Jumanne, 11 Julai 2017

HISTORIA YA NJIA YA MSALABA

Njia ya msalaba ni desturi ya Ibada inayolenga kumfuata Yesu Kristo katika njia ya mateso msalabani hadi kaburini. Asili ya Ibada hii ni nchi takatifu, katika mji wa Yerusalemu ambapo Yesu aliteseka na kufa na mwisho kufufuka kama tunavyosoma katika Maandiko Matakatifu. Inasemekana Mama Bikira Maria alitembelea mara nyingi njia hiyo aliyoipita mwanawe Yesu Kristo katika mateso yake. Baadaye wakrito mbalimbali kutoka nchi za mbali walifanya hija katika njia aliyopita Yesu katika mateso. Rehema na Neema mbalimbali zilipatikana kwa hija katika njia hiyo.

    Mwanzoni ibada ya njia ya Msalaba haikufahamika sana mpaka mwaka 1342, ambapo maeneo haya matakatifu yaliwekwa chini ya uangalizi wa Ndugu wafuasi wa Mt. Fransisko wa Asizi.Baadaye walitambua baadhi ya maeneo ambayo matukio fulani yalitokea katika safari ya mateso ya Yesu. Baadhi ya maeneo hayo ni Yesu alipokutana na Simon Mkirene, Askari walipopigia kura mavazi ya Yesu,

Yesu alipopigiliwa msalabani nk. Ndugu hawa watawa na watu wengine waliyatumia maeneo haya kwa ibada ya kumfuata Yesu katika safari yake ya mateso. Polepole watu kutoka mbali walianza kufanya hija katika maeneo hayo. Kutokana na umbali na gharama hasa kwa wakristo toka Ulaya, katika Karne ya 15 na 16 wakristo wa Ulaya, walitengeneza vituo na kama ilivyokuwa Yerusalemu. Kwa umbali uleule toka kituo hadi kituo ili kuweza kuwasaidia wale walioshindwa kutembelea nchi Takatifu. Hii iliwasaidia kufuata njia ile ile aliyoifuata Yesu katika mateso yake Yerusalemu, lakini wakiwa katika nchi zao.

       Wakitambua utajiri wa ibada hii ya njia ya msalaba na ugumu wa kufanya hija mara kwa mara, ndugu Wafransisko walituma maombi maalum kwa Baba Mtakatifu wakiomba kuruhusiwa kuweka vituo vya njia ya msalaba kwenye makanisa yao ili Watawa wa Kifransisko wasioweza kufanya hija katika nchi Takatifu wafanye ibada hiyo pale walipo. Mwaka 1686, Papa Innosent XI aliruhusu na kutangaza rasmi kwamba “Rehema na Neema zilizopatikana kwa kufanya hija katika nchi takatifu, zingeweza kupatikana pia katika makanisa haya ya ndugu Wafransisko.” Ruhusa hii iliwahusu ndugu Wafransisko tu. Mwaka 1726, Papa Benedict XIII aliruhusu kwamba wakristo wote wangeweza kusali katika makanisa yenye vituo vya njia ya msalaba vilivyowekwa na mapadre wafransisko na kupata Neema na Rehema zilezile. Mwaka 1731, Papa Klementi XII, aliruhusu makanisa yote kuwa na vituo vya njia ya msalaba. Sharti moja ilikuwa lazima vituo hivi viwekwe na padre mfransisko kwa ruhusa ya Askofu wa Jimbo husika. Katika mwaka huo ndipo vilitambuliwa vituo 14 tunavyotumia sasa.

       Mwaka 1857, Maaskofu wa Uingereza waliruhusiwa na Papa kuweka vituo vya njia ya msalaba pale ambapo mapadre wafransisko hawakuwepo. Na mwaka 1862, Maaskofu wote au wawakilishi wao waliruhusiwa kuweka vituo hivi. Sharti la padre mfransisko liliondolewa.

       Hii ndiyo maana, katika makanisa ya kikatoliki huwa kuna picha 14 zilizopangwa kwa kawaida ukutani, kwa umbali fulani ili kuwezesha waamini kutembea kati ya moja na nyingine huku wakiendelea kutafakari juu ya mateso ya Yesu, jinsi ambavyo wangefanya mjini Yerusalamu ili kuweza kuelewa zaidi upendo wa Mungu, kuchukia dhambi na kuzifidia. Hata baadhi ya Walutheri na Waangalikana wanapenda ibada hiyo.

       Ibada hii, inaweza kufuatwa na mtu mmoja mmoja au kwa makundi. Mbali ya kila Ijumaa ya mwaka, waamini wengi hufuata njia hiyo wakati wa Kwaresima na kwa namna ya pekee Ijumaa Kuu.

       Mbali ya vituo 14 vilivyozoeleka zaidi, wengine wanapenda kuviongeza, kuvipunguza au kuvibadilisha hasa kwa kufuata zaidi habari za Injili na kumalizia na Ufufuko wake, (Kituo cha 15).

Tufuate njiiiiii a yaaa Msa laaba,
Tuifwateee, mpaka Kalvario oo,
Tusimamepo bila haaaaya,
Msaaalaba aa, msaalaba huponyaaaa roho!

Maoni 1 :

  1. asante, nami nitoe pia maoni yangu kuhusu njia ya msalaba kwa namna nyingine..fungua somo hili >> https://wingulamashahidi.org/2019/01/01/njia-ya-msalaba/

    JibuFuta