Jumanne, 11 Julai 2017

MTU KUSEMA “AMEOKOKA” NI UPINGA KRISTO, UPINGA MAANDIKO NA UPINGA BUSARA YA MAISHA YA KAWAIDA

Vijana mmenitaka niwaandikieni mambo mengi. Basi, leo nakuleteeni andiko juu ya “kuokoka” au “wokovu”. Somo ni refu lakini lisomeni kwa uvumilivu. Kwa kuanza tu, acha niseme kwamba Wakatoliki, kwa tahadhari, hatutumii falsafa au teolojia ya “kuokoka”. Kwa nini? Kwa sababu wokovu ni taji baada ya mashindano. Ni nishani baada ya kufuzu mtihani. Ni taji katika siku ya kutawazwa. Ni mapato baada ya uwekezaji mgumu. Ni mapato baada ya kuhangaika duniani. Ni kulia kivulini baada ya kuchumia juani. Ni faraja baada ya dhiki. Kwa hiyo, kujitangazia kuokoka leo hii si kawaida yetu. Sisi tunafanya tahadhari ya kauli. Tunatahadhari. Huwezi mtu ambaye upo katika mapito ya dunia hii, kwa fahamu zako, kujitangazia kwamba umeokoka kwa sababu hujamaliza safari. Siku zote tuishipo hapa duniani safari ni mbichi kabisa.
Ndiyo, kwa mujibu wa ubatizo kila aliyebatizwa ana kianzio cha utakatifu. Yaani hadi hapo mtu angeliweza kujitangazia kuokoka. Lakini kuanza safari si kuimaliza. “Safari usihakikishe”. Lakini, kama si kutahadhari, wanadamu wote tungeliweza kutamba hivyo kwa vile midomo yetu hailipiwi VAT hata tuseme maneno milioni moja kwa siku. Kusema ni bure hapa duniani.
Basi, kwa jinsi mambo yalivyo, ukimsoma Yesu, ukisoma Maandiko Matakatifu na ukiyasoma maisha, mwanadamu kujitangazia “ameokoka” ni balaa tatu: ni upinga Kristo, upinga Maandiko Matakatifu na upinga busara ya kawaida. Tulia, usilipuke, nitakueleza leo hii hii.
BALAA YA KWANZA NI UPINGA KRISTO. Kwa vipi? Kwa sababu Yesu tunayemfuata nasi kujiita kwa jina lake, “WAKRISTO”, alisema, “Atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka” (Mk 13:13). Katika Kigiriki imeandikwa hivi: ὁ δὲ ὑπομείνας εἰς τέλος οὗτος σωθήσεται. Unasoma, “Ho de hupomeinas eis telos hutos soothesetai”.  Neno hilo la mwisho ndilo tunalolijadili hapa. “Soothesetai” ni wakati ujao “ATAokoka”. Nenda kokote ukamuulize yeyote anayejua Kigiriki atakuambia “soothesetai” ni wakati ujao (future tense) na maana yake ni “ATAokoka”.
Kwa hiyo, Yesu mwenyewe ametumia wakati ujao (future tense). Na katika kila lugha vitenzi vina nyakati na nyakati zina maana nzito. Wakati uliopita si wakati uliopo, na wakati uliopo si wakati ujao. Wakati uliopita ndiyo huweza kuwa uliotimilika katu siyo wakati ujao. Katika lugha yoyote ile, wakati ujao huwa usiotimilika.
Ndiposa, mtu kujitangazia kuokoka akisema, “Nimeokoka” (ndio wakati uliotimilika – perfect tense) ni UPINGA KRISTO kwa sababu ni kusimama na kusema kinyume kabisa na alichosema Yesu tuliyeambiwa tumsikilize. Imeandikwa, “Huyu ndiye mwanangu ninayependezwa naye, msikilizeni yeye” (Mk 9:7). Wakristo tusipomsikiliza Yesu tumsikilize nani? Hivi, kutumia wakati uliotimilika katika kauli aliyotumia Yesu wakati ujao ni kumpinga. Ni kumfanya “hamnazo”. Ni kumfanya Yesu “kilaza”. Na kwa namna hii, huko si kumpinga tu bali ni kumtukana pia. Lakini, Mwana wa Mungu hawezi kusema kitu kama “kihiyo”. Yeye amesema “ATAKAyevumilia (kwa kuchukuana na kitenzi kikuu cha sentensi) mpaka mwisho ndiye ATAKAyeokoka” (Mk 13:13). Sasa mtu anabadilije “wakati ujao” (future tense) na kuweka wakati wa kitenzi kilichotimilika (perfect tense) “NIMEokoka”? Ushujaa wa kumpinga Kristo namna hii unatoka wapi?
Basi, kubadili WAKATI wa kitenzi ni UPINGA KRISTO WA WAZI KABISA. Jamani, kama hatusikilizi anachosema Yesu tunajidaije sisi kuwa wafuasi wake? Hapo hatuna utii wala adabu kwake. Mtu huwezi kubadili maneno ya mkubwa wako ukabaki bado na adabu kwake.
Mtume Petro alipokanusha alichosema Yesu, mara moja alilinganishwa na Shetani. Alilinganishwa na Shetani kwa sababu alibadilisha maneno ya Mungu ambayo mwanadamu hakuwa na haki ya kuyabadili.  Soma habari hii katika Mk 8:31-33. Sikiliza aya ya 33 inavyosema “Akamkea Petro akisema, ‘Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu’”. Kwa jinsi hiyo hiyo na kwa ukali wa kiwango hicho hicho, anayesema “AMEOKOKA” akibadilisha alivyosema Yesu “ATAOKOKA” ilipaswa alinganishwe na Shetani na kufukuzwa mbele ya Yesu kwa sababu ni mpinzani wake.
Lakini hilo jambo la kuweka wokovu mwishoni mwa historia, YAANI WAKATI UJAO, halitokei katika Mk 13:13 peke yake bali hata katika Mk 16:16. Hapo Yesu anasema, “Anayeamini na kubatizwa ATAokolewa. Asiyeamini ATAhukumiwa”. Yaani hapa napo Yesu anatumia wakati ujao ATA… Halafu si Yesu peke yake aliyetumia wakati ujao, hata Paulo, Mtume wa Mataifa, ametumia wakati ujao vile vile. Unaniuliza wapi? Tusiandikie mate na wino ungalipo. Mtume Paulo ameandika hivi:
“Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, UTAokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu na kukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema, ‘Kila anayemwamini HATAaibishwa. Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya  Wayahudi na wasio Wayahudi. Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema ‘Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana ATAokolewa” (Rum 10:9-13).
Unanielewa sasa? Ni kwamba hata katika nukuu hii, tunatembezwa katika WAKATI UJAO siyo WAKATI ULIOPO seuze uliotimia. Sasa Mkristo anayetii neno la Mungu anabadilije wakati hadi kujisema “AMEokoka”? Ndugu zanguni, kama huo si “upinga Kristo” ni kitu gani? Narudia na kusisitiza, kama kweli tunajua sarufi za lugha, kila lugha ina nyakati zake: wakati uliopita, uliopo, ujao na kadhalika. Wakati uliopita si wakati uliopo, wakati uliopo si wakati ujao na kadhalika. Nakuapia kila lugha, hata Kimakonde, Kichina, Kitaliano na Kinyamwezi vina nyakati zake. Na wakati wa kitenzi una maana, tena maana kubwa sana.
Hata hivyo, ili uelewe ninachosema, acha nikuulize kwa mfano mmoja wa kawaida kabisa. Eti, ukikutana na wanadamu wawili, mmoja anayekuambia “Nimekula” na mwingine anayekuambia, “Nitakula” utampa chakula yupi? Je, hutaelewa kwamba walichosema watu hao wawili si sawa? Je, hutampa chakula huyo anayesema “Atakula”? Naona ndivyo utakavyofanya kama unaelewa lugha. Sasa mwamini akidai “nimeokoka” na mwingine akisema, “nitaokoka” Mungu atamsaidia yupi? Je, hatamsaidia huyo anayesema “ataokoka” na kumwacha huyo anayesema “ameokoka”? Kwa mantiki ya moja kwa moja, naona ndivyo. Basi, nawasihini, tumsitangazie Mungu kwamba “tumeokoka” tutajifungia milango ya kusaidiwa naye kwani, kwa kujua au kutojua, ndivyo tulivyomwambia kwamba hatuhitaji msaada wake tena.
Kwa maneno mengine nataka kusema kwamba kwa ukweli huu wa kawaida, kila anayedai “AMEOKOKA” anajinyimisha msaada na neema kutoka kwa Bwana kwa sababu amejitoa mwenyewe kwenye orodha ya watu wa kusaidiwa. Kifupi, anajiponza kwa maneno yake mwenyewe. Ndiposa, nakuomba msomaji wangu, kusudi uendelee kusikilizwa na kusaidiwa na Bwana usiseme “umeokoka”. Usiseme hivyo kwa sababu ni lugha ya kujikinai. Ni lugha ya kujigamba mbele ya Mungu mkuu. Ni lugha ya majivuno, tena inayotoka kwa majisifu kinywani mwako mwenyewe.
BALAA YA PILI NI UPINGA MAANDIKO MATAKATIFU. Ni hivi, pamoja na upinga Kristo ni upinga Maandiko Matakatifu kwa ujumla. Kwa vipi? Kwa sababu Maandiko Matakatifu yanaonya mara kwa mara dhidi ya mtu kutamba kwamba amekamilika. Katika Mit 27:1-2 tumeandikiwa: “Usijisifie ya kesho, hujui nini kitatokea leo mpaka kesho. Acha watu wengine wakusifu kuliko mdomo wako wewe mwenyewe”. Tena si mahali hapa tu, bali katika YbS 11:27-28  tumeandikiwa: “Matatizo ya muda mfupi tu humsahaulisha mtu raha; mtu hujulikana alivyo mwishoni mwa uhai wake. Usiseme fulani ana heri kabla hajafa, maana ushahidi wote hutolewa baada ya kufa”.
Pamoja na sehemu hizi, usisahau Mk 13:13 inayotuambia, “Atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka”. Kisha soma tahadhari iliyo katika 1Kor 10:11-12, mahali tusomapo, “Anayedhani amesimama, aangalie asianguke”. Zaidi ya yote, mintarafu kukosekana kwa uhakika wa “kuokoka”, Yesu ametangaza mara kwa mara kwamba kwa Mungu kuna kipindupindu kikali kwa maana kwamba mtu anayedhania kuwa wa kwanza anaweza kuwa wa mwisho na wa mwisho akawa wa kwanza. Soma kwa ushahidi Mk 10:31.
Sasa, ndugu zanguni, kwa nukuu zote hizi, mtu bado anatangaza amemalizana na dhiki naye “ameokoka”? Huo kama siyo upinga Maandiko Matakatifu ni nini tena? Jamani, mtu apingane na nukuu ngapi hata ahesabike mpinga Maandiko Matakatifu? Najijibu mwenyewe. Hata aya moja tu inatosha kumfanya mpinga Maandiko Matakatifu.
Hakuna cha kumalizana na kazi mapema, kabla ya muda hapa. Kwa nini? Kwa sababu ukiisoma Biblia vizuri utaona usalama wa Mkristo ni wa masharti (conditional security). Ni kwamba tukiishi vyema ndipo tutapata uzima wa milele. Usinibishe. Soma Fil 2:12, Rom 8:38-39, Yn 10:28-29 na Efe 1:13-14 na kisha Mt 24:11-13, Rom 8:12-14, 1Kor 15:1-2 na Gal 6:7-9. Ukimaliza kusoma sehemu hizi zote utagundua kwamba hizo nukuu za pili zimezifunika kabisa aya za kwanza. Hata kama tumeanza safari kwa ubatizo, tutapata wokovu ikiwa…..tuta…..
BALAA YA TATU NI UPINGA BUSARA YA KAWAIDA. Mwishowe ni upinga busara ya kawaida. Kwa kumalizia na kushadidisha jibu langu, nahama kutoka kwa Yesu na Biblia namalizia kwa busara ya kawaida tu. Yaani hata busara ya kawaida inatukataza kujitangazia kuokoka tungali hatarini bado. Sikiliza, kama tunayajua Maandiko, ni dhahiri shayiri kwamba Shetani anatutafuta kila siku atuangushe (rej. 1 Pet 5:8). Hii maana yake ni kwamba anatuwinda au anatufukuzia kwa nyuma. Kama ndivyo, tukubaliane sote kwamba wanadamu tupo hatarini siku zote. Sasa inawezekanaje mtu timamu anayejua kwamba anafukuzwa na simba kukimbia huku akisema: “Nimeokoka, nimeokoka, nimeokoka!” au “Niko salama, niko salama, niko salama”?
Nadhani tunakubaliana, kwa kawaida mambo hayaendi hivi. Mtu anayejijua kuwa yupo hatarini, kama kweli ni timamu, yaani hajalewa “viroba” na wala hachezi “Ze comedy” lazima atakuwa akikimbia huku akisema zaidi ya ukweli wenyewe wa hatari, atakuwa akisema: “Ninakufa, ninakufa, ninakufa!” Ndivyo atakavyolia hata kama atakuwa bado hajakamatwa na simba. Mtu huyo ataweza tu kutangaza ameokoka akifanikiwa kuingia ndani na kufunga mlango.
Ndivyo sisi Wakristo inavyotupasa kufanya. Tukingali bado hapa duniani lazima tufumbe kinywa kwa tahadhari tusijitangazie tumeokoka. Yaani tungoje hadi tufike kwa Mungu, ndipo tuseme kwa fahari: “Tumeokoka” na siyo sasa tungalipo hapa duniani tukichachafwa na malimwenguni. Watakatifu walio mbinguni saa hizi ndiyo pekee wanaoweza kujitangazia WAMEokoka na siyo mimi na wewe tunaorandaranda bado duniani hapa.
Kama tukisema hivyo ni majigambo yetu na wala kweli haimo ndani yetu. Tutakuwa hatusemi kweli kwa sababu kiuhalisia mitego ya shetani na dhambi hatujamalizana nayo. Na Biblia inatuonya tusijihakikishie kwamba hatuna dhambi (1Yoh 1:8). Biblia inasema tukisema hivyo tutakuwa siyo tu tunajidanganya wenyewe bali tutakuwa tukimfanya hata Mungu kuwa mwongo. Na kumbe hiyo itakuwa ole kubwa zaidi, mwanadamu kumfanya Mungu mwongo. Ni heri mara elfu useme Pd. Titus Amigu ni mwongo kuliko kusema Mungu ni mwongo.
Hatimanye, lugha zote hufanya muhtasari wa busara zake katika misemo mbalimbali. Na katika lugha nyingi ni katika methali. Kumbe, hata methali za Kiswahili nazo zimejaa busara ambayo si vyema kuipinga. Kuna methali, “Hujafa hujaumbika”, “Safari usihakikishe”. “Usitukane wakunga na uzazi ungalipo” na “Usimtukane mamba kabla mto hujavuka”. Bado kuna methali nyingine inayosema “Usipige kelele ungali bado msituni” kwa sababu chochote kinaweza kukupata utakapokuwa unapita kwenye msitu wa wenyewe.
Methali hizi zote ni busara ya kawaida n azote zinataka kutuambia kwamba mambo ya mbele ni bado giza kwetu. Hiyo maana yake aliye mwema leo anaweza akabadilika na kuwa mwovu kesho na aliye mwovu leo anaweza kubadilika akawa mwema kesho. Ni yamkini tu. Yuda alikuwa mwema kwa miaka mingi, mwishoni mwa maisha yake akasambaratika. Kinyume chake, mwizi aliyesulibiwa kulia kwa Yesu alikuwa mwovu katika maisha yake, akabadilika angali kufani pale msalabani. Kumbe, sote tunaweza kubadilikia upande wa chanya au wa hasi. Hayo ndiyo mapinduzi ya wa kwanza kuwa wa mwisho na wa mwisho kuwa wa kwanza. Ndiyo maana inasemwa ukibahatika kuingia mbinguni, utashangaa mambo matatu: kwanza kwamba mwenyewe umeingia mbinguni, pili kwamba uliowategemea kuwamo hawapo na tatu kwamba usiowategemea kuwamo wapo. Basi, kaa chonjo!
ASILI YA FALSAFA AU TEOLOJIA YA KUOKOKA: Falsafa au teolojia ya mtu kujitangaza “ameokoka” iliasisiwa na watu wasio na sakramenti ya Kitubio ili kufunika haja ya kuungama. Kwa vipi? Kwa sababu mtu akishajitangazia “ameokoka” hana haja ya kwenda kwa padre au kwenye kiti cha kitubio kuungama kwani hana dhambi kwa vile ameshamalizana na dhambi zote, jambo ambalo halikuwa kweli kwa sababu tungali hapa duniani sisi ni wadhambi bado. Tusijidanganye na wala tusimfanye Mungu mwongo (1Yoh 1:8).
BUSARA YA WAKATOLIKI: Wakatoliki hatujiingizi katika kujiliwaza huko kwa bure. Kumbe, kwa tahadhari na unyenyekevu, tunajiachia bado fursa ya kukiri kwamba tu wadhambi ili tupate kutumia sakramenti ya Kitubio. Hakika, usipokiri kwamba una dhambi, huwezi kwenda kuungama dhambi zozote.
Kumbe, kutokana na yote niliyosema hapo juu, ndipo inapochipuka busara ya Kanisa Katoliki ya kujihadhari katika kauli. Jambo hili lipo katika sura mbili tu: mosi kubaki na neno WONGOFU na pili kuutambua wokovu wa mwanadamu katika ukamilifu wa hatua tatu.
NENO WONGOFU (METANOIA): Ni kwamba mwanadamu anaweza kufanya maamuzi ya kubadilika (metanoia). Lakini uamuzi huo ni wa kuengwaengwa sana maana uamuzi wa leo si lazima udumu hadi kesho. Kwa wongofu tunamaanisha uwezo wa binadamu kufanya maamuzi kwa akili na utashi wake kubadilika na kuwa tofauti.
Nakupa mifano. Mtu wa dini ya jadi anaweza kuamua kuacha upagani na kuishika imani mpya ya Ukristo. Mwovu anaweza kuamua kubadilika na kuwa mwadilifu. Mwizi anaweza kuamua kujitosa katika kuwa mwaminifu. Mwongo anaweza kuamua kujitosa kuanza kuishi maisha ya mkweli. Mlevi anaweza kuamua kujitosa katika maisha ya kutokunywa kabisa au maisha ya kushika kiasi. Fisadi anaweza kuamua kuishi maisha ya kuwafikiria na kuwajali wengine na kutumia mali kwa manufaa ya wote. Mwasherati anaweza kuamua kujitosa katika kujitunza, kufunga ndoa na kuwa mwaminifu. Mzinzi anaweza kuamua kutunza uaminifu kwa mwenzi wake wa ndoa. Dhalimu anaweza kuamua kujitosa kuwa mwema na kadhalika. Huo ndio wongofu (metanoia).
Hata hivyo, kwa kuwa uamuzi wa kubadilika unaweza kugeuka saa na siku yoyote, ndiyo kisa aliyejitosa kwenye wongofu (metanonia) lazima ajibidishe kuomba neema ya kudumu katika maamuzi yake huku akiwa tayari kukimbilia kiti cha Kitubio ikiwa ahadi imemshinda au maamuzi yake yamemponyoka. Kifupi, kitubio ndiyo zahanati, kituo cha afya au hospitali ya kiroho. Ndiyo mahali pa kuinukia mtu aliyeanguka. Hii ni tofauti na mtu aliyejitangazia kuokoka, kwa vile huyo wa pili “anadai ameishiana na dhambi na hivyo hahitaji hospitali wala mahali pa kuinukia kwa vile haanguki tena”. Lakini huku ndiko nilikosema ni kujiamini kunakopinga yote: maneno ya Yesu, Maandiko Matakatifu na hata busara ya maisha ya kawaida.
Kumbe, wongofu (metanonia) inakwenda bega kwa bega na toba na sakramenti ya Kitubio. Ndiyo maana wongofu (metanoia) si “kuokoka” bado. Ndipo wongofu (metanoia) inapata sapoti ya nyanja zote tatu: Yesu Kristo, Maandiko Matakatifu na busara ya maisha ya kawaida. Wongofu unalingana na alichosema Yesu: “Atakayevumilia mpaka mwisho, ATAokoka” Unaoana na Maandiko Matakatifu yanayosema, “Anayedhani amesimama, aangalie asianguke”, “Mtu asijiite mwenye heri kabla hajafa” na kadhalika kama nilivyonukuu Maandiko katikati ya andiko hili. Hali kadhalika, wongofu (metanoia) unapata sapoti methali za lugha mbalimbali pamoja na za Kiswahili, kama, “Hujafa hujaumbika”, “Uzazi ungalipo usitukane wakunga” “Usipige kelele ungali msituni” na kadhalika.
WOKOVU KATIKA UKAMILIFU WA HATUA TATU ZA KUFUATANA: Kanisa Katoliki hutambua WOKOVU KATIKA UTIMILIFU WA HATUA TATU. Hatua ya kwanza ni ubatizo, yaani kutangaza na kuweka nia ya kumfuasa Mungu moyoni na maishani (rej. 1 Pet 3:21). Hatua ya pili ndiyo ya kupambana na maisha halisi. Na hatua ya tatu ni kutangaziwa “UMEOKOKA” na Mungu mwenyewe siku ile ya mwisho wa historia (rej. Mt 25:32-46). Kabla yake ni bahati nasibu tu. Kabla yake ni pata potea tu.
Namalizia. MKATOLIKI BAKI ULIPO. Nimekudadavulia mambo yalivyo. Usidanganyike. Asikubandue mtu kwa mafundisho ya upinga Kristo, upinga Maandiko na upinga hata busara ya maisha ya kawaida. Hivi usipeperushwe na mafundisho ya kigeni (Ebr 13:7-9). Kwa mantiki hii, tangu leo, ukimwona mtu anajitangazia ameokoka, na labda anakughasi umsikilize, una fursa ya kumshangaa mara sita.
Mara ya kwanza, mshangae kwa nini anampinga Yesu Kristo tuliyeagizwa tumsikilize asemacho na asemavyo. Yesu amesema “ATAokoka” na siyo “AMEokoka”. Mshangae hilo analolisema amepata kutoka kwa nani!
Mara ya pili, mshangae kama kweli anajua Maandiko Matakatifu na kauli zake za mwanadamu kutojihakikishia kumaliza safari kabla ya mauti yake (mfano Mit 27:1-2, YbS 11:27-28 na Mk 13:13). Kumbe, kimaandiko hata aya moja tu ingelimtosha kumwahadharisha: “Asijiite mwenye heri kabla hajafa” (Mk 13:13).
Mara ya tatu, mshangae kwa nini anajisifu mwenyewe wakati Biblia imekataza kufanya hivyo (Mit 27:1-2). Biblia inasema mtu kujisifu mwenyewe si maungwana.
Mara ya nne, mshangae kama kweli anajua nyakati za lugha kwa vile wakati ujao si wakati uliotimilika hata kwa utani. Yaani hata kwa nini “ATAOKOKA” siyo “AMEOKOKA”.
Mara ya tano, mshangae kama kweli ana busara ya kuishi duniani kwa tahadhari; kama hajafa anatambaje kuwa amemalizana na dhambi (1Yoh 1:8)?
Mwishowe, mara ya sita, mshangae kama kweli anazijua methali za busara za Kiswahili tunazozitumia mitaani na majumbani mwetu, kama vile, “Hujafa hujaumbika”, “Safari usihakikishe”, “Uzazi ungalipo, usitukane wakunga”, “Usitukane mamba kabla hujavuka mto” na “Usipige kelele ungali bado msituni”.  Methali zote hizo hazisemi kitu kwake? Kwa heri kwa leo. Kwa aliyesombwa na UPINGA KRISTO, UPINGA MAANDIKO MATAKATIFU NA UPINGA HATA BUSARA YA MAISHA YA KAWAIDA, namualika arudi nyumbani kwake, aache kuhamia chooni. Natumaini tumeelewana na imetosha sana.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni