Katika suala la Sabato, asisingiziwe mtu yeyote..
SWALI SI NANI KAIBADILI SABATO ISIPOKUWA NANI KAIRUDISHA
Vijana tumepafikia mahali patamu katika mada ya aibu ya Sabato. Mimi nilipataka hapo hapo. Sasa macho yenu yamefumbuliwa. Mpewa ushahidi wa kigeugeu cha wanaojinasibu kujua Biblia. Mnajionea wenyewe, linapokuja suala la Sabato, wale wale wanaojidai kunukuu Biblia kwa ushahidi wa kila kitu, pasipo haya, huiruka na kwenda kuwanukuu wanadamu. Kwa ajili ya swali la sabato watakwenda kunukuliwa Mfalme Konstantiono, au Kardinali fulani, au Papa fulani, au katekisimu fulani au kitabu fulani cha Kanisa Katoliki.
Leo Biblia imewekwa pembeni kabisa. Mnaona hapa ametajwa kardinali mmoja, mihadhara na katekisimu. Ndiyo hivyo haikuguswa Biblia isipokuwa Cardinal James Gibbons (1978); Catholic Priest T. Enright CSSR, Lecture at Hartford; Catholic Records (September 1, 1923), Ferraris Roman Catholic Prompta Bibliotheca, Vol. VI; Catholic American Sentinel (1893) na The Convert’s Cathechism of Catholic Doctrine (1957). Sina hakika kama maandishi haya wanayajua na wamesoma kweli. Nina mashaka hivi kweli « Umombo » unatosha kusomea maandishi hayo? Wamesoma au wamesomewa. Na sijui hata kama wanayo. Mimi sijui.
Biblia imewekwa kando kabisa. Sana sana kama ni Maandiko, mtaona watakapotoa utetezi wa ziada, watakwenda kunukuu Agano la Kale na kukwepa nukuu za Agano Jipya. Watanukuu Agano la Kale utadhani wao ni Wayahudi. Kumbe, hiyo ndiyo njia ya mwongo inavyokwenda. Ni fupi kama mkia wa mbuzi. Watakwenda mbele na kurudi nyuma wakati huo huo, kwa kuwa hawatakuwa na pakushikia. Watakuwa wameleweshwa na hadithi za binadamu tu, akina William Miller, Samwel Snow, Hiram Edson, Joseph Bates na Ellen White. Vijana msizugike. Wanaowasumbueni wala hawafuati Maandiko isipokuwa hadithi na ndoto za hao watano niliowataja kwa majina.
Kumbe, Wakristo tuache masihara. Tuache kuruka tikitaka hivi. Leo ni leo naomba tubaki kwenye Biblia. Katika suala la Sabato, asisingiziwe mtu yeyote. Mungu mwenyewe ndiye aliyeifuta Sabato. Nukta. Soma Biblia katika sehemu tano zifuatazo, zinatosha kabisa: Isa 1: 13, Hos 2 :11, Ebr 4: 4-10, Kol 2: 16-17 na Rum 14: 1-10. Naomba uzisome kwa mfululizo huu huu, utabaini ninachosema. Tafadhali usirukeruke.
Basi, kwa aya hizo, swali tunaloulizwa Wakatoliki ni batili. Eti tunaulizwa « Nani kabadili siku ya sabato kwenda Dominika au Jumapili? » Si hivyo. Mtu akisoma kweli Biblia, swali halisi ni: « Nani kairudisha Sabato? » Kitu kilitupwa nani kakiokota tena? Nani kaurudisha mkeka wa zamani?
Sasa kusudi msipate tabu ya kutafuta Biblia kuhakikisha ninayosema nanukuu mwenyewe aya nilizopiga hapo juu.
Kifupi, Isa 1 :13 na Hos 2 :11 zinaeleza kwamba Mungu alichukizwa na Sabato na akaahidi kuifutilia mbali.
Isa 1 :13 inasema: « Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana, ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, SABATO na mikutano ya ibada. Sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. »
Sikieni anavyosema Mungu mwenyewe siyo Mfalme Konstantino, Papa fulani, au Kardinali fulani au katekisimu fulani. Mungu mwenyewe anasema sabato ilikuwa ni ibada isiyo na maana na ibada iliyochanganyika na dhambi.
Hosea 2:11 inasema “Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato na sikukuu zote zilizoamriwa.” Mungu anaahidi kuifutilia mbali na Mungu hasemi uongo. Alifanya kweli.
Ebr 4 :4-10 inaeleza kwamba Sabato ilikuwa kazi bure. Haikutimiza malengo yake na hivyo Mungu anaifuta na kuiweka siku nyingine (ndiyo Dominika – Jumapili - yaani siku ya Bwana ndiyo siku ya matukio yote makubwa – kufufuka, kuwatokea mitume, Pentekoste na hivyo kuanzisha Kanisa. Tusome: “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuiogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanyikana na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile: Kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu.
Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingalinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi yake. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano huo huo wa kuasi.”
Kol 2 :16-17 inaeleza kwamba Sabato ilikuwa kivuli na sote tunajua kivuli huwezi kukishonea suti labda uwe umekunwa « viroba ». Tusome: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.
Rum 14 :1-10 inasema mtu anayeililia Sabato ana imani dhaifu naye ni mtu wa kuhurumiwa tu. Tumeagizwa tusibishane naye, isipokuwa tuachane naye tu. Tusome: “ Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye kuhusu mawazo yake binafsi. Watu huhitilafiana mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kita kitu naye ambaye hula mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu maana Mungu anamkubali.
Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku; mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe, je! mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.”
SASA TWENDE KATIKA VINAGANAGA
SWALI: JE, NANI KAIRUDISHA SABATO KWISHA KUFUTWA NA MUNGU?
Mashtaka: Wakatoliki wote na viongozi wao hasa Papa wameibadili Sabato kwenda Dominika (Jumapili). Mfalme Konstantino pia ndiye hasa aliyeyafanya mabadiliko hayo na hivyo, kwa vyovyote, ni binadamu na siyo Mungu aliyefanya mabadiliko hayo. Kwa hali hiyo Wakatoliki wanafuata mapokeo ya wanadamu!
Jibu fupi: Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalifanywa na Mungu mwenyewe na mwisho wenyewe umetangazwa mara nne katika Biblia. Zizome sehemu hizo kama zinavyofuatana hapa: Hos 2:11, Ebr 4:4-10, Rum 14:4-10 na Kol 2:16-17. Kwa kifupi kabisa, Biblia inasema Mungu mwenyewe ndiye aliyebadili. Kilichotokea ni aibu tu, yaani waasisi wa Kanisa la Sabato kuirudisha sabato ambayo ilishatupwa na Mungu na Wakristo wa kwanza wakaanza kuitumia siku mpya, ndiyo Jumapili. Lakini bahati mbaya na kiroja cha mwaka ni kwamba Wasabato hawawaruhusu watu kuijua historia ya kurudishwa kwa sabato kwa mbinu mbili. Mosi ni kwa mbinu ya kukatazwa vitabu vya historia vinavyoelezea mkasa na aibu hiyo na pili kwa kufanya juhudi kubwa ya kulitukana Kanisa Katoliki ili watu wasiwe na muda wa kulitazama na kulihoji Kanisa la Sabato. Lakini, basi katika kijitabu hiki mimi ninajitolea kukufunulia aibu hiyo. Makinika nami.
Jibu refu: Mabadiliko Yalitabiriwa, Yalitangazwa, Yalifanywa na Yalitekelezwa
Biblia ipo wazi kabisa kuhusu mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili). Tufuatane.
Mosi, mabadiliko hayo yalitabiriwa na Hosea (rej. Hos 2:11-13). Yeye alitabiri akisema, “Tena nitaikomesha furaha yake yote na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi na sabato zake na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.”
Pili, mabadiliko hayo yalifafanuliwa kwa maneno na matendo ya Yesu Kristo (rej. vifungu mbalimbali vya Injili, hususan, Mt 12:1-12, Mk 3:2-4, Lk 13:14-16, 14:1-5, Yn 9:16). Hata hivyo, Yesu hakueleweka wala kuaminika kutokana na fikra mgando za watu wa wakati ule, wakiwamo hata mitume wake mwenyewe.
Tatu, mabadiliko yametangazwa katika Ebr 4:4-10. Hapa tunasoma hivi, “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuiogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanyikana na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile: Kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu.
Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingalinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi yake. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano huo huo wa kuasi.”
Nne, Sabato imebainishwa kuwa ilikuwa kivuli tu Kol 2:16. Hapa tunasoma hivi, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.
Na hatimaye siku zote zimetangazwa katika Rum 14: 4-10 kuwa sawa mbele ya Mungu mwenyewe na kwamba anayegombea kutambuliwe tofauti ni mtu mwenye imani dhaifu, anayehitaji kuhurumiwa. Hapo tunasoma ifuatavyo tokea aya ya kwanza: “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku; mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe, je! mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.”
Hiyo ndiyo Barua kwa Waebrania, barua ambayo inatangaza vifo vya vitu vingi. Mambo mengi yalipinduliwa hivyo na Mungu mwenyewe. Hebu nikuorodheshea kidogo mambo yanayosimuliwa na Barua kwa Waebrania kwamba yalikufa kwa kusudi ya kuyapisha mambo mapya muhimu ya Agano Jipya. Inasimulia kwamba hekalu la Yerusalemu lilikufa kulipisha hekalu la kweli, yaani makazi ya Mungu mwenyewe mbinguni; ukuhani wa Kiyahudi ulikufa kuupisha ukuhani mkamilifu na wa milele wa Yesu Kristo pamoja na watu wote wanaobatizwa katika jina lake na sadaka za Kiyahudi zilikufa kuipisha sadaka timilifu ya Yesu Kristo msalabani. Kumbe ni katika tangazo hili la kifo, kitabu cha Ufunuo kinapotangaza kwamba Sabato iliuawa kuipisha Siku ya Bwana, yaani Jumapili.
Bila shaka Maandiko Matakatifu haya yanakukonga roho na kukubainishia kwamba mabadiliko yalifanya na Mungu mwenyewe. Tazama, tumesoma kwamba Mungu mwenyewe alimtabirisha Nabii Hosea mabadiliko aliyoyakusudia kutoka Sabato kwenda Jumapili yaani Dominika. Halafu, tumezitaja nukuu nyingi za Injili zinazomwonesha Yesu akiyaeleza mabadiliko hayo, ijapokuwa Wayahudi hawakumwelewa vilivyo. Kumbe baada ya kifo cha Yesu, mabadiliko hayo yalifanyika pale mitume wa Yesu walipopambazukiwa akilini mwao.
Hata hivyo, haikuwa wote walioelewa suala hilo, wengine wakawa bado wanaililia Sabato hiyo. Kufuatia kituko hicho, mwandishi wa Barua kwa Waebrania akawaandikia wazi wazi wazi habari hiyo (Ebr 4:1-10) naye Paulo akakizima kilio cha wasiokubali mabadiliko katika Rum 14:4-10 na kuwatawanyisha wapigakelele waliokuwa wakiwahangaisha wenzao juu ya Sabato na sikukuu zingine za kiyahudi kwa maneno murua yaliyomo katika Kol 2:16-17.
Mungu Mwenyewe Aliikataa Sabato na Mabadiliko Yake Yalitabiriwa
Sasa hebu tujipatie muda wa kuliweka jibu hili kirefu. Tufuatane kwa utulivu sasa. Awali ya yote, Biblia inaonesha kwamba Mungu alishamfanya Hosea ayatabiri mabadiliko hayo. Hosea 2:11 inasomeka wazi wazi kabisa: “Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato na sikukuu zote zilizoamriwa”. Neno Sabato katika Kiebrania “shabat” linamaanisha “kupumzika”. Kwa wayahudi siku hiyo ilikuwa siku ya Bwana wa huruma na walipaswa kuiweka wakfu kwake (rej. Law 23:3). Katika siku hiyo walimheshimu Mungu (rej. Mt 12:5, Yn 7:23) kwa kumtolea sadaka, kusali na kupumzika kazi kabisa (rej. Isa 56:2, 58:13-14).
Kama kivuli cha mapumziko halisi yatakayopatikana mbinguni kwa njia ya kifo na ufufuko wa Yesu Krsto, Mungu aliwawekea wayahudi Sabato kusudi wajipatie picha ya mambo halisi yajayo mbele yao. Ndipo alipowapa sababu za kujifunza kupumzika kama mazoezi ya maonjo ya mapumziko halisi. Sababu alizowapa zilikuwa tatu: kwanza kwamba wamwige Yeye mwenyewe aliyepumzika baada ya kukamilisha kazi ya kuumba ulimwengu pamoja na vitu na watu waliomo ndani yake (rej. Kut 20:8-11), pili kwamba Sabato ni ishara ya Mungu kwa wayahudi kwamba yeye ndiye aliyewatakasa na kuwafanya taifa lake teule (rej. Kut 31:13-18, Eze 20:20) na tatu waishike kama kumbukumbu ya kukombolewa kwao kutoka Misri (rej. Kum 5:11-15).
Kumbe kadiri Wayahudi walivyojaribu kuishika Sabato, kusudi kukwepa adhabu zilizotangazwa dhidi ya kuifuja Sabato, walizidisha ugumu. Walimu wa dini na waandishi waliifafanua amri ya Sabato na kuunga vipengele vingi sana hata ikawa ni mzigo mzito kwa watu. Aina thelathini na tisa za kazi zilikatazwa kufanywa katika siku ya Sabato, kati yake zikiwamo kazi za kuvuna, kuwinda, kuchuna ngozi, kufuta herufi mbili, kuandika herufi mbili, kuchoma mkaa, kupika, kutembea zaidi ya mwendo wa Sabato, kuponya magonjwa yasiyo ya dharura na kadhalika. Mambo yaliyokatazwa yalikuwa mengi sana na vipengele vidogo vidogo vikaongezeka hata amri yenyewe ikatisha kama miiba ya nungunungu. Zaidi ya hayo, zikawekwa Sabato chungu mzima, kama vile Sabato za ardhi, Sabato za miaka ndiyo jubilei mbali mbali na kadhalika (rej. Law 25:1 – 26:46).
Kwa mtindo huu wa mambo, ikadhihirika wazi kwamba mtu alikuwa anawajibika kwa Sabato kana kwamba aliumbwa kwa ajili hiyo, wakati Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu apate kustarehe na hivyo kujionjesha Sabato ya kweli itakayokuja mwishoni mwa historia. Kifupi, kiutendaji, mtu aligeuzwa mtumwa kwa Sabato, starehe ikakosekana kukabaki mashaka na wasiwasi mwingi sana. Wayahudi waliiogopa sana Sabato, si hasa kwa sababu ya kumpenda na kumtii Mungu isipokuwa kwa sababu ya adhabu zake, hasa kuangamizwa kwa Yerusalemu na kupelekwa utumwani (rej. Yer 17:19-27, Eze 20:20-24).
Mabadiliko Yalitangazwa na Yesu Kristo
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalifafanuliwa kirefu kwa maneno na matendo ya Yesu Kristo (rej. sehemu mbalimbali za Injili). Mungu alipowaona wayahudi wakihangaika na Sabato akazidi kuchanua katika nia yake ya kuifuta. Ndipo, Bwana wetu Yesu Kristo, alipokuja akawaelimisha watu kwamba binadamu hakuumbwa mtumwa wa Sabato hata kidogo. Badala yake, Yesu Kristo, aliwaelimisha wote, kwa maneno na matendo yake kwamba Yeye alikuwa ni Bwana wa Sabato na hivyo, kwa mamlaka hayo na kwa utume wake aliopewa na Baba, anawaalika watu kutenda mema badala ya kujiumiza kwa wasi wasi wa kuivunja Sabato na hivyo labda kuadhibiwa na Mungu (rej. Mk 2:27f).
Yesu alijitangaza kuwa Mungu mwenye mamlaka ya kuibadili hiyo Sabato kwa sababu aliiweka yeye mwenyewe. Na hiyo ni kawaida na mantiki, aliyeitunga sheria ndiye anayeweza kuitangua. Yesu aliwaambia Wayahudi, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwandamu kwa ajili ya Sabato, Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia” (Mk 2:27f). Japokuwa Yesu alitangaza jambo hili, Wayahudi hawakumwelewa hata kidogo na kwa namna hiyo walimlalamkia yeye na wafuasi wake ambao kutokana na kumwelewa mwalimu wao walishaanza kuonesha dalili za kutoitilia maanani Sabato kwa mtindo wa kiyahudi (rej. Mt 12:1-12, 3:2-4, Lk 13:14-16, 14:1-5, Yn 9:16).
Hatimaye, Yesu alihitimisha mabadiliko yenyewe kwa kukamilisha matendo ya ukombozi katika siku ya kwanza ya juma (kwa hesabu za kiyahudi), ndio Jumapili au siku ya Bwana. Siku hiyo alifufuka katika wafu kwa utukufu mkuu. Kumbe hapo hapo, ukiangalia nyuma, utaona kumbe ilikuwa siku kama hiyo Mungu alipoumba ulimwengu kwa Neno, hii maana yake kwa ufufuko wake, Yesu aliye Neno, Mungu anaumba upya ulimwengu. Na tena siku ya namna hiyo hiyo, ndiyo atakayoitumia huko mbele kuwatokea wafuasi wake na hatimaye kuwaletea Roho Mtakatifu atakayelizindua Taifa jipya la Mungu, yaani Kanisa. Basi Pentekoste ikawa pia Jumapili. Kwa haya yote, Jumapili ikatekwa yote na Bwana na ndipo kifupi ikawa SIKU YA BWANA, kwa vile jinsi kila jambo kuu la Bwana, alivyokuwa akilifanya siku hiyo. Basi kwa Kilatini SIKU YA BWANA ndiyo DOMINIKA. Kwa hali hii basi akadhihirisha kwamba Yeye, aliyekuwa akisubiriwa ameshafika na yote yaliyokuwa yakifanyika na wayahudi, sikukuu za mwezi na hata Sabato yalikuwa ni vivuli tu (rej. Kol 2:16-17).
Juhudi hizi za Yesu hazikuzaa matunda mara moja. Kumbe, elimu aliyotoa Yesu Kristo kuhusu Sabato, kwa maneno na matendo tunayoyaorodhesha hapa, haikuingia kabisa vichwani mwa wayahudi na hata wafuasi wake walisitasita kuipokea. Kwa kisa hicho, baada ya Yesu kupaa mbinguni, wayahudi waliendelea kuishika Sabato na kukusanyika kwa ibada katika siku hiyo. Basi Mtume Paulo alipotaka kuwakuta Wayahudi wamekusanyika kwa wingi pamoja aliwatafuta katika siku ya Sabato (rej. Mdo 13:14, 42, 44, 16:13, 17:2, 18:4), kwa Wakristo alijua ilikuwa siku ya Dominika (rej. Mdo 20:7). Hata hivyo, kiujumla, kwa sababu ya uzito na woga wa kubandukana na siku waliyoizoea kusudi kuifuata siku mpya, wafuasi wa Yesu walikuwa njia panda na hivyo wakawa wanahudhuria Sabato pamoja na wayahudi wote na SIKU YA BWANA ilipofika wakawa wanajikusanya peke yao ili kusali, kusoma maandishi yao (ndiyo yaliyogeuka baadaye Agano Jipya) na kuumega mkate (rej. Mdo 20:7).
Mabadiliko Yalitekelezwa na Wafuasi wa Yesu
Kitendo cha wafuasi wa Yesu kusali huku na huku, Sabato na Wayahudi na Dominika peke yao, hakikuchukua muda mrefu kubainika. Wakuu wa wayahudi waling’amua kwamba kuna wayahudi wenye tabia za pande mbili. Wanajiunga na ibada za wayahudi na kishapo siku ya pili yake wanasali peke yao, wakisoma maandishi yao na kumega mkate huku wakimkiri Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu na mkombozi wa wanadamu. Ndipo walipotunga ombi la kumi na mbili na kulitia kati ya sala yao ya maombi kumi na nane (tefillah), sala iliyokuwa ikisaliwa kila Sabato na wayahudi wote katika mwendo wao wa ibada.
Ombi la kumi na mbili halikuwa ombi, bali sala ya kulaani waasi wa dini na hivyo wakiwamo ndani yake Wakristo. Ombi hilo lilisema: “Kusiwe na tumaini kwa waasi wa dini na uung’oe kwa haraka utawala wenye kiburi (dola ya kirumi) katika siku zetu. Wanazareni (Wayahudi Wakristo) na ‘minim’ (Wayahudi wazushi) wafe mara moja; wafutwe kwenye kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki”. Mwisho mwa ombi hili, kama ilivyotakiwa kwa kila ombi, watu waliokusanyika kwa ibada iliwapasa kuitikia, “Utukuzwe wewe, Bwana unayenyenyekesha kiburi”.
Kwa kweli, kwa ombi hili au laana hii, Roho Mtakatifu, mfariji na mkumbushaji wa mafundisho ya Yesu, aliwakumbusha wafuasi wa Yesu kwamba Bwana wao alishawawekea siku mpya, yaani ile SIKU YAKE, ndiyo siku ya kwanza ya juma. Siku hiyo ilikuwa njema na bora kwa kila hali kwani ilikuwa ni siku ya ufufuko wa Bwana mwenyewe, siku ya kuimarishwa kwao na Roho Mtakatifu na kuzaliwa Kanisa la Kristo (Pentekoste), siku aliyoitumia Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya ufufuko wake na hata, kihistoria, siku Mungu alipoanza kuumba ulimwengu. Na mathali, Pasaka au ufufuko wa Bwana ni uumbaji mpya wa ulimwengu, siku ya kwanza ya juma ilikuwa kama siku mambo yalipoumbwa upya. Kwa sifa hizo zote, Wakristo wa mwanzo waligundua haja na uhalali wa kuhamia siku mpya na kuiadhimishwa kwa Bwana.
Basi Wakristo, mara wakaacha kabisa kuhudhuria ibada za Sabato, wakawa tangu wakati huo wanakusanyika Dominika tu. Hivyo akitafutwa mtu aliyeanza kuiacha Sabato turudi hadi kwa mitume katika karne ile ile ya kwanza. Kwa nini walifanya hivyo? Walifanya hivyo kwa sababu walimwelewa vizuri Kristo kwamba busara inadai usishonee kiraka kipya kwenye nguo ya zamani na wala usitie divai mpya kwenye viriba vya zamani. Hayo aliyasema Yesu alipokuwa akiwaeleza Wayahudi kwamba mafundisho yake mapya hayaoani na desturi zao za kale. Alisema, “Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote” (rej. Mt 9:16-17).
Kifupi, wanafunzi wa kwanza wa Yesu, ndio mitume na wafuasi wengine, walioanza, kimatendo, kuachana na Sabato. Tena hayo yanashuhudiwa hata na maandishi ya kale pia. Mtakatifu Ignasio wa Antiokia, mtu ambaye alimfuatia Mtume Petro kama kiongozi wa jumuiya hiyo ya mahali maarufu sana, mahali ambapo jina “Wakristo” lilianza pia kutumika (rej. Mdo 11:26), alipokuwa akienda kuuawa huko Roma aliandika barua saba za mafundisho na mawaidha muruwa kwa Wakristo. Kati ya barua hizo, ile iliyoelekezwa kwa wamagnesia, inasema wazi juu ya mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika. Ameandika hivi, “Watu (yaani Wakristo) ambao hapo awali walifuata mfumo wa kale wamefika kwenye tumaini jipya. Hawaifuati tena Sabato kwa sababu wanaweka kitovu cha maisha yao katika Siku ya Bwana, ambapo Yeye na kifo chake kilitupatia uhai” (rej. namba 6-9). Na kisha kuhusiana na Wakristo kung’ang’ania mambo ya kiyahudi anaendelea kusema, “Ni upumbavu kuwa na Yesu midomoni na wakati huo huo kufuata mila za kiyahudi” (rej. namba 10-15).
Wengine Walibaki Kuililia Sabato ya Kale
Hata hivyo, kuachana na Sabato hakukupokeleka na Wakristo wote. Ndiyo kisa basi Mtume Paulo na watu wengine waliomwelewa na kumwamini Yesu pasipo mashaka, hawakuacha kuwaelewesha Wakristo kuhusu mabadiliko hayo, asili yake na sababu zake na kwamba kama Wakristo hawakupasika kubabaishwa tena kuhusu sikukuu za kiyahudi na Sabato (rej. Mdo 20:7, Kol 2:16, Rum 14: 4-10).
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yametangazwa katika Ebr 4:1-10. Mwandishi wa Barua kwa Waebrania, alijihusisha na kuwaelewesha Wakristo juu ya mabadiliko ya siku kutoka Sabato kwenda Dominika au Jumapili. Ndipo alipowafafanulia kwamba Mungu alishaifuta Sabato na kuitangaza siku nyingine, ndiyo Dominika. Na sababu ya Mungu kuifuta Sabato ilikuwa moja tu, ilishindwa kuwaelekeza watu kwenye kusudio la kuwekwa kwake. Badala ya kuwaelekeza watu kwenye raha ya milele, iliwatia watu hofu na usumbufu mwingi tu. Kuhakikisha haya soma vizuri Ebr 4:1-10.
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalisubiriwa hata kimantiki kwa sababu Sabato yenyewe iliwekwa kama kivuli tu (rej. Kol 2:16). Mtume Paulo au mwandishi wa Barua kwa Wakolosai, awaye ye yote yule, aliingia naye katika shauri hilo hilo la mahangaiko ya watu na mambo ya kiyahudi. Barua kwa Wakolosai inasema na kusisitiza kusudi kila mkristo afahamu wazi wazi kwamba sikukuu za kiyahudi pamoja na sabato vyote vilikuwa vivuli. Yesu alipofika, ukawa mwisho wa vitu hivyo na hivyo mtu asijaribu kuwababaisha Wakristo kwa kuwadai warejee huku kwenye mambo ya kiyahudi (rej. Kol 2:16-17).
Sabato Isivyo Chochote Kijiografia
Nadhani hatukupoteza muda daarasani tukisoma Jiografia. Somo hilo nalo linatufumbulia aibu ya Sabato. Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) ni pia mapinduzi ya uelewa mpevu kwa vile, mbele ya Mungu, siku zote ni sawa. Mungu ni mmoja na siku si jambo la kwake. Hivyo, ni wanadamu katika ufupi wao wa uhai wanaohangaika na siku, majuma, miezi, miaka, miongo, karne na milenia. Kwa Bwana miaka mingi ni kama siku moja tu na siku moja ni kama miaka mingi (rej. 2Pet 3: 8).
Basi kwa ukweli huu, siku yoyote inaweza kuadhimishwa kwani inaadhimishwa kwa Bwana na wala si kwa siku kama siku (rej. Rum 14: 4-10). Biblia, ni kitabu kilichoandikwa kwa uvuvio na si utunzi wa akili za waandishi tu. Hilo linadhihirika pia kwenye suala hili hili la Sabato. Kumbe Mtume Paulo alisemeshwa kinabii na Roho Mtakatifu atufunulie jambo lingelilojulikana vyema baadaye kwa kukua kwa elimu ya jiografia na kosmolojia. Mtume Paulo katika Rum 14:4-10 alisemeshwa atuambie tuache mabishano juu ya Sabato, kwa sababu, mbele ya Bwana, siku zote ni sawa. Jambo hilo kumbe ni kweli kama mtu atajielimisha katika jiografia.
Kwa kweli, ukijua vizuri Jiografia huwezi kujisumbua na kuing’ang’ania siku inayoitwa Sabato au Jumamosi maana siku hiyo hiyo wakati huo huo mahali pengine ni Jumapili au Jumamosi. Unanibisha? Basi, hujui Jiografia au labda ulikariri tu huko darasani kwako. Ikiwa hivyo, kaa jamvini pako nikujuvye. Ni hivi, Jiografia inaweka wazi kwamba, kutokana na kusigana kwa dunia kuliona jua, kuna siku mbili duniani. Wanakoliona jua kwanza ndiyo huingia asubuhi na mchana kabla ya kule kuliko na giza bado. Basi, mstari wa kufikirika unaoitwa “mstari wa tarehe wa kimataifa” (international date line) umechorwa sehemu fulani huko pande za New Zealand kuitenga dunia katika siku mbili zake. Ndipo basi, huko mashariki zaidi huwa siku nyingine tofauti na magharibi zaidi. Hivi, mathalani, upande wa mashariki ukiwa ni Jumamosi, upande wa magharibi ni Ijumaa ama mashariki kukiwa ni Jumapili, magharibi ni Jumamosi. Kumbe kwa Mungu ni siku moja tu, Yeye hana siku za kusigana. Hivyo, kwa ukweli wa kijiografia, hakuna Jumamosi au Sabato iliyo Sabato. Inategemea ulipo, Sabato ile ile inaweza kuwa ni Jumapili au Ijumaa. Hivi, ubishi wa Sabato kama siku kuabudu duniani ni upuuzi mtupu.
Kama hujanielewa hebu nikulete, mara moja, kwenye kitendawili cha kitoto. Ikiwa watu, huku magharibi, watang’ang’ania kwenda kusali Jumamosi, watakuwa wamekwenda kusali siku gani kwani masaa yale yale kwa upande wa magharibi ni bado Ijumaa? Au siku moja baadaye, wengine watakapokwenda kusali waking’ang’ania kuwa Jumapili, wanakuwa wanakwenda kusali siku gani wakati huko magharibi ndiyo Jumamosi? Kumbe siku ni mbili kwa binadamu tunaotegemea kuzipima siku zetu kwa jua. Mbele ya Mungu, asiye na siku, siku yake ni moja ile ile. Kwa hali hiyo, ukweli unakuwa mmoja kwamba, mbele ya Mungu, siku zote ni sawa na hivyo ye yote anayekusudia kuadhimisha siku, aiadhimishe kwa Bwana tu asijisumbue na jina la siku (rej. tena Rum 14:4-10).
Tangu Zamani Wakristo Walikutana Dominika (Jumapili)
Kwa vile Wakristo waligundua kwamba Jumapili, ndiyo iliyokuwa siku yao, walijizoeza kukutana Jumapili kusali, kumsifu Mungu, kutoa sadaka na michango kwa ajili ya wenye dhiki. Kwamba mambo yalikwenda hivyo tunasoma katika Biblia hususan katika 1 Kor 16:1-2. Hapa tunasoma, “Kwa habari ya ile michango kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. Siku ya kwanza ya juma (ndiyo siku ya Bwana, Jumapili) kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.”
Kwa maneno haya, hakuna ubishi kwamba Wakristo walijipatia desturi ya kukutana Jumapili kwa sala na shughuli za pamoja. Na hivi walioing’ang’ania Sabato walikuwa watu wagumu wa kuyapokea mambo mapya, watu ambao hawakosekani katika shughuli na mahali popote duniani.
Kaisari Konstantino Aliipa Nguvu Kawaida Iliyokuwapo
Baada ya Biblia kuweka sawa habari za Sabato namna hiyo, na Wakristo kujasiri kuishika siku ya Bwana badala ya siku muflisi, Sabato, katika miaka ya karne ya nne, alitokea katika historia Kaisari aliyeupenda Ukristo. Yeye alikuwa ni matokeo ya sala za Wakristo kuwaombea viongozi wa dunia wausaidie Ukristo ukue duniani. Kaisari huyo aliitwa Konstantino, aliyetawala tangu 306-337 B.K., aliupatia Ukristo amani kutoka kwenye madhulumu ambayo makaisari wengi walikuwa wakilifanyia Kanisa. Yeye akatangaza rasmi kwamba ile siku inayoshikwa na Wakristo kwa masuala ya sala kwa Mungu wao iwe siku rasmi ya mapumziko kwa watu wote katika dola yake, yaani dola ya kirumi. Ndipo mapumziko ya Dominika yakawa rasmi tangu wakati ule. Hii maana yake ni kwamba Konstantino siye aliyeiunda Dominika na wala siye aliyeanzisha mambo ya ibada yawe katika siku hiyo. Yeye anakuja kuipatia Jumapili nguvu ya kidola tu.
Hapa huanzishwa hoja zisizo na miguu wala mikono. Wengine humtaja Konstantino au Papa fulani, kama mwanzilishi wa Dominika. Historia fupi iliyotolewa hapo juu, yaani mintarafu nyakati za Yesu na baadaye wanafunzi wake, ndiyo inayotuonesha kwamba Dominika ilianza kuwa siku ya ibada kwa Wakristo zamani za karne ya kwanza tayari na wala siyo katika karne ya nne. Basi, kichekesho cha kumtaja Konstantino au Papa fulani kama mwanzilishi wa Dominika kinaweza kulingana na kichekesho cha mtu atakayemtaja kiongozi fulani wa leo kama mwanzilishi wa taratibu ya kula au kuvaa kwa binadamu. Itakuwa ni kichekesho cha mwaka kwa sababu watu wamekuwa wakila na kuvaa hata kabla kiongozi huyo hajaliona jua la ulimwengu huu. Ndivyo ilivyo kwa Konstantino, hawezi kuanzisha kitu katika karne ya nne, kitu kilichoanza kabla hajazaliwa mwenyewe katika karne ya kwanza.
HATIMA
Nahitimishia hapo. Kumbe, sasa unganishia ile historia halisi ya kiroja cha kurudishwa kwa sabato walichokifanya akina William Miller, Samwel Snow, Hiram Edson, Joseph Bates na Ellen White kama nilivyowatangulizieni. Umeiona aibu hilo. Mbele ya wasomi na wachambuzi wa mambo hakuna tena mahali pa kufichia uso. Nawashukuruni kwa kuisoma hoja hii ndefu. Asanteni wote.
Lakini mkitaka kuchangia msikose kuzisoma kurasa hizi kwa ukamilifu.
Ameandika Pd. Titus Amigu.
Ubarikiwe Sana Baba Padre, Titus Amigu.
JibuFuta