407)-1568*
•Basili (329-379)-1568*
•Gregori wa Nazianzo(329-390)-1568*
•Thoma wa Akwino,Doctor Angelus (1225-1274)-1568*

Na Baadaye waliendelea kutangazwa kama ifuatavyo:

•Bonaventura wa Bagnoregio, Doctor Seraphicus (1217-1274)-1588

•Anselm wa Canterbury, Doctor Magnificut (1033-1109)-1720
•Isidori wa sevilla (560-636)-1722*
•Petro Krisologo(450-580)-1729*
•Leo I (400-461)-1754*
•Petro Damian(1007-1072)-1828
•Bernardo wa Claivaux,Doctor Mellifluous (1090-1153)-1830
•Hilari wa Poitiers (315-367)-1851
•Alfonso Maria wa Liguori,Doctor Zelantissimus(1696-1787)-1871
•Francisco wa sales (1567-1622) Doctor caritatis 1877
•Sirili wa Alexanderia,Doctor Incarnationis (370-444)-1883*
•Sirili wa Yerusalem* (315-386)-1883
•Yohane wa Damasco (676-749)-1883
•Beda (672-735)-1899*
•Efrem Mshamu (306-373)-1920*
•Petro Kanisi (1521-1597)-1925
•Yohane wa Msalaba, Doctor Mysticus (1542-1591)-1926
•Roberto Bellarmino (1542-1621)-1931
•Alberto, Doctor Universalis (1205-1280)-1931
•Antoni wa Padua Doctor Evangelicus (1195-1231)-1946
•Laurenti wa Brindisi, Doctor Apostolicus (1559-1619)-1959
•Teresa wa Yesu {1515-1582)-1970
•Katerina wa Siena (1347-1380)-1970
•Theresa wa Mtoto Yesu Doctrix Amoris (1873-1897)-1997
•Hildegarda wa Bingen (1098-1179)-2012
•Yohane wa Avila (1500-1569)-2012

      Mwaka wa kutangazwa ukifuatwa na Nyota unaonesha Wanaoheshimiwa na Waorthodoksi pia, ingawa kwao Hakuna Cheo cha Mwalimu wa Kanisa .

       Tofauti na orodha hiyo hapa chini tutawapitia Mmoja Mmoja kufuatana na Historia ya Kanisa ,kuanzia mababu wake wa Karne IV Hadi Mwalimu wa Mwisho aliyefariki mwaka 1897 tu.

WAFAHAMU MAPAPA HAWA

Moja ya Mapapa waliowahi lifanyia kazi kanisa kwa mda mfupi zaidi,

34.Mt. Markus, Mwaka 336(miezi 10)
66.Mt. Boniface III, Mwaka 607(miezi 9)
87.Mt. Sisinnius , Mwaka 708(siku 18)
100.Mt. Valentino, Mwaka 827(siku 40)
112.Mt. Boniface VI, Mwaka 896(siku 15)
115.Mt. Theodore II, Mwaka 897(siku 20)
118.Mt.Leo V, Mwaka 903(mwezi 1)
123.Mt.Leo VI, Mwaka 928(miezi 6)
140.Mt.YohaneXVI, Mwaka 1003(miezi 6)
147.Mt.Benedicto IX, Mwaka 1047-1048(Mara        ya tatu)
151.Mt.Damasi II, Mwaka 1048(siku 23)
185.Mt.Innocent V, Mwaka 1276(miezi 6)
186.Mt.Adriano V, Mwaka 1276(siku 38
192.Mt.Celestino V, Mwaka 1294(miezi 4)
215.Mt.Pius III, Mwaka 1503(siku 26)
222.Mt.Marceli II, Mwaka 1555(siku 20)
230.Mt.Innocent IX, Mwaka 1591(miezi 2)
263.Mt.Yohani Paulo I, Mwaka 1978(siku 34)

Hapo utagundua pamoja na Papa Benedicto XVI Kujiuzuru na wapingaji wengi kuiita ni khashfa ila amelitumikia sana kanisa, Tumuombee zaidi aimarike kiafya pia.

MANENO “UCHAWI” AU “MCHAWI” KWA DHANA ZA KIAFRIKA HAYASTAHILI KUWAMO KWENYE BIBLIA

Katika kutolea maoni kibwagizo changu cha  jana cha “WOTE KIMYAA!!”, mwenzetu Deonatus F. N. Mutani ametaka kutuchanganya sote. Mimi nawatafuta “wachawi” au “watu wenye uchawi” wanyeshe mvua siku hizi tupone. Nataka wajitokeze tuone. Nataka wajitokeze hadharani watende kitu cha kutufaa sote.
Nimekataa uwapo wa uchawi na wachawi kati yetu. Tulionao ni wababaishaji na watu tunaowatuhumu kwa kuwasengenyasengenya tu. Wachawi kiukweli hawapo na bado ninawatafuta. Ninataka wajitokeze na nimesema kama kuna anayewajua awataje, atuitie au atuoneshe wenzake. Mwenzetu Deonatus Mutani ametoka huko niliko na kusema eti Biblia inakiri kuwapo kwa uchawi na wachawi. Ndipo amenishangaa mimi ni padre wa aina gani kukataa uwepo wa uchawi ambao kwa kadiri yake unashuhudiwa na Biblia yake.
Sawa. Lakini leo hii tukimuuliza mwenzetu huyu Biblia gani hiyo, bila shaka atasema ni Biblia ya Kiswahili au ya Kiingereza fulani. Kumbe, hapo ndipo atakapokosea na ndipo panaponipa mimi fursa ya kutoa somo la lugha asilia za Biblia, japo kwa ufupi tu.
Nisikilizeni vijana na wasomaji wangu. Ni hivi, kwenye Biblia hakuna hata mahali pamoja palipoandikwa kwa Kiswahili neno “mchawi” au “uchawi” kwa mastahili. Biblia za Kiswahili zimetutumbukizia maneno hayo pasipo simile. Maneno hayo yaliyotumbukia humo hayabebi maana na dhana halisi ya kilichosemwa katika lugha asilia za Kiebrania au Kigiriki. Dhana ya Kiafrika juu ya “uchawi” na “wachawi” haiingii kwenye Biblia hata kidogo.
Nina hoja. Nadhani mnaweza kukubaliana nami kwamba katika makabila yetu dhana au fasili ya uchawi si nyepesi. Ni dhana mtambuka. Dhana au fasili yetu ya “wachawi” ni ya watu wenye nguvu za ajabu za kufanyia mambo ya ajabu kama tunavyosema wenyewe, labda kuruka angani kwa nyungo, fisi, mbweha, pembe au mikeka; kunyesha mvua hata kiangazi; kupiga radi wapendavyo; kuingia majumbani mwa watu kwa kupitia milango na hata madirisha yaliyofungwa, kuroga tokea mbali, kutazama na kudhuru watu kwa macho au kauli, kuwabadili watu wakawa labda mainzi, nyoka au ngedere na kadhalika. Orodha ni ndefu mno. Kwa lugha yenu vijana, “orodha ni ndefu kishenzi!”.
Ndipo kwetu sisi “wachawi” ni watu wenye uwezo wa kuwatoa wafu makaburini na kuwala nyama maiti; wenye uwezo wa kufanya mikutano usiku pasipo watu wengine kuwaona; watu wenye kuwatengeneza na kuwatunza watu kama misukule; watu wenye uwezo wa kuroga wengine kutoka mbali; watu wasioweza kuonekana wanapofanya shughuli zao; watu wenye kutembea usiku uchi wa mnyama; watu wanaoweza wakawatazama watu kwa macho ya aina yake wakadhurika vibaya; watu wanaoweza kuwasemea wenzao maneno ya laana  au mikosi wakadhurika na kadhalika.
Naomba maweza mengine muyaongezee wenyewe maana, bila mashaka, kwenu dhana hii ipo nanyi, kama humwamini wenyewe, walau mmesikia habari zake. Zaidi sana, imani hiyo mnaijua ilivyotuganda Waafrika wengi kiasi cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kutuonea huruma katika mausia yake Africae Munus namba 93 yaliyoelekezwa kwa Waafrika wote pale mwaka 2009 kufuatia Sinodi ya Pili ya Afrika.
Aghalabu, mnajua jinsi tunavyodhuriana katika jamii zetu, kujichonganisha, kupoteza muda na pesa nyingi, kwa shughuli za jamaa kushikana na kwenda “kunyoana” kwa waganga wa kienyeji; watu kuwaalika “akina Lambalamba” na “kusafisha vijiji” vyao; watoto kuwatuhumu na kuwaua wazazi wao; wanavijiji kubomoleana nyumba au kuchomeana moto wakifukuzana kwa ukatili mkubwa; watu kuwaua vikongwe na wazee; watu kuwafukuzia watuhumiwa wao kwenye vijiji vya wachawi; watu kuwapiga na kuwachomea wengine nyumba moto au kuwaharibia mazao na mali zao wakidaiwa kuzuia mvua; timu zetu za michezo kutumia pesa nyingi kulipia “mabenchi ya ufundi” yaani waganga wa kienyeji; wachezaji wetu kupewa masharti magumu au kulazwa makaburini kabla ya mechi; watu kuzindika nyumba zao kwa hirizi; watu kuwaua au kuwadhuru albino wakitafuta viungo vyao wapate vyeo na utajiri; watu kutafuta mifupa na mafuvu ya binadamu kwa ajili ya kuboreshea biashara au ajira zao; akina mama kuuawa kwa sababu ya sehemu zao za siri; watu kunyofolewa macho, ndimi na masikio; watu kutafuta, kuchukua na kuvaa hiziri na kadhalika.
Sina mashaka, haya yote mnayajua; imani na vitendo vilivyoipa Tanzania nafasi ya kwanza Afrika katika kuamini uchawi, kwa kadiri ya utafiti wa mwaka 2009 wa PEW Research Centre ya Washington D.C., Marekani.
Lakini habari ngeni kwenu nyote ni hii kwamba Biblia haina dhana hiyo, hata chembe na hakuna panapostahili kutokea neno “uchawi” au “mchawi” ndani yake. Maneno hayo yanatokea isivyostahili.
Msishtuke. Ndipo hapo hapo ninapojaribu kulitangaza jambo hili pasipo kusadikika. Wengi wananishangaa sana. Lakini si kitu nimeunda jeshi la mtu mmoja! Hata ndugu yetu Deonatus Mutani ananishangaa sana. Kumbe, nguvu ya hoja yangu ni lugha asilia zilizotumika kuandikia Biblia. Nawahakikishieni nyote kwamba dhana yetu ya uchawi na wachawi haimo kwenye Biblia maana maneno yote asilia yaliyotumika humo hayana MAANA ZETU.
Msinibishe. Nendeni kwenye lugha asilia Kiebrania (Agano la Kale) na Kigiriki (Agano Jipya). Biblia katika lugha zake asilia hazina maneno yenye maana zetu. Ndiyo maana nakataa kwa nguvu na kwa kujiamini kabisa. Tafsiri za Kiswahili na Kiingereza zinatupotosha. Kwa bahati njema baadhi ya watafsiri wa nakala za Kiingereza wamejitahidi sana ama kuepuka au kutumia kiusahihi maneno: “witchcraft”, “sorcery” na “magic”. Katika Kiswahili tuna maksi ya karibu sefuri.
Tusiandikie mate, wino ungalipo. Hebu tuthubutu kujitengea muda siku fulani tujisomee na kutafakari kwa utulivu sehemu zifuatazo: Mwa 41:8.21, 1Sam 28:7, Kut 7:11.22, 8:7.18.19, 9:11, Law 19:26, Kum 18:10-11, Isa 3:3, 47:9.12, Dan 1:20, 2:2.10.27, Nah 3:4, Mdo 13:6.8, 19:19, Gal 5:20 na Ufu 22:15. Hizi ndizo sehemu maarufu kwa maneno “uchawi”, “mchawi” au “wachawi”. Zatupasa kuzichambua kwa makini. Maneno yametumika kwa kupwaya mno.
Nawahakikishieni tena kwamba tukizitalii sehemu hizi katika lugha zake asilia, hatutapata maana ya wachawi katika dhana ya Kiafrika isipokuwa mojawapo ya maana hizi: mabingwa wa kutumia visivyo utaalamu mbalimbali, wachanganya madawa, wacheza mazingaombwe, watu wenye kuwatinga wenzao kwa utaalamu, wataalamu wa nyota, watabiri, wapiga ramili, waona maono, watu wanaotafuta ushauri wa wafu au mapepo, watafsiri ndoto na kadhalika.
Maana hizi ndizo zilipaswa kuchaguliwa vyema na waliotutafsiria Biblia katika Kiswahili zamani zile. Kumbe, wote waliotajwa hivyo, kwenye Biblia, kwa Wayahudi, walikuwa wataalamu waliokuwa wanajulikana na watu na utaalamu wao uliwekwa kwenye vitabu vyenye kusomeka bayana (rej. Mdo 19:19).
Ndipo, basi, tusidanganyike tukachukua dhana yetu ya uchawi ya Kiafrika tukaiingiza kwenye Biblia takatifu. Tutakuwa waongo na wakufi wa weledi. Narudia na kusisitiza kwamba katika Biblia hicho kinachotafsiriwa kama “uchawi” kilikuwa aina ya elimu au utaalamu. Ndiyo maana kulikuwa na vitabu vyake kama nilivyosema sasa hivi (rej. Mdo 19:19) na watu wenye elimu hiyo walikuwa wakijulikana na wengine. Wataalamu wenyewe hawakumwonea mtu yoyote haya na wala hawakujificha. Ndiyo maana waliwahi kuitwa na Farao wakatokea barazani (Kut 7:11) na waliwahi kuitwa na mfalme Nebukadneza huko Babiloni wakajumuika na wataalamu wengine (rej. Dan 2:2). Hali kadhalika tazama jinsi Simeoni “mcheza mazingaombwe” alivyokuwa anajulikana na watu (rej. Mdo 13:6.8).
Tusemeje? Wale waliokuwa wanachuana na Musa wakati ule wa mapigo, hawastahili kuitwa wachawi kwa kadiri ya dhana yetu, isipokuwa “maprofesa wa mazingaombwe” maana wakati ule kulikuwa na shule ya kufundishia uchezaji mazingaombwe kule Misri. Ndiyo maana, kama maprofesa wenye elimu yenye kikomo, walishindwa kufanyiza vituko vya mapigo kadhaa. Mwanzoni mwa shughuli zake za kufanyiza miujiza, Yesu alidhaniwa kuwa amesomea katika chuo cha namna hiyo. Kwa ushuhuda, rejea maana ya watu wa Nazareti walivyojikwaa kwake katika Mk 6:1-6. Kifupi, katika tukio hilo la Nazareti, watu wa kijiji chake walikuwa wakihoji Yesu alipataje ada ya kusomea mazingaombwe wakati familia yake ilikuwa na kipato cha maseremala tu.
Hali kadhalika, wale waliokuwa wanaitwa na Mfalme Nekabudneza wamtafsirie ndoto yake wanastahili kutafsiriwa kama “makuhani watafsiri mambo” na siyo wachawi kwa kadiri ya dhana yetu. Soma vyema Dan 1:20 na 2:2.
Naendelea kukujuza. Usichoke kusoma. Kama wataalamu, watu tunaowasoma katika Biblia zetu za Kiswahili kama wachawi, walikuwa wanajulikana na watu. Nimesema wala hawakujificha. Zaidi ya hayo, kama wataalamu hawakuwa peke yao. Ndiyo maana wakati wa matatizo walipokuwa wanaitwa wasaidie walikuwa hawaitwi peke yao isipokuwa pamoja na wataalamu wengine, kama vile, waganga, wenye hekima, mamajusi (tukitaka wanajimu), Wakaldayo (yaani watu wenye akili sana) na kadhalika (rejea tena Kut 7:11 na Dan 2:2).
Kinyume chake, huku kwetu tunasema sema tu majumbani au vijiweni mwetu. Tuseme tunasengenya tu. Huku kwetu nani anawajua “wachawi” wetu na nani anaweza kutuitia “wachawi” hao? Wako wapi? Nani anawajua? Hayupo Kwa nini hayupo anayewajua? Kwa sababu dhana yetu ya uchawi na wachawi ni tofauti kabisa na ile ya Biblia. Katika Biblia unazungumziwa utaalamu sisi tunazungumzia uovu.
Biblia za Kiswahili zinatupotosha kama “hatujiongezi”. Dhiki ya tafsiri imetufikisha pabaya pasipo kukusudia. Ndugu zanguni au rafiki zangu, maneno yaliyokosewa kutafsiriwa vizuri katika Biblia zetu za Kiswahili hata tukawa na maneno “uchawi” na “mchawi” ndanimwe ni haya:  katika Kebrania “artam” na “artamim”, “oobh” na “baelath oobh”. Neno “artam” lilistahili kutafsiriwa kama “kuhani mfasili mambo”, au “mtafsiri wa ndoto” au “kuhani msomaji mambo”. “Baelath oobh” maana yake ni “mwona maono” au “mtu anayetafsiri mambo kwa kuwasiliana na wafu”.
Katika Kigiriki ni “farmakeia” na “farmakos”, “mageia” na “magos”.  Kwa upande wake maneno “farmakeia” lilistahili kutafsiriwa kama “utaalamu wa uchanganyaji madawa” na hivyo “farmakos” kuwa “mchanganya madawa”. Neno “farmakeia” ndilo lililozaa neno la Kiingereza “pharmacy” neno tunalotumia sisi na kuliweka katika Kiswahili kama “sehemu ya dawa” au “duka la madawa”. Mnanielewa vizuri? Mnaona hapo? Mbona hatuiti  “PHARMACY” “duka la uchawi”? Na mbona hatumwiti anayehusika na “pharmacy” mchawi?
Mintarafu neno “mageia” linalozaa neno “magic” lilistahili kutafsiriwa “utumiaji wa mbinu au elimu fulani kupata matokeo fulani”, kwa mfano kutumia ujuzi fulani, dawa fulani, maneno fulani, matamshi au formula fulani. Na mwenye kutumia mbinu hizo ndiye anayeitwa “magos”. Ndipo hapa walipoingia wale wataalamu wa kusoma nyota kutoka mashariki (rejea sikukuu ya Epifania au Tokeo la Bwana). Wataalamu hawa wanaitwa kwa Kiingereza “magi” au “astrologers” nasi Waswahili tunawaita mamajusi au watu wenye hekima na siyo wachawi.
Ndipo hapa Waingereza walipojitengenezea istilahi za “black magic” kama utaalamu wa kudhuru watu na “white magic” kama utaalamu wa kufanya maajabu bila kudhuru watu, yaani mazingaombwe ya kawaida.
Kwa vyovyote, watu wanaoujua lugha asilia za Biblia hawawezi kuingia katika wepesi wa kutafsiri maneno “artam”, “artamim”, “oobh”, “baelath oobh”, “farmakeia”, “farmakos”, “mageia” na “magos” kama “uchawi” au “mchawi” kwa dhana za Kiafrika. 
Katika mstari huo huo, tusiwe watu wepesi wa kuchukulia na watumiaji Biblia wanaotusonga siku kwa siku kwa kudai wanajua Biblia. Imani yetu ni ya gharama, jamani. Hivi, tujitahidi sana tusimruhusu mtu yeyote aliyepitisha macho juu juu kwenye Biblia atupotoshe baada ya yeye mwenyewe kupotoshwa na Kiswahili kilichomletea maneno “uchawi” na “wachawi” bila tafakari.
Nitaeleza na ninaeleza sasa hivi. Ni hivi, tunachozugwa sisi na Biblia zetu za Kiswahili tukaelewa ni “uchawi” ulikuwa ni utaalamu au kazi. Utaalamu huo ulikuwa ukitumika kwa ngazi mbalimbali. Aidha, kadiri ya Biblia, utaalamu (au kazi hiyo) unajulikana kwa majina mengi vile vile. Katika ngazi ya juu wanasimama “mamajusi” na katika ngazi ya chini wanasimama wanaoitwa “wadanganyifu”. Msihangaike, tutawafahamu hivi punde.
Nimesema katika ngazi ya juu kabisa wanasimama “mamajusi’, yaani “wataalamu wa mambo ya nyota” au “watu wenye hekima”. Hawa ndio waliotajwa katika Mathayo 2 na katika Danieli 1 na 2.  Katika kitabu cha Danieli wataalamu hawa huitwa vile vile Walkadayo, yaani watu kutoka Kaldea ambako enzi zile kuliaminika kuwako watu wenye akili sana.
Ndiyo kisa, Danieli alipoonekana kuwa mtaalamu sana aliwekwa kuwa mkuu wa wataalamu wa Babiloni (Kiswahili chetu kikinyoosha husema “mkuu wa wachawi” tu). Danieli alifanywa mkuu wa wataalamu (“wachawi” kwa Kiswahili chetu rahisi) kwa sababu “roho ya miungu watakatifu, mwanga na elimu na hekima, kama hekima ya miungu, vilionekana ndani yake”. Kwa ushuhuda soma vizuri Dan 5:11.29.
Basi, kama mmenielewa vizuri, sasa tunazungumzia utaalamu na siyo uchawi kwa dhana yetu ya Kiafrika. Nimeshadokeza. Katika ngazi ya chini ya utaalamu huo walikuwa “wadanganyifu” au “matapeli” waliokuwa wanacheza kwa viinimacho vyao kama wacheza mazingaombwe wanavyofanya leo hii kati yetu. Juu ya wadanganyifu hao Paulo anaandika, “Watu waovu na wadanganyifu wanaendelea kuwa wabaya, wakidanganya wengine, na wao wenyewe wakidanganywa” (2 Tim 3:13).
Katikati ya ngazi hizo mbili, yaani katikati ya mamajusi na wadanganyifu (matapeli) walikuwa watu waliobabaisha wenzao kwa pilikapilika za ulozi, kupiga ramli, kupandisha mapepo na waganga waliokuwa wakijitafutia nguvu za pekee kwa kutamka maneno, kutumia majani na mizizi na madawa mbalimbali.  Basi, hivi ndivyo isemavyo Biblia.
Natumaini tupo bado pamoja. Hadi hapa nimeshazinyooshea kidole Biblia za Kiswahili kwa kutokutuletea tafsiri muafaka. Lakini tuwasamehe watafsiri wake. Labda mnaweza kuniliuza, limetokeaje jambo hilo? Nisikilizeni tena. Miaka ile ya 1937, kule Zanzibar, Wazungu waliposimamia zoezi la kutafsiri Biblia katika Kiswahili, hawakuketi na kujaribu kutuletea dhana halisi ya maneno “artam”, “artamim”, “oobh”, “baelath oobh”, “farmakeia”, “farmakos”, “mageia” na “magos”. Ndipo kwa kunyoosha mambo wao na wasaidizi wao wakawa wanapachika neno “uchawi” au “mchawi” popote pale pasipo simile.
Labda sijaeleweka. Nitawaelewesha kwa mifano. Mfano wa kwanza ni huu wa mtafsiri wa maandishi fulani ambaye atatumia neno “pombe” kutafsiri maneno kadha wa kadha: divai, bia, whisky, gongo, mbege, ulanzi, tembo, uraka, komoni, chibuku, kangara, wanzuki, gundi ya seremala, “ketamine”, dawa ya panya na chochote chenye nguvu ya kumlewesha mtu. Ataweza kufanya hivyo lakini hatakuwa sahihi kwa maana divai ni tofauti na komoni, mbege ni tofauti na ulanzi, gongo ni tofauti na wanzuki, gundi ya seremala ni tofauti na whisky, “ketamine” ni tofauti na dawa ya panya na kadhalika. Hapo itabidi msomaji awe na akili ya kujiongeza. La sivyo, atasema vyote hivyo ni sawa tu kwa vile vimetafsiriwa vyote kwa neno moja “pombe”.
Natoa mfano mwingine. Ni kama mtu anavyopaswa kuwa na akili ya kujiongeza anaposoma misemo kama hii: “Baada ya kufanya vibaya katika Ligi Kuu, timu ya Majimaji inamtafuta mchawi”, “Kaka yangu alikuwa mchawi wa hesabu”, “Newton alikuwa mchawi wa sayansi”, “Pele alikuwa mchawi wa kabumbu”, “Maradona alikuwa mchawi wa chenga”, “Bibi Kalembwani alikuwa ananyoa wachawi Mahenge”, “akina Lambalamba wapo Dodoma kuwashika wachawi” na kadhalika. Ikiwa msomaji husika ataelewa misemo hiyo yote sawa, basi yeye atakuwa amefeli medani ya lugha.
Kwa hiyo, ni tafsiri kumbakumba ya Zanzibar iliyotuingiza katika kadhia ya kuwa na maneno “uchawi” na “mchawi” isivyojuzu kwenye Biblia ya Kiswahili. Maneno mengine yanayopaswa kuwekwa sawa kitaalamu kabisa na pengine kufutwa kabisa ni: YEHOVA, JINI na UZINZI. Siku moja nitawafafanulieni kwa jinsi gani maneno haya yanasikitisha kuonekana katika Biblia zetu za Kiswahili.
Kumbe, natamatisha somo langu, kwa kusisitiza kunena kwamba katika sehemu mbalimbali tunapoona Kiswahili kimetunyooshea tafsiri kwa maneno “uchawi” au “wachawi” ni tafsri  ya maneno “kuona maono”, au “kucheza mazingaombwe” au “kuchanganya madawa” au “kutumia ujuzi kutafsiri mambo” na kadhalika.
Kwa mantiki hii, ndugu zanguni, tukirudi kwenye lugha asilia za Biblia, yaani Kiebrania na Kigiriki tutakuwa na fikra mbadala. La sivyo, tutaendelea kukaidiana juu ya dhana yetu ya uchawi, tukiamini Biblia ipo upande wetu.
Haya shime hatujachelewa kuingia kwenye mabadiliko haya ya fikra kwa njia ya lugha asilia za Biblia. Ndiyo, Kiswahili ndiyo hicho, lakini kuna sehemu na maneno ya Biblia fulani fulani ambapo lazima “tujiongeze”.
Leo nimekuhadithieni maneno “uchawi” na “mchawi”. Nimesema hayakustahili kuingizwa katika Biblia kama yalivyoingizwa. Yamekosewa. Matokeo yake, yanawapotosha na kuwatia ubishi watu wengi. Hali kadhalika, nimedokeza kwamba kuna maneno mengine ya mkasa wa aina hiyo hiyo, hususan maneno YEHOVA na JINI. Ni mambo ya kuelimishana na wala tusione haya kuulizana tunapokwama kuielewa Biblia maana elimu haina mwisho na kusoma sana siyo mwisho wa ujinga. Yule afisa Mwitheopia aliposhindwa kuelewa maneno ya Nabii Isaya aliyokuwa anayasoma, hakuona haya kujieleza kwa Filipo akisema, “Nitawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” (Mdo 8:31). Filipo alijitolea kumwelewesha naye akaelewa. Natumaini njia ya afisa yule inaweza kuwa njia yetu pia. Tusione haya kuulizana mambo ya Biblia. KARIBUNI WOTE!