Ijumaa, 24 Novemba 2017

BIKIRA MARIA HAKUWA NA WATOTO WENGINE ZAIDI YA YESU KRISTO
Enyi vijana, ninaendelea kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali mliyoniomba niyatolee ufafanuzi. Leo ni zamu ya swali la kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu au la. Kwa swali hili, naomba nianze kwa kumpa pole Mama Bikira Maria. Pole kwa sababu baada ya kuwazalia wanadamu Mkombozi, shukrani anayopata haikidhi haja. Mnajua, kutendewa ubaya na mtu uliyemfaa inauma sana tena mno.
Lakini, ndivyo inavyodhihiri kwa Bikira Maria. Saa hii hii, wapo wanadamu wanaotoka jasho na kusema mengi wakitaka adharauliwe kama bahasha inavyodharauliwa baada ya barua kutolewa ndani yake. Wapo wanaosema anaheshimiwa mno wakati alikuwa adharauliwe kabisa. Wapo wanaokereka na heshima inayooneshwa kwake. Wapo wanaotibuka nyongo wakisikia watu wanafanya ibada katika miezi ya Mei, Agosti na Oktoba kusudi aendelee na maombezi yake kwa mwanawe. Wapo wanaopata hasira wanaposikia watu wakisali awaombee wanadamu kwa mwanawe kwa kupitia rosari, litania na sala mbalimbali. Wapo wasiotaka kusikia sala ya Salamu Maria. Wapo wanaochukia na kutamani kufumba macho wanapoiona picha au sanamu ya Bikira Maria imewekwa kwa  heshima mahali pazuri.
He, weye, kuna mengi wasiyoyataka wasiompenda. Nadhani Mama Bikira Maria angelikuwa anaishi bado hapa duniani, mara kwa mara, angelikuwa anaanguka chini kwa shinikizo la damu kwa kuwa angelikuwa anaishi katika ushahidi endelevu wa methali ya “Shukrani ya punda mateke”. Lakini sivyo. Kwa kuwa yeye alikingiwa dhambi ya asili  na vile vile kwa kuwa alikumbana ana kwa ana na kituko cha kutoshukuriwa kule Kana, hata baada ya kuwaombea watu muujiza wa maji kugeuzwa divai, “angelipotezea” yote hayo na kusema tu, “Mwanangu uwasamehe, maana hawajui walitendalo. Ni maajabu ya mtu kupenda boga asilitake ua lake.” Si siri, tangu alipokuwa hapa duniani, dhambi ilikuwa si jambo lake. Kwa nini? Kwa sababu kwa kukingiwa dhambi ya asili Mama Bikira Maria alikuwa “baunsa” kiroho. Haya ya kutoshukuriwa inavyostahiki yalikuwa kwake na bado yangali kwake mambo ya kitoto tu.

Lakini, tuachie hayo pembeni, tujikite kwenye mada halisi ya leo. Ni hivi, watu wengine hupeperushia bendera mambo ya kuambiwa, kwa mfano, mintarafu swali kama Maria alikuwa na watoto wengine au la. Wengi wa wale wanaowauliza Wakatoliki kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo, hawajasoma Biblia wenyewe kwa kusudi la kutafuta jibu la swali hilo. Kumbe, leo nataka kuliweka jambo hili sawa.
Kuna makundi mawili ya watu wanaouliza swali hili: kundi la watu ambao hawakusoma Biblia hata kidogo na kundi la walioisoma. Watu wa kundi la kwanza wamewasikia watu wakiuliza swali hilo au  wamepata wenyewe kuulizwa swali hilo na wao ndio wanauliza pia swali hilo hilo. Si kitu. Kwa wale waliosoma Biblia na kisha kuibuka na swali hili najua huwa wanakorofishwa na nukuu hizi mbili: Mt 1:25 na Mk 6:1-3. Kwa hawa, baada ya kusoma Mt 1:25 na Mk 6:1-3 huhisi Maria alijamiiana na Yosefu na hivyo kuwazaa watoto wengine mbali ya Yesu. Si kitu. Lakini, yote juu ya yote, ni kwamba watu wa makundi yote mawili huvurugwa na majina ya “watoto wa Maria” wanaotajwa na Biblia kuwa  Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na  mmoja wa dada zao aliyeitwa Salome. Hapo ndipo linapoibuka swali ninalotaka kulijibu leo.

Sikiliza. Tutakuwa na jibu refu hivi punde, lakini tukijibu kifupi ni kwamba Bikira Maria hakuwa na mtoto mwingine zaidi ya Yesu Kristo na yeye mwenyewe kama alivyokuwa bikira kabla ya kumzaa Yesu, alibaki bikira wakati wa kumzaa Yesu na baada ya kumzaa Yesu (rejea Mt 1:25). Hii ndiyo sababu Wakatoliki tunamheshimu Maria kama Bikira wa daima.

Sasa twende kwenye maelezo marefu. Ni hivi, usiniambie lolote, najua neno fulani kuhusu wewe. Najua unataka kunibisha hata kabla sijaanza somo. Lakini kabla sijakupatia jibu kwa swali lako yafaa tujikumbushe vyanzo vya swali. Vyanzo hivyo ndivyo chokochoko yenyewe. Mazingira yanayoibusha swali hili yanaanzia kwenye aya hii hii Mt 1:25. Aya hii ni chokochoko ya swali letu kwa sababu ya utata wa maneno yake: “Lakini hakulala naye hadi Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu”. Maana ya maneno haya ndiyo inayowatatanisha wengi. Yaani, kwa maneno hayo inaonekana kana kwamba Yosefu, hapo baadaye alimjua Maria na kumzalia watoto wengine, hao wanaonekana kutajwa katika Mk 6:1-3. Lakini, tulia, mambo hayapaswi kueleweka hivyo.
Nakufafanulia. Awali ya yote, kusudi tujue kama Bikira Maria alikuwa na watoto wengine au la, yafaa kusoma Mt 1:25, Mk 6:1-3 na 15:40.47, 16:1 na hatimaye kuyafafanua mazingira ya Yn 19:25-27.  Hebu twende pole pole.
SWALI LINAANZIA MT 1:25
Aya hii haizungumzii nyakati za mbele isipokuwa inashughulikia uzazi wa Yesu kwamba alizaliwa bila mchango wa kimapenzi wa Yosefu. Kwa hali hiyo, habari za ndoa ya Bikira Maria na Yosefu haziwezi kutoshelezwa na maelezo hayo tu. Basi, kwa kusudi la kuyafahamu vizuri maisha ya wanandoa hao wawili, Mapokeo Matakatifu, yaani taarifa za masimulizi ya wale walioishi wakati wa Yesu, Yosefu na Maria ni muhimu. Hao basi, ndio waliolipokeza Kanisa taarifa kwamba  Maria alibaki bikira, kabla, wakati na baada ya kumzaa  Yesu.
Utaniuliza swali, je, Mapokeo Matakatifu yana uhalali wowote? Jibu ni ndiyo. Uhalali wa mapokeo umedokezwa kwenye Biblia yenyewe kwa namna mbili. Mosi, binadamu tunaambiwa  tuwaulize wazee wetu watueleze mambo ya kale (rejea Kum 32:1-12 na Yer 6:16). Basi, kati ya mambo hayo ya kale ni mambo kama haya yahusuyo ndoa ya Yosefu na Maria na uzazi wa Yesu Kristo Bwana wetu.
Pili, Biblia inatuambia kwamba mambo yaliyoandikwa ni machache tu nayo yamechaguliwa kukidhi haja ya kuwasadikisha watu Yesu Kristo alikuwa ni nani na kwa kumsadiki kwamba alikuwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa watu, wanadamu waupate uzima wa milele. Kumbe, kwa dokezo hili, lazima tuelewe kwamba mambo yaliyoachwa pasipo kuandikwa kwenye Biblia ni mengi kuliko yaliyomo kwenye Biblia. Ndiposa, imeandikwa kwamba mambo hayo yangeliandikwa yote dunia isingaliweza kutosha kuyashika maandishi husika (rejea Yn 20:30-31, 21:25).
Lakini, mambo hayo ambayo hayakuandikwa si kwamba yamepotea yote. Wale walioyashuhudia na kuyajua ndiyo wanaotufikishia kwa masimulizi yao ya kupokezana (1Yoh 1:1-4). Usinibishe. Biblia inadokeza kwamba mambo yote yaliyotufikia yalianzia kwenye kusimuliana kwa kupokezana. Yale yaliyoishia kuandikwa ndiyo yakatufikia kama Biblia (Agano la Kale na Jipya) na mengine yaliyokosa kuchaguliwa na kuandikwa ndiyo hayo yanayoendelea kama masimulizi bado. Hii ni kusema basi Biblia ni mapato ya mapokeo na ni mapokeo vile vile maana tumeipokea Biblia kutoka kwa wale waliotuandikia na kuidhinisha maandishi yenyewe. Agano la Kale liliidhinishwa mwaka 95 B.K. na Agano Jipya katika karne ya pili B.K. Hapa ndipo ulipo uhalali wa Mapokeo Matakatifu katika Kanisa. Je, umenipata uzuri?
SWALI LINAKOMAA KATIKA MK 6:1-3
Acha tusonge mbele. Tukisonga mbele na nukuu zetu, baada ya Mt 1:25 tunafika kwenye Mk 6:1-3 iliyo sawa na Mt 13:53-58 na Lk 4:16-30. Aya hizi zinasimulia habari za watu wa Nazareti kukwazika na maneno sawia na matendo ya Yesu Kristo. Katika kushangaa kwao, watu wa Nazareti wanajigamba kwamba wanawajua ndugu zake Yesu. Ndipo wanawataja “mabaunsa” wa kiume wanne: Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni. Hata hivyo, dada zake hawaorodheshwi.
Orodha ya “mabaunsa” hawa ndiyo inayopambisha moto fikra za watu kwamba walikuwa watoto wa Maria mama wa Yesu na hivyo Yesu kutozaliwa peke yake katika tumbo la mama yake. Aya inawataja vijana hao wa kiume na wa kike wasiotajwa majina kwa cheo cha kuwa ndugu wa Yesu. Ndipo swali halali linapoibuka, kama ndivyo inawezekanaje kuwa Yesu alikuwa mtoto pekee wa Bikira Maria? Poa. Hili si swali lililokosa jibu Bibliani.
BIBLIA YENYEWE INAJIBU SWALI LETU
Biblia ina ajabu moja, huwa inaibua swali na kujijibu yenyewe. Kumbe, mashaka yote ya kwamba vijana na dada waliotajwa katika Mk 6:1-3 ni ndugu wa Yesu au la, yanafutwa na Mk 15:40. 47 na 16:1. Akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni walikuwa watoto wa nani, jibu lipo katika aya hizi. Katika aya hizi wanatajwa wanawake waliokuwa wamesimama chini ya msalaba wa Yesu siku ile ya kusulibiwa kwake. Kumbe, katika kuwataja kwake tunaona wazi kwamba jina Maria lilikuwa likitumiwa na wanawake wengi na mmoja wa akina Maria hao alikuwa ni mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni na, katika mstari huo huo, kuwa hata mama wa wale dada waliodokezwa katika Mk 6:1-3 na Mt 13:53-58.
Tusibishane, leo tusome, maana tusiandikie mate na wino ungalipo. Mwandishi anatuandikia hivi, “Walikuwako pia wanawake wakitazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome, na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose”. Kutajwa kwa Maria huyu wa mwisho pasipo  kuandikwa neno “mama” na kivumishi cha moja kwa moja “yake Yesu” au “wa Yesu” ndiko kunakotuonesha kwamba Maria mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni hakuwa Maria mama yake Yesu. Vinginevyo mwandishi angeliandika na kivumishi cha moja kwa moja kama alivyofanya mwandishi wa Injili ya Yohane.
Mwandishi wa Injili ya Yohane ameweka mambo kama yalivyokuwa, “Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa na Maria Magdalena” (rejea Yn 19:25).
Kama jambo hili linagomba nitaeleza sasa hivi kwa mfano wetu wenyewe. Ikiwa wewe una ndugu zako wa tumbo moja, mathalani, Damas, Pius, Corbinian, Imelda na Melina, siku utakapotembelewa nao, yule atakayekujulisha ujio wa mama yako, labda aliye nje na mahali ulipokaa, atasema moja kwa moja, “Kuna mama yako nje, anataka kukuona” au “Kuna mama yako mzazi nje, anataka kukuona”. Huyo mwelezaji akisema,  “Kuna mama yao akina Damas, Pius, Corbinian, Imelda na Melina nje anataka kukuona” kuna mawili ama hajui kwamba yule ni mama yako mzazi au kwamba yule si mama yako ndiyo maana anakutajia majina ya watoto wake kusudi upate kumtambua vizuri”.
Kwa kesi yetu hii, mwandishi wa Injili ya Marko hawezi kufafanuliwa kwa hilo la kwanza eti kwamba hamkujua sawa sawa mama wa Yesu au la. Hata kama alisimuliwa habari hii na Mtume Petro, kwa vile mwandishi asivyokuwa mtume mwenyewe, asingelikosa kujulishwa vyema habari za mama wa Yesu. Kwa mantiki hii, limebaki hilo la pili tu kwamba yule Maria hakuwa mama wa Yesu isipokuwa mama wa akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni tu. Na hivi yeye ametuandikia hivi tupate kuwapambanua vyema akina Maria wale wengi.
MAZINGIRA YA YN 19:25-27 YANASHADIDISHA HOJA
Mazingira ya Yn 19:25-27 ndiyo yanayotukamilishia ukweli kwamba Bikira Maria hakuwa na mtoto wala watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo Bwana wetu. Kwa nini? Kwa sababu watoto wa kiyahudi walisisitiziwa sana kuwatunza wazazi wao hata kama wakiwa wazee au wagonjwa (rejea Mit 19:26, 23:22-25, 28:14, YbS 3:3-18). Basi kitendo cha Yesu kumkabidhi mama yake kwa rafiki yake ni ishara wazi kwamba “mabaunsa” akina Yakobo, Yose, Yuda na Simeoni na dada zao waliotajwa katika Mk 6:1-3 na sehemu zinazosadifu hawakuwa ndugu wa moja kwa moja wa Yesu. Basi, kwa kuwa walikuwa na wazazi wao wenyewe, jukumu lao lilikuwa kwao na si kwa Maria, mama wa Yesu.
Hii ni kusema, Yesu alikuwa peke yake, vingineyo mabaunsa hayo na dada hao, baada ya kifo cha kaka yao Yesu, ndio wangelichukua jukumu la kumtunza mama yao na si huyo rafiki wa Yesu. Kifupi, kitendo cha Yesu kumkabidhi rafiki yake mama yake, ni ushuhuda wa upweke wake.
Aidha, kitendo hicho ni ushuhuda wa mambo mawili mengine ya msingi sana. Mosi, ni ushuhuda wa kwa nini Bikira Maria aliwachukua watoto wa Maria mwingine na kukaa nao. Yaani kwa vile Yesu alikuwa mtoto pekee naye alikuwa akitembea huko na huko, mama Maria aliwachukua watoto wa Maria huyo mwingine kusudi apate “kampani” maana mwanamke na watoto ni mate na ulimi. Tena, mama yao wenyewe alikuwa katika utume wa hiyari wa kumfuata na kumtumika Yesu (rejea Mk 15:40). Hapa pameandikwa hivi: “Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia.”
Pili, ni ushuhuda unaodokeza kifo cha Yosefu, mume wa Maria na baba mlishi wa Yesu. Hapa tunapashwa habari kwamba Yosefu alikuwa ameshakufa na hivyo hakuwapo duniani wakati Yesu anakufa msalabani. Kwa vipi? Kwa sababu Yesu asingeliweza kutenganisha ndoa ya “wazazi” wake. Kama Yosefu angelikuwa mzima, pasipo mashaka yoyote, angeliendelea na matunzo ya mkewe na  hivi kitendo cha Yesu kumkabidhi mama yake kwa rafiki yake kingelikuwa kitendo haramu. Kitendo chake kingelikuwa kitendo cha kutenganisha ndoa nzima.
MSAADA WA LUGHA ZA KISEMITI
Hatimaye, ieleweke kwamba neno “ndugu” katika lugha za Kisemiti, mathalani, Kiebrania na Kiarabu, na hivyo tafsiri yake katika Kigiriki “adelphoi” (wingi kwa kiume) au “adelphai (wingi kwa upande wa kike), ni neno pana sana. Katika lugha za Kisemiti, “ndugu” inamaanisha wote, ndugu wa damu, wa ukoo na jamaa wote wa karibu. Ndipo watoto wa mama mdogo au mkubwa ni ndugu. Watoto wa baba mkubwa au mdogo ni ndugu. Binamu wote ni ndugu na kadhalika. Hivi “ndugu” wa Yesu kwa Maria waliotajwa katika Injili inawezekana walikuwa ama watoto wa mama mdogo au mama mkubwa au hata watoto wa shangazi yake.
Kwa kumalizia basi, naomba matumizi haya ya neno “ndugu” yasituletee “ushangazi” mwingi  hasa sisi Waswahili. Sisi nasi tunalitumia neno hilo kwa mapana hayo hayo ya Kisemiti. Ndiposa, ukweli umebakia na unadumu ule ule mmoja: Maria hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu Kristo na hivyo Maria alikuwa bikira, kabla, wakati na baada ya kumzaa Yesu Kristo. Narudia nishindilie hoja iliyojibiwa: Yesu alikuwa mtoto wa pekee wa Bikira Maria na hivyo Maria hakuwa na watoto wengine wa ziada.
HATIMA
Natumaini jibu langu limekuelea. Na sasa, ili uulambe utamu wake vizuri, hebu malizia kwa kuzisoma aya zote tulizozijadili kwa mfululizo wa kimantiki kama ifuatavyo:
Mt 1:25 - “Lakini (Yosefu) hakulala naye hadi Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu”.
Mk 6:1-3 -   “Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akafuatwa na wanafunzi wake. Siku ya Sabato ilipofika alianza kufundisha katika sinagogi. Wengi walipomsikia walishangaa, wakasema, ‘Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya? Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria, na ndugu yao akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?’ Basi, wakawa na mashaka naye.”
Mk 15:40 – “Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia.”
Yn 19:25-27 - “Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa na Maria Magdalena”. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, ‘Mama!, Tazama, huyo ndiye mwanao.’ Halafu akamwambia yule mwanafunzi, ‘Tazama, huyo ndiye mama yako.’ Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake”.
Mk 15:47 – “Nao Maria Magdalena na Maria mama yake Yose walipaona alipolazwa”.
Mk 16:1 – “Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalena na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.”
Mwishoni kabisa, najumlisha niliyosema kama ifuatavyo: Yosefu hakujuana na Bikira Maria kwa kumpisha Mungu aliyemtwaa mkewe kwa matumizi maalumu. Zaidi sana, Mt 1:25 haisemi kwamba baada ya kumzaa Yesu, Yosefu alijitwalia haki yake ya ndoa na mwishowe Mk 6:1-3 lazima ieleweke katika mazingira ya Kisemiti ambapo hata jamaa na ndugu wa familia moja hujulikana kama “ndugu”. Kwa hali hiyo, majina ya akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na Salome wao hayasemi lo lote dhidi ya ubikira wa mama Maria. Mwisho wa yote Mk 15:40.47 na 16:1 zinakata maneno kwa kutuambia kwamba akina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni na Salome walikuwa na mama yao wenyewe. Na ndiyo kisa Yesu alipaswa kumtafuta mtu mwingine kumtunza mama yake kama tunavyosoma katika Yn 19:25-27.
Kwa mara nyingine kwa herini. Ikiwa jibu hili hujalielewa vyema nakuomba uisome mada yangu mara mbili au mama tatu. Ukifanya hivyo, sitegemei kabisa kwamba utatoka kapa mara zote hizo. Kwa heri!
NI AIBU KWA MKRISTO KUPAGAWA NA SHETANI
Natamatisha mada ya Bikira Maria kutokuwa na watoto zaidi ya Yesu Kristo. Ilikuwa rahisi kama maji. Mk 6:1-6 imejibiwa vizuri na Mk 15:40.47 na 16:1-2. Acha jazba, usome sehemu hizi kwa utulivu. Yesu alikuwa mtoto pekee wa Mama Bikira Maria. Kwa kutamatisha mada hiyo, maana yake wakati wa kuwaleteeni mada nyingine ndiyo umejifungua.
Lakini, kabla sijawaleteeni mada nyingine katika mfululizo wa kujibu maswali yenu, karibuni vijana kwa kibwagizo cha mwezi. Kibwagizo chetu ni aibu kubwa tena kubwa sana kwa Mkristo kupagawa na Shetani. Lakini, hebu tuwekane sawa kabla hatujapiga mbizi kwenye kibwagizo chetu. Shetani yupo na anaweza kumpagaa mwanadamu lakini ni aibu ikiwa mwanadamu huyo ni MKRISTO. Kwa nini? Nitakujibu mwenyewe tena mara moja. Ni aibu kwa sababu ni ushahidi wa wazi kwamba kuna kitu si sawa kwake. Ni ushahidi kwamba hajasimama wima Kikristo. Mkristo alipaswa aogopwe na Shetani kwa sababu ya vipengele vinne: ushindi wa Kristo, ulinzi madhubuti alionao, silaha sita anazomvalia Shetani na mbinu aliyopaswa kuitumia. Nitaeleza kwa mapozi kipengele kimoja baada ya kingine. Haya tuanze na tufuatane vizuriMa.

USHINDI WA KRISTO: Pasina shaka yoyote Kristo amemshinda Shetani na hayo ni mapato tarajiwa ya mradi wake mkubwa wa kuwakomboa wanadamu. Mapato ya kazi ya Kristo hayakuwa ya kitoto. Yesu aliachilia kwa muda fahari zake za kimungu, akajifanya mtu kwa kuutwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake Bikira Maria ili kwa damu na nyama yake amtolee Mungu sadaka iliyotukuka kwa upatanisho na Baba. Soma sehemu zifuatazo uelewe vyema fumbo la umwilisho: Yn 1:1-14, Lk 1:26-48, Plp 2:6-11 na Ebr 10:5-10.
Kwa kifupi, Kristo amemshinda Shetani kwa niaba ya wanadamu wote. Ushindi wake siyo wa kutafutwa na tochi. Ulikuwa ushindi wa kipigo cha mbwa kwa Shetani. Kwa damu yake azizi na sadaka yake ya msalabani, yeye ameung’oa, kuharibu, kuangamiza na kuuteketeza ufalme wa Shetani na mahali pake amejenga na kupanda ufalme wa Mungu (Yer 1:4-10). Mwenyewe alisema: “Lakini ikiwa  ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwsha fika kwenu. Au anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang’anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang’anya mali yake”.
Kwa kusema hivi Yesu hakuwa anausifia ujambazi, isipokuwa kuwahakikishia wanadamu kwamba yeye ndiye “baunsa” atakayemzidi nguvu Shetani, mfalme wa dunia kwa wakati ule, na kisha kuwanyakua watu waliokuwa chini ya milki yake na kuwafanya wafuasi wake, yaani WAKRISTO. Wakristo tumenyakuliwa na Kristo kutoka ufalme wa Shetani, tukaingizwa naye katika ufalme wa Mungu kwa Ubatizo. Ndiyo maana kazi hii tukufu inaitwa Injili, yaani Habari Njema ya Furaha kwa wanadamu wa kila mwendo wa maisha (Lk 4:18). Asiyebatizwa peke yake ndiye mwanadamu anayebahatisha bahatisha  bado nje ya ufalme wa Kristo. Lakini huyo naye siku atakapobatizwa tu atajiwekea sawa mambo yake. Sasa inakuwaje Shetani aliyefungwa na Yesu Kristo aishi ndani ya yule aliyekombolewa naye? Ndipo inapokuja aibu kwa “Mkristo aliyepagawa”. Tumwulize kwa haki, kulikoni tena? Sasa naeleza kidogo mambo yanavyoshangaza kwa Mkristo anayeweweseka, kutetemeka, kulialia, kuanguka anguka na kugaagaa eti kwa kupagawa na Shetani. Jamani, mambo!

ULINZI MADHUBUTI ALIONAO MKRISTO: Mkristo analindwa kwa namna sita: amepakwa mafuta ya wakatekumeni siku ya Ubatizo wake, ana malaika mlinzi, ana majina ya Yesu na Maria, analindwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo, yupo kwenye ngome ya Kanisa na ana akili na utashi.
• Mkristo amepakwa mafuta ya wakatekumeni: Mkristo amepakwa mafuta ya wakatekumeni siku ya Ubatizo wake kwa kinga yake dhidi ya Shetani. Au tuseme hatujui maana ya mafuta yale wanayopakwa wabatizwa kifuani? Basi, leo sikiliza. Siku ya ubatizo Mkristo alipakwa mafuta ya wakatekumeni kifuani kumwinga Shetani. Sasa Shetani anarudije kuishi ndani ya Mkristo? Kama nyumba ilifagiliwa na jambazi aliyekuwa anajificha humo ametimuliwa, jambazi huyo anarudije kukaa ndani ya nyumba ile ile tena? Amepitia mlangoni au wapi? Kwa vipi mwenye nyumba amemwacha afike tena? Je, amevunja dirisha?
Hakika kuna kitu Mkristo alichofanya hata kumpatia Shetani fursa ya kurudi tena. Hakika si bure, maana imeandikwa: “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika asipate. Hapo husema, ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka’, lakini anaporudi na kuikuta tupu imefagiliwa na kupambwa, huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali yake mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu’” (Mt 12:43-45).
Je, unanibisha bado? Unataka kusema sijaeleweka? Kama hujanielewa nitakufafanulia kwa kuhoji. Shetani anapataje fursa ya kuja siyo tu kuichafua nyumba ya Mkristo bali kuja kukaa tena kama Mkristo mwenyewe hana hatia? Mkristo amefanya nini hata mafuta ya wakatekumeni aliyopakwa siku ya Ubatizo wake yakachotora (expire)? Kwa maneno mengine, Mkristo alilingana na chupa ya dawa ya kunguni, iweje kunguni aishi ndani yake tena? Ndipo inapokuja aibu kwa Mkristo mhusika.
• Mkristo ana malaika mlinzi: Kila mwanadamu amepewa malaika mlinzi mmoja wa kumlinda. Imeandikwa, “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu. Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori…” (Kut 23:20-23). Soma pia jinsi tulivyo na malaika wetu mbele ya uso wa Mungu (Mt 18:10). Je, imeeleweka sawa sawa?
Sasa nisikilize vizuri. Shetani ni malaika na malaika mlinzi ni malaika. Ikiwa ndivyo, Shetani anamshindaje tena malaika mlinzi  wa mtu hata yeye kuhamia kabisa moyoni mwa mwanadamu huyo? Bila shaka, ni kwa sababu ya Mkristo kutoshirikiana vyema na malaika wake mlinzi. Bila shaka, kwa sababu ya ufurufuru na dhambi zake binafsi, Mkristo ashikani mkono na malaika wake mlinzi. Kumbe, ndipo inapokuja tena aibu kwake.
• Mkristo ana majina ya Yesu na Maria kinywani na moyoni mwake: Majina ya Yesu na Maria “yanamtoa baruti” Shetani kwa sababu anayaogopa sana. Ni majina ya “wabaya wake” waliomshinda katika ushirikiano wao. Yaani kila majina hayo yanapotamkwa Shetani hutoka mbio. Basi, ikiwa Mkristo anayatamka majina haya pasipo Shetani kukimbia, Shetani anamjua mtu huyo kwamba ni mnafiki au anayataja majina hayo bure na pasipo heshima yoyote.
Katika kitabu cha Matendo ya mitume, watoto wa Skeva, watoa pepo wa Kiyahudi, ambao kwa kawaida walikuwa wanawatoa pepo kwa kumpachika mgonjwa vitu vya kunuka pamoja na kumtukana Shetani matusi makubwa makubwa, walilitumia jina la Yesu pasipo kumwamini Yesu mwenyewe. Shetani aliwafedhesha kadamnasi siku hiyo.
Imeandikwa hivi: “Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia,  wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: ‘Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri’.
“Watoto saba wa Skeva, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, ‘Ninamfahamu Yesu, namjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?’ Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skeva wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi ana asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote wakaingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. Waamini wengine walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya imani ya kishirikina hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha hamsini elfu. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi” (Mdo 19:11-20).
Je, unaelewa sasa ninachosema? Nakuomba leo uchague kuelewa. Kumbe, jina la Yesu si la kutaniwa na kutajwa ovyo ovyo. Ndipo, kwa Kkujibari na fedheha za mtindo wa fedheha ya watoto wa Skeva, Kanisa Katoliki liliweka Sheria ya Kanisa na. 1172 paragrafu 1 na 2 ili atakayelitumia jina la Yesu alitumie kwa hadhi yake naye afanikiwe kupunga pepo wa kweli.
Sheria hii inasema mtu wa kuwinga pepo awe padre aliyeruhusiwa na Askofu, kwa maandishi, baada ya kubainika kuwa na sifa nne binafsi: uchaji, ujuzi, busara na uadilifu. Padre mwenye sifa hizi anayeweza kufanikisha upungaji pepo wa kweli, la sivyo ni uzandiki, usanii na “upangaji miujiza” tu.
• Mkristo analindwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo: Yesu Kristo ametangaza ulinzi wa pekee kwa wafuasi wake kiasi hiki walipaswa wasimwogope Shetani kana kwamba ni yatima wa kiroho. Mtu ukiwa na kaka yako mwenye nguvu sana lazima ujisikie salama kabisa. Yesu ndiye kaka yetu wa namna hiyo, Shetani anatuhangaishaje tena? Sikiliza jinsi Yesu alivyolizungumzia jambo hili yeye mwenyewe. Tunasoma alisema ifuatavyo: “Kondoo wangu huisikia sauti yangu, nami nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele, nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. Mimi na Baba tu mmoja” (Yn 10:27-30). Sikiliza maneno hayo ya kulindwa vizuri kabisa!
Sasa, hadi Mkristo anapagawa anatokaje mikononi mwa Yesu Kristo? Ikiwa ametoka kweli mikononi mwa Yesu naye kugeuzwa “nyumba ya Shetani” kuna kitu kibaya kweli kweli alichokifanya kiroho. Ni nini hicho asichokwenda kukifuta kwenye kiti cha Kitubio? Ndipo inapokuja tena aibu kwake.
• Mkristo yupo kwenye ngome ya Kanisa: Mtu awapo na wenzake, hupata kulindwa na mshikamano wake na wenzake. Kule kuwa kati ya watu wengi tu ni ngome ya ajabu. Wingi wa wanakanisa ni ngome. Mtu aliye ndani ya ngome yupo salama. Mtu aliyejishikamanisha na kundi ni salama, hata awe ni mzee sana, mgonjwa sana au mtoto sana. Kinyume chake, mtembea pweke, au mtu yeyote awapo nje ya ngome huwa chambo cha Shetani anayezunguka zunguka huko na huko akitafuta mtu anayezubaa zubaa ammeze (1Pet 5:8). Kifupi, nje ya ngome ya Kanisa si salama. Mtu kutembea na kulala nje ya ngome ya Kanisa ni kujihatarisha mwenyewe. Shetani hawezi kumvaa Mkristo aliyekamilika isipokuwa “mzee katika imani”, “mgonjwa katika imani” au “mtoto katika imani”. Mtu kama huyo ni chambo rahisi cha Shetani.
Lakini, ilitakiwa chambo cha Shetani asiwe Mkristo bali mtu wa imani au dini nyingine asiyeishi katika ngome ya Kanisa kwa kuwa hajaiingia bado. Sasa ikiwa kweli Mkristo amepagawa na Shetani anatupa ushahidi kwamba ametoka nje ya ngome ya Kanisa. Ni ushahidi kwamba hana mshikamano wa kweli na Kanisa. Lakini ni kwa nini? Kumbe, ndipo inapokuja aibu kwake. Aheri mtu kama huyo ajirudishe haraka haraka ndani ya Kanisa.
• Mkristo na akili na utashi: Vipaji vya akili na utashi ndivyo vinavyomfanya mwanadamu awe sura na mfano wa Mungu (Mwa 1:26-28). Kwavyo anaweza kuchagua mema na kukataa mabaya. Lakini ikiwa mtu hatumii vipaji hivi anakuwa dhaifu kama ng’ombe au mbuzi vile. Na mtu dhaifu namna hiyo, Shetani anampenda kiasi cha kuhamia kwake moja kwa moja kwani si chochote isipokuwa mtu laini kama mchicha, tembele au mlenda. Kifupi, mtu wa namna hiyo ni mboga ya Shetani.

SILAHA SITA MKRISTO ANAZOMVALIA SHETANI: Mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso amependekeza silaha sita za kumvalia Shetani: ukweli, uadilifu, hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani, imani, kuupokea ukombozi na neno la Mungu.
Kuhusu jambo hili, Mtume Paulo ametuandikia ifuatavyo: “Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama dirii kifuani, na hamu ya kutanga Habari Njema ya amani iwe kama buti miguuni mwenu. Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. Ukubalini ukombozi kama kofia yenu ya chuma (helmeti) na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu” (Efe 6:14-18).
Kutokana na haya, Mkristo anayetutangazia wenzake kwamba amepagawa na Shetani anatuambia kwamba ametindikiwa ukweli, uadilifu, hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani, imani, kukubali ukombozi na neno la Mungu. Je, kali eh? Ukweli ndiyo ulivyo hautazami sura wala majira. Basi, ndivyo lilivyo neno la Mungu linakata pale mfupa ulipoungana na nyama! Mkristo aliyepagawa na Shetani anatupa ushahidi wa wazi kwamba hajamvalia Shetani silaha zilizopendekezwa na Mtume Paulo, yaani ni kama mtu anayetembea katika nchi ya baridi na fulana tu.

MBINU ALIYOPASWA MKRISTO KUITUMIA: Yakobo alitoa mbinu nzuri ya kumshindia Shetani ndiyo kumpinga Shetani na kumkaribia Mungu. Ameandika hivi, “Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Shetani naye atawakimbieni. Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenye enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki! (Yak 4:7-8). Kumbe, kwa maneno haya, Mkristo kupagawa na Shetani ni ushahidi kwamba hajafanya juhudi za kutosha kumpinga Shetani na wala hajafanya juhudi za kutosha kumkaribia Mungu. Kifupi, Mkristo huyo ana hatia binafsi. Ndipo hapo inapokuja tena aibu kwake.

HATIMA
Narudia mara kurudia. Kwa Mkristo kupagawa na Shetani ni dalili ya shida yake mwenyewe, yaani dhambi yake mwenyewe. Kwa sababu hii ilikuwa aone haya na hivyo ajifiche mbele ya Wakristo wenzake. Ilikuwa augue peke yake moyoni mwake na kujirudi katika vipengele nilivyovieleza katika kibwagizo hiki. Niruhusu nitumie lugha ya picha kali sana. Ashkum si matusi, Mkristo kupagawa na Shetani ni kama mtu mzima kutokwa na haja ndogo au kubwa hadharani, ni aibu.
Ni aibu kwa sababu mtu mzima asiye mgonjwa, anategemewa kujizuia asitokwe na haja mbele ya watu. Kumbe, mkasa kama huo huonewa haya ya uso. Hauonewi fahari, isipokuwa humlazimisha mtu mzima kwenda kujificha mahali pa faragha, kujisafisha, kujitia manukato na kurudi hadharani kwa soni ya aina yake. Hivi ingekuwa aibu kwa Mkristo kutetemeka, kuweweseka, kulialia, kuanguka na kugaagaa hadharani, mathalani, kwenye mkutano wa sala, kongamano seuze kanisani kwa hoja eti amepagawa na Shetani. Ni aibu kwake mwenyewe na aibu isionewe fahari.
Lakini, ajabu siku hizi Wakristo, tena si mmoja bali kwa makumi na mamia, wanakula mieleka hadharani na kugaagaa eti wamepagawa na Shetani. Ajabu ya Firauni! He, Shetani amewajaa Wakristo hivi, kana kwamba Kristo hamkumshinda Shetani kwa niaba yao! Aibu! Jamani, aibu! Wakristo wengi hivi wana mapepo! Huku ni kuufedhehesha Ukristo. Eti watu wakisema hawautaki Ukristo kwa sababu Wakristo wengi ni “nyumba za Shetani”, tutashangaa! Tutashangaa nini wakati tunasema hivyo kwa vitendo vyetu wenyewe? Tushangae nini, kwani watu hawatuoni tunapoanguka hadharani kama embe dodo? Jamani, mchezo wetu ni kifo cha dini yetu wenyewe. Tukome kuuaibisha Ukristo hivi. Tukomeke!
NATOA MWITO. MAMBO YA KUPAGAWA, TUSIFANYIE MASIHARA KWA HESHIMA YA DINI YETU YA HESHIMA SANA. TANGU SASA, KILA MKRISTO AONE AIBU KUDHIHIRIKA KWAMBA AMEPAGAWA NA SHETANI. NI AIBU INAYOTANGAZA HADHARANI KWAMBA HAYUKO SAWA KIIMANI NA AIBU HAIONESHWI NJE. KAMA MTU UNA PEPO CHUTAMA KWENYE KONA YA MBALI HUKO USAIDIWE SIRINI NAWE UTAPONA.
LAKINI KABLA YA MSAADA MWINGINE WOWOTE JIPELEKE MWENYEWE KWANZA KWENYE KITUBIO UKAONDOE HICHO KILICHOMFUNGULIA SHETANI MLANGO WAKO! NAKUOMBA USIJISINGIZIE KUTOKUWA NA DHAMBI (REJ. 1YOH 1:8-110). LAKINI KAMA KWELI HUNA DHAMBI YOYOTE, BASI, SHIDA YAKO NI YA KISAIKOLOJIA TU. HUENDA NI NUROSISI AU SKIZOFRENIA AU “MULTIPERSONALITY” AU UMANYETO (HYSTERIA) NA KADHALIKA. KAMA NDIVYO ITENGENEZE SHIDA HIYO KWA MATIBABU YA KISASA (PSYCHOTHERAPY)! USISUBIRI TENA KITU. UKICHANGANYIKIWA ZAIDI UTAPELEKWA MIREMBE BURE! OOOH! HUKO MBELE USISEME HAKUKUWA NA PADRE ALIYEONYA. HAITAKUWA KWELI, NILIKUWEPO MIMI!
MWAFRIKA ANAPASUKA VIPANDE KWA SABABU WALIMU WAKE WENGI MNO
Baada ya mjadala wetu uliopita tusonge mbele na mada zetu. Kama ninavyoahidi ninaandikia moja moja mpaka ziishe kwenye benki. Leo ni suala la utengamano wa Mwafrika. Mwafrika si mmoja. Mwafrika ni mtu wa kuhurumiwa. Anapaswa ahurumiwe kwa sababu anapasuliwa vipande vipande na walimu wake ambao ni wengi mno. Usinibishe. Ni hivi, kuna wengi mno wanaompatia Mwafrika majibu kwa matatizo yake. Si siri, majibu yanapokuwa mengi lazima yatakuwepo ya uongo, hususan yale yanayofungamanishiwa malipo ya kutatanisha.
Kitu kinachoshangaza ni hiki, tatizo hata likiwa moja, Mwafrika atashauriwa kwa namna zisizopungua sita na watu sita tofauti. Nitajieleza kwa mfano wala usihangaike. Chukulia matatizo yafuatayo: ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu.
Mwenye matatizo kama haya ole wake asijitulize. Akijitembeza tu “ametembezwa”. MOSI, akimwendea mwalimu wa Chuo Kikuu atamweleza kwa namna ya kutinga na nukuu za vitabu vikubwa sababu za ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu. Atamshauri dawa za aina mbalimbali hata mwenye dhiki anaweza kuona kizunguzungu. Kwa huyu anaweza kuacha “mshiko kidogo” kama asante kwa huduma. Haya, mwache huyo pembeni.
PILI, akimwendea mtu aliyejinyakulia wadhifa wa kutoa mapepo atampa jibu dogo tu kwa yote hayo. Yeye atamweleza kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu ni matatizo yanayosababishwa na mapepo na dawa yake ni kutolewa mapepo tu. Si siri, kwa mtu huyo na maswahiba wake kila kitu watakieleza kama pepo: kukosa ajira pepo, kukosa mke au mume pepo, malaria pepo na kadhalika. Yaani kwao matatizo mengi jibu moja - mapepo na dawa moja –kutolewa pepo.
Ndiyo kisa, yeye na wenzake wanafundisha, kwa bidii, kuwasemesha watu sala ya toba na kuwapaka mafuta kwa kusudi la kuwatoa watu mapepo.  Kwa mtu huyo aliyejinyakulia wadhifa wa kutoa mapepo watu, baada ya huduma ya kutolewa mapepo, atatolewa “upepo” mfukoni pia. Lakini, basi, mwache huyo naye pembeni.
TATU, mwenye dhiki huyo huyo akienda kwa mganga wa kienyeji ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu, vyote vinatokana na kurogwa na dawa yake ni kupewa kinga tu dhidi ya ulozi.
Zaidi ya hayo, mshirikina huyo atamwaminisha “mteja” wake mambo mazuri chungu mzima, kwa mfano, kwamba kuruka ni jambo rahisi tu kwani ni kitendo cha kukaa juu ya ungo mdogo, au kumpanda fisi, au kujiingiza ndani ya pembe ndogo, kufumba macho na kuruka kwenda anakotaka kwa spidi ya ajabu. Hapo hapo, ataaminishwa kwamba akitaka kupata cheo wala asihangaike maana ni kitu rahisi sana, akifunga moyo wake na kumkata kidole albino atakuwa amemaliza kazi. Aidha, akitaka kupata pesa asiumize kichwa kwani ni kitendo cha kumiliki “chuma ulete” na pesa kuhamia kwake. Hata kulima kusimkoseshe usingizi hata kidogo kwani ni shauri dogo tu kama ilivyo kunywa uji, yaani akitaka kulima shamba kubwa ni shauri la kupata dawa ya kuwaamshia watu waliolala na kuwapeleka shambani kwake na vivyo hivyo akiwa na mizigo mizito, kwa dawa yake mahsusi, ataweza kuwaamsha watu na kuwabebesha mizigo yake yote na kwa namna hiyo hahitaji gari lolote lile.
Lakini, mwishoni mwa shughuli za mganga wa kienyeji, “mteja” atakuwa amemwachia, kwa kadiri ya maneno yam ganga mwenyewe, mathalani, jogoo mweupe anayejifunza kuwika, mbuzi mwenye kidevu, nazi sita zilizovunwa katikati ya wiki, upande mmoja wa kitenge kisichofuliwa na lundo la kufaa la noti nyekundu. Mwache huyo pia pembeni.
NNE, kishapo mwenye dhiki huyo akijifikisha kwa mganga wa kitabu au muumini wa imani za majini, ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na majini na dawa yake ni ndogo tu, ndiyo kusomewa dua na kusilimu kuwafukuza majini. Kwa ushauri wa aina hii, mwenye dhiki anaweza kusilimishwa papo hapo.
Muumini wa imani za majini akiwa Mkristo baada ya kusema matatizo ya mteja wake yanasababishwa na majini atatoa suluhisho la “kukemea majini” na mwishowe kummwagia maji ya baraka mteja wake. Lakini, wote hao wawili watamalizia kwa kumwomba mteja wao asante katika sura ya pesa. Haya, tuwaache hawa wawili pembeni.
TANO, mwenye dhiki huyo huyo akienda kwa muumini wa nadharia ya laana anayewaendeshea watu “maombezi ya nguvu” ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na laana na dawa yake ni ndogo tu, yaani kuzikataa dhiki hizo kwa sala ya kukemea, kuvunja mti wa familia au ukoo na kufanya ibada ya kufunguliwa. Mwishoni, huko kwa muumini wa nadharia ya laana, mteja husika, atakuwa ametakiwa kuacha kitu anachofikiri kinaweza kuwa mchango wa ukarimu kwa huduma za maombezi.
HATIMAYE, SITA, mwenye dhiki huyo akijing’azisha kwa mchungaji ataelezwa kwamba ulevi, uzinzi, umaskini, kukosa ajira, kutoolewa, pesa kutokukaa na magonjwa ya asthma, malaria, shinikizo la damu, kisukari, ukimwi na pumu vinasababishwa na dhambi zake mwenyewe na dawa yake ni ndogo tu, ndiyo kumkiri Yesu kwa kinywa, kuongozwa katika sala ya toba na kisha kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wake. Kifupi, atashauriwa “aokoke” kusudi mambo yake yakae sawa. Mambo hayo, wandugu! Nadhani mmenipata uzuri katika kauli zangu.
Lakini, kabla hajaondoka kwa mchungaji husika, mwenye dhiki wetu, atakuwa ametakwa achangie awezavyo kusudi mchungaji na mkewe wapate kujikimu na hivyo kupata nguvu ya kuendeleza huduma kwa watu. Ndipo atakuwa ameshaelekezwa atume pesa kwenye MPESA, AIRTEL MONEY, TIGO PESA au atume chochote kwenye akaunti fulani ya CRDB, Axim Bank, NMB, NBC na kadhalika. Kumbe, tumwache mchungaji naye pembeni.
Naona nimesema kutosha nataka leo nisikuchoshe. Nafurahi leo kufaulu kukuambia ya kutosha pasipo kukuchosha. Lakini hapo ndipo linapokuja swali moja halali sana: “Katika hao wote sita Mwafrika amsikilize nani hasa?” Jibu langu ni sijui, kazi kwake mwenyewe.
Lakini hapo ndipo inapokuja ole yake, ole ya utengamano wake wa kimwili na kiroho. Mwenye dhiki wetu, hadi anamaliza safari yake ya kujitembeza huko na huko kwa watu AMEPASUKA. Yaani, kama atakuwa hajapasuka vipande atakuwa ameshageuka mhangaikaji mkubwa, kwani ndiyo hivyo atakuwa juzi alimtegea sikio huyu, jana alimtegea sikio fulani, leo anamtegea fulani, kesho mwingine na keshokutwa mwingine.
Matokeo ya kutangatanga kwake yatakuwa kushindwa kujua kwa kuelekea kwa sababu “miluzi” ameshapigiwa mingi mno. Lakini tusisahau wahenga wamezoea kusema, “Miluzi mingi humpoteza mbwa njia”.
Kumbe, kwa kadiri yangu, hii ni moja ya sababu zinazomfanya Mwafrika ashindwe kukua na kuendelea. Mwafrika hana utulivu wa kubuni kitu cha kwake. Anategemea “wasemavyo” wengine. Lakini, kwa maisha ya namna hii, Mwafrika anajinyima fursa ya kufikiri peke yake. Amejizoeza na anaendelea kujizoesha kuwangoja wengine wamemfafanulie kinachomsibu, yakiwa maelezo ya kweli heri, yakiwa ya uongo sawa pia. Hayo ni mintarafu roho na mwili wake.
Ndiyo kisa, kimwili, anajikuta akisubiri watu wavumbue vitu yeye “ashambaikie” tu. Ndivyo alivyoshambaikia viatu, nguo, saa, radio, tochi, umeme na kadhalika. Na ndivyo anavyoendelea kushambaikia simu (sasa smartphones), baiskeli, pikipiki, bajaji, magari, treni, ndege na kadhalika. Kwa kweli, inasikitisha, Mwafrika hana chake cha kujivunia mbele ya watu wa mataifa mengine mbali ya ngoma.
Sasa nahitimisha kwa kusema ombi moja. Vijana katika ghubu hilo, dumuni katika kulisikilza Kanisa kwani hilo huelezea mambo yote pasipo dawa kumbakumba. Linapambanua mambo kwanza, litakutengea vizuri, matatizo ya kimwili, matatizo ya kijamii, matatizo ya kiuchumi, matatizo ya kitamaduni, matatizo ya kisaikolojia na kadhalika.  Ndipo, pamoja na kukulea katika imani iliyotukuka litakushauri umkimbilie elimu kwa sababu si maungwana uangamie kwa kukosa elimu (rejea Isa 5:13 na Hos 4:6).
Jisomee vifungu hivi wewe mwenyewe. Babu Isaya alisema, “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa” na Hosea anarudia jambo hilo hilo akisema, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.” Kwa sababu hii, leo nakuasa sana wewe uchomoke huko uliko! Nakusihi, usiwe mmoja wa watu wanaoangamia kwa kukosa maarifa na tena usisahau watu wameshabadili ile methali ya zamani iliyosema, “Wajinga ndio waliwao” kuwa “Wenye imani iliyokaa henamu ndio waliwao”.
Kumbe, wewe usiwe mmoja wa wanaoliwa leo. Utamaliziwa pesa yako. Pesa ya biashara yako au kilimo chako itaishia mikononi mwa wajanja na watu wakishashikishwa pesa hawajui “reverse”. Utamaliziwa mbuzi wako. Utamaliziwa kuku wako. Utamaliziwa bata wako. Utamaliziwa kondoo wako. Utamaliziwa ng’ombe wako nawe kuzama katika utapiamlo wa kiroho na kimwili kadhalika. Matokeo ya jumla yatakuwa kuishiwa pesa mfukoni na imani rohoni. Chonde, chonde, jizatiti; matatizo yako yasiwe mtaji wa ‘wapiga hela’ leo. KWA HERI TENA!
KESI YA BIBLIA KUBWA NA BIBLIA NDOGO, MUNGU MKUBWA NA MUNGU MDOGO
Vijana tunaendelea na mada zetu. Nadhani nimewapeni muda wa kutosha kutafakari mada yetu ya mwisho, yaani juu ya imani inayotudumaza ya “uchawi” au “ushirikina”. Leo nina mada ya ajabu kidogo, lakini ndiyo itakayoweza kuweka wazi sababu ya malumbano yanayojitokeza au pengine yanayoendelea kati yetu Wakristo. Kifupi, mzizi mkuu wa malumbano yetu ni kuwapo kwa Biblia kubwa na Biblia ndogo na hivyo kuwa na Mungu mkubwa na mungu mdogo. Wakristo tuna Biblia mbili na hivyo inaonekana tuna miungu miwili, Mungu mkubwa wa Biblia kubwa na mungu mdogo wa Biblia ndogo. Hiki ni kisa cha kushangaza, lakini ndivyo kilivyo, na leo nitasema ukweli ili mambo yawe bayana kwetu sote. Hiki ni kisa cha Kanisa Katoliki kuwa na Biblia kubwa na hivyo kuwa na Mungu mkubwa kuliko mungu wa makanisa mengine.
Hebu nianze na jambo lililo dhahiri zaidi. Wala hatuna mashaka, tuna Biblia mbili tofauti, Biblia kubwa (vitabu 72 au 73) na Biblia ndogo (vitabu 66). Kumbe, kwa vile makanisa mengine yana Biblia ndogo, yaani ya vitabu 66 tu, yana Mungu mdogo. Nahukumu kwa kufuata maweza yao. Yupo  mungu mdogo kwa sababu hajui na wala hawezi mengi sana. Mungu mdogo hatofautiani sana na mimi Pd. Titus Amigu. Atakuwa hajui mengi ya kesho. Atakuwa hakumbuki alichosema. Atakuwa mwongo. Ataweza kusingiziwa mengi na kadhalika. Mkasa huu unatokeaje? Unatokea kwa sababu Biblia ya vitabu 66 ni ndogo. Udogo huu ni pendekezo la mwanadamu mmoja tu. Ni hivi, udogo huo umetokana na Martin Luther, hapo mwaka 1517 kuchagua kuwafuata Wayahudi wa Palestina ambao walivikataa vitabu vya Wayahudi wenzao waliokuwa wakikaa huko Aleksandria, Misri.
Wayahudi waliokuwa wakikaa nje ya Palestina (Diaspora) walikuwa na vitabu vingi zaidi. Inaonekana jamii yao ilikuwa na waandishi wengi hodari. Jambo hilo si ajabu. Wamakonde, Wandonde, Waigbo, Wanubi, Wajerumani, Wamarekani au Wachina wanaokaa nje ya nchi yao wanaweza kuwa hodari zaidi kuliko watu waliobaki kwao. Kumbe, Wayahudi waliokuwa wakikaa nje ya Palestina, ndio Diaspora, waliandika vitabu vingi vizuri. Ndiyo kisa walipovitafsiri vitabu hivyo katika Kigiriki wakatoka na vitabu vingi zaidi kuliko wenzao waliobaki Palestina. Tafsiri hii ya Maandiko ilifanywa huko Misri chini ya ushauri wa Mfalme Philadelphus (Ptolemy II) katika miaka ya 285 -247 Kabla ya Kristo.
Kwa taarifa yako, Wakatoliki wanafuata orodha yenye vitabu 45 au 46 katika Agano la Kale na vitabu 27 katika Agano Jipya. Agano la Kale lina vitabu 45 au 46 kutokana na kusigana katika kuvihesabu vitabu viwili, kitabu cha Nabii Yeremia na kile cha Maombolezo. Baadhi ya watu huvihesabu kama vitabu viwili kutokana na kusadiki kwamba vimeandikwa na waandishi wawili tofauti wakati watu wengine husema vitabu hivyo vimeandikwa na mwandishi mmoja na hivyo ni kitabu kimoja tu. Kumbe, vitabu hivyo vikihesabiwa kama viwili, Agano la Kale linakuwa na vitabu 46 wakati vikihesabiwa kama kimoja , idadi ya vitabu vya Agano la Kale hushuka kwa kitabu kimoja na hivyo kuwa 45 tu.
Makanisa ya Kiprotestanti hufuata orodha iliyokuwa au inayofuatwa bado na Wayahudi huko Palestina, orodha yenye vitabu 24 katika Agano la Kale kutokana na kuvihesabu vitabu vyote 12 vya manabii wadogo (Hosea, Yoeli, Amosi, Obadia, Yona, Mika, Nahumu, Habakuki, Sefania, Hagai, Zekaria na Malaki) kama kitabu kimoja. Lakini, vitabu hivyo vikitenganishwa na kuhesabiwa kimoja kimoja, orodha hiyo hutanuka na idadi ya vitabu kupanda hadi 39 katika Agano la Kale.
Vitabu saba na sehemu za vitabu zinazoleta tofauti hiyo ni vitabu vya Tobiti, Yudithi, 1 na 2 Makabayo, Hekina ya Sulemani, Yoshua ben Sira, Baruku na Barua ya Yeremia pamoja na sehemu zifuatazo: Wimbo wa Vijana Watatu kwenye Tanuru (Dan 3:24-90), Simulizi la Susana (Dan 13) na Hadithi ya Bel na Joka (Dan 14).
WAYAHUDI WA DIASPORA WALIKUWA NA VITABU ZAIDI:  Tunaulizana. Kwa nini Wayahudi wa Diaspora walikuwa na vitabu zaidi? Asili ya tofauti hii ni ukweli kwamba hapo zamani kabla ya orodha ya vitabu (canon) vya Agano la Kale, yaani Biblia ya Kiyahudi haijafungwa rasmi, Wayahudi waliokuwa wakiishi uhamishoni, yaani nje ya Palestina (Diaspora), walikuwa na vitabu vingi zaidi kuliko vile walivyokuwa navyo Wayahudi wenzao waliokuwa wakiishi bado huko Palestina (Israeli au Uyahudi). Nimeshaomba jambo hili lisichukuliwe kama ajabu ya pekee sana kwani uandishi waweza kustawi popote pale hata nje ya nchi fulani. Kwa hali hii, tunaweza kusema kwamba huko nje ya Palestina walikuwepo Wayahudi waandishi wazuri wengi zaidi.
Ukweli huu unashuhudiwa na taarifa iliyotufikia kwa kumbukumbu ya Barua ya Aristes. Barua hiyo inasimulia kwamba Wayahudi wa huko Aleksandria (Misri) walipoonekana wakishindwa kusoma vitabu vyao vya dini katika lugha ya Kiebrania, mfalme Philadelphus (Ptolemy II) aliyeishi kati ya 285 na 247 K.K. aliamua kuwasaidia kuvitafsiri vitabu vyao katika lugha ya Kigiriki kilichotawala katika Diaspora.
Basi, waliitwa watafsiri kutoka Israeli sita sita kutoka kila kabila la Israeli. Hivi,  jumla yao kutoka makabila 12 ilikuwa 72 (au 70 kwa makumi ya karibu). Barua ya Aristes inasema watafsiri hao walifungiwa katika vyumba 72 tofauti kila mmoja na kutafsiri vitabu alivyopewa katika siku 72. Barua inatangaza ajabu kubwa kwamba mwishoni mwa kazi yao, tafsiri zao zilipolinganishwa, zilifanana neno kwa neno. Kumbe, hii ndiyo tafsiri maarufu ya Agano la Kale inayojulikana kwa Kilatini hadi leo hii kama Septuaginta (yaani 70 ambayo kwa Kilatini huandikwa hivi LXX).
Lakini ajabu kubwa zaidi ilikuwa kwamba, kiidadi, vilipolinganishwa vitabu vya Agano la Kale la Septuaginta, ilizidi vile vilivyokuwa vikisomwa huko Palestina (Israeli au Uyahudi) kwa vitabu saba na sehemu za vitabu nilizotaja hapo juu.
JE, WAKRISTO WA MWANZO WALIPOKEA TAFSIRI YA SEPTUAGINTA? Ndiyo, tena ndiyo kubwa, kwani tangu enzi hizo, ndiyo karne ya kwanza na ya pili, Agano la Kale la tafsiri ya Septuaginta ndilo lililopokelewa na Kanisa la Kristo. Hiyo ndiyo tafsiri iliyopokelewa na kutumika sana na mababa wa Kanisa, kama vile, Tertuliani,  Ambrose, Augustino wa Hippo na kadhalika hasa kwa vile walikuwa weledi wa Kigiriki na hawakujua Kiebrania cha kutosha.
Zaidi ya hayo, tafsiri ya Septuaginta ambayo ilikuwa katika Kigiriki ilioana vyema na vitabu vya Agano Jipya (27) ambavyo tangu mwanzo viliandikwa katika Kigiriki cha kawaida (ndiyo koine, yaani Kigiriki cha kawaida) wakati vitabu vya Wayahudi huko Palestina vilikuwa bado vikitumiwa katika Kiebrania, tena Kiebrania cha zamani.
Basi, Agano la Kale la tafsiri ya Septuaginta likapata kuwa sehemu ya Biblia ya Kanisa la Mungu hata ikatafsiriwa pamoja na Agano Jipya katika Kilatini cha kawaida (ndiyo Vulgata) na akina Mt. Jerome, msimamizi wa taaluma ya Biblia.
Kumbe, ndiyo Biblia (LXX na Agano Jipya) hii iliyotumika na Kanisa na Wakristo wa Magharibi (kwani Wakristo wa Mashariki, ndio Waorthodoksi wana orodha ya vitabu vya Biblia kubwa zaidi, yaani vitabu zaidi ya 73) hadi karne ya 16. Septuaginta ilikuwa na vitabu 45 au 46 kujumlisha vitabu 27 vya Agano Jipya na hivyo kufanya Biblia ya Kanisa la Mungu kuwa na jumla ya vitabu 72 au 73.
Lakini, ajabu ya kupinduka chali ikatokea katika karne ya 16. Ni katika karne hii, Martin Luther aliposababisha mtengano wa Kanisa naye kuifumua Biblia kwa kuviondoa vitabu vile saba na sehemu za vitabu nilizowatajia, yaani, Tobiti, Yudithi, 1 na 2 Makabayo, Hekima ya Sulemani, Yoshua bin Sira, Baruku na Barua ya Yeremia pamoja na Wimbo wa Vijana Watatu kwenye Tanuru (Dan 3:24-90), Simulizi la Susana (Dan 13) na Hadithi ya Bel na Joka (Dan 14).
Ndiyo kusema basi, tangu wakati wa Martin Luther, Wakristo wote wanaojitenga na Kanisa Katoliki huamua kumsikiliza Martin Luther na hivyo kuiacha orodha ya Septuaginta (yaani Biblia ya Wayahudi wa uhamishoni) na kuifuata ile ya Palestina, yaani ile yenye vitabu pungufu kwa saba na ushehi. Ndiyo kisa basi, hadi leo hii, makanisa yote ya Kiprotestani na madhehebu yake mapya yanayozaliwa kila kukicha, hufuata orodha yenye vitabu vichache wakati Kanisa Katoliki likiendelea na orodha ile asilia kwa Wakristo yaani Septuaginta.
Hivi, kuhusu idadi ya vitabu kwenye Biblia, asikudanganye mtu yeyote yule, iwe amekujia na “suitcase” au na mkoba wa ngozi ya mbuzi. Si kwamba WAKATOLIKI WAMEONGEZA VITABU kwenye Biblia isipokuwa ni kinyume chake kwani ukweli ni kwamba Martin Luther AMEVIPUNGUZA VITABU kwenye Biblia.
Usinikodolee macho! Unashangaa nini? Hii ni hesabu ya kawaida, hata chekechea haiwashindi kuilewa. Kama ukianza na namba 72 au 73 ukashuka hadi 66 maana yake umetoa au umepunguza. Ingekuwa kwamba mtu ameanza na namba 66 na kupanda nayo hadi 72 au 73 ingekuwa kweli ameongeza. Kumbe, haikuwa hivyo, katika historia ya orodha rasmi ya vitabu vya Biblia, yaani canon.
Nadhani tumeelewana kabisa. Haya tuendelee. Hoja ya kufuata orodha ya vitabu vichache ni kwamba makanisa yaliyojitenga, kwa kadiri ya mawazo ya Martin Luther, huona kwamba vitabu vile vya ziada na sehemu zile za nyongeza havikuvuviwa, yaani havikuangaziwa na Roho Mtakatifu katika uandishi wake. Ndipo, basi, Wakristo wote wanaomsadiki, kumsikiliza na kumfuata Martin Luther, huita vitabu hivyo na sehemu za Maandiko nilizozitaja kwa msamiati wa Kigiriki ‘apokrifa’.
Kumbe, Kanisa Katoliki, kwa upande wake, linavitambua bado vitabu hivyo pamoja na sehemu zile za nyongeza kwamba vimevuviwa na kwamba vinastahili kuitwa orodha ya nyongeza, ama kwa maneno mengine, ORODHA YA PILI ya vitabu vitakatifu, maana vimetoka kwa Wayahudi wenyewe tena wakati ule ule waandishi wengine wa kimungu walipokuwa wakiyaandika Maandiko Matakatifu katika nchi ya Palestina (Israeli au Uyahudi). Ndipo basi, Kanisa katoliki huviita vitabu hivyo na sehemu nilizokutajia kwa jina lililotoholewa kutoka Kigiriki, ‘DEUTEROKANONI’, yaani ‘ORODHA YA PILI’.
MASWALI MADOGO MAWILI:
Swali 1. Pd Martin Luther alitoa hoja kuwa havikuvuviwa na Roho Mtakatifu. Lakini Kanisa Katoliki linatambua vilivuviwa na Roho Mtatikatifu kwa kuwa vilitoka kwa Wayahudi walewale japo walikuwa uhamishoni.
Je, wakati wa kukusanya vitabu vya Biblia Wayahudi waliwakataa Wayahudi wenzao waliokuwa uhamishoni walipokuja na mafundisho ya Biblia ile ile??

Jibu: Ndiyo, Wayahudi waliwakataa Wayahudi wenzao. Kiujumla, Wayahudi wa Palestina walivikataa vitabu tulivyovitaja pamoja na sehemu za vitabu ya Esta na Danieli. Walivikataa hasa kwa sababu Wakristo walikuwa wanavitumia tayari katika kufafanulia mafundisho yao. Ndiyo kisa, kuvikataa huku kulifanyika huko Jamnia mwaka 95 Baada ya Kristo. Kabla yake, vitabu hivyo vilikuwa vinatumika kwa kujulikana kabisa, kwa mfano kitabu cha Yoshua ben Sira kilikuwa kikitumika na Wayahudi wote kama kitabu cha kiada katika kuwafundisha vijana maadili.
     
Swali 2. Je, Kanisa Katoliki limezingatia hoja zipi za msingi  zinazosahihisha hoja alizotumia Pd. Martin Luther katika kuvipunguza vitabu hivyo ukiachana na hiyo ya kuvuviwa na Roho Mtakatifu alikosema.

Jibu: Hoja ya kwanza - kukataa kwa Martin Luther kunabainisha kwamba hakujua Maandiko Matakatifu maana nukuu za vitabu alivyovikataa zipo kwa namna moja au nyingine katika nukuu za waandishi wa vitabu vya Agano Jipya, kwa mfano, Waraka kwa Waebrania na nyaraka kwa watu wote zaYakobo na Petro. Hii inamaanisha alikataa kitu ambacho kipo kwenye Biblia tayari. Ilikuwa kama mtu kukataa nyama iliyokaa juu ya wali wakati mchuzi wake umeshachanganywa na wali huo huo unaokula.
Hoja ya pili: Mafundisho ya vitabu alivyovikataa yalikuwa yanajulikana na jumuiya za Kikristo, yalikuwa hayapingani na mafundisho yaliyokuwa kwenye vitabu alivyovikubali, yalikuwa mafundisho yanayoweza kuhimiza imani na upendo na kadhalika, mambo ambayo kwa yenyewe yalikuwa vigezo (criteria) vya kuteulia vitabu vilivyoingia katika orodha ya vitabu vya Agano Jipya vilivyoandikwa na Wakristo wenyewe.

Huenda nimekuporomoshea mambo mapya mno na huenda, kichwani na moyoni mwako, unadhani nimesahau hoja ninayoijenga. La hasha! Nimekutaarifu kwamba Biblia ya Wakristo ilipunguzwa kutoka vitabu vya asilia 72 au 73 hadi vitabu 66. Kwa mkasa huo, Biblia ilifanywa NDOGO na kwa kufanywa huko ndogo Mungu akakumbwa na balaa la kupunguzwa kutoka Mungu mkubwa hadi kuwa MUNGU mdogo. Kwa nini? Kwa sababu mambo anayoshuhudiwa katika vitabu vile 7 na sehemu zilizokanwa na Martin Luther yatakanwa kwake. Sasa hivi nitakupa mifano kusudi usipupe pupe kana kwamba nimekunasisha kwenye mtego wa kware. Katika mada zote nakusudia kukuelimisha vyema.
MIFANO YA KUPUNGUZA VITABU SABA KULIVYOATHIRI MAFUNDISHO YA KIKRISTO
1. KWA KUKATAA KITABU CHA TOBITI, lazima mtu ukatae fundisho la watakatifu na malaika kuwa na uwezo wa kuwaombea wanadamu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na Tobiti 12:11-21. Hapa pameandikwa hivi:
“‘Sasa nitawajulisheni ukweli wote bila kuwaficheni chochote. Nilikwishawaambia kwamba yafaa kuitunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tobiti! Wewe ma Sara mlipokuwa mnasali wakati ule, mimi ndiye niliwasilisha sala zenu mbele ya Bwana aliye mtukufu. Na kila ulipokuwa unawazika wafu, mimi niliwasilisha matendo yako mbele yake. Wakati wewe hukusita hata kidogo kuinuka na kukiacha chakula ukaenda kumzika mtu aliyekufa, Mungu alinituma nikujaribu. Lakini pia alinituma kukuponya na kumwokoa mke wa mwanao, Sara. Mimi ni Rafaeli, mmoja wa wale malaika saba wanaokaa tayari daima mbele yake Bwana aliye mtukufu kumtumikia’.
“Tobiti na Tobia wakashikwa na hofu kubwa, wakasujudu wakiogopa sana. Lakini Rafaeli akawaambia: ‘Msiogope! Muwe na amani. Mtukuzeni Mungu milele. Mimi nilipokuwa kati yenu haikuwa kwa kutaka kwangu mwenyewe, bali kwa kutaka kwake Mungu. Yeye ndiye mnayepaswa kumsifu. Ninyi mlidhani mliniona nikila chakula, lakini ni kwa kuonekana tu na haikuwa hivyo. Basi, sasa mtukuzeni Bwana duniani na kumshukuru. Mimi narudi sasa kwake yeye aliyenituma kutoka juu. Andikeni mambo hayo yote yaliyokukia.’ Kisha Rafaeli akatoweka, wasimwone tena. Basi, wakamsifu Mungu kwa nyimbo, wakamshukuru kwa ajili ya matendo yake makuu aliyowafanyia malaika wake Mungu alipokuwa amewatokea.”
Kumbe, kama huna kitabu hiki katika Biblia yako lazima ushindwe kujua na kukubali kweli mbili: mosi, kwamba malaika na watakatifu wanawasilisha sala mbele ya Mungu nao wanaripoti juu ya matendo  yetu mema. Kumbe, ni kwa sababu ya ukweli huu, Wakatoliki hawasiti kuwaomba malaika na watakatifu mbalimbali wawaombee kwa Mungu. Hapo ndipo zinapoingia sala na ibada mbalimbali kwa Bikira Maria AWAOMBEE wanadamu wote, wema kwa wakosefu, wazima kwa wafu. Ukweli huu unaungwa mkono kwa kiashirio kizuri kilicho katika maombezi ya Maria kwa Yesu ili waliokuwa wanaishiwa divai wasaidiwe (soma Yn 2:1-12).
Pili, kwamba Bikira Maria, malaika na watakatifu hawaabudiwi isipokuwa kupitia kazi zao na maombezi yao Mungu anatukuzwa. Hakika ukisoma vizuri Tobiti 12:11-21, utajua kwamba Bikira Maria, malaika na watakatifu hawaombwi kwa wenyewe bali wanaombwa wasimame kama waombezi wa wanadamu “wanaolimbana” na malimwengu haya yanayowachachafya.
Lakini kutokana na mtu kukataa jambo mahali fulani, hulazimika akatae popote na chochote kitakachoelekea kupindua msimamo wake. Kumbe, kanusho moja huzaa kanusho lingine hata kama ni kwa kulazimisha tu. Ndiyo kisa basi, mtu anaposhuhudia mambo ya watakatifu kuwa na uwezo wa kuombea kwa kunukuu Ufu 5:8, 8:3-4, huwa kama anayechota maji kwa pakacha tu.
2. KWA KUKATAA KITABU CHA HEKIMA YA SULEMANI, lazima ukatae fundisho la Hekima (Roho Mtakatifu au Yesu Kristo) kuwa Nafsi ya Mungu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na Hekima ya Sulemani 9: 6.9-12. Hapa pameandikwa hivi:
“Hata kama mtu yeyote akiwa mkamilifu kiasi gani, bila Hekima atokaye kwako atakuwa bure tu. Hekima yupo pamoja nawe, naye ajua matendo yako, alikuwa pamoja nawe wakati ulipouumba ulimwengu. Hekima anajua yanayokupendeza na yaliyo sawa kulingana na amri zako. Umpeleke, basi kutoka mbingu tukufu, kutoka kiti chako cha enzi kitukufu, ili akae nami na kufanya kazi pamoja nami, nipate kujifunza yale yanayokupendeza, maana Hekima anajua na anaelewa mambo yote, naye ataniongoza kwa busara katika matendo yangu, kwa utukufu wake atanilinda, hapo matendo yangu yatakubalika, nitawahukumu watu wako kwa haki na kustahili kuwa katika kiti cha enzi cha baba yangu.”
Basi, kama huna kitabu hiki katika Biblia yako lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli kwamba katika Mungu kuna Nafsi, Mwana na Roho Mtakatifu. Kama hutakaidi kabisa basi utasema Yesu alikuwa ni mwanadamu mwema tu na Roho Mtakatifu nguvu za Mungu kutendea kazi tu. Huko ndiko kutakuwa kuzikana Nafsi mbili za Mungu kati ya tatu tunazopaswa Wakristo kuzikiri.
3. KWA KUKATAA KITABU 2 MAKABAYO, lazima ukatae uhalali wa kuwaombea marehemu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na 2Mak 12:38-45. Hapa pameandikwa hivi:
“Kisha Yuda aliwaongoza watu wake kwenda mjini Adulamu. Hiyo ilikuwa siku kabla ya Sabato, kwa hiyo wakajitakasa kadiri ya desturi ya Kiyahudi, kisa wakaadhimisha Sabato hapo. Siku iliyofuata waliona ni harakia na muhimu kukusanya miili ya wenzao waliokuwa wameuawa vitani, na kuizika katika makaburi ya wazee wao. Lakini katika kila maiti, walikuta zimefichwa nguoni sanamu ndogondogo za miungu iliyoabudiwa Yamnia, jambo ambalo sheria inawakataza Wayahudi kuzivaa. Hapo kila mtu alijua kwa nini hao walikuwa wameuawa.
“Hivyo, wakazisifu njia za Bwana, hakimu mwenye haki, afichuaye vilivyofichika na wakamwomba Bwana awafutilie mbali dhambi hiyo. Kisha Yuda yule mtu mwadilifu, akawataka watu waepuke dhambi, kwa sababu walikuwa wamejionea wenyewe yaliyokuwa yamewapata wale waliokuwa wametenda dhambi. Pia alichangisha kutoka kwa watu wake fedha ipatayo drakma elfu mbili akapeleka Yerusalemu kwa ajili ya dhabihu ya kuondolea dhambi. Yuda alifanya tendo hilo jema kwa sababu aliamini juu ya ufufuo wa wafu. Kama asingekuwa na imani kwamba wafu watafufuliwa, ingekuwa ni upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. Lakinii akiwa anatazamia tuzo nzuri waliowekewa waliokufa wakiwa waaminifu kwa Mungu hilo lilikuwa wazo jema na takatifu. Kwa hiyo, Yuda alitolea dhabihu ya upatanisho ili wapate kuondolewa dhambi zao”.
Kama huna kitabu hiki katika Biblia yako lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli huu. Wakatoliki huwa tunawaombea marehemu si kwa sababu tunampelekea Mungu maombi mapya la hasha, ila kwa sababu sala zetu zilishajulikana na Mungu kabla mtu yule hajafa, wakati mtu anakufa na baada ya mtu yule kufa. Mungu anayejua yaliyopita, yaliyopo na yajayo ndiye Mungu mwenyezi. Mungu asiyejua hivyo si mwenyezi, huyo ni sawa na Pd. Titus Amigu tu.
4. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA, lazima ukatae mafundisho ya ulazima wa imani kuwekwa katika matendo kwa maana jambo hilo limekaziwa na kitabu kizima. Kitabu hiki kilichokuwa kikitumiwa kama kitabu cha kiada mwanadamu anahimizwa aishi vyema maana ndilo deni kwa akili na utashi alivyopewa kwa kutofautishwa na wanyama wafugwao na hayawani wanaoishi kwa silika tu. Yoshua ben Sira inazungumzia uzuri wa kuishi kiadilifu katika kila uwanja, malezi, kazi, urafiki, heshima, ndoa na kadhalika. Kumbe, kwa kukikataa kitabu cha Yoshua ben Sira sawa na Hekima ya Sulemani, lazima mtu akane umuhimu wa matendo katika kumtafuta Mungu naye ajikite zaidi kwenye misimamo ya “kwa neema tu” na “kwa imani tu” maana huna mafundisho mazuri juu ya matendo yaliyotukuka. Kumbe, hapo ndipo alipolazimika Martin Luther kuishia.
5. KWA KUTAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima ukatae mafundisho ya uhalali wa kunywa divai kwa wakati wake na kiasi chake kwa maana jambo hilo limeandikwa katika YbS 31:25-31. Hapa pameandikwa hivi:
“Usijioneshe kwuwa hodari wa kunywa mvinyo, maana mvinyo umewaangamiza wengi.  Tanuru hupima ugumu wa chuma na mvinyo hupima mioyo ya watu katika shindano la wenye kiburi. Mvinyo ni kama uhai kwa mtu ukinywa kwa kiasi. Maisha yafaa nini bila mvinyo? Imeumbwa iwafurahishe wanadamu. Kunywa mvinyo wakati wake na kwa kiasi, kwaleta shangwe moyoni na furaha rohoni. Lakini kunywa mvinyo kupita kiasi kunaleta kuumwa kichwa, uchungu na fedheha. Ulevi huongeza hasira ya mpuumbavu akajiumiza mwenyewe. Humdhoofisha na kumwongezea majeraha. Usimkaripie jirani yako kwenye mvinyo, wala usimdharau anapoifurahia karamu. Usimwambie neno la kumwonya wala umsimsumbue kwa kumtaka alipe deni”.
Kumbe, kama huna kitabu hiki katika Biblia yako, lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli wa kwamba divai si haramu ikinywewa kwa wakati wake na kwa kiasi. Lakini, huu ndio ukweli uliomruhusu Yesu awe anakula na kunywa anapoalikwa na vile vile uliomruhusu awape watu waliokuwa kwenye sherehe ya harusi ya Kana divai (“oinos” siyo “gleukos”) ya kutosha.
6. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima ukatae fundisho la sakramenti ya Kitubio au Upatanisho kwa maana fundisho hilo limedokezwa katika YbS 5:4-7. Hapa pameandikwa hivi:
“Usiseme, ‘Nimetenda dhambi lakini nimepata balaa gani?’ Usitegemee kupata msamaha hata kuongeza dhambi juu ya dhambi. Usiseme, ‘Huruma yake ni kubwa, yaye atanisamehe dhambi zangu nyingi’. Kumbuka, yeye ana huruma na ghadhabu na hasira yake huwakumba wenye dhambi. Usichelewe kumrudia Bwana wala usighairishe kurudi siku hata siku. Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla na wakati wa hukumu utaaangamia.”
Hali kadhalika, KWA KUKATAA KITABU CHA BARUKU, lazima ukatae pia fundisho la sakramenti ya Kitubio au Upatanisho kwa maana fundisho hilo limedokezwa vile vile katika Baruku 4:27-30. Hapa pameandikwa hivi:
“Jipeni moyo wanangu na kumlilia Mungu kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni. Kama vile mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu mara kumi zaidi. Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa hizi atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele. Jipe moyo, ee Yerusalemu, Mungu aliyekuita kwa jina lako atakufariji.”
Kumbe, kama huna kitabu cha Baruku katika Biblia yako, lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli huu kwamba Mungu alikusudia kuwaasisia wanadamu sakramenti ya Upatanisho au Kitubio. Sakramenti hii ndiyo sakramenti inaiyotendea haki sadaka ya msalaba aliyoitolea Yesu kwa ufanisi mkubwa.
7. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima mtu ubaki katika utumwa wa kuamini ndoto hata baada ya Yesu kuufikisha ufunuo kileleni (Mk 9:7-8, Ebr 1:1-4). Lakini neno la Mungu lasema ndoto zote ni upuuzi, isipokuwa zile zitokazo kwa Mungu tu (yaani zinazotokea mara kadhaa, kuwa na ujumbe maalumu na ujumbe wake kutopingana na mafundisho ya Kanisa). Jambo hili limeandikwa katika YbS 34:1-8.
Hapa pameandikwa hivi: “Mtu mjinga huwa na matumaini ya bure na ya uongo. Ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka. Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo ndivyo alivyo mtu anayeamini ndoto. Ndoto ni kama kioo, sura inayoukabili uso. Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na uchafu? Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo? Kupiga bao, ramli na ndoto ni upuuzi, akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua. Usizitie maanani ndoto isipokuwa kama zinatoka kwa Mungu Mkuu. Maana ndoto zimewadanganya wengi na wale wanaozitumaini wameaibishwa. Sheria ni kamili bila udanganyifu huo, nayo hekima ni kamilifu kwa mtu mwaminifu.”
Kumbe kwa kutumia Biblia ndogo, kwa maana ya kwamba isiyo na kitabu cha Yoshua ben Sira mwanadamu utaendelea na kusumbuka kutafuta maana ya kila ndoto. Zaidi ya hayo, utanunua vitabu vyote vinavyodaiwa kutafsiri ndoto za watu na hali kadhalika kuhangaika kuwaendea “wafasiri wa ndoto” wote ijapokuwa wenyewe ni waongo wasiojua jambo lolote la ajabu.
8. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN SIRA TENA, lazima mtu ukatae uhalali wa dawa za asili hata kama zinatumiwa kwa uadilifu kwa maana jambo hilo limeandikwa katika YbS 38:1-14. Hapa pameandikwa hivi:
“Mpe daktari heshima anayostahili, kwa sababu ya huduma zake kwako, kwa vile naye aliumbwa na Bwana. Maana kipaji chake cha kuponya chatoka kwa Mungu Mkuu naye hupata zawadi kutoka kwa mfalme. Ujuzi wa dakrari humfanya maarufu, naye huheshimiwa miongoni mwa wakuu. Bwana  aliumba dawa zote kutoka ardhini na mtu mwenye nusara hawezi kuzidharau. Je, si kwa kijiti maji yaligeuzwa kuwa mazuri ili Mungu awaoneshs watu nguvu zake? Bwana aliwapa watu maarifa na ujuzi ili atukuzwe katika kazi zake za ajabu. Kwa dawa huwapaonya watu na kuondoa maumivu, mchanganya dawa hutengeneza mchanyiko wake. Kazi za Bwana hazina mwisho, afya yote duniani hutoka kwake.
“Mwanangu, ukiugua usiwe mzembe juu ya ugonjwa, bali mwombe Bwana naye atakuponya. Acha makosa yako, uamue kutenda mema, na kutakasa moyo wako dhambi zote. Mtolee Bwana dhabihu ya harufu nzuri na dhabihu ya unga safi. Umiminie dhabihu zako mafuta  kadiri unavyoweza kupata. Kisha mengine mwachie daktari maana Bwana ndiye aliyemuumba; usikubali akuache maana unamhitaji.  Kuna wakati ambapo kupona kuwategemea madaktari. Maana nao pia wanamwomba Bwana ili awape mafanikio katika uchunguzi wao na katika kuponya ili kuokoa maisha. Mtu aliyetenda dhambi dhidi ya  Muumba  wake mwache aangukie mikononi mwa daktari.”
Kumbe, usipokuwa na Biblia yenye nukuu hii, utakuwa “unapinduka pinduka tikitaka” nyingi za kiakili kutaka kuhakikisha kwamba dawa za asili, kwa zenyewe, ni haramu.
Nakomea hapa. Nadhani nimekujengea vyema hoja na kukutolea mifano mizuri kwamba makanisa mengine yana mungu mdogo kwa sababu ya kutumia Biblia ndogo. Kitendo cha kupunguza vitabu vya Biblia kutoka 72 au 73 hadi 66 kimetupa nje mafundisho mazuri ya Kanisa na kubana uelewa wa mafundisho yanayodumishwa na Kanisa Katoliki. Matokeo yake ya jumla ni kuzaliwa kwa mabishano endelevu kwa sababu ya kutofautiana vitabu vya rejea.
Na hili ni jambo la kawaida kama watu wanajadiliana jambo, tuseme la Fizikia, hawawezi kuelewana ikiwa mmoja anatumia muhtasari wa darasa la saba (yaani muhtasari mdogo) wakati mwingine anatumia kitabu cha Sekondari kwa mfano kitabu cha A.F.ABBOT. Kumbe, mtu anayehama kutoka Kanisa Katoliki, Kanisa lenye Biblia kubwa na hivyo lenye Mungu mkubwa na kuhamia kanisa lenye Biblia ndogo na hivyo kujihusisha na mungu mdogo lazima ajiunge katika taabu ya kwanza kujielewesha na kishapo kuyatetea mafundisho madogo. Naomba mnipate uzuri. Kwa heri kwa leo pia!

Pd. Titus Amigu