Jumanne, 11 Julai 2017

MTU ANAYECHUKIA SANAMU ANAFIKIRI KWA KURUKA NA KUSOMA BIBLIA KWA KURUKARUKA

Leo nimepata muda wa kufungua ukurasa wangu wa Facebook na kusoma ujumbe mwingi kutoka kwenu vijana. Jamani nipo, lakini nipo Windhoek, Namibia, na huku nimebanwa na kazi fulani. Lakini tuache hili pembeni tufanye mazungumzo yetu.
Wengi wametaka nizingumzie uhalali wa sherehe ya Pasaka. Nitafanya hivyo; lakini nilishajiweka tayari kukurushieni habari za sanamu. Acheni basi, nikurushieni kwanza mada hiyo na siku tano zijazo nitakurushieni mada ya Pasaka.
Mada ya leo ni ndefu kidogo kwa sababu mada mbili pacha: MADA YA SANAMU KWA UJUMLA NA KISHA MADA JUU YA KILE TUNACHOFANYA KILA IJUMAA KUU “KUABUDU MSALABA”. Basi, nawasihi msome kwa uvumilivu sana.
Nadhani vijana ninyi si wageni hata kidogo kwa mashtaka maarufu kabisa kwa Wakatoliki mintarafu sanamu. Najua siyo wageni, ndiyo kisa wengi wenu mmenisihi mara nyingi niiandikie mada hii. Ndiyo, ni mashtaka ya kwamba Wakatoliki wanaabudu sanamu na picha na  kwamba  kanisani mwao kuna ibada ya sanamu na picha. Binafsi nimejibu mashtaka haya, kwa sauti na kwa kalamu, karibu mara mia lakini nikagundua sijafaulu kuyazima mashtaka hayo. Nilijigundua nilikuwa ninachota maji kwa pakacha au kuyatwanga maji kwenye kinu tu. Kwa nini? Nilipowaza na kuwazua nikagundua tatizo linapoanzia. Jamani linaanzia kwenye mikasa miwili: kwanza washtaki kufikiri kwa kuruka na pili kusoma Biblia kwa kurukaruka.

KUFIKIRI KWA KURUKA
Mkasa wa kwanza ni kufikiri kwa kuruka. Anafikiri huku akiwa anasahau. Anatazama huku akiwa analala. Mtaniuliza, mshtaki anafikirije kwa kuruka? Anafikirije huku akiwa anasahau na anatazamaje huku akiwa analala? Anafikiri kwa kuruka, anafikiri huku akisahau na anatazama huku akilala pale anapopita bila kutafakari Mwa 1:26-27.
Hapa pameandikwa hivi: Mungu akasema na tufanye mtu kwa mfano wetu na kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama na nchi yote pia na kila chenye uhai kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba”.
Ndugu zanguni, kama si kufikiri kwa kuruka anakosaje mtu kuelewa jambo linalosomeka kama maji kama hili kwamba yeye mwenyewe mwanadamu ni sanamu? Nina hakika ya asilimia mia kwamba mtu angelifikiri kwa “mapozi” hapa asingelikosa kuelewa kwamba yeye mwenyewe ni sanamu. Lakini ukiona mtu anayejinasibu kusoma Biblia hatui kwenye Mwa 1:26-27 bali anarukia kwenye Kut 20:5 ujue anasoma kwa kuruka kana kwamba yeye ni kiumbe wa jamii ya chura. Usinibishe, nadhani katika mjadala huu huu, tutapata ushahidi wa mkasa huu. Watakuwepo wengine watakaoturusha juu ya Mwa 1:26-27. Hawatatua hapa hata kidogo.

KUSOMA KWA KURUKARUKA
Mkasa wa pili ni kusoma kwa kurukaruka. Mtaniulza tena, mshataki anasomaje Biblia kwa kurukaruka? Jibu ni kwamba anasoma kwa kurukaruka pale anaposhindwa kushonanisha sehemu zinazokataza kutengengeneza sanamu na zile zinazoruhusu kutengeneza sanamu, kwa mfano kuunganisha Kut 20:4-5a na Kut 25:18-20. Wewe fikiria mtu anashindwaje kujua kwamba Musa yule yule aliyekatazwa asitengeneze sanamu aliruhusiwa kutengeneza sanamu katika kitabu kile kile? Jiulize, mtu kama huyo anasoma  Biblia kwa mstari ulionyooka kweli? Hivi, mtu halioni jambo hili kwa ajali au kwa makusudi? Lakini mkasa huu unatufanya wasomaji wa Biblia tuonekane kama watoto wa chekechea ambao ukiwapa kitabu mara moja watakifunua mpaka mwisho wakitafuta picha. Nadhani katika mjadala huu huu, tutapata ushahidi wa mkasa huu. Watakuwepo wengine watakaoturusha juu ya Kut 20:4-5a na Kut 25:18-20. Hawatapenda kutua hapo hata kidogo.

NAJIBU HAMNA IBADA KWA SANAMU KATIKA KANISA KATOLIKI
Vijana, nachukua fursa hii kurudia kujibu kwa mashtaka niliyoyaainisha. Ni kwamba Wakatoliki hawaaziabudu sanamu wala picha na wala ibada ya kuabudu sanamu au picha haipo kwenye Kanisa Katoliki. Lakini kwa kusudi ya kulielewa vyema jambo hili, kila mtu anapaswa aelewe vyema kinachosemwa na Biblia kuhusu sanamu na picha. Kwa kifupi, Biblia ina sehemu zinazopiga marufuku na nyingi zaidi zinazoruhusu. Kumbe, sanamu ama picha zinakatazwa pale zinapopewa daraja la Mwenyezi Mungu tu. Vinginevyo, hatari hiyo isipokuwepo Mungu hagombi.

Mada hii itaonesha kwamba mambo yamefikia yalipofikia sasa kwa sababu kumekuwa na ukuaji wa uelewa katika historia. Hilo limewezekana kwa sababu Roho Mtakatifu amelisaidia Kanisa kuelewa vyema zaidi na zaidi kama Kristo mwenyewe alivyoliahidi Kanisa kabla hajafa, kufufuka na kupaa mbinguni. Kwamba Kanisa lingelisaidiwa kuelewa mafundisho yake na hata yale yaliyokuwa moyoni mwake, Kristo alisema: “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu naye atakuwa ndani yenu.... Huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.....Yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atanena na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari (Yn 14:16-17, 26, 16:13-14).

UBAYA WA SANAMU UPO KATIKA KUZISUJUDIA NA KUZITUMIKIA
Ukifuatilia mshororo wa Maandiko lazima ugundue kwamba sanamu zimepigwa marufuku na ni haramu pale tu ZINAPOPEWA DARAJA LA MUNGU yaani pale zinapotumikiwa na kusujudiwa. Hii ndiyo maana ya msingi ya marufuku iliyomo katika amri kumi za Mungu ambazo zimeandikwa kwanza Kut 20:3-5 na kupata nakala ya pili katika Kumb 5:7-10. Tatizo lipo katika watu kusoma sehemu hizi wakiwa wanarukaruka. Kwa sababu hiyo hawazimalizi aya na hivyo kuona kwamba Mungu anakataza zisisujudiwe yaani siziabudiwe. Makini na yafuatayo sasa.

MUSA ALIKATAZWA KUTENGENEZA SANAMU
Ni kweli Musa alikatazwa asitengeneze sanamu (Kut 20:4-5a). Lakini ukisoma kwa kutulia utajua kwa digrii ipi ya ubaya. Tusiandikie mate na wino ungalipo. Tusome, “Usijifanyie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia”. Wenye kuruka hapa hushindwa kutilia maanani hilo suala la “usivisujudie wala kuvitumikia”. Shida inasababishwa na mruko huu unaofanyika kwa kujua au kwa kutojua.

MUSA YULE YULE ALIAMRIWA ATENGENEZE SANAMU
Lakini sanamu ziliruhusiwa zitengenezwe na hata Musa yule yule isipokuwa kwa matumizi yale yasiyohusisha kuzitumikia ama kuzisujudia. Aliamriwa azitengeneze pale zisipopewa daraja ya Mwenyezi Mungu. Nashuhudia kwa mifano miwili. Aliambiwa katika Kut 20:18, “Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu, uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja na kerubi la pili mwisho wa pili. Fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku”.
Halafu Musa huyo huyo, wala siyo mtoto wake au mtu mgeni fulani, anaambiwa tena katika Hes 21:8, “Jifanyie nyoka wa shaba, ukaiweke juu ya mti na itakuwa kila aliyeumwa aitazamapo ataishi”. Tafadhali hapa soma bila kuruka, fikiri bila kusahau na tazama bila kulala; kama sanamu zingelikuwa haramu kwa zenyewe tu, Musa angeambiwa azitengeneze sanamu mbili za makerubi na kuziweka juu ya sanduku la agano au angeamriwa amtengeneze nyoka wa shaba ili watu wamtazame na kujiponya na nyoka wa moto waliokuwa wakiwang’ata? Na je, Mungu angekuwa “ana akili” kweli kuwakufurisha watu wake mwenyewe? Mungu angelikuwa na akili kweli kujipinga mwenyewe?
Basi, nawasihi tushonanishe mshororo wa Maandiko Makatifu. Kumbe, tukifanya hivyo itakuwa dhahiri maana ya nukuu zifuatazo: Kut 25:18-20, 26: 31, 29:37, Hes 21:8-9 (= Yn 3:14-15), 1Fal 7:29, 2Nya 3: 10, 4:4, Hek 16:7, Eze 41:17-21, Ebr 9:5. Hali kadhalika, tutafahamu kwamba, pasipo kumkufuru Mungu, mfalme Sulemani naye alilipamba hekalu kwa picha pamoja pazia la Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu. Kama Musa na Sulemani walifanya hayo yote pasipo kumkufuru Mungu, Kanisa Katoliki linashutumiwaje katika kuwa na sanamu na picha katika majengo na makanisa yake? Bila shaka ni kwa mruko wa kusoma Biblia tu.

MUNGU MKUU HAGOMBI NA SANAMU NA PICHA
Kutokana na ukweli huu, Mungu hagombi juu ya vinyago visivyo na madhara. Mungu ni mkuu mno kugombana na sanamu isiyopewa daraja yake. Kushuhudia hili soma msimamo wake kuhusu Sanduku la Agano (Hes 10:35-36), kisibau cha kuhani mkuu (Amu 8:26-27, 17:4-5), vinyago vya nyumbani (Amu 18:14, 17-18, 20) na nyoka wa shaba (2Fal 18:4, Hes 21:8-9).  Katika nafasi hizi Mungu alijua kwamba vitu hivyo havipewi nafasi yake ya umungu isipokuwa sana sana vinawaelekeza watu kwake. Mathalani, wale walioitazama sanamu ya nyoka wa shaba waliweza kupeleka mawazo yake “nyuma ya sanamu” hadi kwa Mungu aliyeamrisha itengenezwe na kumbe kwa kufanya hivyo walikuwa wakimkiri Mungu na kwa namna hiyo kujiponya. Na mwendo huu wa fikra ndiyo unaowaponya watu wanaomwona Yesu nyuma ya mti wa msalaba. Kwa kuutazama mti, watu wenye macho ya imani, huweza kumwona Yesu Kristo na hivyo wanajiponya na matatizo yao kwa kumwamini Mwana wa Mungu. Rejea Hes 21:8-9 na Yn 3:14-15 ushuhudie mwendo huo wa fikra ya kiimani.

BINADAMU HAWEZI KUKWEPA SANAMU AU PICHA
Mwishoni kabisa, ikumbukwe kwamba binadamu anahitaji sanamu na picha ili kuyafikia na kuyaelewa mambo ya nadharia. Ukweli wa kilele ni kwamba hakuna hata mtu mmoja asiyejihusisha na sanamu au picha. Tukitaka kujenga nyumba, tunakuwa na picha yake kichwani. Tukitaka kulima shamba, tunakuwa na picha yake kichwani. Tukitaka kwenda nchi ya mbali, tunakuwa na picha yake kichwani. Tukisikia habari ya miji ya mbali ambao hatujawahi kuiteembele hata mara moja, huwa tunajichorea picha ya aina Fulani kichwani. Tukisikia habari za mtu ambaye hatujawahi kumwona, huwa tunajichorea picha yake vichwani mwetu. Picha za namna hii hakuna mtu timamu ambaye huwa hazichori yaani anabaki mtupu tu. Picha hizo zote si haramu kwa sababu hayo ni maumbile na uwezo wa mwanadamu. Mnyama hawi na picha kama hizo kwa sababu hana kipaji cha kufikiri na hivyo hawezi kuweka kumbukumbu  kama mwanadamu. Kifupi, ni mjinga.
Ingawa binadamu ana uwezo huo wa kujichorea picha mbalimbali, si kwamba picha zake ni sahihi daima. La hasha, mara nyingi sana picha za mambo ambayo hajapata kuyaona huwa si sahihi sana nazo husahihisha anapoliona jambo lenyewe waziwazi. Watu ambao walikuwa na picha ya New York vichwani mwao huweza kuona jinsi walivyokuwa wametunga picha isiyo sahihi siku ile watakapoingia jijini New York. Wasiowahi kuniona mimi, bila shaka wanajitungia picha yangu vichwani mwao, lakini wawe tayari kuibadili siku watakaponiona. Na sisi sote ambao hatujawahi kumwona Mungu ana kwa ana tuna picha ya Mungu vichwani mwetu, lakini tuwe tayari siku tutakapomwona Mungu ana kwa ana (rejea 1Kor 13:12, 1Yh 3:2).

HATA MWENDAWAZIMU ANATENGENEZA PICHA
Kwa hayo niliyosema, tuseme kama hatima kwamba hakuna hata mtu mmoja asiyetunga picha. Wote tunatunga picha hizo, hata wale wanaodai kwamba wakatoliki wanaabudu sanamu. Kama hawana uwezo wa kutunga picha kichwani, basi ubinadamu wao utiliwe mashaka. Ni ajabu kuwapo wanadamu wasioweza kutunga picha kichwani mwao maana kiutaalamu inajulikana kwamba hata wendawazimu na walevi huwa na picha vichwani mwao ingawaje huwa picha mbovu. Ndiyo maana mlevi huweza kuiona barabara kama mto wa maji uendao kasi na hivyo akaanza kupanga mbinu za kuuruka. Mwendawazimu huweza akaona fukutu kama nyumba akaanza kuiingia. Wenye akili timamu ndio watakaojua kwamba wale ndugu wamechanganyikiwa vichwani.
Basi Mungu hagombi juu ya uwezo huu wa kutunga picha, maana uwezo wenyewe ni zawadi yake mwenyewe kwa binadamu. Kama mtu hazipi daraja ya Mungu picha hizo na zile “anazozipakuwa nje” kwa umbo la sanamu ya kuchonga au ya kuumba au picha ya kuchora, Mungu hagombi kwa sababu hazijamwingiza mtu katika dhambi. Ubaya wa picha au sanamu hizo unaanza pale mwanadamu anapozipa daraja ya Mungu na kuanza kuziabudu na kuzitumikia.

WAPI INAPOLALA IBADA YA SANAMU
Basi ibada kwa sanamu inakuwapo pale ambapo mtu akiwa na nia ya kuabudu sanamu iliyo mbele yake anaifanyia sanamu mambo yafuatayo: kuitolea sadaka, kwa mfano, sanamu ya kuteketeza (rejea Hos 4:13) au ya vyakula, nafaka au umwagaji wa vinywaji (rejea 2Fal 5:17); kuitolea ubani kwa nia ya kuiabudu siyo kuiheshimu tu (rejea
1Fal 11:8, Isa 57:6, Yer 7:18), kuitambikia (rejea Isa 57:6), kuzichezea ngoma na wakatii mwingine hata kujikatakata kwa vifaa vikali (rejea 1Fal 18:26 -28) na kuiandikia meza (rejea Isa 65:11). Vitendo vingine ambavyo mtu akivifanyia sanamu kwa nia ya kuiabudu vinamtia mtu katika hatia ya kuabudu sanamu ni: kuitolea zaka ya sehemu ya kumi ya mapato ya mwaka na mazao ya kwanza ya mashambani (rejea Hos 2:8), kuibusu kwa kuisujudia kama kitu chenye enzi na mamlaka (rejea 1Fal 19:18, Hos 13:2, Ayu 31:2), kuiinulia mikono katika kuisujudia (rjea Isa 44:20) na kuiangukia kifudifudi ama kuipigia magoti kusudi kuiabudu (rejea 1Fal 18:26 -28). Katika vitendo vyote hivi, lakini, nia ya kuibudu sanamu lazima iwepo. La sivyo haiwi ibada ya kuabudu. Mfano mdogo, mtu akipiga magoti chini ya gari ili kuitengeneza, kupiga magoti kule si ibada kwa gari. Mtu akipiga magoti mbele ya mtu kumwomba radhi, kupiga magoti kule hakumaanishi kwamba mkosefu anamwabudu yule aliyemkosea. Aidha, mhindi akiinama mlangoni kwa sababu ya urefu wake, si kwamba anauabudu mlango.

MWANADAMU UTAISHI WAPI PASIPO NA SANAMU?
Mwishowe tuulizane, ndugu yangu. Eti, ingelikuwa kumiliki au kuwa na picha au sanamu ni dhambi kwa yenyewe nani angeliokoka? Binadamu mwenyewe ni sanamu, sasa ajifanyeje? Mwa 1:27 inasema mtu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu, maana yake ni sanamu. Je, iweje sasa? Kwa hali hii kuzaa nako ni kutengeneza sanamu. Na hivyo ni kusema mtu ye yote anayeoa au kuolewa anatenda jambo haramu kwani anaichukua sanamu nyingine na kukaa nayo na kwa mahusiano yao kama masamu wanakusudia kutengeneza sanamu kwa kuzaa kwao, tena sanamu maradufu kwani mtoto kwanza hufanana na wazazi wenyewe na kishapo na Mungu wanayemsadifu wote.
Halafu, ukienda kwenye ustaarabu wa kusoma, mambo yanashangaza tena. Tazama ukijua kusoma maana yake unajihusisha na sanamu maana herufi ni sanamu za sauti. Ndiyo kisa wachina, walatini, wagiriki, waarabu, waethiopia na kadhalika wanatofautiana katika kuzichora au kuzichonga herufi. Kishapo vitu vyote tunavyotumia vilikuwa kwanza akilini mwa yule aliyevitengeneza hivyo ni “masanamu” ya yale yaliyokuwa mawazoni. Kwa mantiki hiyo, nyumba zetu, magari, ndege zetu, baiskeli zetu, nguo zetu na kadhalika ni “masanamu”.

KUSOMA NI KUCHEZA NA SANAMU NA PICHA
Sidhani kama tunafikiri tunaposema. Ndipo niliposema, anayepinga sanamu anafikiri huku akisahau na anatazama huku akilala. Ni hivi, anayeng’ang’ania uharamu wa sanamu kwa kitendo cha kuwa nazo tu, asijifunze kusoma, kama anajua tayari aachane nako kwani anajishughulisha na sanamu za sauti. Herufi ni sanamu, ndiyo kisa kila walioanzisha alfabeti walianzisha kadiri ya vichwa vyao. Linganisha herufi za Kiebrania, Kihabeshi, Kilatini, Kihindi, Kiarabu na kadhalika. Kisha pata picha ya herufi picha za Kichina. Kifupi kujua kusoma ni kuweza kuzitafsiri picha za sauti na kushindwa kusoma ni kutoka kapa katika hilo.
Kwa hiyo, mtu anayedai anachukia sanamu wakati huo huo anaandika na kusoma kama hajui ni mtu wa kumhurumia na kama anajua ni mnafiki mwongo wa kujibari naye. Yaani ni mtu anayesema uongo mbele ya macho yako na pua yako kabisa. Kumbe, mpinge, usimwonee haya. Hii ni karne ya ishirini na moja marufuku kudanganyana kitoto hivyo.

ANAYECHUKIA SANAMU ASIOE WALA ASIOLEWE
Sidhani kama tunafikiri tunaposema. Ndipo niliposema, anayepinga sanamu anafikiri huku akisahau na anatazama huku akilala. Anayeng’ang’ania uharamu wa sanamu wala asioe au kuolewa kwani kwanza yule mwenzi wake ni sanamu na wakizaa watakuwa wanatengeneza sanamu, tena maradufu, kwanza kwa kufafana na Mungu na kisha kwa kufanana na wao wenyewe.
Kwa hiyo, mtu anayedai anachukia sanamu wakati huo huo “anaizimikia sanamu” na kuiambia “anaipenda – I love you”, kisha anaoa au anaolewa na sanamu na kisha kuzaa nayo sanamu (watoto) zinazofanana na mwenyewe na pia na Mungu, kama hajui ni mtu wa kumhurumia na kama anajua ni mnafiki mwongo wa kujibari naye. Yaani ni mtu anayesema uongo mbele ya macho yako na pua yako kabisa. Kumbe, mpinge, usimwonee haya. Hii ni karne ya ishirini na moja marufuku kudanganyana kitoto hivyo.

ANAYECHUKIA SANAMU ASILALE KWENYE NYUMBA WALA ASITUMIE USAFIRI
Sidhani kama tunafikiri tunaposema. Ndipo niliposema, anayepinga sanamu anafikiri huku akisahau na anatazama huku akilala. Anayeng’ang’ania uharamu wa sanamu asilale nyumbani kwani ni kulala ndani ya sanamu. Nyumba husanifiwa kwanza kichwani. Tena asisafiri kwa usafiri wa chombo chochote cha usafiri (baiskeli, pikipiki, bajaji, gari, treni, ndege n.k.) kwani ni kusafiri ndani au juu ya sanamu iliyopakuliwa kutoka kichwani mwa mtengenezaji wake. Aidha, asitumie kitu wala chombo chochote (bakuli, kijiko, saa, jembe, shoka, peni, daftari, kitabu n.k) maana ni kushikashika sanamu ya yule aliyekitengeneza. Hapo, ndipo kilipo kina cha kichekesho hiki. Hakuna kitu kinachotengenezwa na binadamu bila kuwako mawazoni mwake kwanza. Vyombo ni mpakuo wa picha za vichwani.
Kwa hiyo, mtu anayedai anachukia sanamu wakati huo huo, anajenga nyumba na kulala ndani yake au ananunua chombo cha kusafiri na kukitumia kama hajui ni mtu wa kumhurumia na kama anajua ni mnafiki mwongo wa kujibari naye. Yaani ni mtu anayesema uongo mbele ya macho yako na pua yako kabisa. Kumbe, mpinge, usimwonee haya. Hii ni karne ya ishirini na moja marufuku kudanganyana kitoto hivyo.

UPINZANI DHIDI YA SANAMU SI MPYA
Kulishatokea kanisani ugomvi kuhusu uhalali wa sanamu (iconoclastism). Waamini si haba wakawa wanazivunjavunja sanamu. Ugomvi huo uliamuliwa katika mtaguso wa Konstantinople IV ulioitishwa tangu tarehe 5 Oktoba 869 hadi 28 Februari 870 na Papa Nicolaus I (858-867) na kumaliziwa kimaandishi na Papa Adrian II (867-872). Kwa mtaguso huu mababa wengi walikutana katika vikao kumi tofauti. Basi, pamoja na mambo mengine waliyojadili, uhalali wa kuheshimu sanamu ulithibitishwa. Je, sisi tunataka tueleweshwe upya? Nadhani hakuna haja, kama si kwa kiburi cha makusudi.

HATIMA NDOGO
Ndipo katika jibu hili tumethibitishwa upya, kibiblia na kiutu, uhalali kuwa Mungu, tangu zamani, hakutukataza sanamu kama sanamu na picha, wala hakutukataza kuwa nazo, isipokuwa ametukataza katika kuzipa daraja la Mwenyezi Mungu kwa kuitumikia na kuisujudia.

MADA DADA – JE, IJUMAA KUU HUABUDIWA SANAMU?

Wakatoliki tunafanana na watu wanaofunguliwa kesi moja yenye vipengele vingi ili mshatikiwa akipangua hiki abaki na kingine na kingine mpaka akutikane na kosa la kutiliwa ndani. Katika suala la sanamu kuna mashtaka mawili, la kwanza kuhusu sanamnu kwa ujumla na la pili kuhusu tunachofanya na msalaba siku ya Ijumaa Kuu. Kumbe, baada ya kupangia hoja ya sanamu kwa ujumla wake,  tunabakiwa na mashtaka dada kwamba Wakatoliki huiabudu sanamu katika ibada ya Ijumaa Kuu na  ule mti wa msalaba wanaouweka mbele yao ndio wanaouabudu.

Mintarafu mashtaka haya najibu kwamba siku ya Ijumaa Kuu, haiabudiwi sanamu wala picha yo yote KAMA SANAMU AU PICHA isipokuwa msalaba ULIOUNGANA KABISA KABISA NA YESU KRISTO. Kwa maneno mengine, anayeabudiwa ni YESU KRISTO ambaye jina lake halimaanishi kitu kingine chochote isipokuwa WOKOVU. Usinibishe, WOKOVU ni YESU Kristo kwani hiyo ndiyo maana ya jina lake. Kwa vipi? Tulia nitakupa maelezo tena hivi punde.

JINA LA TUNACHOKITENDA IJUMAA KUU LINATUANGUSHA
Ili nikushibishe kwa maelezo yangu, niruhusu nianzie nyuma kidogo. Ninakuomba sana tusiachane njia katika maelezo yafuatayo. Ninayatoa ili tuelewane. Hivi, usikae kando tukashindwa kuelewana. Sisi wote ni watoto wa Mungu na inatupasa tushikane mikono katika imani Katoliki.
Ni kwamba siku ya Ijumaa Kuu haibudiwi sanamu. Acha nikiri kwa niaba yako kwamba, kwa ibada ya Ijumaa Kuu, lugha inatuangusha kidogo kwa sababu tunaposema“tunauabudu msalaba” tunatumia lugha ya mkato mno huku tukikusudia kusema kitu kizito cha kiimani. Unajua wanadamu hatujaamriwa tukiabudu kitu chochote zaidi ya Mungu. Basi, kama kuna chochote tunachosema tunakiabudu lazima kiwe na muunganiko mkubwa kabisa na Mungu.
Je, kuna muunganiko gani kati ya Mungu na msalaba wa Ijumaa Kuu? Kihistoria, zamani hizo watu walikuwa wakiwekewa mbele yao msalaba halisi alioutumia Yesu. Msalaba ule kwa vile ulikuwa umemning’iniza Yesu, nao ulikuwa umeloweshwa DAMU halisi ya Yesu, ulikuwa umembeba kweli Mungu. Damu ni uhai. Damu ya Yesu ni Yesu. hakuna ubishi. Ndipo msalaba wake uliabudiwa kwa uhalisia. Ndipo basi, inapokuja kwetu sisi tunajiunga kwenye ibada ya kuabudu kwa uelewa ule ule wa kujiunganisha kiroho na msalaba asilia. Hatujiungi kwa msalaba ule wa zamani bali tunajiunga na ibada ile kwa fikra ya kiimani. Unanipata uzuri hapa?

AINA NYINGINE YA MAELEZO YA IBADA YA IJUMAA KUU
Leo nakula nawe sahani moja. sishindwi kuzungumza na akili na moyo wako. Ndugu yangu, labda maelezo ya hapo juu yanakutinga na yanasababisha kichwa chako kiwake moto. Basi, ninaomba nikuunganishie msalaba wa Ijumaa Kuu kwa njia ya jina la Yesu. Jina la Yesu lina maana gani? Kumbuka, katika yale maneno ambayo kwayo tunaitiwa tuujongee msalaba wa Ijumaa Kuu, kunatajwa jina la Yesu. Ni hilo neno WOKOVU. Ni hivi, WOKOVU ni YESU kwa lugha ya Kiebrania. Jina “YESU” ni kifupi cha jina “YOSHUA” yaani kama ilivyo jina “Deo”, kifupi cha jina “Deogratias”, jina “Mage”, kifupi cha jina “Magdalena”, jina “Jose”, kifupi cha jina “Joseph”, jina “Beti”, kifupi cha jina “Elizabeti”, na “Bill”, kifupi cha jina “William, jina “Imma”, kifupi cha jina “Emmanueli” na kadhalika.
Kumbe, siku ya Ijumaa Kuu hapo tunapoalikwa tuufikirie na kujiunganisha na WOKOVU, tunaitwa tumfikirie na kujiunganisha na YESU, yaani kwamba tumwabudu Yesu Kristo ambaye maana ya jina lake ni WOKOVU. Kitendo hiki kinatakiwa kitendeke kiimani ndiyo maana tunaita ibada na siyo maigizo au tamthiliya. Nukta. Natumaini sijakutinga kwa mara nyingine.

Au acha nigeuze maneno. Ni hivi, tunachoabudu hutangazwa kwenye mwito unaotolewa dakika chache kabla ya ibada yenyewe. Mwito unaotolewa wa kurudiwa mara tatu ni wa kusogea mbele kwenye msalaba na kuabudu wokovu ambao umefungamanishwa kabisa na msalaba ulioletwa. Mwito huo husema: HUU NDIO MTI WA MSALABA AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE. NJONI, NJONI, NJONI  TUABUDU.
Kwa mwito huu, tujiulize, hiyo “u” iliyojificha katika neno “tuabudu” inamrejea nani au inarejea kwenye nini? Tuuabudu mti kama mti au tuuabudu wokovu? Ndugu yangu, ni mojawapo kati ya hayo mawili. Haya tuendelee.
Wokovu ni nani? Wokovu ni Yesu, kutokana na kifupisho cha jina refu la Kiebrania “Yoshua” (WOKOVU).  Kumbe hiyo “u” iliyojificha katika neno “tuabudu”  inamlenga Yesu Kristo, Bwana wetu aliyefunganishwa kifikra na kiroho na msalaba tunaooneshwa. Kifupi, wala hairejei kwenye mti kama mti. Ndipo mwito “njoni tuabudu” ni mwito kwenda kuuabudu WOKOVU.
Kumbe, kuuabudu “WOKOVU” ni kumwabudu “YESU” na kumbe kumwabudu YESU si kosa kwani ni Mungu na Mungu ndiye pekee wa  kuabudiwa. Na ndugu yangu, kumwabudu Mungu tumeamriwa wote na kufanya kinyume cha hapo ni dhambi ya ufurufuru wa mawazo (rej. Kut 20:2-6, Kum 5:6-12).

KUNA HITAJI LA MACHO YA KIIMANI SIKU YA IJUMAA KUU
Basi, hiki ndicho kinachofanyika, watu wenye imani na macho ya roho humwona pale msalabani WOKOVU ambaye ni YESU na huyo ndiye huinamiwa au kubusiwa kwa shukrani ya kutuokoa. Kwa namna hii, WOKOVU ndiye anayeabudiwa naye ni Mungu, Nafsi ya Pili ya Mungu wa Utatu Mtakatifu. Kumbe, mtu yeyote anayeshindwa kumwona WOKOVU pale msalabani kwa macho yake ya kiimani, aheri asijongee mbele siku ile ya Ijumaa Kuu maana ataabudu msalaba kama mti tu.
Si siri, imani inayotakiwa mbele ya msalaba katika Ijumaa Kuu inalingana sana na imani ya Wayahudi waliokuwa wakiumwa na nyoka na kujiponya kwa kuitazama nyoka ya shaba aliyoammriwa Musa aitengeneze. Wayahudi walipona si kwa sababu ya  nyoka ile ya shaba, la hasha. Walipona kwa uwezo wao wa kuvuka kiimani ng’ambo ya nyoka ile ya shaba na kumwona Mungu ANAYEPONYA AU KUOKOA (rej. Hes 21:8). Ninatumaini tupo pamoja bado. Nafurahi kama tunaelewana.

HATIMA YA JUMLA
Ndugu zanguni, tunalaumiana na kushambuliana kwa sababu ya jazba na munkari tu. Tusikose busara. Dawa ni kusoma vizuri Maandiko Matakatifu na kuyatafakari vyema kwa kutazama ndani na nje yake. Hiki kituko cha kuwa wanadamu – vyura si cha kiungwana. Tusifikiri kwa kuruka na wala tusisome Biblia kwa kurukaruka. Nasisitiza sisi ni wanadamu siyo watoto wa chura. Hatufanyi vyema tunapokurupuka na kubwata bwata tu kama radio za Mchina.
Tusifikri huku tunasahau. Tusitazame huku tunalala. Madhali sisi sote tumeumbwa kwa “mfano na sura ya Mungu”, wanadamu wote ni sanamu. Kumbe, sisi wenyewe ni sanamu namba wani. Wenzetu, jirani zetu, wake zetu, waume zetu, watoto wetu na wote wanaotuzunguka ni sanamu. Kwa jinsi hii sisi na sanamu ni kama chembe chembe za damu na damu, yaani ni kitu kile kile.
Kumbe, tunaishi na sanamu, tunakula nazo, tunaongea nazo, tunacheka nazo, tunagombana nazo, tunashirikiana nazo, tunaooana nazo, tuzaa nazo, tunazizaa, tunalala nazo na kadhalika. Tusifikiri kwa kuruka hapa (rej. Mwa 1:26-28). Zaidi ya ukweli huu, nimekuhakikishieni kwamba hakuna mtu yeyote mwenye akili na uhai duniani hapa asiyehusiana na sanamu au picha. Sote tunashughulika nazo vichwani mwetu, hata yule ambaye anazikataa hadharani huku akitutunashughulika nazo mashuleni, magazetini, vitabuni na kadhalika. Au hatuelewi picha na sanamu ni nini? Sasa kama unazikataa sanamu na picha wakati wewe mwenyewe ni vile vile sanamu na picha utajifanyaje? Basi, chukua kamba ujinyonge maana ni sanamu wewe! Kama huna, njoo kwangu nikupe moja nene ya nailoni. Asanteni kwa leo!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni