BIKIRA MARIA HAKUWA NA WATOTO WENGINE ZAIDI YA YESU KRISTO
Enyi vijana, ninaendelea kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali mliyoniomba niyatolee ufafanuzi. Leo ni zamu ya swali la kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu au la. Kwa swali hili, naomba nianze kwa kumpa pole Mama Bikira Maria. Pole kwa sababu baada ya kuwazalia wanadamu Mkombozi, shukrani anayopata haikidhi haja. Mnajua, kutendewa ubaya na mtu uliyemfaa inauma sana tena mno.
Lakini, ndivyo inavyodhihiri kwa Bikira Maria. Saa hii hii, wapo wanadamu wanaotoka jasho na kusema mengi wakitaka adharauliwe kama bahasha inavyodharauliwa baada ya barua kutolewa ndani yake. Wapo wanaosema anaheshimiwa mno wakati alikuwa adharauliwe kabisa. Wapo wanaokereka na heshima inayooneshwa kwake. Wapo wanaotibuka nyongo wakisikia watu wanafanya ibada katika miezi ya Mei, Agosti na Oktoba kusudi aendelee na maombezi yake kwa mwanawe. Wapo wanaopata hasira wanaposikia watu wakisali awaombee wanadamu kwa mwanawe kwa kupitia rosari, litania na sala mbalimbali. Wapo wasiotaka kusikia sala ya Salamu Maria. Wapo wanaochukia na kutamani kufumba macho wanapoiona picha au sanamu ya Bikira Maria imewekwa kwa heshima mahali pazuri.
He, weye, kuna mengi wasiyoyataka wasiompenda. Nadhani Mama Bikira Maria angelikuwa anaishi bado hapa duniani, mara kwa mara, angelikuwa anaanguka chini kwa shinikizo la damu kwa kuwa angelikuwa anaishi katika ushahidi endelevu wa methali ya “Shukrani ya punda mateke”. Lakini sivyo. Kwa kuwa yeye alikingiwa dhambi ya asili na vile vile kwa kuwa alikumbana ana kwa ana na kituko cha kutoshukuriwa kule Kana, hata baada ya kuwaombea watu muujiza wa maji kugeuzwa divai, “angelipotezea” yote hayo na kusema tu, “Mwanangu uwasamehe, maana hawajui walitendalo. Ni maajabu ya mtu kupenda boga asilitake ua lake.” Si siri, tangu alipokuwa hapa duniani, dhambi ilikuwa si jambo lake. Kwa nini? Kwa sababu kwa kukingiwa dhambi ya asili Mama Bikira Maria alikuwa “baunsa” kiroho. Haya ya kutoshukuriwa inavyostahiki yalikuwa kwake na bado yangali kwake mambo ya kitoto tu.
Lakini, tuachie hayo pembeni, tujikite kwenye mada halisi ya leo. Ni hivi, watu wengine hupeperushia bendera mambo ya kuambiwa, kwa mfano, mintarafu swali kama Maria alikuwa na watoto wengine au la. Wengi wa wale wanaowauliza Wakatoliki kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo, hawajasoma Biblia wenyewe kwa kusudi la kutafuta jibu la swali hilo. Kumbe, leo nataka kuliweka jambo hili sawa.
Kuna makundi mawili ya watu wanaouliza swali hili: kundi la watu ambao hawakusoma Biblia hata kidogo na kundi la walioisoma. Watu wa kundi la kwanza wamewasikia watu wakiuliza swali hilo au wamepata wenyewe kuulizwa swali hilo na wao ndio wanauliza pia swali hilo hilo. Si kitu. Kwa wale waliosoma Biblia na kisha kuibuka na swali hili najua huwa wanakorofishwa na nukuu hizi mbili: Mt 1:25 na Mk 6:1-3. Kwa hawa, baada ya kusoma Mt 1:25 na Mk 6:1-3 huhisi Maria alijamiiana na Yosefu na hivyo kuwazaa watoto wengine mbali ya Yesu. Si kitu. Lakini, yote juu ya yote, ni kwamba watu wa makundi yote mawili huvurugwa na majina ya “watoto wa Maria” wanaotajwa na Biblia kuwa Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na mmoja wa dada zao aliyeitwa Salome. Hapo ndipo linapoibuka swali ninalotaka kulijibu leo.
Sikiliza. Tutakuwa na jibu refu hivi punde, lakini tukijibu kifupi ni kwamba Bikira Maria hakuwa na mtoto mwingine zaidi ya Yesu Kristo na yeye mwenyewe kama alivyokuwa bikira kabla ya kumzaa Yesu, alibaki bikira wakati wa kumzaa Yesu na baada ya kumzaa Yesu (rejea Mt 1:25). Hii ndiyo sababu Wakatoliki tunamheshimu Maria kama Bikira wa daima.
Sasa twende kwenye maelezo marefu. Ni hivi, usiniambie lolote, najua neno fulani kuhusu wewe. Najua unataka kunibisha hata kabla sijaanza somo. Lakini kabla sijakupatia jibu kwa swali lako yafaa tujikumbushe vyanzo vya swali. Vyanzo hivyo ndivyo chokochoko yenyewe. Mazingira yanayoibusha swali hili yanaanzia kwenye aya hii hii Mt 1:25. Aya hii ni chokochoko ya swali letu kwa sababu ya utata wa maneno yake: “Lakini hakulala naye hadi Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu”. Maana ya maneno haya ndiyo inayowatatanisha wengi. Yaani, kwa maneno hayo inaonekana kana kwamba Yosefu, hapo baadaye alimjua Maria na kumzalia watoto wengine, hao wanaonekana kutajwa katika Mk 6:1-3. Lakini, tulia, mambo hayapaswi kueleweka hivyo.
Nakufafanulia. Awali ya yote, kusudi tujue kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine au la, yafaa kusoma Mt 1:25, Mk 6:1-3 na 15:40.47, 16:1 na hatimaye kuyafafanua mazingira ya Yn 19:25-27. Hebu twende pole pole.
SWALI LINAANZIA MT 1:25
Aya hii haizungumzii nyakati za mbele isipokuwa inashughulikia uzazi wa Yesu kwamba alizaliwa bila mchango wa kimapenzi wa Yosefu. Kwa hali hiyo, habari za ndoa ya Bikira Maria na Yosefu haziwezi kutoshelezwa na maelezo hayo tu. Basi, kwa kusudi la kuyafahamu vizuri maisha ya wanandoa hao wawili, Mapokeo Matakatifu, yaani taarifa za masimulizi ya wale walioishi wakati wa Yesu, Yosefu na Maria ni muhimu. Hao basi, ndio waliolipokeza Kanisa taarifa kwamba Maria alibaki bikira, kabla, wakati na baada ya kumzaa Yesu.
Utaniuliza swali, je, Mapokeo Matakatifu yana uhalali wowote? Jibu ni ndiyo. Uhalali wa mapokeo umedokezwa kwenye Biblia yenyewe kwa namna mbili. Mosi, binadamu tunaambiwa tuwaulize wazee wetu watueleze mambo ya kale (rejea Kum 32:1-12 na Yer 6:16). Basi, kati ya mambo hayo ya kale ni mambo kama haya yahusuyo ndoa ya Yosefu na Maria na uzazi wa Yesu Kristo Bwana wetu.
Pili, Biblia inatuambia kwamba mambo yaliyoandikwa ni machache tu nayo yamechaguliwa kukidhi haja ya kuwasadikisha watu Yesu Kristo alikuwa ni nani na kwa kumsadiki kwamba alikuwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa watu, wanadamu waupate uzima wa milele. Kumbe, kwa dokezo hili, lazima tuelewe kwamba mambo yaliyoachwa pasipo kuandikwa kwenye Biblia ni mengi kuliko yaliyomo kwenye Biblia. Ndiposa, imeandikwa kwamba mambo hayo yangeliandikwa yote dunia isingaliweza kutosha kuyashika maandishi husika (rejea Yn 20:30-31, 21:25).
Lakini, mambo hayo ambayo hayakuandikwa si kwamba yamepotea yote. Wale walioyashuhudia na kuyajua ndiyo wanaotufikishia kwa masimulizi yao ya kupokezana (1Yoh 1:1-4). Usinibishe. Biblia inadokeza kwamba mambo yote yaliyotufikia yalianzia kwenye kusimuliana kwa kupokezana. Yale yaliyoishia kuandikwa ndiyo yakatufikia kama Biblia (Agano la Kale na Jipya) na mengine yaliyokosa kuchaguliwa na kuandikwa ndiyo hayo yanayoendelea kama masimulizi bado. Hii ni kusema basi Biblia ni mapato ya mapokeo na ni mapokeo vile vile maana tumeipokea Biblia kutoka kwa wale waliotuandikia na kuidhinisha maandishi yenyewe. Agano la Kale liliidhinishwa mwaka 95 B.K. na Agano Jipya katika karne ya pili B.K. Hapa ndipo ulipo uhalali wa Mapokeo Matakatifu katika Kanisa. Je, umenipata uzuri?
SWALI LINAKOMAA KATIKA MK 6:1-3
Acha tusonge mbele. Tukisonga mbele na nukuu zetu, baada ya Mt 1:25 tunafika kwenye Mk 6:1-3 iliyo sawa na Mt 13:53-58 na Lk 4:16-30. Aya hizi zinasimulia habari za watu wa Nazareti kukwazika na maneno sawia na matendo ya Yesu Kristo. Katika kushangaa kwao, watu wa Nazareti wanajigamba kwamba wanawajua ndugu zake Yesu. Ndipo wanawataja “mabaunsa” wa kiume wanne: Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni. Hata hivyo, dada zake hawaorodheshwi.
Orodha ya “mabaunsa” hawa ndiyo inayopambisha moto fikra za watu kwamba walikuwa watoto wa Maria mama wa Yesu na hivyo Yesu kutozaliwa peke yake katika tumbo la mama yake. Aya inawataja vijana hao wa kiume na wa kike wasiotajwa majina kwa cheo cha kuwa ndugu wa Yesu. Ndipo swali halali linapoibuka, kama ndivyo inawezekanaje kuwa Yesu alikuwa mtoto pekee wa Bikira Maria? Poa. Hili si swali lililokosa jibu Bibliani.
BIBLIA YENYEWE INAJIBU SWALI LETU
Biblia ina ajabu moja, huwa inaibua swali na kujijibu yenyewe. Kumbe, mashaka yote ya kwamba vijana na dada waliotajwa katika Mk 6:1-3 ni ndugu wa Yesu au la, yanafutwa na Mk 15:40. 47 na 16:1. Akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni walikuwa watoto wa nani, jibu lipo katika aya hizi. Katika aya hizi wanatajwa wanawake waliokuwa wamesimama chini ya msalaba wa Yesu siku ile ya kusulibiwa kwake. Kumbe, katika kuwataja kwake tunaona wazi kwamba jina Maria lilikuwa likitumiwa na wanawake wengi na mmoja wa akina Maria hao alikuwa ni mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni na, katika mstari huo huo, kuwa hata mama wa wale dada waliodokezwa katika Mk 6:1-3 na Mt 13:53-58.
Tusibishane, leo tusome, maana tusiandikie mate na wino ungalipo. Mwandishi anatuandikia hivi, “Walikuwako pia wanawake wakitazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome, na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose”. Kutajwa kwa Maria huyu wa mwisho pasipo kuandikwa neno “mama” na kivumishi cha moja kwa moja “yake Yesu” au “wa Yesu” ndiko kunakotuonesha kwamba Maria mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni hakuwa Maria mama yake Yesu. Vinginevyo mwandishi angeliandika na kivumishi cha moja kwa moja kama alivyofanya mwandishi wa Injili ya Yohane.
Mwandishi wa Injili ya Yohane ameweka mambo kama yalivyokuwa, “Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa na Maria Magdalena” (rejea Yn 19:25).
Kama jambo hili linagomba nitaeleza sasa hivi kwa mfano wetu wenyewe. Ikiwa wewe una ndugu zako wa tumbo moja, mathalani, Damas, Pius, Corbinian, Imelda na Melina, siku utakapotembelewa nao, yule atakayekujulisha ujio wa mama yako, labda aliye nje na mahali ulipokaa, atasema moja kwa moja, “Kuna mama yako nje, anataka kukuona” au “Kuna mama yako mzazi nje, anataka kukuona”. Huyo mwelezaji akisema, “Kuna mama yao akina Damas, Pius, Corbinian, Imelda na Melina nje anataka kukuona” kuna mawili ama hajui kwamba yule ni mama yako mzazi au kwamba yule si mama yako ndiyo maana anakutajia majina ya watoto wake kusudi upate kumtambua vizuri”.
Kwa kesi yetu hii, mwandishi wa Injili ya Marko hawezi kufafanuliwa kwa hilo la kwanza eti kwamba hamkujua sawa sawa mama wa Yesu au la. Hata kama alisimuliwa habari hii na Mtume Petro, kwa vile mwandishi asivyokuwa mtume mwenyewe, asingelikosa kujulishwa vyema habari za mama wa Yesu. Kwa mantiki hii, limebaki hilo la pili tu kwamba yule Maria hakuwa mama wa Yesu isipokuwa mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni tu. Na hivi yeye ametuandikia hivi tupate kuwapambanua vyema akina Maria wale wengi.
MAZINGIRA YA YN 19:25-27 YANASHADIDISHA HOJA
Mazingira ya Yn 19:25-27 ndiyo yanayotukamilishia ukweli kwamba Bikira Maria hakuwa na mtoto wala watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo Bwana wetu. Kwa nini? Kwa sababu watoto wa kiyahudi walisisitiziwa sana kuwatunza wazazi wao hata kama wakiwa wazee au wagonjwa (rejea Mit 19:26, 23:22-25, 28:14, YbS 3:3-18). Basi kitendo cha Yesu kumkabidhi mama yake kwa rafiki yake ni ishara wazi kwamba “mabaunsa” akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni na dada zao waliotajwa katika Mk 6:1-3 na sehemu zinazosadifu hawakuwa ndugu wa moja kwa moja wa Yesu. Basi, kwa kuwa walikuwa na wazazi wao wenyewe, jukumu lao lilikuwa kwao na si kwa Maria, mama wa Yesu.
Hii ni kusema, Yesu alikuwa peke yake, vingineyo mabaunsa hayo na dada hao, baada ya kifo cha kaka yao Yesu, ndio wangelichukua jukumu la kumtunza mama yao na si huyo rafiki wa Yesu. Kifupi, kitendo cha Yesu kumkabidhi rafiki yake mama yake, ni ushuhuda wa upweke wake.
Aidha, kitendo hicho ni ushuhuda wa mambo mawili mengine ya msingi sana. Mosi, ni ushuhuda wa kwa nini Bikira Maria aliwachukua watoto wa Maria mwingine na kukaa nao. Yaani kwa vile Yesu alikuwa mtoto pekee naye alikuwa akitembea huko na huko, mama Maria aliwachukua watoto wa Maria huyo mwingine kusudi apate “kampani” maana mwanamke na watoto ni mate na ulimi. Tena, mama yao wenyewe alikuwa katika utume wa hiyari wa kumfuata na kumtumika Yesu (rejea Mk 15:40). Hapa pameandikwa hivi: “Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia.”
Pili, ni ushuhuda unaodokeza kifo cha Yosefu, mume wa Maria na baba mlishi wa Yesu. Hapa tunapashwa habari kwamba Yosefu alikuwa ameshakufa na hivyo hakuwapo duniani wakati Yesu anakufa msalabani. Kwa vipi? Kwa sababu Yesu asingeliweza kutenganisha ndoa ya “wazazi” wake. Kama Yosefu angelikuwa mzima, pasipo mashaka yoyote, angeliendelea na matunzo ya mkewe na hivi kitendo cha Yesu kumkabidhi mama yake kwa rafiki yake kingelikuwa kitendo haramu. Kitendo chake kingelikuwa kitendo cha kutenganisha ndoa nzima.
MSAADA WA LUGHA ZA KISEMITI
Hatimaye, ieleweke kwamba neno “ndugu” katika lugha za Kisemiti, mathalani, Kiebrania na Kiarabu, na hivyo tafsiri yake katika Kigiriki “adelphoi” (wingi kwa kiume) au “adelphai (wingi kwa upande wa kike), ni neno pana sana. Katika lugha za Kisemiti, “ndugu” inamaanisha wote, ndugu wa damu, wa ukoo na jamaa wote wa karibu. Ndipo watoto wa mama mdogo au mkubwa ni ndugu. Watoto wa baba mkubwa au mdogo ni ndugu. Binamu wote ni ndugu na kadhalika. Hivi “ndugu” wa Yesu kwa Maria waliotajwa katika Injili inawezekana walikuwa ama watoto wa mama mdogo au mama mkubwa au hata watoto wa shangazi yake.
Kwa kumalizia basi, naomba matumizi haya ya neno “ndugu” yasituletee “ushangazi” mwingi hasa sisi Waswahili. Sisi nasi tunalitumia neno hilo kwa mapana hayo hayo ya Kisemiti. Ndiposa, ukweli umebakia na unadumu ule ule mmoja: Maria hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo na hivyo Maria alikuwa bikira, kabla, wakati na baada ya kumzaa Yesu Kristo. Narudia nishindilie hoja iliyojibiwa: Yesu alikuwa mtoto wa pekee wa Bikira Maria na hivyo Maria hakuwa na watoto wengine wa ziada.
HATIMA
Natumaini jibu langu limekuelea. Na sasa, ili uulambe utamu wake vizuri, hebu malizia kwa kuzisoma aya zote tulizozijadili kwa mfululizo wa kimantiki kama ifuatavyo:
Mt 1:25 - “Lakini (Yosefu) hakulala naye hadi Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu”.
Mk 6:1-3 - “Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akafuatwa na wanafunzi wake. Siku ya Sabato ilipofika alianza kufundisha katika sinagogi. Wengi walipomsikia walishangaa, wakasema, ‘Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya? Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria, na ndugu yao akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?’ Basi, wakawa na mashaka naye.”
Mk 15:40 – “Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia.”
Yn 19:25-27 - “Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa na Maria Magdalena”. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, ‘Mama!, Tazama, huyo ndiye mwanao.’ Halafu akamwambia yule mwanafunzi, ‘Tazama, huyo ndiye mama yako.’ Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake”.
Mk 15:47 – “Nao Maria Magdalena na Maria mama yake Yose walipaona alipolazwa”.
Mk 16:1 – “Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalena na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.”
Mwishoni kabisa, najumlisha niliyosema kama ifuatavyo: Yosefu hakujuana na Bikira Maria kwa kumpisha Mungu aliyemtwaa mkewe kwa matumizi maalumu. Zaidi sana, Mt 1:25 haisemi kwamba baada ya kumzaa Yesu, Yosefu alijitwalia haki yake ya ndoa na mwishowe Mk 6:1-3 lazima ieleweke katika mazingira ya Kisemiti ambapo hata jamaa na ndugu wa familia moja hujulikana kama “ndugu”. Kwa hali hiyo, majina ya akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na Salome wao hayasemi lo lote dhidi ya ubikira wa mama Maria. Mwisho wa yote Mk 15:40.47 na 16:1 zinakata maneno kwa kutuambia kwamba akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na Salome walikuwa na mama yao wenyewe. Na ndiyo kisa Yesu alipaswa kumtafuta mtu mwingine kumtunza mama yake kama tunavyosoma katika Yn 19:25-27.
Kwa mara nyingine kwa herini. Ikiwa jibu hili hujalielewa vyema nakuomba uisome mada yangu mara mbili au mama tatu. Ukifanya hivyo, sitegemei kabisa kwamba utatoka kapa mara zote hizo. Kwa heri!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni