BIBLIA INASEMA KWA UJUMLA NDOTO NI UBATILI (YbS 34:1-8)
Vijana, acheni tuwekane sawa kisayansi na kibiblia kuhusiana na suala la NDOTO. Tusisumbuke nazo mno. Zimeshapoteza maana yake ya kale kwa sababu ya ujio wa Yesu Kristo.
Ni hivi hapo zamani sana ndoto zilikuwa njia maalumu ya ufunuo lakini siyo sasa baada ya Yesu Kristo kukamilisha kazi yake hapa ulimwenguni. Hapo kale sawa, lakini siyo siku hizi. Ndiyo maana kuna ripoti za ndoto zilizowapatia ujumbe watu fulani fulani katika Biblia, yaani Agano la Kale na Agano Jipya. Wakati ule, njia nyingine ya ufunuo ilikuwa maono.
Lakini kwa kufika Kristo, Mwana wa Mungu, ulimwenguni, ufunuo ulifikia kilele na hivyo mambo ya ndoto na maono kutohitajika tena kwa namna ya pekee. Ndiyo maana imeandikwa, ”Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, lakini siku hizi za mwisho amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote, yeye ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akautegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu” (Ebr 1:1-3).
Wenzetu wengi wa mataifa yaliyoendelea wameshaachana na ndoto, kwa namna ya pekee Wayahudi, ndiyo maana wametuacha maili nyingi katika sayansi. Mwamini ndoto hawezi kutafiti mambo ya juu kwa sababu atabaki akijishughulisha na mambo ya maweruweru tu. Wenzetu wamejitahidi kujitoa katika mambo hayo yasiyo na miguu wala vichwa. Kwa nini? Kwa sababu hazina mashiko yoyote.
Kimsingi, tuliobaki tukihangaika na ndoto ni hasa sisi Waafrika. Siku zote, sisi ndio tuliozoea kushikilia walichotupa wenzetu. Sisi tunakuwa wa mwisho kuachana na waliyoachana na wenzetu. Mfano mkubwa ni imani za uchawi. Wenzetu wamejitahidi kuacha, lakini sisi inakuwa kama tumejipa hatimiliki. Kwa kweli, sisi Waafrika tu watu wa chini nasi tunaridhika sana na mambo ya chini, mathalani, laana, imani juu ya uchawi (ushirikina), ndoto na maono. Wakati wenzetu wanatafiti jinsi ya kwenda anga za mbali, sisi tumebaki kuamini na kutishika na mambo ya hapa chini “majini”, panya, mijusi, bundi, mende na kadhalika. Balaa kweli! Wenzetu wamekwenda mwezi na wamepeleka vyombo Mars na Jupiter! Inasikitisha. Siku hizi wenzetu wanafanya utafiti jinsi ya kuwapeleka wanadamu Mars, sisi tunahangaishana juu ya ndoto. Nimesoma leo mtandao mtu akijinasibu kujua zaidi ya Waafrika wenzake. Jambo hili lisivumilike. Ni mchango mbaya wa kudumazana.
Kumbe, sayansi inaweza kutusaidia kueleza ndoto ni nini. Ndugu zanguni, kuota ndoto ni jambo linaloendana na uwezo wa binadamu kulala usingizi. Ni hivi, Mungu ametupatia wanadamu uwezo wa kulala usingizi kwa makusudi ya kupumzisha na kukarabati ubongo wetu.
Kimaumbile na kisayansi, mwanadamu hulala usingizi wa aina mbili kwa kusiganishwa: usingizi mzito na usingizi mwepesi. Mungu ametuumba hivyo na sayansi imegundua hilo (YbS 43:31-33). Basi, tuendapo kulala, kwa kawaida huwa tunalala kwanza usingizi mzito masaa mawili, halafu usingizi mwepesi masaa mawili, kisha usingizi mzito masaa mawili tena na kishapo usingizi mwepesi masaa mawili tena na kadhalika. Mabadilishano haya huweza kufanyika mara tano kulingana na mtu alivyowahi kulala.
Usingizi mzito ni kwa ajili ya ubongo kupumzika na usingizi mwepesi ni kwa ajili ya ubongo kujikarabati. Wakati wa usingizi mzito ubongo hutulia sana. Ni wakati wa usingizi mwepesi ndipo mwanadamu anapoota ndoto. Kila siku, kila mwanadamu huota ndoto isipokuwa huwa tunazisahau. Mwota ndoto huambulia kukumbuka ndoto ya mwisho anayoigutukia.
Sasa sikiliza. Kwa kuwa mwanadamu huota ndoto wakati wa usingizi mwepesi, huwa anaona kana kwamba jambo analoliota ni “live” wakati sivyo. Kwa kuwa analoliota ni jambo la ndotoni, mwotaji hukosa uwezo wa kuitawala ndoto yake. Hata kama ni ndoto ya kumwona mtu fulani, mwotaji hukosa uwezo wa kumkamata kwa sababu yote si kweli. Mwota ndoto hushindwa kumkamata mtu anayemwona ndotonio kwa sababu, kwanza mtu yule hayupo pale na mwotaji mwenyewe hushindwa kujimudu kwa sababu ya usingizi unaomwendesha.
Twendeni kwenye Biblia. Kwa ujumla ndoto ni upuuzi na kivitendo tunazipuuza. Sasa sijui kwa nini tunazitolea macho. Sikiliza. Eti, ukiota ndoto leo, umepata shilingi milioni moja nawe umekwenda kwa furaha madukani, huko umejinunulia viatu vipya, kofia, kikoi, suti, baiskeli na viroba vitatu vya unga na kubakiza chenji yako mfukoni, unapoamka asubuhi na kujikuta upo nyumbani pako bado na vitu hivyo havipo pale, unakwenda polisi kuripoti kwamba umeibiwa? Bila shaka huendi kuripoti polisi na ukithubutu kwenda kuripoti wizi wa namna hiyo, utaonekana “hamnazo” nawe pasipo ajizi utarudi na ngeu. Au tukiota ndoto tunakula wali kisha tunaamka pasipo kuuona, mbona hatuendi polisi kushtaki kwamba tumeibiwa wali? Ama tukiota ndoto tumepata fedha nyingi kisha tukaamka pasipo kuziona, mbona hatuendi polisi kushtaki kwamba tumeibiwa? Au ukiota ndoto umefika New York na kutumbua raha kule, unapoamka asubuhi na kujikuta upo nyumbani pako bado, unawauliza ndugu zako nani aliyekurudisha toka kwenye? Bila shaka humuulizi mtu habari hiyo kwa sababu unajua ni ndoto tu. Kivitendo hatubwetekei ndoto. Katika uelewa huo, Biblia inatusimanga ikisema,
“MTU MJINGA HUWA NA MATUMAINI YA BURE NA YA UONGO, NDOTO HUMPA MPUMBAVU MABAWA YA KURUKA. KAMA MTU ANAYEJARIBU KUSHIKA KIVULI NA KUFUKUZA UPEPO NDIVYO ALIVYO MTU ANAYEAMINI NDOTO. NDOTO NI KAMA KIOO SURA INAYOUKABILI USO. NI KITU GANI KIWEZACHO KUTAKASWA NA UCHAFU? JE, UKWELI WAWEZA KUPATIKANA KWA UONGO? KUPIGA BAO, RAMLI NA NDOTO NI UPUUZI, AKILI HUWA NA MAWAZO KAMA YA MAMA ANAYEJIFUNGUA. USIZITIE MAANANI NDOTO ISIPOKUWA KAMA ZIMETOKA KWA MUNGU MKUU MAANA NDOTO ZIMEWADANGANYA WENGI NA WOTE WANAOZITUMAINI WAMEAIBISHWA. SHERIA NI KAMILIFU BILA UDANGANYIFU HUO NAYO HEKIMA NI KAMILIFU KWA MTU MWAMINIFU” (YbS 34:1-8). Ndugu zanguni, nukuu hii nimeandika makusudi kwa herufi kubwa kusudi isomeke kirahisi na kusisitiza ukweli wake.
Kwa bahati mbaya, Wakristo wengi wasio Wakatoliki hawana fursa ya kuyajua Maandiko haya ya busara kubwa kwa sababu kwa kuingizwa mkenge na Martin Luther wanatumia Biblia ndogo, yaani Biblia iliyopunguzwa vitabu saba kutoka 73 hadi 66. Huu ndio mkasa aliouanzishwa Martin Luther miaka ile ya 1520. Kwa maoni yake binafsi kabisa akapunguza vitabu vya Biblia asilia kutoka 73 hadi 66 na hivi kujinyima mwenyewe na wafuasi wake neno la Mungu lililo kwenye vitabu vya Tobiti, Yudithi, Hekima ya Sulemani, Yoshua bin Siraki, Baruku, 1 na 2 Makabayo. Jamani huu ulikuwa mkasa wa aina yake!
Kumbe Biblia, kama inavyosomeka katika YbS 34:1-8, ilishatupilia mbali shauri la kuzitilia maanani ndoto, ndiyo maana Yesu hazizungumzii ndoto hata mahali pamoja katika Agano Jipya. Yesu alijijua kwamba yeye ndiye kilele cha ufunuo na hivyo kubwaga chini ndoto na maono. Hivi, kwa ujumla ndoto ni upuuzi mtupu.
Waafrika wengi huwa tunajitahidi kupuuza ndoto kama mzee Yoshua bin Siraki anavyotutaka. Lakini wengine wetu hawana nguvu na ushujaa wa kuzipuuza ndoto, hasa ndoto za majinamizi. Ndoto za majinamizi ni zile za kutisha, mathalani, kuota watu wakikufukuza, wakikutoboa macho, wakikutumbukiza lindini, wakikupiga pasi ya moto mgongoni na kadhalika. Watu hao wakiota ndoto za namna hiyo hushindwa kuzipuuza. Wao ndio kwanza hudhani kuna uchawi kwa sababu ya kujikuta wakiota ndoto za kutisha kama hizo. Husema katika ndoto hizo wameoneshwa wabaya wao “live”, jambo ambalo si kweli. Kifupi, wenzetu hao hushindwa kuzipuuza ndoto za majinamizi kama wanavyojitahidi kuzipuuza ndoto zingine wakati ndoto ni ndoto tu.
Nasisitiza, hizi ni ndoto maalumu tu. Jina la ndoto hizi za kutisha ni majinamizi, kwa Kiingereza “nightmares”, nazo zisichukuliwe kama ushahidi wa uwepo mambo ya “kichawi”. Ndoto za majinamizi ni mapato mengine ya ubongo kufanya kazi kwa fujo kunakotokea mtu akiwa usingizini, yaani mawimbi ya umeme wa mwilini ALPHA, BETA, THETA na DELTA yanapofanya kazi kwa msepetuko. Wakati wa ndoto za majinamizi ni wakati ambapo mambo ya kwenye mtima hujiibusha kwa fujo kutokana labda na kuchoshwa kwa ubongo ama na ugonjwa au kemikali zenye athari. Mawimbi ya mwilini ALPHA, BETA, THETA na DELTA huweza kufanya kazi isivyo kawaida kutokana na kulewa pombe, kulewa madawa ya kulevya, kuumwa malaria inayokimbilia kichwani, kusongwa na mawazo mazito, kutatizwa na matatizo ya ndoa na unyumba, kuchanganywa na matatizo ya jamii na kadhalika.
Kumbe, tunapoteza muda mwingi kuzijali ndoto zisizo na maana yoyote. Naomba makala hii iwaelimishe watu ambao wakiota ndoto za majinamizi wakamwona mtu ambaye kwa kawaida wanamwogopa kama “mchawi” akiwajia na kuwakaba koo au kuwatisha, husema kwamba mtu yule ni mchawi maana aliwajia usiku nao wamemwona “live”. Ndipo kwa kufuata ndoto hiyo humwendea mtu huyo na kutaka kumshambulia kwa ngumi, mateke au silaha. Lakini hiki ni kichekesho, mbona tukiota ndoto tunapinduka kwenye gari, hatuendi kulishambulia gari lile? Mbona tukiota ndoto tunashambuliwa na simba kwa nini hatuendi porini kumtamfuta simba tumshambulie?
Ndoto hatuwezi kuzizuia kwa sababu hutokewa pasipo sisi kuzitawala. Wakati wa usingizi mwepesi ukishatufikia ndoto zinaweza kuja za rangi yoyote ile. Lakini ukitaka usiote ndoto za majinamizi ya watu wakikudhuru, ishi maisha yenye kuwapendeza watu na wala usiwe unalala na hofu zako kichwani au moyoni (Efe 4:26). Ishi na wote kwa amani na upendo, ndoto zako zitakuwa laini na tamu. Lakini ukiishi katika kisirani, hofu na wasiwasi tegemea kuota ndoto mbaya mbaya. Ni ukweli wa kiutafiti kwamba mtu mwenye msongo wa mawazo huota ndoto mara tatu au mara nne zaidi ya mtu asiyesumbuliwa na msongo wa mawazo.
Kwa taarifa yako, mwili nao hufanya kazi na kupumizika vile vile. Kila jioni na usiku, kati ya saa tatu jioni na saa kumi alfajiri, mwili unapopunguza shughuli zake mbalimbali zikiwamo shughuli za umeng’enyaji. Ndiyo kisa jioni ukila wali sinia moja, kunde bakuli mbili, parachichi sita, mahindi ya kuchoma manne na kadhalika, ukaenda kulala hivyo, wakati mwili unapunguza shughuli zake, utavimbiwa vibaya. Utavimbiwa kwa sababu shughuli za umeng’enyaji zinapunguzwa huo na hivyo vyakula vyako havitameng’enywa. Ndiyo maana wanadamu hawavimbiwi mchana hata wakila sana.
Lakini mwili unapopunguza shughuli zake si kwamba hufa, la hasha. Wakati mwili unapopunguza shughuli zake usiku shughuli za kisaikolojia huendelea. Mathalani, hofu na hasira zote za mchana huzamwisha katika kutojitambua (subconscious). Hayo yanayomezwa usiku ndiyo yanayokuwa malighafi ya ndoto zetu. Ole wako mwili wako uwe unawameza watu mbalimbali unaowaogopa. Ole wako mwili wako uwe unameza hasira. Nakwambia hao unaowaogopa au unaowafanyia hasira siku moja watatokea katika ndoto zako za majinamizi na kukusumbua kwa vivuli vyao. Wanadamu hao hawatakuwa wachawi, bali picha zao zitakusulubu kwa sababu umefanya uzembe wa kuwameza wakiwa katika hali ya kutisha labda kwa kuzeeka kwao, kwa macho yao mekundu, au kwa vibiongo vyao au kwa mapengo yao ya vinywani na kadhalika. Mfano, watu wakimmeza bibi fulani kwa sura ya kutisha, watamwota mara kwa mara akiwavamia kiasi kwamba watamvumisha kuwa mchawi na hatimaye watu wale wanaweza kufikia katika kumchukulia hatua ya kumcharanga mapanga na kuumuua. Kifupi, watakuwa wamemwonea bure, wakati kosa ni lao wenyewe, yaani kule kummeza katika sura ya kutisha. Ndivyo yanavyowafika madhila ya ajabu ajabu wazee na vikongwe wetu. Mintarafu mwendo huu wa mambo, ushauri wangu wa bure ni kwamba tuwe tunalala kila siku kwa furaha na upendo. Kama Biblia inasema lolote kwako, basi soma tena Efe 4:26-27 uone jinsi Mtume Paulo alivyokushauri usibaki na hasira kutwa nzima.
Tuachane na kuzijali ndoto. Hapo juu tumesoma jinsi mzee Yoshua bin Siraki alivyotuandikia. Katika hayo aliyosema amesema ndoto (hali kadhalika maono) za kutilia maanani ni zile zitokazo kwa Mungu, ambazo kwa kweli lazima ziwe chache kwa vile Yesu Kristo amekamilisha ufunuo. Tunaweza kuzibaini ndoto zitokazo kwa Mungu ikiwa zinatimiza vigezo vitatu vifuatavyo: mosi, kutokea mara kadhaa, pili, kuwapo kwa ujumbe maalumu na tatu ujumbe huo kutopingana na mafundisho ya Kanisa Katoliki pale ujumbe wake unapopimwa kiteolojia, kiimani au kimaadili.
Kwa mujibu wa vigezo hivyo vitatu, usipokee ndoto iliyotokea mara moja tu. Ndoto isiyojirudia ni rahisi kutokana na shida fulani ya mwotaji mwenyewe mathalani ulevi au ugonjwa. Tena usipokee ndoto ambayo haina ujumbe wowote wa maalumu. Ndoto ya kutilia maanani lazima iwe na ujumbe maalumu maana kimsingi ufunuo umeshakamilika katika Yesu Kristo. Ndiyo kisa tumeambiwa tumsikilize yeye tu (Mk 9:7). Hali kadhalika, usipokee ndoto yenye ujumbe unaopingana na mafundisho ya kweli, kwa mfano, kutumwa kuiba, kutumwa kumuua mtu, kutumwa kufanya tendo la ndoa na mtu fulani, kuagizwa kutokwenda kanisani, kuagizwa kuwataja watu kuwa “wachawi” na kadhalika.
Vivyo hivyo kuhusu maono. Maono kwa ujumla ni ubatili isipokuwa kama yametoka kwa Mungu. Maono yaliyotoka kweli kwa Mungu hutimiza vigezo vitatu tulivyovitajaa hapo juu, la sivyo ni utapeli mtupu. Lakini, watu wengine hujitafutia “ujiko” kwa kutoa “ushuhuda” dhalili wa kutokewa eti na Mungu au watakatifu au marehemu wa kale. Basi, simama kidete usije ukadanganywa na watu waliozoea kuwadanganya wanadamu wenzao kwa kutoa ushuhuda wa maono yasiyokidhi vigezo vyovyote. Wapuuze watu wa namna hiyo. Hivyo wala usipokee kama kweli maono yaliyotokea mara moja tu, ni rahisi maono hayo kutokea kutokana na shida fulani ya mwotaji mwenyewe, mathalani, ulevi au ugonjwa wake wa akili. Hali kadhalika, usipokee maono ambayo hayana ujumbe wowote wa pekee. Nasisitiza, kama ni maoni ya kutilia maanani lazima yawe na ujumbe maalumu maana kimsingi ufunuo umeshakamilika katika Yesu Kristo (Ebr 1:1-3). Kama kweli Mungu atataka kutupatia ufunuo wa ziada kwa mtindo wa ndoto au maono lazima kutakuwa na ujumbe maalumu maana utakuwa tofauti na ufunuo wa Bibliaa, jambo ambalo halina umuhimu wa pekee leo hii.
Nimesema mengi nikiwaasa tuachane na kuzijali ndoto kwani neno la Mungu linatuasa tufanye hivyo (YbS 34:1-8). Hata hivyo sina furaha wala amani. Kinachonitisha na kunisikitisha mimi ni kwamba vijana na wengine wanaojinasibu kuwa “wasomi” wanatudidimiza Waafrika wenzao katika mambo dhalili kama ndoto, laana, imani za uchawi (ushirikina), hofu juu ya majini na hofu juu ya Frimasoni, badala ya kujaribu kutuvusha wenzao katika kudharaulika ambako kumetosha sasa. Yaani badala ya kutusaidia Waafrika wenzao tupate uwezo wa kushindana na watu wa mabara mengine katika sayansi ndani ya karne hii ya sayansi na teknolojia, wao wanatudidimiza wenzao matopeni. Yana faida gani mafundisho juu ya ndoto, mafundisho juu ya laana, mafundisho juu ya imani za uchawi (ushirikina), mafundisho juu ya majini na hofu juu ya Frimasoni na kadhalika? Hata hivyo, vijana na watu wa aina hiyo wanatuaandikia wenzao “vimakala” na vijitabu koko vikijaribu kutoa tafsiri za ndoto. Ninameviona vikiuzwa na kununuliwa vitabu juu ya ndoto na tafsiri zake. Vitabu vibaya sana hivyo. Ni vitabu vyenye kumtia mtu matumaini feki. Ni kutupotezea muda na kutudumaza. Kuyasoma na kumakinika na maandishi kama hayo ni kujididimiza, sana sana ni kujiongezea hofu na wasiwasi na hatimaye kujikosesha kujiamini. Ni kujifunga pingu kichwani na mikononi. Ni kujikosesha nguvu ya kufikiri na kuyakabili mambo ya dunia hii macho kwa macho. Ndugu zanguni, katika “kupigika” kama huku, kusomeshana mambo ya ndoto ni kutia chumvi kwenye vidonda vyetu wenyewe. Ni kuziba fursa za Waafrika kuchangamkia mambo ya maana zaidi ya karne hii ya ishirini na moja. Kumbe, hata kama kungekuwa na mwanga wa vijana wa Afrika kuchipuka katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia watachinjiwa baharini tu.
Kwa kumalizia, nawasihi tusome tena na tena masikitiko ya Baba Mtakatifu Benedikto XVII na. 93 anapotusikitikia Waafrika kwa kujifunga wenyewe minyororo ya kutojiamini. Kwa herini vijana!
Jumanne, 11 Julai 2017
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni