Ijumaa, 24 Novemba 2017

MWAFRIKA ANAPASUKA VIPANDE KWA SABABU WALIMU WAKE WENGI MNO
Baada ya mjadala wetu uliopita tusonge mbele na mada zetu. Kama ninavyoahidi ninaandikia moja moja mpaka ziishe kwenye benki. Leo ni suala la utengamano wa Mwafrika. Mwafrika si mmoja. Mwafrika ni mtu wa kuhurumiwa. Anapaswa ahurumiwe kwa sababu anapasuliwa vipande vipande na walimu wake ambao ni wengi mno. Usinibishe. Ni hivi, kuna wengi mno wanaompatia Mwafrika majibu kwa matatizo yake. Si siri, majibu yanapokuwa mengi lazima yatakuwepo ya uongo, hususan yale yanayofungamanishiwa malipo ya kutatanisha.
Kitu kinachoshangaza ni hiki, tatizo hata likiwa moja, Mwafrika atashauriwa kwa namna zisizopungua sita na watu sita tofauti. Nitajieleza kwa mfano wala usihangaike. Chukulia matatizo yafuatayo: ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu.
Mwenye matatizo kama haya ole wake asijitulize. Akijitembeza tu “ametembezwa”. MOSI, akimwendea mwalimu wa Chuo Kikuu atamweleza kwa namna ya kutinga na nukuu za vitabu vikubwa sababu za ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu. Atamshauri dawa za aina mbalimbali hata mwenye dhiki anaweza kuona kizunguzungu. Kwa huyu anaweza kuacha “mshiko kidogo” kama asante kwa huduma. Haya, mwache huyo pembeni.
PILI, akimwendea mtu aliyejinyakulia wadhifa wa kutoa mapepo atampa jibu dogo tu kwa yote hayo. Yeye atamweleza kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu ni matatizo yanayosababishwa na mapepo na dawa yake ni kutolewa mapepo tu. Si siri, kwa mtu huyo na maswahiba wake kila kitu watakieleza kama pepo: kukosa ajira pepo, kukosa mke au mume pepo, malaria pepo na kadhalika. Yaani kwao matatizo mengi jibu moja - mapepo na dawa moja –kutolewa pepo.
Ndiyo kisa, yeye na wenzake wanafundisha, kwa bidii, kuwasemesha watu sala ya toba na kuwapaka mafuta kwa kusudi la kuwatoa watu mapepo.  Kwa mtu huyo aliyejinyakulia wadhifa wa kutoa mapepo watu, baada ya huduma ya kutolewa mapepo, atatolewa “upepo” mfukoni pia. Lakini, basi, mwache huyo naye pembeni.
TATU, mwenye dhiki huyo huyo akienda kwa mganga wa kienyeji ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu, vyote vinatokana na kurogwa na dawa yake ni kupewa kinga tu dhidi ya ulozi.
Zaidi ya hayo, mshirikina huyo atamwaminisha “mteja” wake mambo mazuri chungu mzima, kwa mfano, kwamba kuruka ni jambo rahisi tu kwani ni kitendo cha kukaa juu ya ungo mdogo, au kumpanda fisi, au kujiingiza ndani ya pembe ndogo, kufumba macho na kuruka kwenda anakotaka kwa spidi ya ajabu. Hapo hapo, ataaminishwa kwamba akitaka kupata cheo wala asihangaike maana ni kitu rahisi sana, akifunga moyo wake na kumkata kidole albino atakuwa amemaliza kazi. Aidha, akitaka kupata pesa asiumize kichwa kwani ni kitendo cha kumiliki “chuma ulete” na pesa kuhamia kwake. Hata kulima kusimkoseshe usingizi hata kidogo kwani ni shauri dogo tu kama ilivyo kunywa uji, yaani akitaka kulima shamba kubwa ni shauri la kupata dawa ya kuwaamshia watu waliolala na kuwapeleka shambani kwake na vivyo hivyo akiwa na mizigo mizito, kwa dawa yake mahsusi, ataweza kuwaamsha watu na kuwabebesha mizigo yake yote na kwa namna hiyo hahitaji gari lolote lile.
Lakini, mwishoni mwa shughuli za mganga wa kienyeji, “mteja” atakuwa amemwachia, kwa kadiri ya maneno yam ganga mwenyewe, mathalani, jogoo mweupe anayejifunza kuwika, mbuzi mwenye kidevu, nazi sita zilizovunwa katikati ya wiki, upande mmoja wa kitenge kisichofuliwa na lundo la kufaa la noti nyekundu. Mwache huyo pia pembeni.
NNE, kishapo mwenye dhiki huyo akijifikisha kwa mganga wa kitabu au muumini wa imani za majini, ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na majini na dawa yake ni ndogo tu, ndiyo kusomewa dua na kusilimu kuwafukuza majini. Kwa ushauri wa aina hii, mwenye dhiki anaweza kusilimishwa papo hapo.
Muumini wa imani za majini akiwa Mkristo baada ya kusema matatizo ya mteja wake yanasababishwa na majini atatoa suluhisho la “kukemea majini” na mwishowe kummwagia maji ya baraka mteja wake. Lakini, wote hao wawili watamalizia kwa kumwomba mteja wao asante katika sura ya pesa. Haya, tuwaache hawa wawili pembeni.
TANO, mwenye dhiki huyo huyo akienda kwa muumini wa nadharia ya laana anayewaendeshea watu “maombezi ya nguvu” ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na laana na dawa yake ni ndogo tu, yaani kuzikataa dhiki hizo kwa sala ya kukemea, kuvunja mti wa familia au ukoo na kufanya ibada ya kufunguliwa. Mwishoni, huko kwa muumini wa nadharia ya laana, mteja husika, atakuwa ametakiwa kuacha kitu anachofikiri kinaweza kuwa mchango wa ukarimu kwa huduma za maombezi.
HATIMAYE, SITA, mwenye dhiki huyo akijing’azisha kwa mchungaji ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na dhambi zake mwenyewe na dawa yake ni ndogo tu, ndiyo kumkiri Yesu kwa kinywa, kuongozwa katika sala ya toba na kisha kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wake. Kifupi, atashauriwa “aokoke” kusudi mambo yake yakae sawa. Mambo hayo, wandugu! Nadhani mmenipata uzuri katika kauli zangu.
Lakini, kabla hajaondoka kwa mchungaji husika, mwenye dhiki wetu, atakuwa ametakwa achangie awezavyo kusudi mchungaji na mkewe wapate kujikimu na hivyo kupata nguvu ya kuendeleza huduma kwa watu. Ndipo atakuwa ameshaelekezwa atume pesa kwenye MPESA, AIRTEL MONEY, TIGO PESA au atume chochote kwenye akaunti fulani ya CRDB, Axim Bank, NMB, NBC na kadhalika. Kumbe, tumwache mchungaji naye pembeni.
Naona nimesema kutosha nataka leo nisikuchoshe. Nafurahi leo kufaulu kukuambia ya kutosha pasipo kukuchosha. Lakini hapo ndipo linapokuja swali moja halali sana: “Katika hao wote sita Mwafrika amsikilize nani hasa?” Jibu langu ni sijui, kazi kwake mwenyewe.
Lakini hapo ndipo inapokuja ole yake, ole ya utengamano wake wa kimwili na kiroho. Mwenye dhiki wetu, hadi anamaliza safari yake ya kujitembeza huko na huko kwa watu AMEPASUKA. Yaani, kama atakuwa hajapasuka vipande atakuwa ameshageuka mhangaikaji mkubwa, kwani ndiyo hivyo atakuwa juzi alimtegea sikio huyu, jana alimtegea sikio fulani, leo anamtegea fulani, kesho mwingine na keshokutwa mwingine.
Matokeo ya kutangatanga kwake yatakuwa kushindwa kujua kwa kuelekea kwa sababu “miluzi” ameshapigiwa mingi mno. Lakini tusisahau wahenga wamezoea kusema, “Miluzi mingi humpoteza mbwa njia”.
Kumbe, kwa kadiri yangu, hii ni moja ya sababu zinazomfanya Mwafrika ashindwe kukua na kuendelea. Mwafrika hana utulivu wa kubuni kitu cha kwake. Anategemea “wasemavyo” wengine. Lakini, kwa maisha ya namna hii, Mwafrika anajinyima fursa ya kufikiri peke yake. Amejizoeza na anaendelea kujizoesha kuwangoja wengine wamemfafanulie kinachomsibu, yakiwa maelezo ya kweli heri, yakiwa ya uongo sawa pia. Hayo ni mintarafu roho na mwili wake.
Ndiyo kisa, kimwili, anajikuta akisubiri watu wavumbue vitu yeye “ashambaikie” tu. Ndivyo alivyoshambaikia viatu, nguo, saa, radio, tochi, umeme na kadhalika. Na ndivyo anavyoendelea kushambaikia simu (sasa smartphones), baiskeli, pikipiki, bajaji, magari, treni, ndege na kadhalika. Kwa kweli, inasikitisha, Mwafrika hana chake cha kujivunia mbele ya watu wa mataifa mengine mbali ya ngoma.
Sasa nahitimisha kwa kusema ombi moja. Vijana katika ghubu hilo, dumuni katika kulisikilza Kanisa kwani hilo huelezea mambo yote pasipo dawa kumbakumba. Linapambanua mambo kwanza, litakutengea vizuri, matatizo ya kimwili, matatizo ya kijamii, matatizo ya kiuchumi, matatizo ya kitamaduni, matatizo ya kisaikolojia na kadhalika.  Ndipo, pamoja na kukulea katika imani iliyotukuka litakushauri umkimbilie elimu kwa sababu si maungwana uangamie kwa kukosa elimu (rejea Isa 5:13 na Hos 4:6).
Jisomee vifungu hivi wewe mwenyewe. Babu Isaya alisema, “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa” na Hosea anarudia jambo hilo hilo akisema, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.” Kwa sababu hii, leo nakuasa sana wewe uchomoke huko uliko! Nakusihi, usiwe mmoja wa watu wanaoangamia kwa kukosa maarifa na tena usisahau watu wameshabadili ile methali ya zamani iliyosema, “Wajinga ndio waliwao” kuwa “Wenye imani iliyokaa henamu ndio waliwao”.
Kumbe, wewe usiwe mmoja wa wanaoliwa leo. Utamaliziwa pesa yako. Pesa ya biashara yako au kilimo chako itaishia mikononi mwa wajanja na watu wakishashikishwa pesa hawajui “reverse”. Utamaliziwa mbuzi wako. Utamaliziwa kuku wako. Utamaliziwa bata wako. Utamaliziwa kondoo wako. Utamaliziwa ng’ombe wako nawe kuzama katika utapiamlo wa kiroho na kimwili kadhalika. Matokeo ya jumla yatakuwa kuishiwa pesa mfukoni na imani rohoni. Chonde, chonde, jizatiti; matatizo yako yasiwe mtaji wa ‘wapiga hela’ leo. KWA HERI TENA!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni