Jumanne, 11 Julai 2017

YALIYOJIRI JUMAMOSI KUU NA DOMINIKA YA PASAKA
Jumamosi Kuu

a) Yesu alizikwaje?

Kifupi, Yesu alizikwa kwa kadiri ya kanuni za mazishi ya kiyahudi, yaani
·        Alioshwa,
·        Kupakwa mafuta,
·        Kufunikwa sanda na
·        Kuwekwa katika kaburi lililochongwa mwambani na kufungiwa kwa jiwe zito.
·        Ziada kwa mazishi ya Yesu, ilikuwa ni kaburi lake kupigwa muhuri na kulindwa na askari.
Tukizungumza kirefu, tukumbushane kwamba, mazishi ya mtu aliyesulibiwa, halikuwa jambo la kawaida, bali msulibiwa alishushwa chini aoze au aliwe na mbwa ama ndege wala mizoga. Yaani, katika wakati wa Yesu, tabia ya kuwaacha wasulibiwa msalabani usiku kucha kulishaaanza kutoweka. Basi, kama hawakumzika msulibiwa, walau walimwondoa msalabani na kumbwaga chini, tulivyokwisha kusema. Kumbe, Yesu katika kupendwa kwake na marafiki zake akina Yosefu Arimatheya na Nikodemo na wanawake waliofuatana naye, alipata mazishi. Alioshwa, alipakwa mafuta na alivikwa sanda na kuwekwa kaburini. Alizikwa kwenye kaburi la Kiyahudi lililochongwa mwambani. Aina hii ya kaburi ni tofauti na makaburi yaliyokuwako na yaliyopo hadi leo hii kando kando ya eneo la hekalu, ambapo watu huzikwa na mifupa yao kuondolewa baadaye, ili wengine wapate kuzikwa pale wakimsubiri Masiha.

Kaburi la mwambani, lilichongwa kwa ufundi na kuwekwa kwanza chumba ambacho watu wawili au hata zaidi, waliweza kuingia na kusimama. Katika ukuta au kuta mbili, kulichongwa mwanandani ambamo waliiweka maiti. Kwa mtindo huo wa kaburi, watu waliweza kuitoa maiti na kuitengeneza na kuipaka mafuta watakavyo hata baada ya mazishi. Hiyo ndiyo hali iliwaruhusu wanawake waliokwenda kaburini siku ya Jumapili (siku ya kwanza ya juma), kwenda kaburini kwa nia ya kuipaka maiti ya Yesu mafuta. Kama tulivyokwisha kusema, kuipaka maiti mafuta ilikuwa ni desturi ya kawaida katika mazishi ya Kiyahudi. Kaburi la Yesu lilikuwa kwa chini kidogo na kwa sababu hiyo, ilipasa kuinama na kuchungulia.

Kaburi, lenye chumba kikubwa kwa namna tulivyoeleza, lilihitaji mlango. Kwa hitaji hilo, Wayahudi walitumia jiwe kubwa kuviringisha kuzibia mlango wa kaburi. Jiwe la kuzibia mlango mkubwa, kwa vyovyote lilikuwa ni kubwa lenye kuhitaji zaidi ya mmoja kuliviringisha mbali. Ndipo basi, wanawake watatu walipokiri kutokuweza kuliviringisha lile lililotumika kufi kaburi la Yesu.

Kwa kawaida kaburi halikulindwa, kwani wezi hawakuhitaji maiti za watu wakati ule. Lakini, kwa vile Wayahudi walimwogopa Yesu kwa maneno yake ya kusema angelifufuka, walilidhibiti kaburi lake. Kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, hafufuki na wanafunzi wake hawafanyi njama ya kumwiba, walipiga kaburi lake muhuri na kuwaweka walinzi walilinde (Mt 27:64). Huo kwa wenyewe ni ushuhuda kwamba, Wayahudi hawakuridhika kupata uhakika wa kummaliza kwa kumuua kimwili tu, ila walitaka kuua na kukomesha hata mawazo na matendo. Hicho ndicho kina cha chuki ya Wayahudi kwa Bwana wetu Kristo. Walikuwa hawampendi siyo yeye mwenyewe tu, bali hata mawazo na maneno yake walikuwa hawayapendi.

b) Yesu alishuka kuzimu, maana yake nini?

Kwamba Yesu alishuka kuzimu, maana yake ni kwamba aliingia kwenye hali ya wafu, yaani katika ulimwengu wa wafu (rej Zab 16:10 na Mdo 2:27). Sisi hatuzungumzii upande wa kuzimu kijiografia, kwani kuzimu siyo hasa mahali, bali ni hali kama zilivyo hali za kiroho za mbinguni, tohorani na motoni. Hiyo ndiyo teolojia kwani roho za wafu hazihitaji mahali na nafasi, bali zinahitaji hali tu.

Lakini, kwa makusudi, tubaki bado na mawazo ya kiyahudi. Kijiografia, Wayahudi waliamini kuzimu ni shimo kubwa giza lililokuwako chini ya ardhi. Huko ndiko, wafu wote walikoishi. Ulimwengu huo wa wafu, ulikuwa ni hali ya kivulini zilimoingia roho za wafu wote, hadi siku aliyokufa Yesu na kuja kuikomesha. Katika ulimwengu huo wa wafu ziliingia roho zote, yaani za wema na za wabaya, kwani saa ya kuingia na Mungu, ama kwenda motoni moja kwa moja ilikuwa haijawadia, maana ingeliletwa na Yesu Kristo mkombozi. Basi, roho za wafu ziliingia katika ulimwengu, ili kusubiri kufunguliwa milango ya mbingu na Yesu Kristo (rej. Ayu 3:13-19, Zab 88:1-5, Isa 38:18, Eze 31:17, 32:18-32). Basi, katika ulimwengu wa wafu zilikuwepo roho za akina Adamu, Eva, Kaini, Abeli, Nuhu, Ibrahimu, Musa, Yakobo na wengine wengi pamoja na mababu zetu.

Yesu alipoingia kuzimu, alizitangazia roho zilizokuwako kule kufunguliwa kwao. Yaani, huko kuzimu alizitangazia roho Habari Njema ya Wokovu, lakini siyo kwamba alibadili hali za roho hizo yaani, kwa mfano, kuzifanya zile mbaya zigeuke kuwa njema, la hasha. Kila roho ilikipata kile mtu mwenyewe alichokipanda, aliyepanda katika mwili, alivuna uharibifu na aliyepanda katika roho, uzima wa milele.

Ndipo kwa kitendo cha Yesu kufa na kuingia katika ulimwengu huo wa wafu, ulimwengu huo ulipokomeshwa. Ndipo basi, roho za wafu wema zikapasishwa kuingia mbinguni, na zile za wafu wabaya zikapasishwa rasmi kutupwa motoni. Kwa hali hii ya mambo, hapa tunapozungumza, hali ya kuzimu haipo tena. Tangu Yesu aifunge hali hiyo siku ile alipokufa na kuingia katika hali ile yeye mwenyewe, watu wakifa, roho zao zinaingizwa mbinguni au zinatupwa motoni moja kwa moja. Yaani, hakuna kuzungukia hali ya kuzimu tena.

Kwa maneno mengine, tunapokiri katika Kanuni ya Imani kwamba, Yesu alishuka kuzimu tunakiri kwamba, kweli Yesu alikufa na kwa kifo chake alichotufilia sisi, alikishinda kifo na alimshinda Shetani ambaye alikuwa anamiliki nguvu za kifo (rej. Ebr 2:14). Kwa lugha tena ya kibiblia, hali ya kuzimu iliyokomeshwa na Yesu kwa kifo chake cha kiukombozi, ndiyo hali ya kuwa katika "kifua cha Ibrahimu" kama tunavyosoma katika mfano wa Yesu wa tajiri na maskini Lazaro (rej. Eze 32:17-32, Lk 16:22-26).

B. Siku ya Pasaka Yenyewe

1. Ufufuko wa Yesu

a) Yesu alifufuka lini? Kweli baada ya siku tatu?

Yesu alifufuka Jumapili. Wayahudi wenyewe waliita siku siku ya kwanza ya juma, kwani hawakuwa na majina kama haya tuyatumiayo sisi ya Jumapili, Jumatatu, Jumanne, Jumatano na kadhalika. Wao walikuwa na majina yafuatayo:
·        Siku ya Kwanza ya Juma ndiyo Jumapili yetu,
·        Siku ya Pili ya Juma ndiyo Jumatatu yetu,
·        Siku ya Tatu ya Juma ndiyo Jumanne yetu,
·        Siku ya Nne Juma ndiyo Jumatano yetu,
·        Siku ya Tano ya Juma ndiyo Alhamisi yetu,
·        Siku ya Sita ya Juma ndiyo Ijumaa yetu na
·        Siku ya Saba Juma, kwa jina maarufu Sabato ndiyo Jumamosi yetu.
Siku hizi zote zilianza jioni na kwisha jioni. Yaani kama leo ilivyo Jumamosi, itakapofika saa ya machweo yaani jua litakapoanza kuzama, Jumamosi itakwisha na mara Jumapili kuanza. Hivi, kuanzia jioni ya leo itakuwa ni Jumapili hadi kesho saa za jioni jua litakapoanza kuzama. Ni kusema, Wayahudi hawakuzihesabu siku tangu saa sita ya usiku hadi saa sita ya usiku siku inayofuata tufanyavyo watu siku hizi.

Siku aliyofufuka Yesu ilikuwa ni siku ya tatu, kama ilivyoandikwa (rej. Hos 6:1-3) kwa vile alizikwa Siku ya Sita ya Juma, yaani akabaki mle kaburini Siku mzima ya Jumamosi yaani Sabato hadi mapambazuko ya Siku ya Jumapili. Walimzika kwa haraka haraka jioni ya siku hiyo ya sita ya juma, kwani siku iliyokuwa ikifuatia jioni ile ile ilikuwa ni Sabato na hivyo wasingeliweza kumzika Yesu kwani, kati ya kazi nyingi zilizopigiwa marufuku kufanyika siku ya Sabato, ilikuwepo kazi ya kuzika.

Basi, aliwekwa kaburini Ijuma jioni, akabaki humo Jumamosi hadi asubuhi ya Jumapili. Hizo ni siku tatu: Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Tunazihesabu tatu, siyo kwa sababu ya masaa ishirini na nne, bali kwa kadiri ya majina ya siku yalivyo Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, siku tatu.

b) Kufufuka kwa Yesu kunatatizwa na nini?

Kuna matatizo mawili makubwa yanayotatiza kutangaa kwa ukweli wa ufufuko wa Yesu. Tatizo la kwanza ni wivu wa baadhi ya binadamu. Watu wa aina hiyo, hapo kale hawakukubaliana na ukweli wa ufufuko wa Yesu.

Hao ndio waliwapa hongo askari waseme Yesu aliibwa na wanafunzi wake (rej. Mt 28:11-15). Basi, ukiwaona watu leo hii wanabisha ukweli wa ufufuko wa Yesu kwa mitindo ya kashfa, ndiyo "kabila" hilo hilo la Wakuu wa Kiyahudi. Ugonjwa wao ni wivu. Wao wana namna nyingi za kuvuruga ufufuko wa Yesu, baadhi hudai:
·        Mwili wa Yesu ulioza kwenye kaburi mahali fulani paliposahauliwa, wakati wengine hudai kwamba
·        Mwili wa Yesu haukuzikwa, bali walitupiwa mbwa. Hayo ndiyo baadhi ya wanayosema watu wanaojaribu kuvuruga ufufuko wa Yesu kwa ndimi zao.

Tatizo la pili, linasababishwa na waandishi wasaka fedha, yaani wenye uchu wa fedha. Hao huandika vitabu vya ajabu vyenye mawazo kama hayo ya kwamba, mwili wa Yesu uliachwa uoze au kwamba walipewa mbwa waule.

Wengine huandika kwamba Yesu hakufa, bali aliendelea kuishi miaka mingi baadaye. Waislamu, hasa Waahmadiya hueneza habari kwa vitabu, majarida na vipeperushi kwamba Yesu hakufa, bali aliepuka kifo. Baada ya kuepuka kifo alikwenda huko Kashmir, Asia, ambako aliishi kirefu hadi alipokuwa akiwa na umri wa miaka 120. Wao wanadai kaburi lake limegundulika huko Kashmir.

Waandishi wanaopinga ufufuko wa Yesu hujitokeza mara kwa mara katika historia ya dunia hii. Mmoja aliyetoa mpya zaidi kwa kalamu yake, alikuwa ni Bibi Barbara Thiering. Yeye alidai kwamba aligundua katika maandishi ya kale yaliyogunduliwa huko Kumrani (ufukoni mwa Bahari ya Chumvi, Israeli) kwamba Yesu hakusulibilwa Yerusalemu, bali huko Kumrani. Bibi huyo alipata mwanya wa kuandika habari hizo za ajabu, kabla maandishi hayo ya Kumrani hayajachapwa na kuwekwa wazi kwa walimwengu wote. Basi katika kitabu chake, Yesu na Kitendawili cha Maandishi ya Kumrani, Bibi Thiering alidai kwamba, Yesu alisulibiwa huko Kumrani na akazikwa pangoni huko huko Kumrani. Anasema watu walimzika wakidhani amekufa, kumbe alikuwa amezimia tu.

Bibi Thiering anadai kwamba, dawa aliyopewa Yesu msalabani ilikuwa ni sumu iliyofanya kazi pole pole. Simoni Mchawi, yule aliyetajwa katika Biblia (rej. Mdo 8:9-25) alimpa dawa ya kusafisha mwili pamoja na manemane iliyosaidia kurekebisha ngozi laini tumboni mwa Yesu. Ndipo kwa misaada hiyo Yesu alipoamka. Kisha kuamka, Bibi Thiering alidai kwamba, Yesu alimwoa Maria Magdalene (rej. Mt 27:55-56, 61; Mk 15:40; Lk 8:2; Yn 20:4) na kuzaa naye watoto watatu. Baadaye, Yesu alimpa Maria Magdalena talaka na akamwoa Lyidia (rej. Mdo 16:14-15) na kishapo akafia mjini Roma, Italia.

Bibi Thiering aliitetemesha dunia ya wasomaji kwa kitabu chake. Kumbe maandishi ya Kumrani yalipochapwa, watu wakagundua kwamba bibi huyo aliongopa vibaya sana, hakuna hata paragrafu moja ya Maandishi ya Kumrani inayosema hivyo anavyodai yeye. Ndipo aibu ilipomshika Bibi Thiering na kitabu chake kikawa kati ya vitabu vya kipumbavu sana duniani. Heri waongo wengine wanaopinga ufufuko wa Yesu wangeliabishwa namna hii hii!

c.   Je, Yesu kweli alifufuka? Kuna ushahidi wo wote?

Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni hakika kwa sababu ya shuhuda kubwa sita.
·        Mosi, tunaanza na ushuhuda wa mbali wa kabla ya kufa kwenyewe. Huo ni ushuhuda wa maisha yake mwenyewe. Yeye aliishi maisha ya kiadilifu na ya muungano na Mungu Baba. Tena Yesu alisema waziwazi kwamba atafufuka, yaani hekalu la mwili wake litabomolewa, lakini katika siku tatu atalijenga tena na kama tujuavyo Yesu, kama Mwana wa Mungu alikuwa hasemi uongo kabisa. Ndipo mambo yalidhihiri pale alipotoka kaburini kwa nguvu ya ufufuko. Ndipo maneno yake  yakawa kweli kabisa.

·        Pili, kunakuja ushuhuda wa karibu, ushuhuda unaoitwa kisheria ushuhuda wa kimazingira. Huo ndio ushuhuda wa kaburi wazi. Mwili wa Yesu haukuibiwa na ye yote, maana kaburi lilitiwa muhuri na kulindwa na askari. Sasa mwili wake uko wapi? Amefufuka na ataonekana kwa wafuasi wake. Mtu aliyekufa kweli, ukimwona anatembea tena na kula pamoja na watu maana yake nini? Maana yake amefufuka. Yesu alionekana na kula na wanafunzi wake tena. Basi, kweli Yesu alifufuka kutoka wafu.

·        Tatu, ushuhuda kutoka kwa wale ambao kiutamaduni hawakuruhusiwa kuwa mashahidi wa jambo lo lote. Wanawake hata kama walikuwa mia moja, katika utamaduni wa Kiyahudi, hawakuweza kusema cho chote cha uzito wa kuwa ushahidi wa jambo lo lote. Basi, kama wafuasi wangelipanga kusema uongo kwamba Yesu amefufuka, wangelipanga vyema uongo huo kwamba walikuwa ni wanaume kadhaa walioshuhudia kufufuka kwa Yesu. Kumbe, wafuasi bila kudanganya wala kutunga hadithi wanasema wazi kwamba, jambo hilo la ajabu la kufufuka Yesu halikutegemea wanaume, ila kwamba Mungu kwa maajabu yake aliwateua wanawake wawe mashahidi wa tukio hilo. Yaani, waliodhaniwa ni dhaifu, ndiyo waliopewa zawadi kubwa ya kushuhudia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, kweli Yesu alifufuka kutoka wafu.

·        Nne, ushuhuda wa kubadilika kwa wafuasi. Baada ya kufa Yesu mitume walikuwa na woga mwingi, hata wakajifungia chumbani. Lakini, walipopata habari kwamba Yesu amefufuka, walijawa na nguvu ya kutoa ushuhuda mbele ya watu bila woga tena. Laiti jambo hilo lingekuwa ni la uongo, wangelizidi kuingiwa na woga badala ya kujawa na nguvu ya ajabu. Basi, kweli Yesu alifufuka kutoka wafu.

·        Tano, ushuhuda wa kuundwa na kudumu kwa Kanisa la awali. Kama Yesu asingelifufuka, wanafunzi wangelitawanyika na Kanisa lisingelizaliwa na kudumu kama lilivyotokea. Basi, kweli Yesu alifufuka kutoka wafu.

·        Na sita, ushuhuda wa Injili. Injili zote zinatangaza kwa nguvu moja kwamba, Yesu alikuwa mzima tena baada ya kifo chake. Hakuna Injili inayositasita kushuhudia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, kweli Yesu alifufuka kutoka wafu.
Kufufuka kwa Yesu, kuna maana kubwa sana kwa Mungu Mwenyezi na kwetu sisi wanadamu. Maana ya ufufuko wa Yesu kwanza ni:
·        Utukufu wa Mungu na pili kwetu sisi
·        Ni wokovu wetu.
Tumekombolewa na mauti na tumefanywa huru kutoka utumwa wa shetani na upotevu wa milele. Mlango wa paradisi uliofungwa kutokana na dhambi ya Adamu, unafunguliwa kwa kifo na ufufuko wa Adamu wa pili, yaani Mwana wa Eva wa pili yaani Maria.

Tufahamu vyema kwamba, ukombozi huo siyo kwa ajili yetu tu, ila kwa wanadamu wote. Wote watakaomtafuta Mungu kwa moyo wao wote, kwa nguvu zao zote na akili zao zote, wakiifuata sauti ya Mungu iliyo mioyoni mwao, ndiyo dhamiri zao, wataokoka pia.

Hili ni jambo la furaha kuu, ambalo kwalo ni budi tuimbe Allelluyah Kuu. Kwa sababu hiyo, hata wazee wetu waliokufa kabla ya kufikiwa na ukristo, watapata wokovu na sasa hata watu wasio wakristo wanaweza kuupata wokovu pamoja nasi. Tunaposema hivi maana waislamu wema, wabudha wema na watu wema wa madhehebu na imani zingine, wanaweza pia kuokoka pamoja

a)     Kwa nini Yesu hakumtokea Pilato baada ya ufufuko?

Baada ya kufufuka, Yesu hakumtokea Pilato wala watesi wake, kwani hakuwa na nia ya kujigamba mbele ya adui zake. Ikumbukwe pia kwamba Yesu hakufanya lo lote kwa kujionesha tu, ila alifanya mambo pale alipoona kitendo au vitendo vyake, muujiza au miujiza yake, itachochea imani kati ya a wanaoshuhudia tukio au matukio hayo. Kwa kweli, kama angelijitokeza kwa Pilato ama Wayahudi waliomsabibishia angeliweza kuzusha zogo jingine. Bila shaka wangelitaka kumkamata tena kwa kudhani kwamba, alikurupuka kifo kama walivyojitahidi kumkomesha. Kwa hali kama hiyo, ii isingelichochewa hata kidogo. Ndipo kwa manufaa ya kiroho, alipowatokea wateule mitume na wafuasi waliomwamini, kusudi imani yao iimarike na wautangazie ulimwengu kama mashahidi kamambe wa ufufuko wake. Na kwa mtindo huo, ndipo amefaulu kufanya habari za ufufuko zitangae na kutufikia sisi.

2. Kupaa mbinguni

Yesu alipaa mbinguni baada ya siku 40 tangu kufufuka. Ka kipindi hicho cha siku 40 alikuwa anaishi wapi?

Yesu alipofufuka aliingia katika hali ya utukufu wa kimungu, au utukufu wa kimbingu na ye yote mwenye utukufu wa kimbingu anaungana na Mungu moja kwa moja. Ndipo basi, Yesu alipofufuka aliingia katika utukufu wa kimungu au kimbingu moja kwa moja. Na siyo kuanzia siku ya ufufuko tu, bali aliingia katika hali hiyo mapema tangu siku aliyokufa na kuingia kuzimu kuzifungulia milango roho za wafu waliokuwa huko kabla yake. Ndiyo namna hiyo, hakufungwa tena na saa au siku.

Siku ya kimungu au ya kimbingu ni moja tu, haina wakati uliopita au ujao, daima ni wakati uliopo tu. Aidha, roho ikishajipatia hali ya utukufu, haifungwi tena na mipaka ya muda wala na mipaka ya mahali, bali roho hiyo huweza kuwepo po pote itakapo, bila ya kuhitaji kufunga safari ya kutembea kutoka mahali pamoja hadi pengine.

Ndiyo maana alipomwambia yule mwivi mwema kwamba, leo hii utakuwa nami peponi hakumdanganya, bali katika siku ile ile ya kimungu, roho ya Yesu na ya yule mwizi mwenye toba, zilifika kuzimu na pia kuingia katika makao ya Baba wa mbinguni.

Ni kusema, Yesu katika siku zile 40, alikuwa kwa Baba yake na alikuwa akitokea katika hali hiyo ya kimbingu alipokuwa akiwatokea wanafunzi wake. Kwa namna hiyo, kumaliza siku ya arobaini ni msemo wa picha, wenye maana ya kipindi kamili cha kukamilishia jambo. Hivyo, katika kipindi kamili, Yesu alimaliza kazi ya kuwatokea Mitume na Wafuasi wake kuwasadikisha kwamba, amefufuka na kwamba tangu wakati huo ilikuwa zamu yao kuiendeleza kazi ya kumkusanyia Mungu watu wa kila kabila, lugha, jamaa, rangi na taifa.

Tuseme kwa maneno mengine, kupaa mbinguni hakukuwa sa­fari ya kutoka duniani kwenda Mbinguni, bali kulikuwa ni kuingia rasmi katika Utukufu wa Mungu, hali inayowakilishwa na wingu lililompokea na kumfunika Yesu. Kwa kuingia rasmi katika Utukufu wa Mungu, Yesu alianza rasmi kuketi kuumeni kwa Baba, yaani kumiliki enzi na mamlaka ya duniani na mbinguni kama bingwa wa ukombozi wa wanadamu. Hivi basi, kuketi kuumeni kwa Baba ni kupewa kwake rasmi mamlaka ya kuitawala mbingu na dunia, baada ya kazi yake mwanana sana.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni