Jumanne, 11 Julai 2017

JINA JEHOVAH SI JINA LA MUNGU ISIPOKUWA KOSA BAYA
Leo nawaleteeni jibu la swali moja kati ya mengi mliyoniuliza enyi vijana. JIbu ni refu lakini someni kwa utulivu. Ni juu ya jina JEHOVAH. Hali halisi ni kwamba kuna watu tunasadiki kuwa jina ‘JEHOVAH’ ni jina pekee la Mungu kwa vile linatokea mara 6832 katika Biblia zetu za Kiswahili au Kiingereza. Ndipo tunatamka kwa mbwembwe jina hilo na kuendeshea makongamano na sala kwa sauti za juu kabisa. Lakini nawataarifuni kwamba tumedanganyika na tumepotea kwa sababu hatujui jina hilo lilikotokea na hata watafsiri wa Biblia hawajachukua hatua ya kuondokana nalo. Kifupi, jina “Jehovah” ni mapato ya kosa la usomaji Kiebrania kimbumbumbu lililofanywa na Padre Peter Galantin, muungamishi wa Baba Mtakatifu Leo X na labda kabla yake kama inavyosomeka pia katika maandishi ya Raymond Martin (1270 B.K. hivi). Unajua, usilolijua ni kama usiku wa giza.
Usishtuke, nitakuelezea sasa hivi kosa lilivyofanyika. Lugha ya Wayahudi au Waisraeli ni Kiebrania, kama ilivyo lugha ya Watanzania Kiswahili. Hivyo Wayahudi wanazungumza Kiebrania. Ndiyo lugha waliyozungumza kabla ya kuchukuliwa utumwani Babeli. Lakini wakati wa utumwa wa Babeli hadi waliporudi kutoka utumwani na kisha kuendelea hadi wakati wa Yesu lugha yao ya siku kwa siku ilikuwa Kiaramayo, ijapokuwa Biblia yao, ndiyo Agano la Kale, kwa ujumla wake, iliendelea bado kusomwa katika Kiebrania chao cha zamani. Baadaye walipotawaliwa na Wagiriki (Waseleusidi), Wayahudi wakapaswa wajifunze Kigiriki (Kiyunani). Tangu mwaka 63 K.K., wakoloni wapya Warumi walipowafurusha Wagiriki wakaishika pia Israeli (Uyahudi), Wayahudi wakalazimika kujifunza Kilatini pia. Kumbuka, Kilatini ilikuwa lugha ya watu wa Dola ya Kirumi (ndio tunaowaita Warumi).
Ndiyo kisa wakati ule wa Yesu, nchini Israeli (Uyahudi) kulikuwa na lugha nne: Kiebrania, Kiaramayo, Kigiriki na Kilatini. Lugha hizo zilitumika ifuatavyo. Walisoma Maandiko Mtakatifu hekaluni na katika sinagogi katika Kiebrania; mitaani walizungumza Kiaramayo; askari wa Kirumi na wengine waliojifunza kwa  wepesi walizungumza Kilatini na wasomi waliandika na kuzungumza Kigiriki. Ndiyo maana kibao cha mashtaka ya Yesu kiliandikwa katika lugha tatu: Kiebrania (kwa kweli kwa maana ya Kiaramayo) kwa ajili ya Wayahudi kusoma, Kilatini kwa ajili ya askari wa kigeni na wengineo na Kigiriki kwa ajili ya wasomi (rej. Yn 19:20).
Baada ya nchi ya Uyahudi kuanguka na Wayahudi kutawanyika (mwaka 70 B.K), kokote walikotawanyikia walijitahidi kurudi kwenye Kiebrania chao. Madhulumu na mateso waliyopewa na Adolf Hilter, kule Ujerumani, kabla na wakati wa vita kuu ya pili ya dunia (1939-1945) yaliutia ulimwengu zimanzi na wazo la kurudi Israeli na kujenga tena taifa lao likazaliwa.
Ndipo tangu mwaka 1948, kwa msaada wa Umoja wa Mataifa (wa wakati ule) na wa mataifa makubwa ya Marekani na Uingereza,  Wayahudi walisaidiwa kurudi nyumbani kusudi wakalijenga upya taifa lao. Tangu taifa la Israeli lilipozaliwa (mwaka 1948), Kiebrania kikashika kasi, lakini Kiebrania kilichobadilika katika mengi. Hata hivyo, katika Biblia yao (ndiyo Agano la Kale), Kiebrania kimetunzwa kile kile cha zamani kwa maana wanaamini hakuna ruhusa kubadili neno la Mungu. 
Ndiyo kisa Kiebrania kinachozungumzwa siku kwa siku siku hizi kimekuwa kipya, yaani kinatofautiana kwa namna fulani na Kiebrania cha kwenye Biblia yao. Tofauti hiyo ni kama iliyopo kati ya Kilatini na Kiitaliano, au kati ya Kilatini na Kireno au kati ya Kilatini na Kihispania. Usihangaike. Hatujapotea njia, nilitaka kukujuza japo kidogo historia ya Wayahudi. Sasa turudi kwenye neno letu la “JEHOVAH”.
Katika Kiebrania chao, Wayahudi huandika jina la Mungu wao kwa herufi nne YHWH. Hiyo herufi ya kwanza “Y” unaweza pia kuiandika na kuitamka kama “J” na hivi kuwa JHWH. Halafu hiyo herufi ya tatu “W” unaweza pia kuiandika na kuitamka kama “V” na hivi kuwa JHVH. Herufi hizi ndizo zinazofumbata lile jina aliloambiwa Musa katika Kut 3:14. 
Basi, herufi za jina la Mungu wa Wayahudi huandikwa kwa herufi hizo nne YHWH au JHVH. Kwa Wayahudi hizo ni herufi takatifu kabisa, tena takatifu bin mno. Katika ulimwengu wa  taaluma ya Biblia ni herufi zinazojulikana kwa istilahi maarufu “tetragrammaton”. Hebu nirudie na kusisitiza, herufi hizo ni herufi takatifu kabisa kabisa.
Sasa tuje kwenye uandikaji na usomaji wake. Herufi hizo zinapoandikwa katika Kiebrania huandikwa kwa kupindua, yaani herufi inayosomeka katika nafasi ya kwanza katika Kiswahili chetu, ndiyo ya mwisho katika uandishi wa Kiebrania. Kwa nini? Kwa sababu Wayahudi huandika na kusoma lugha yao ya Kiebrania kwa kuanzia kulia kwenda kushoto, yaani hivi HWHY. Uandikaji na usomaji huu wa kutoka kulia kwenda kushoto unalingana na uandikaji na usomaji wa lugha nyingine za Kisemiti, hususan, Kiaramayo na Kiarabu.
Nifuatilie vyema. Nimeshadokeza hapo juu kwamba herufi hizo nne (ndiyo tetragrammaton) zinatokea mara 6832 katika Biblia ya Wayahudi, ndiyo tunaloita sisi Agano la Kale. Sasa sikiliza kiroja hiki. Ijapokuwa herufi hizo zinatokea mara nyingi hivyo kwenye Biblia yao, Wayahudi wote wa kawaida walikuwa na bado hawaruhusiwi kuzisoma, si kwa sauti wala kwa kimya kimya kwa sababu ya utakatifu wa jina la Mungu wao. Kwa nini? Kwa sababu kuzisoma bure bure kungelingana na utovu wa heshima kwa Mungu mkuu na kuivunja amri ya Mungu ya kutolitaja bure jina lake.
Ndipo ilikuwa marufuku na bado ni marufuku kabisa Myahudi wa kawaida kuzisoma na kuzitamka herufi hizo. Hapo ndipo utakaponiuliza: Sasa walifanyaje walipokumbana na herufi hizo mara 6832 katika Maandiko yao matakatifu? Tulia nikueleze sasa hivi. Ni hivi, kusudi watu wasizisome wala kuzitamka, hususan watoto, Wayahudi walifundishana kuziruka kwa kutamka mojawapo ya maneno manne ya mbadala ‘ADONAI’ (Bwana wangu), au MAQOM (Mahali), au SHEM (Jina) au SHAMAIM (Mbingu). Hata hivyo, kati ya mibadala hii minne, wengi walipendelea sana kutumia mbadala wa ‘ADONAI’.
Ndipo kwa mibadala yao hiyo minne, hakukuwa na taabu ya kuzidi kwa Wayahudi wenyewe, maana kila walipokumbana na herufi hizo walisoma “kwa raha zao”  ‘ADONAI’, au MAQOM, au SHEM au SHAMAIM. Lakini hatari ya watoto kuzisoma herufi zile kwa kukosa kuzoea  mibadala iliyokuwa ikijulikana na wakubwa wote iliendelea pale pale.
Hebu sikiliza kitu kingine. Kabla ya karne ya 11 K.K., maneno yote ya Biblia ya Wayahudi yalikuwa yameandikwa kwa konsonanti tu. Yaani kama katika Kiswahili chetu, kwa neno “mama”, tungeliandika “mm” tu, kwa neno “baba” tungeliandika “bb” tu, kwa neno “kuku” tungeliandika “kk” tu, kwa neno “mimi” tungeliandika “mm” tu, kwa neno “kiko” tungeliandika “kk” tu, kwa neno “bibi” tungeliandika “bb” tu, kwa neno “korokoroni” tungeliandika “krkrn” tu na kadhalika. Kutofautisha kati ya “kk” ya “kuku” na “kk” ya “kiko” ingelitegemea mazoea na muktadha tu.
Baadaye, Wayahudi waliamua kurahisisha usomaji wa lugha yao kwa kuzitia vokali.  Basi, waandishi wao walioitwa Masoreti walifanya kazi kubwa ya kutia vokali maneno yote ya Biblia yao katika karne ya 11 K.K.
Lakini sikiliza jambo lingine, vokali za Kiebrania huandikwa chini ya konsonanti (isipokuwa katika maneno machache sana mbele ya konsonanti). Hivi katika usomaji, unaanzia kulia, unachukua konsonanti juu na kuokotea vokali yake chini (au katika maneno machache mbele yake) ili kujenga silabi na hivyo hivyo kuendelea kushoto hadi unamaliza neno na mstari wako unaosoma.
Sasa waandishi hao kwa kukinga hatari ya watoto na hata wakubwa wengine wenye papara, wasisome herufi takatifu “YHWH” au “JHVH” waliandika vokali  za mbadala wao maarufu “ADONAI” chini ya herufi hizo takatifu. Vokali za jina “ADONAI” ni e, o na a zilizoandika pia kutoka kulia kwenda kushoto kadiri ya herufi “YHWH” au “JHVH” zilizoandikwa vile vile kutoka kulia kwenda kushoto. Hivi wakaandika e, o na a chini ya herufi “HWHY” au “HVHJ”. Ndipo ikawa imefanana na hivi, “HaWoHeY” na “HaVoHeJ” ila soma kwa kujipindua, yaani kutoka kulia kwenda kushoto. Sasa angali hatari. Hapo haikutakiwa kuziunganisha konsonanti na vokali hivyo, kwani hizo konsonanti zilikuwa za jina takatifu lisilopaswa kutamkwa na hizo vokali zilikuwa za jina “ADONAI” lililoruhusiwa na kutakiwa kutamkwa.
Sasa Padre Peter Galantin alifanyaje kosa lake la kiusomaji? Alifanya ifuatavyo. Katika kutokujua kwake kwamba konsonti “HWHY” au “HVHJ” zilikuwa za jina takatifu lisilopaswa kusomwa wala kutamkwa na Myahudi wa kawaida na vokali e, o na a zilikuwa vokali za jina mbadala “ADONA” akasoma kwa kuunganisha kila kitu kama nilivyoonesha hapo juu. Yaani akachanganya mambo, konsonanti HWHY au HVHJ ambazo zilikuwa ni jina la  Mungu lisilotamkwa na Wayahudi wa kawaida na vokali e, o na a za jina la mbadala ‘ADONAI’ (Bwana wangu) lililoruhusiwa kutamkwa na mtu yeyote yule kama mbadala wake. 
Ndipo katika kosa hilo, akasoma kimbumbumbu kutoka kulia kwenda kushoto na kupata HaWoHeY au HaVoHeJ yaani YeHoWaH au JeHoVaH ndiyo YEHOWAH au JEHOVAH. Kumbe, hili kosa la mwaka.
Nadhani sasa unaelewa na wala hujalewa. Kumbe alichokifanya Padre Peter Galantin siyo tu kilikuwa hakikubaliki kati ya Wayahudi wenyewe bali ilikuwa pia kufuru kubwa. Kwa nini? Kwa sababu usomaji wa herufi zile nne (tetragrammaton) ulikuwa mtakatifu sana na wa pekee sana. Nimeshasema konsonanti hizo zilikuwa zimekatazwa kutamkwa na watu wa kawaida. Niulize tu wala usisite: Sasa zilikuwa zinasomwaje au lini?
Nisikilize vyema. Herufi hizo zilikuwa zinasomwa NA KUHANI MKUU PEKE YAKE, TENA SIKU MOJA TU KATIKA MWAKA PALE ALIPOINGIA PEKE YAKE PATAKATIFU PA PATAKATIFU. Hiyo ilikuwa katika siku ile ya toba ya taifa (ndiyo Yom Kippur). 
Basi, kwa jinsi hii, waamini wa kawaida hawakuwa hata na picha ya matamshi yake.  Sasa kama Wayahudi wa kawaida hawakujua na hawajui hata leo hii namna ya herufi zile zinavyotamkwa wewe na mimi watu wa Bongo hii tunajinasibu vipi kujua zinavyotamkwa? Eti, tujue sisi wakati Wayahudi wenye Biblia yao hawajui? Lazima sisi tuwe waongo wa kutupwa. Kumbe, tunasema uongo mubashara!
Naongeza kusema. Nakwambia hivi, hata matamshi  ya “YAHWEH” ni matamshi ya kusadifisha tu. Wote sisi hatujui jinsi herufi “YHWH” au “JHVH” zilivyotamkwa. Usinikaidi. Watafute hata Wayahudi wenyewe popote pale walipo, kwa karibu zaidi hapo jijini Dar es Salaam, uwaulize, watakwambia hawajui, sasa wewe na mimi ni nani katika suala hili hata tujidai na jina YEHOVAH? Basi, ni uongo wetu na aibu yetu. Nawasihini tuachane na jina YEHOVAH. Sisi Waafrika na Waswahili, jina MUNGU linatutosha kabisa. Tusiyatake makubwa tusiyoyaweza wala kuyajua.
Acha niongeze kusema tena. Tena siku hizi matamshi ya herufi hizo takatifu yametatizika zaidi na zaidi kwa sababu, kwa vile Wayahudi hawana tena Makuhani Wakuu na wala hekalu lao halipo tena, siyo tu hawana mtu wa kuzitamka bali hawana pia hata mahali pa kuzitamkia hata kama ni hiyo mara moja kwa mwaka. Hii maana yake hata namna ya kuzitamka herufi hizo kunapotelea kabisa angani.
Sasa namaliza somo langu. Nakupeni mfano wa kosa lilozaa matamshi yasiyojuzu ya YEHOWAH au JEHOVAH. Kosa hili tukilieleza kwa mfano wa Kiswahili ni hivi ifuatavyo. Waswahili tunamwita Muumba mbingu na nchi “MUNGU”. Sasa ingelikuwa kwamba jina hilo haliandikwi kwa herufi zote isipokuwa konsonanti MNG tu na kisha Waswahili wa kawaida tungelikuwa tunakazana na kuzitamka isipokuwa Askofu Mkuu tu, tena mara moja tu kwa mwaka pale angalipojificha nyuma ya altare peke yake. Na kwa watu wa kawaida tungelikuwa tunaruhusiwa kutamka jina “BWANA” kila herufi “MNG” zinapoonekana katika Biblia yetu. Baadaye upitishwe uamuzi wa kuandika vokali za jina BWANA yaani a na a chini ya konsonanti “MNG” kama hivi MANGA kwa kusudi la kuwasaidia wasomaji, hasa watoto, wasome neno BWANA bila kutamka herufi tukufu na takatifu “MNG”.
Halafu baada ya karne nyingi Biblia iwafikie labda Wachina ambao hawajui Kiswahili vizuri na halafu mmoja wao adhani kwamba kuandika MANGA ni sawa na yeye anyooshe usomaji wa jina MNG kwa kuunganishia vokali A na A za jina BWANA na hivyo ahitimishe kwa kusema jina la Muumba mbingu na nchi kwa Waswahili ni MANGA. Hapo Mchina huyo angelikuwa amewaingizwa wenzeke kwenye kosa la mwaka na ndipo jina MANGA lisingekuwa jina halisi la Muumba mbingu na nchi bali jina la utani mkubwa. Basi, ndivyo linavyofanana na kosa lililoibua matamshi ya YEHOWAH au JEHOVAH.
Kwa vyovyote iwavyo tumepotezwa na kosa la kiusomaji la Padre Peter Galantin na wote tunaotamba na matamshi hayo JEHOVAH hatujui tunachotamba nacho. Ni kama siku hizi sisi watu weusi tunavyotamba na jina baya kama “NIGGAZ” wakati ni tusi la Wamarekani weupe kuwatukania weusi wenzetu. Ni kama mtu asiyejua Kiingereza anavyoweza kuvaa T-shirt iliyoandikwa “MORTUARY ATTENDANT” (yaani mhudumu wa chumba cha maiti) kwenye sikukuu. Ni kama mkulima maskini anayetamba kijijini na T-shirt ya mtumba iliyoandikwa “SEX PISTON” na kadhalika. Maskini tuhurumiane! Lakini sasa kisomo kinatuwekea wazi kosa la matamshi ya JEHOVAH lilivyotokea, kumbe tuamue kukubali na kujinasua kutoka matamshi hayo batili. Wala si aibu kurudi nyuma na kuacha. Yeyote anayehusika, wakati ni leo.
Kumbe, basi, kati ya maneno ya kuondolewa kwenye Biblia zetu za Kiswahili na Kiingereza, pale zitakapofikia fursa zingine za kuboreshwa, ni neno JEHOVAH. Tulieni, nitawaonesheni maneno mengine katika nafasi zingine za usoni. Hiyo si kazi ya kila mtu, isipokuwa ni kazi ya watafsiri wa Biblia, yaani wale watu waliosomea Sayansi ya Biblia. Natumaini tumeelewana. Kwa herini, kwa leo!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni