Ijumaa, 24 Novemba 2017

NI AIBU KWA MKRISTO KUPAGAWA NA SHETANI
Natamatisha mada ya Bikira Maria kutokuwa na watoto zaidi ya Yesu Kristo. Ilikuwa rahisi kama maji. Mk 6:1-6 imejibiwa vizuri na Mk 15:40.47 na 16:1-2. Acha jazba, usome sehemu hizi kwa utulivu. Yesu alikuwa mtoto pekee wa Mama Bikira Maria. Kwa kutamatisha mada hiyo, maana yake wakati wa kuwaleteeni mada nyingine ndiyo umejifungua.
Lakini, kabla sijawaleteeni mada nyingine katika mfululizo wa kujibu maswali yenu, karibuni vijana kwa kibwagizo cha mwezi. Kibwagizo chetu ni aibu kubwa tena kubwa sana kwa Mkristo kupagawa na Shetani. Lakini, hebu tuwekane sawa kabla hatujapiga mbizi kwenye kibwagizo chetu. Shetani yupo na anaweza kumpagaa mwanadamu lakini ni aibu ikiwa mwanadamu huyo ni MKRISTO. Kwa nini? Nitakujibu mwenyewe tena mara moja. Ni aibu kwa sababu ni ushahidi wa wazi kwamba kuna kitu si sawa kwake. Ni ushahidi kwamba hajasimama wima Kikristo. Mkristo alipaswa aogopwe na Shetani kwa sababu ya vipengele vinne: ushindi wa Kristo, ulinzi madhubuti alionao, silaha sita anazomvalia Shetani na mbinu aliyopaswa kuitumia. Nitaeleza kwa mapozi kipengele kimoja baada ya kingine. Haya tuanze na tufuatane vizuriMa.

USHINDI WA KRISTO: Pasina shaka yoyote Kristo amemshinda Shetani na hayo ni mapato tarajiwa ya mradi wake mkubwa wa kuwakomboa wanadamu. Mapato ya kazi ya Kristo hayakuwa ya kitoto. Yesu aliachilia kwa muda fahari zake za kimungu, akajifanya mtu kwa kuutwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake Bikira Maria ili kwa damu na nyama yake amtolee Mungu sadaka iliyotukuka kwa upatanisho na Baba. Soma sehemu zifuatazo uelewe vyema fumbo la umwilisho: Yn 1:1-14, Lk 1:26-48, Plp 2:6-11 na Ebr 10:5-10.
Kwa kifupi, Kristo amemshinda Shetani kwa niaba ya wanadamu wote. Ushindi wake siyo wa kutafutwa na tochi. Ulikuwa ushindi wa kipigo cha mbwa kwa Shetani. Kwa damu yake azizi na sadaka yake ya msalabani, yeye ameung’oa, kuharibu, kuangamiza na kuuteketeza ufalme wa Shetani na mahali pake amejenga na kupanda ufalme wa Mungu (Yer 1:4-10). Mwenyewe alisema: “Lakini ikiwa  ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwsha fika kwenu. Au anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang’anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang’anya mali yake”.
Kwa kusema hivi Yesu hakuwa anausifia ujambazi, isipokuwa kuwahakikishia wanadamu kwamba yeye ndiye “baunsa” atakayemzidi nguvu Shetani, mfalme wa dunia kwa wakati ule, na kisha kuwanyakua watu waliokuwa chini ya milki yake na kuwafanya wafuasi wake, yaani WAKRISTO. Wakristo tumenyakuliwa na Kristo kutoka ufalme wa Shetani, tukaingizwa naye katika ufalme wa Mungu kwa Ubatizo. Ndiyo maana kazi hii tukufu inaitwa Injili, yaani Habari Njema ya Furaha kwa wanadamu wa kila mwendo wa maisha (Lk 4:18). Asiyebatizwa peke yake ndiye mwanadamu anayebahatisha bahatisha  bado nje ya ufalme wa Kristo. Lakini huyo naye siku atakapobatizwa tu atajiwekea sawa mambo yake. Sasa inakuwaje Shetani aliyefungwa na Yesu Kristo aishi ndani ya yule aliyekombolewa naye? Ndipo inapokuja aibu kwa “Mkristo aliyepagawa”. Tumwulize kwa haki, kulikoni tena? Sasa naeleza kidogo mambo yanavyoshangaza kwa Mkristo anayeweweseka, kutetemeka, kulialia, kuanguka anguka na kugaagaa eti kwa kupagawa na Shetani. Jamani, mambo!

ULINZI MADHUBUTI ALIONAO MKRISTO: Mkristo analindwa kwa namna sita: amepakwa mafuta ya wakatekumeni siku ya Ubatizo wake, ana malaika mlinzi, ana majina ya Yesu na Maria, analindwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo, yupo kwenye ngome ya Kanisa na ana akili na utashi.
• Mkristo amepakwa mafuta ya wakatekumeni: Mkristo amepakwa mafuta ya wakatekumeni siku ya Ubatizo wake kwa kinga yake dhidi ya Shetani. Au tuseme hatujui maana ya mafuta yale wanayopakwa wabatizwa kifuani? Basi, leo sikiliza. Siku ya ubatizo Mkristo alipakwa mafuta ya wakatekumeni kifuani kumwinga Shetani. Sasa Shetani anarudije kuishi ndani ya Mkristo? Kama nyumba ilifagiliwa na jambazi aliyekuwa anajificha humo ametimuliwa, jambazi huyo anarudije kukaa ndani ya nyumba ile ile tena? Amepitia mlangoni au wapi? Kwa vipi mwenye nyumba amemwacha afike tena? Je, amevunja dirisha?
Hakika kuna kitu Mkristo alichofanya hata kumpatia Shetani fursa ya kurudi tena. Hakika si bure, maana imeandikwa: “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika asipate. Hapo husema, ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka’, lakini anaporudi na kuikuta tupu imefagiliwa na kupambwa, huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali yake mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu’” (Mt 12:43-45).
Je, unanibisha bado? Unataka kusema sijaeleweka? Kama hujanielewa nitakufafanulia kwa kuhoji. Shetani anapataje fursa ya kuja siyo tu kuichafua nyumba ya Mkristo bali kuja kukaa tena kama Mkristo mwenyewe hana hatia? Mkristo amefanya nini hata mafuta ya wakatekumeni aliyopakwa siku ya Ubatizo wake yakachotora (expire)? Kwa maneno mengine, Mkristo alilingana na chupa ya dawa ya kunguni, iweje kunguni aishi ndani yake tena? Ndipo inapokuja aibu kwa Mkristo mhusika.
• Mkristo ana malaika mlinzi: Kila mwanadamu amepewa malaika mlinzi mmoja wa kumlinda. Imeandikwa, “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu. Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori…” (Kut 23:20-23). Soma pia jinsi tulivyo na malaika wetu mbele ya uso wa Mungu (Mt 18:10). Je, imeeleweka sawa sawa?
Sasa nisikilize vizuri. Shetani ni malaika na malaika mlinzi ni malaika. Ikiwa ndivyo, Shetani anamshindaje tena malaika mlinzi  wa mtu hata yeye kuhamia kabisa moyoni mwa mwanadamu huyo? Bila shaka, ni kwa sababu ya Mkristo kutoshirikiana vyema na malaika wake mlinzi. Bila shaka, kwa sababu ya ufurufuru na dhambi zake binafsi, Mkristo ashikani mkono na malaika wake mlinzi. Kumbe, ndipo inapokuja tena aibu kwake.
• Mkristo ana majina ya Yesu na Maria kinywani na moyoni mwake: Majina ya Yesu na Maria “yanamtoa baruti” Shetani kwa sababu anayaogopa sana. Ni majina ya “wabaya wake” waliomshinda katika ushirikiano wao. Yaani kila majina hayo yanapotamkwa Shetani hutoka mbio. Basi, ikiwa Mkristo anayatamka majina haya pasipo Shetani kukimbia, Shetani anamjua mtu huyo kwamba ni mnafiki au anayataja majina hayo bure na pasipo heshima yoyote.
Katika kitabu cha Matendo ya mitume, watoto wa Skeva, watoa pepo wa Kiyahudi, ambao kwa kawaida walikuwa wanawatoa pepo kwa kumpachika mgonjwa vitu vya kunuka pamoja na kumtukana Shetani matusi makubwa makubwa, walilitumia jina la Yesu pasipo kumwamini Yesu mwenyewe. Shetani aliwafedhesha kadamnasi siku hiyo.
Imeandikwa hivi: “Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia,  wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: ‘Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri’.
“Watoto saba wa Skeva, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, ‘Ninamfahamu Yesu, namjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?’ Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skeva wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi ana asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote wakaingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. Waamini wengine walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya imani ya kishirikina hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha hamsini elfu. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi” (Mdo 19:11-20).
Je, unaelewa sasa ninachosema? Nakuomba leo uchague kuelewa. Kumbe, jina la Yesu si la kutaniwa na kutajwa ovyo ovyo. Ndipo, kwa Kkujibari na fedheha za mtindo wa fedheha ya watoto wa Skeva, Kanisa Katoliki liliweka Sheria ya Kanisa na. 1172 paragrafu 1 na 2 ili atakayelitumia jina la Yesu alitumie kwa hadhi yake naye afanikiwe kupunga pepo wa kweli.
Sheria hii inasema mtu wa kuwinga pepo awe padre aliyeruhusiwa na Askofu, kwa maandishi, baada ya kubainika kuwa na sifa nne binafsi: uchaji, ujuzi, busara na uadilifu. Padre mwenye sifa hizi anayeweza kufanikisha upungaji pepo wa kweli, la sivyo ni uzandiki, usanii na “upangaji miujiza” tu.
• Mkristo analindwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo: Yesu Kristo ametangaza ulinzi wa pekee kwa wafuasi wake kiasi hiki walipaswa wasimwogope Shetani kana kwamba ni yatima wa kiroho. Mtu ukiwa na kaka yako mwenye nguvu sana lazima ujisikie salama kabisa. Yesu ndiye kaka yetu wa namna hiyo, Shetani anatuhangaishaje tena? Sikiliza jinsi Yesu alivyolizungumzia jambo hili yeye mwenyewe. Tunasoma alisema ifuatavyo: “Kondoo wangu huisikia sauti yangu, nami nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele, nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. Mimi na Baba tu mmoja” (Yn 10:27-30). Sikiliza maneno hayo ya kulindwa vizuri kabisa!
Sasa, hadi Mkristo anapagawa anatokaje mikononi mwa Yesu Kristo? Ikiwa ametoka kweli mikononi mwa Yesu naye kugeuzwa “nyumba ya Shetani” kuna kitu kibaya kweli kweli alichokifanya kiroho. Ni nini hicho asichokwenda kukifuta kwenye kiti cha Kitubio? Ndipo inapokuja tena aibu kwake.
• Mkristo yupo kwenye ngome ya Kanisa: Mtu awapo na wenzake, hupata kulindwa na mshikamano wake na wenzake. Kule kuwa kati ya watu wengi tu ni ngome ya ajabu. Wingi wa wanakanisa ni ngome. Mtu aliye ndani ya ngome yupo salama. Mtu aliyejishikamanisha na kundi ni salama, hata awe ni mzee sana, mgonjwa sana au mtoto sana. Kinyume chake, mtembea pweke, au mtu yeyote awapo nje ya ngome huwa chambo cha Shetani anayezunguka zunguka huko na huko akitafuta mtu anayezubaa zubaa ammeze (1Pet 5:8). Kifupi, nje ya ngome ya Kanisa si salama. Mtu kutembea na kulala nje ya ngome ya Kanisa ni kujihatarisha mwenyewe. Shetani hawezi kumvaa Mkristo aliyekamilika isipokuwa “mzee katika imani”, “mgonjwa katika imani” au “mtoto katika imani”. Mtu kama huyo ni chambo rahisi cha Shetani.
Lakini, ilitakiwa chambo cha Shetani asiwe Mkristo bali mtu wa imani au dini nyingine asiyeishi katika ngome ya Kanisa kwa kuwa hajaiingia bado. Sasa ikiwa kweli Mkristo amepagawa na Shetani anatupa ushahidi kwamba ametoka nje ya ngome ya Kanisa. Ni ushahidi kwamba hana mshikamano wa kweli na Kanisa. Lakini ni kwa nini? Kumbe, ndipo inapokuja aibu kwake. Aheri mtu kama huyo ajirudishe haraka haraka ndani ya Kanisa.
• Mkristo na akili na utashi: Vipaji vya akili na utashi ndivyo vinavyomfanya mwanadamu awe sura na mfano wa Mungu (Mwa 1:26-28). Kwavyo anaweza kuchagua mema na kukataa mabaya. Lakini ikiwa mtu hatumii vipaji hivi anakuwa dhaifu kama ng’ombe au mbuzi vile. Na mtu dhaifu namna hiyo, Shetani anampenda kiasi cha kuhamia kwake moja kwa moja kwani si chochote isipokuwa mtu laini kama mchicha, tembele au mlenda. Kifupi, mtu wa namna hiyo ni mboga ya Shetani.

SILAHA SITA MKRISTO ANAZOMVALIA SHETANI: Mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso amependekeza silaha sita za kumvalia Shetani: ukweli, uadilifu, hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani, imani, kuupokea ukombozi na neno la Mungu.
Kuhusu jambo hili, Mtume Paulo ametuandikia ifuatavyo: “Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama dirii kifuani, na hamu ya kutanga Habari Njema ya amani iwe kama buti miguuni mwenu. Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. Ukubalini ukombozi kama kofia yenu ya chuma (helmeti) na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu” (Efe 6:14-18).
Kutokana na haya, Mkristo anayetutangazia wenzake kwamba amepagawa na Shetani anatuambia kwamba ametindikiwa ukweli, uadilifu, hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani, imani, kukubali ukombozi na neno la Mungu. Je, kali eh? Ukweli ndiyo ulivyo hautazami sura wala majira. Basi, ndivyo lilivyo neno la Mungu linakata pale mfupa ulipoungana na nyama! Mkristo aliyepagawa na Shetani anatupa ushahidi wa wazi kwamba hajamvalia Shetani silaha zilizopendekezwa na Mtume Paulo, yaani ni kama mtu anayetembea katika nchi ya baridi na fulana tu.

MBINU ALIYOPASWA MKRISTO KUITUMIA: Yakobo alitoa mbinu nzuri ya kumshindia Shetani ndiyo kumpinga Shetani na kumkaribia Mungu. Ameandika hivi, “Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Shetani naye atawakimbieni. Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenye enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki! (Yak 4:7-8). Kumbe, kwa maneno haya, Mkristo kupagawa na Shetani ni ushahidi kwamba hajafanya juhudi za kutosha kumpinga Shetani na wala hajafanya juhudi za kutosha kumkaribia Mungu. Kifupi, Mkristo huyo ana hatia binafsi. Ndipo hapo inapokuja tena aibu kwake.

HATIMA
Narudia mara kurudia. Kwa Mkristo kupagawa na Shetani ni dalili ya shida yake mwenyewe, yaani dhambi yake mwenyewe. Kwa sababu hii ilikuwa aone haya na hivyo ajifiche mbele ya Wakristo wenzake. Ilikuwa augue peke yake moyoni mwake na kujirudi katika vipengele nilivyovieleza katika kibwagizo hiki. Niruhusu nitumie lugha ya picha kali sana. Ashkum si matusi, Mkristo kupagawa na Shetani ni kama mtu mzima kutokwa na haja ndogo au kubwa hadharani, ni aibu.
Ni aibu kwa sababu mtu mzima asiye mgonjwa, anategemewa kujizuia asitokwe na haja mbele ya watu. Kumbe, mkasa kama huo huonewa haya ya uso. Hauonewi fahari, isipokuwa humlazimisha mtu mzima kwenda kujificha mahali pa faragha, kujisafisha, kujitia manukato na kurudi hadharani kwa soni ya aina yake. Hivi ingekuwa aibu kwa Mkristo kutetemeka, kuweweseka, kulialia, kuanguka na kugaagaa hadharani, mathalani, kwenye mkutano wa sala, kongamano seuze kanisani kwa hoja eti amepagawa na Shetani. Ni aibu kwake mwenyewe na aibu isionewe fahari.
Lakini, ajabu siku hizi Wakristo, tena si mmoja bali kwa makumi na mamia, wanakula mieleka hadharani na kugaagaa eti wamepagawa na Shetani. Ajabu ya Firauni! He, Shetani amewajaa Wakristo hivi, kana kwamba Kristo hamkumshinda Shetani kwa niaba yao! Aibu! Jamani, aibu! Wakristo wengi hivi wana mapepo! Huku ni kuufedhehesha Ukristo. Eti watu wakisema hawautaki Ukristo kwa sababu Wakristo wengi ni “nyumba za Shetani”, tutashangaa! Tutashangaa nini wakati tunasema hivyo kwa vitendo vyetu wenyewe? Tushangae nini, kwani watu hawatuoni tunapoanguka hadharani kama embe dodo? Jamani, mchezo wetu ni kifo cha dini yetu wenyewe. Tukome kuuaibisha Ukristo hivi. Tukomeke!
NATOA MWITO. MAMBO YA KUPAGAWA, TUSIFANYIE MASIHARA KWA HESHIMA YA DINI YETU YA HESHIMA SANA. TANGU SASA, KILA MKRISTO AONE AIBU KUDHIHIRIKA KWAMBA AMEPAGAWA NA SHETANI. NI AIBU INAYOTANGAZA HADHARANI KWAMBA HAYUKO SAWA KIIMANI NA AIBU HAIONESHWI NJE. KAMA MTU UNA PEPO CHUTAMA KWENYE KONA YA MBALI HUKO USAIDIWE SIRINI NAWE UTAPONA.
LAKINI KABLA YA MSAADA MWINGINE WOWOTE JIPELEKE MWENYEWE KWANZA KWENYE KITUBIO UKAONDOE HICHO KILICHOMFUNGULIA SHETANI MLANGO WAKO! NAKUOMBA USIJISINGIZIE KUTOKUWA NA DHAMBI (REJ. 1YOH 1:8-110). LAKINI KAMA KWELI HUNA DHAMBI YOYOTE, BASI, SHIDA YAKO NI YA KISAIKOLOJIA TU. HUENDA NI NUROSISI AU SKIZOFRENIA AU “MULTIPERSONALITY” AU UMANYETO (HYSTERIA) NA KADHALIKA. KAMA NDIVYO ITENGENEZE SHIDA HIYO KWA MATIBABU YA KISASA (PSYCHOTHERAPY)! USISUBIRI TENA KITU. UKICHANGANYIKIWA ZAIDI UTAPELEKWA MIREMBE BURE! OOOH! HUKO MBELE USISEME HAKUKUWA NA PADRE ALIYEONYA. HAITAKUWA KWELI, NILIKUWEPO MIMI!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni